Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuchangia Hotuba ya Bajeti ya Waziri Mkuu. Mchana wa leo nitapenda kuchangia katika sehemu iliyopo katika aya ya 215 hadi 218 juu ya Serikali kuhamia Dodoma iliyopo katika ukurasa wa 104 na 105 wa Hotuba ya Bajeti ya Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapochangia hoja yangu, kwanza napenda kutambua jitihada kubwa za Serikali za kuhamisha Makao Makuu kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma. Pia, Watanzania wote wajue kwamba jambo hili lipo kisheria, tayari na hakuna kurudi Dar es Salaam. Maana kuna wakati watu wanadhani kwamba huenda kuna siku tutarudi Dar es Salaam, hapana. Ijulikane pia kwamba maamuzi haya yameshafanywa pia na nchi nyingine. Mwaka 1991 Nigeria walitoa Mji wao Lagos wakapeleka Abuja. Kwa hiyo, siyo jambo ambalo ni geni kufanywa na Serikali za mataifa duniani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika kutambua jitihada za Serikali, nitambue kwamba Serikali imeendelea kutekeleza azimio hili la kuhamia Dodoma kwa ufanisi wa hali ya juu. Kwanza ni kwa jinsi ambavyo Serikali imejenga Ikulu, na tutambue kwamba Ikulu hii imesanifiwa na Watanzania wenyewe, Ikulu iliyo katika eneo kubwa ambayo inaleta mandhari nzuri katika Mji wa Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tutambue jitihada za Serikali kujenga Mji wa Serikali Mtumba, mji ambao ni mzuri. Napenda ni-note kitu hapa, ukiangalia barabara zilizojengwa katika Mji wa Serikali Mtumba, kwa pembeni wamewekewa waenda kwa miguu, jambo ambalo nadhani ni ujenzi wa kisasa. Kwa hiyo, miji yetu inapojengwa, naomba tuchukue template ya Mji wa Serikali Mtumba. Hizi barabara nyingine tunajengea waenda kwa miguu, guta, punda humo humo, hapana. Tuchukue template ya Mtumba maana ni barabara nzuri zilizojengwa katika Mji wa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia utatambua kwamba mihimili yote kwa kutambua kwamba Serikali imehamia hapa, Bunge linapanua maeneo yake ili kuweza kuweka miundombinu bora kwa ajili ya Wabunge na Watumishi. Pia, mhimili wa Mahakama umejenga jengo kubwa ambalo linaelekea kukamilika la Makao Makuu ya Mahakama hapa Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mambo mengine mazuri ambayo yanaashiria kwamba Serikali imehamia na inakuja hapa, ni kuweka barabara za mzunguko ambazo zitaondoa msongamano katikati ya mji, Kiwanja cha Ndege Msalato na pia Chuo Kikuu Kikubwa cha Dodoma hapa nchini. Utaona katika mipango ya Serikali ya kujenga Bwawa la Farqwa hata kama liko katika mipango, ni jitihada za Serikali kuendelea kutoa huduma bora ya maji katika Mji Mkuu wa Nchi hapa Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu iko wapi ninapochangia hoja ya Hotuba ya Waziri Mkuu? Tunapopanga miji yetu, kuna jambo moja linasahauliwa, lilisahauliwa tukiwa bado tupo Dar es Salaam na bado linaendelea kusahauliwa. Hivyo, napenda kuikumbusha Serikali yangu kwamba hili jambo lisiendelee kusahauliwa. Jambo hili ukiangalia katika mipango yake hautaona mahali ambapo Serikali imetenga eneo kubwa zuri la kupendezesha mji la kujenga makumbusho makubwa ya Taifa (museum). Kwa nini napenda kuongelea habari za museum? Yaani ukienda katika majiji makubwa duniani, ndipo ambapo unakwenda kutembelea lakini ukija hapa kwetu sasa hivi, bado hatujaona kama jambo hilo lipo katika mipango yetu. Kwa hiyo, pendekezo langu katika Hotuba ya Bajeti ya Waziri Mkuu ni kwamba, pamoja na mipango mizuri ya kupendezesha Jiji letu, hebu mpango huu tusiuache. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu gani nasema hivi? Ninapendekeza Makumbusho kubwa ya Taifa pamoja na maktaba kubwa iwekwe mahali ambapo inafikika...
