Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipatia nafasi ya pekee leo kuwa ndani ya Bunge hili. Mwenyezi Mungu atukuzwe sana. Vilevile napenda kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia, Mungu azidi kumpa maisha marefu, hekima na busara nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata nafasi hii ya kuweza kuchangia bajeti hii ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri ambazo anafanya pamoja na Mawaziri wake. Namshukuru sana dada yangu Mheshimiwa Mhagama kwa kazi nzuri ambayo anaifanya, tunaona anavyopambana akiwa jimboni, anaitumikia Serikali yake na anafanya kazi nzuri pamoja na Mawaziri wake. Hongereni kwa kazi nzuri na Mwenyezi Mungu aendelee kuwapa afya njema ili kazi iweze kwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nichangie upande wa elimu. Nashukuru kwamba Rais wetu ametupatia madarasa mengi nchi nzima takribani madarasa 23,000. Madarasa ni mengi na ni ya kutosha lakini tatizo ni moja, hakuna madawati. Japo tunajitahidi, lakini bado madawati ni changamoto. Tunaomba kwa upande wa elimu, madawati yaongezwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna shule ambazo ni za muda mrefu, zimechakaa sana, kweli ukifika ukiona yale majengo mapya na hayo ya zamani, yaani hayapendezi na hata shule yenyewe haipendezi. Tunaomba majengo ya zile shule yakarabatiwe ili na zenyewe zionekane kuwa ni mpya na zinafaa. Hata wanafunzi wanaosomea yale majengo mara nyingi hawajisikii raha na wanalalamika sana. Hata tunapokuwa na vikao mbalimbali walimu wanasema hayo yote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende haraka. Napenda niongelee habari ya kikokotoo. Kwa kweli, kikokotoo kinawasumbua sana wafanyakazi na malalamiko haya yamekuwa ni ya muda mrefu. Binafsi niliomba mkae na vyama vya wafanyakazi ili kuweza kukiondoa hiki kikokotoo, kinalalamikiwa sana. Mtu apewe pesa yake afanyie mambo yake mwenyewe, na ninaamini kila mtu huwa anapanga utaratibu. Naomba Serikali ilifanyie kazi hilo. Waziri Mkuu liangalie hili, mama yetu Mheshimiwa Mhagama liangalie hili ili muweze kulifanyia kazi, wafanyakazi wengi wanalalamika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua fainali huwa ni uzeeni, mtu anapopewa pesa kidogo, wengi huwa na maradhi mengi katika uzee, ule lakini hana pesa. Pesa imeshikiliwa, huku anapewa kidogo kidogo kiasi kwamba haimsaidii kitu. Tunaomba basi kwenye kikokotoo Serikali iweze kutusikia jinsi tunavyoomba, wafanyakazi hao wa muda mrefu wasaidiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna habari ya mapunjo ya mafao ya wastaafu, wengi hawajalipwa, wengi wanalalamika. Ukizunguka katika halmashauri nyingi utaona jinsi ambavyo wastaafu wanavyolalamika, ni wengi. Kila leo napigiwa simu, natumiwa message, jamani tunaomba wale watu basi wapewe mafao yao na walipwe haki zao kwa sababu walifanya kazi nchini Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naingia upande mwingine wa pili ambao nitaongelea Habari ya tembo. Tembo katika Mkoa wetu wa Simiyu kwa kweli wamekuwa ni tatizo kubwa. Nimekuwa nikisimama hapa, leo ni mara ya tatu naongelea habari ya tembo. Tembo wanaleta vurugu ya kutosha. Kuanzia kwenye mashamba, tembo anavamia shambani anakula, anaharibu yaani unakuta kila mwaka ni njaa. Wananchi wanajitahidi kulima, lakini bado tembo wanaingia kule wanafanya vurugu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchini Tanzania tumekuwa na mkakati wa kusema kwamba, tunaomba wafugaji wafuge kisasa. Wanapofuga kisasa ina maana anakuwa siyo mchungaji, bali ni mfugaji na yule mfugaji mifugo yake ile michache inampatia faida kubwa, kwa sababu atapata maziwa, atauza, atafanya hiki na hiki, maziwa yanamsaidia. Kwa hiyo, anapokuwa na ng’ombe wachache anaweza kuwamiliki vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nakuja kwa upande wa tembo; tembo wamekuwa wengi sana. Kwa nini tembo asifugwe kisasa? Kwa nini tembo wazaliane kama mbuzi kule porini na wanaingia kwenye hifadhi za watu wanawasumbua? Tunaomba kama tunavyowahamasisha wananchi kwamba wafuge kisasa, tunataka tembo nao wafugwe kisasa. Kwa nini wao wawe wengi zaidi ya binadamu? Wanatuhangaisha kwa kweli. Mnapowahamasisha wananchi, hamasisheni na wale