Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Zuena Athumani Bushiri

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nichangie Hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza nianze kwa kutoa pongezi na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayofanya katika Taifa hili. Pia namshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mawaziri wote katika Wizara zao kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya ambayo Watanzania wanaifurahia. Pia, namshukuru Mheshimiwa Spika pamoja na Naibu Spika na ninyi Wenyeviti kwa kuliongoza vizuri Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo, nitaanza kuchangia mchango wangu katika Sekta ya Maliasili na Utalii. Kwanza naipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii, Watanzania wote tunaona jitihada ambazo mama anazifanya na jinsi ambavyo sasa hivi watalii wameongezeka katika Taifa letu na kuongezeka kwa fedha za kigeni. Pamoja na mafanikio haya mazuri, lakini kidogo kuna maeneo mengine yanakuwa na changamoto ambazo wananchi wanapata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao Mlima Kilimanjaro ambao umezungukwa na msitu ulio katika baadhi ya kata ikiwepo Kata ya Katangara Mbele. Kata hii imekuwa inakumbwa na tatizo la matukio mengi sana ya kuathiriwa na nyani wanaotoka katika msitu huu. Matukio haya yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara na Wabunge wenzangu wa kutoka Kilimanjaro wamekuwa wakiongelea sana hili. Imefika mahali sasa nyani wale ambao wako katika msitu wetu wa TANAPA, KINAPA pamoja na TSF wanakuja mpaka maeneo ya nyumba za watu na hata wakati mwingine wakikosa kitu cha kula wanachukua watoto wadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo la kusikitisha kwa sababu, hili lilitokea Rombo na Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo alifanya mawasiliano na Wizara, akamwita Waziri pamoja na Naibu Waziri na Katibu Mkuu. Walifika Rombo na walifanya mkutano na Wananchi wa Rombo na walitoa ahadi kwamba, watalimaliza tatizo hilo, sasa ni miaka miwili imefika bado halijatekelezwa. Ukweli ni kwamba, asilimia kubwa ya wanaoathirika ni wanawake kwa sababu, wamekosa amani, hawaamini kama wanaweza kumwacha mtoto kwa dakika tano bila kumwona machoni kwa sababu, hawajui usalama wake ukoje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitendo hiki kilitokea, mtoto alichukuliwa na nyani akapelekwa chini ya bonde. Wananchi waliokuwepo walikimbizana wakaenda kutafuta ndizi, walipopata ndizi wakarusha kule chini bondeni walikokuwa wale nyani, na kwa tabia ya nyani huwa wanapenda sana ndizi, kwa hiyo, yule nyani alimwacha mtoto akakimbilia ndizi ndipo wananchi walipoteremka chini ya bonde na kwenda kumwokoa mtoto. Inasikitisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nini Wizara itafanya kwa jitihada za haraka sana ili kuhakikisha kwamba wanawasaidia wale wananchi wanaoishi maeneo yale kuhakikisha kwamba nyani hao wanapotea katika maeneo yale ya makazi ya wananchi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa unyenyekevu mkubwa, naiomba Serikali, natambua Mheshimiwa Rais, Dkt. Mama Samia Suluhu Hassan, anamjali sana mwanamke. Ninatambua mwanamke akikaa mahali kama hana usalama wa mtoto wake, hawezi kufanya chochote, anashindwa kufanya shughuli za uchumi, anashindwa kufanya shughuli yoyote, yeye ndiye anakuwa mlinzi wa mtoto. Kupitia Bunge lako, naomba Wizara ichukue hatua za haraka sana kuhakikisha inakomesha jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumaliza hilo nitaongelea tena Rombo kwenye upande wa barabara. Alikuja Makamu wa Rais wakati anafungua Hospitali ya Wilaya ya Rombo, akatoa ahadi kwamba atatengeneza barabara inayotoka Makao Makuu kwenda Hospitali ya Wilaya kwa kiwango cha lami, ambayo ina urefu wa kilometa tano tu. Ahadi ile mpaka leo haijakamilika. Naiomba Serikali kwa kuwa, huduma ya afya ni huduma inayohitaji barabara iwe nzuri, mwanamke anaweza akashikwa na uchungu akajifungua njiani kama barabara ni mbovu. Naiomba Serikali yangu sikivu, zile barabara ambazo zinapeleka huduma muhimu za jamii kama vile hospitali, Serikali izitilie maanani zitengenezwe kwa uharaka wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuongea habari ya barabara kwa maana ya ujenzi, nitaongelea habari ya uvuvi. Kilimanjaro tuna Bwawa la Kalemawe, ambalo liko Wilaya ya Same ya Mashariki. Bwawa hili lina urefu wa kilometa tatu na urefu wa mita 200. Bwawa hili lilijengwa kipindi cha Wakoloni wa Kiingereza. Lengo lao kubwa lilikuwa ni kuhakikisha kwamba wakulima na wafugaji hawaingii katika Hifadhi ya Mkomazi. Sasa bwawa hili limekuwa chakavu, bwawa hili sasa hivi limejaa matope, bwawa hili sasa hivi limejaa magugu, halina tena thamani ya kuitwa bwawa. Naiomba Serikali, ili kukuza uchumi wa wananchi wa eneo lile, ihakikishe inapeleka msaada wa haraka, kwanza wa kutoa yale magugu na pia, kuhakikisha kwamba bwawa linasimamiwa vizuri ili wananchi wa eneo lile waweze kupata samaki na kukuza uchumi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya bwawa hilo, narudi katika ziwa ambalo kila siku ninaliongelea na sitaacha kuliongelea mpaka litakapokamilika. Naongea kuhusu Ziwa Jipe, Mwanga. Nimeongea mara nyingi humu ndani na hata Mbunge wa Jimbo ameongelea Ziwa Jipe. Sijui shida iko wapi? Sijui ni nini kinakwamisha? Tunatambua wazi kwamba, Ziwa Jipe lina magugumaji mengi na yakitolewa, wananchi wa Mwanga watafaidika na samaki na watakuza uchumi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, viongozi wengi wanakwenda kufanya ziara pale na kila kiongozi anapofika anakutana na malalamiko ya wananchi katika mikutano. Mheshimiwa Mwenyekiti, hata juzi Mheshimiwa Makamu wa Rais Mheshimiwa Mpango, katika ziara yake ya Mkoa wa Kilimanjaro mwezi wa Tatu alikutana na hilo. Naona kila kiongozi anapopewa malalamiko anakubali, lakini utekelezaji wake haupo, haufanyiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yako sikivu, wale wananchi wa Mwanga wanategemea kipato cha mchanga. Kule Moshi tunapokaa mchanga wetu unatoka Mwanga. Hawana kipato kingine zaidi ya mchanga, na Bwawa la Nyumba ya Mungu ambalo sasa hivi samaki wake ni wachache sana, na ni wadogo, kwa hiyo, hawana kipato kingine. Ili kuwasaidia wananchi wa Mwanga, naomba Serikali yako itoe kauli kwa wale wananchi wa Mwanga kwamba ni lini watatoa magugumaji ili nao waweze kuinua uchumi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nitachangia, ni kuhusu…

MWENYEKITI: Mheshimiwa, hitimisha muda wako umekwisha tafadhali.

MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ahsante. (Makofi)