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Waziri, Jenista Mhagama.
TAARIFA
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza, nimpongeze sana Mheshimiwa Profesa kwa msisitizo wake wa kuhakikisha tunakuwa na masterplan nzuri kwa ajili ya Jiji la Dodoma, hasa eneo hili la museum. Naomba nikuhakikishie Profesa, kwenye masterplan tuna eneo kubwa sana kwa ajili ya museum na tayari design ya kuwa na museum ya kisasa inayoendana na Jiji la Dodoma imekwishafanyika. Vilevile, tutakapoanza phase three ya ujenzi wa Makao Makuu ya Nchi Dodoma, ninaamini kwamba eneo hilo litakuwa ni miongoni mwa maeneo ya kufanyiwa kazi. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Waziri. Mheshimiwa Manya unaipokea hiyo taarifa?
MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea taarifa hiyo kwa mikono miwili. Sasa napendekeza mambo yafuatayo: Kama hilo liko katika mpango wa Serikali, unajua unapojenga museum na kama huo ndiyo mpango wetu, sasa mambo haya lazima tuyazingatie. Kwenye museum kimsingi unajua Serikali lazima ijidai, Serikali lazima iji-pride kwamba hii ni mimi na mimi ni Tanzania. Sasa tuna utajiri mkubwa sana, lakini pia tuna urithi wa utamaduni mkubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni katika museum ambayo sasa utajiri wote wa utamaduni ambao ni urithi wa vizazi vyote, historia yako ya Taifa tangu Tanzania kabla ya ukoloni, wakati wa ukoloni na baada ya kuwa huru, historia yote inawekwa pale. Pia ndipo mahali unapotambulisha utajiri wa nchi, wa maliasili na malikale vyote vinawekwa pale. Hata kama kuna uvumbuzi wowote ambao umefanyika hapa nchini, ndipo mahali pa kujidai. Kwa hiyo, kama hili wazo lipo kama alivyosema Mheshimiwa Waziri, tunapenda liweze kupangwa vizuri. Hebu fikiria mgeni akija Dodoma sasa hivi, tukishampeleka Mnadani siku ya Jumamosi kuchoma nyama, halafu atakwenda wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lazima tuwapeleke wageni wetu mahali ambapo tunaweza tukawaonesha kwamba sisi ni Tanzania. Kwa hiyo, sisi tunasema tuna utajiri mkubwa wa madini, lakini utagundua hata hapa ndani, Mheshimiwa Jenista kwa kuwa yeye anatokea Songea atakuwa anajua makaa ya mawe yanafananaje, lakini siyo wote. Kwa hiyo, tunachofanya, unachukua block kubwa tu la makaa wa mawe cubic meter nzuri kubwa unaweka pale unawaambia Tanzania huu ni urithi wenu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Tanzanite, yale madini ambayo kimsingi Serikali imeyanunua sasa hivi bado yako kule BoT tu yamefunikwa. Yaletwe kwenye makumbusho yetu ya Taifa ili kila mtu anayekuja Tanzania, unamwambia angalia utajiri wetu uko pale. Pia, kabla mtu hajaamua kwenda Serengeti kwa mfano, pale ndipo mahali pa kuangalia video clips za wanyama wanapohama, hatimaye anavutiwa na kufanya uamuzi wa wapi aweze kutembelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naona unaangalia muda wako, nimalizie tu kwa kusema kwamba, faida za kuwa na museum itakayokuwa imepangwa vizuri, kKimsingi inatambulisha urithi wetu wa kitamaduni, utajiri wa nchi, na kutunza vema historia ya Tanzania. Katika hilo ninakumbusha tusisahau maktaba nzuri ambayo nayo inaendelea kutunza historia kwa ajili ya vizazi vyetu vyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)