tembo wapunguzwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapoona watalii wanakuja kuangalia wanyama, wanapenda sana kumwona tembo. Wanataka tu wamwone jinsi tembo alivyo na siyo wingi wa makundi ya tembo. Wanataka waone tu tembo yukoje. Sasa kama wanataka waone tembo yukoje, kwa nini hata Mkoa wetu wa Simiyu tusibaki na tembo nane tu? Wanatutosha sana kwa ajili ya watalii kuangalia hao tembo, kuliko kuwa wanaua tu watu. Wameua akina mama, akina baba na watoto wanaoenda shule. Kwani tembo anataka kuwa kama nani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia katika Kitabu cha Maandiko Matakatifu, Hosea 4:6 anasema, “Watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa.” Mungu alivyoumba hii dunia kwa muda wa siku tano alimwandalia binadamu mazingira mazuri: nchi kavu, bahari, maziwa, mito, maua, miti ya matunda na kadhalika. Siku ya sita akamuumba binadamu na akamwambia uwatawale wanyama na vitu vyote vilivyopo duniani, lakini leo sisi tumekuwa wa kutawaliwa na wanyama. Kila siku akina mama wanalia wamefiwa na watoto. Nikiangalia terehe 2/4/2024 kuna kijana mmoja anaitwa Juma Lucas, alivamiwa na tembo akaburuzwa vibaya sana mbavu tano zikavunjika na ndiyo tegemeo kwa mama yake. Akina mama wanalia kwa ajili ya tembo. Hawa tembo wana tatizo gani kuvunwa? Hilo ndilo swali langu la msingi. Mungu alisema sisi binadamu tuwatawale, je, tumekosa maarifa ya kuwatawala hao tembo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepoteza watu wengi. Kweli watu wanapoongea hapa na wengine wanalia wanatoa machozi, ni kweli! Tunapoenda kule kwenye mikutano mbalimbali, mikutano ya ndani na mikutano ya nje swali ni lile lile. Utaongea mambo yote mazuri anayoyafanya Rais wetu, lakini mwisho wa siku akina mama watanyoosha mikono.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Mheshimiwa Waziri atuambie, wameshindwa kuwadhibiti hawa tembo? Kule tembo wako kama mbuzi, yaani tembo wakitoka ni kundi kubwa kiasi kwamba unaweza ukakimbia na kuvunjika miguu. Tunaomba tusaidiwe kwenye habari ya tembo, imefanya hata watoto wa kule Mkoa wa Simiyu wengi wanashindwa kwenda shule. Anapokuwa akienda, njiani anakutana na tembo, akikutana na tembo, tembo anajua ni halali yake, ni kukanyagakanyaga kisha anakwenda zake. Mwananchi anauawa lakini tembo akiuawa inakuwa issue. Yule mtu aliyempiga tembo, atapigwa kama mpira wa kona, mpaka aleweke kwa nini amefanya hivyo, atakuwa ameshateseka sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hili Rais wetu anafanya mambo mazuri sana na inawezekana mambo haya makubwa hayajui jinsi watu wanavyoumia kule tulipo. Tunaomba Serikali yetu isimamie jambo hili ili likome, watu waweze kuishi kwa amani. Hotuba ya Waziri Mkuu ilisema, tunatakiwa kukaa katika hali yenye ulinzi na usalama. Ni kweli ulinzi na usalama upo lakini vipi maisha ya wananchi kwa upande wa tembo? Tembo katika Mkoa wa Simiyu wanaongoza. Ninavyohisi ni wengi hata kuliko watu. Kwa sababu wakitoka porini ni balaa, ni msururu mrefu, unajiuliza hao ni mbuzi wanakwenda mnadani au ni ng’ombe wanakwenda mnadani? Tunaomba jambo hilo lishughulikiwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaongea kwa uchungu kwa sababu kesi nyingi tunaletewa; “ooh, mwanangu amekufa, mwanangu amefanyiwa hivi, mume wangu amekufa.” Akina baba wa Mkoa wa Simiyu ni walinzi siku zote wanalala nje. Ni walinzi, walisomea mambo ya ulinzi lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa tembo nimekwambia kwamba ni wengi kiasi kwamba hata wale wafanyakazi hawatoshi kuwamudu. Ndiyo maana nimesema wavunwe wote kama ni kuuzwa wauzwe wabaki hata nane tu Mkoa wa Simiyu. Sisi hatuwahitaji. Wakibaki hao wanatosha kwa ajili ya watalii. Hata sisi wenyewe Watanzania tutakwenda kuangalia hata hao wachache wanatutosha, kwa sababu wingi wa tembo siyo tatizo, tatizo wanaua watu. Tunaomba hawa tembo waondolewe, wapunguzwe na wabaki wachache. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda sana kushukuru kwa hilo. Ninakwenda sasa sehemu nyingine ya mwisho. Nimesisitiza sana nikiwa na malengo…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Minza, muda wako umekwisha, tafadhali.
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)