Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Anastazia James Wambura

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia hoja ambayo ipo mbele yetu. Kwanza kabisa, nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema, pia ametujalia tumemaliza Kwaresma salama na Pasaka tumeisherehekea vizuri. Tunamwomba Mwenyezi Mungu aendelee kuwalinda wenzetu ambao wako katika Ramadhani na tuombe pia atujalie Eid tuisherehekee vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kukupongeza kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wetu na kwa kweli tunakuamini sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuipongeza sana Serikali yetu ya Chama Cha Mapinduzi ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akisaidiwa na Mheshimiwa Dkt. Isdor Philip Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Baraza lote la Mawaziri kwa kazi nzuri sana ya utekelezaji wa Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa ninapongeza hotuba nzuri sana ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo imetuonesha ni namna gani bajeti ya ofisi yake inakwenda. Kimsingi, hotuba hii imeandaliwa kwa weledi mkubwa, hongera sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, hongera sana Wasaidizi wote, akina Mheshimiwa Jenista, Mheshimiwa Ndejembi na wote ambao wapo katika Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongelea maeneo mawili tu ambayo ni afya na elimu nikizingatia kwamba Serikali yetu ipo katika maandalizi kwa upande wa elimu kutekeleza mtaala mpya, lakini kwa upande wa afya kutekeleza Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote. Kwa hiyo, nitajikita katika maeneo hayo mawili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vigezo vikuu vinne ili tuweze kuwa na elimu bora katika nchi yetu. Kigezo cha kwanza ni mazingira bora ya kujifunzia, kigezo cha pili ni walimu na ufundishaji bora, kigezo cha tatu ni mtaala bora na kigezo cha nne ni tathmini. Kwa hiyo, hivi vigezo ni vya muhimu sana katika kuhakikisha tunakuwa na elimu bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuna tatizo moja, katika bajeti ya TAMISEMI mwaka 2023/2024 tulisikia kuna upungufu wa walimu kwa asilimia 51 katika shule za msingi na asilimia 51 katika shule za sekondari. Ukija kwenye takwimu mbalimbali za mwaka huu, utaona tuna upungufu wa walimu pia kwa asilimia 48 kwa ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa utaona kwamba katika kipindi chote hicho, tangu mwaka 2023 tumeweza kupunguza kwa asilimia tatu tu, kwenye upungufu wa walimu. Ninachotaka kusema ni kwamba tusipoangalia azma yetu ya kutekeleza mtaala mpya na azma yetu ya kuwawezesha Watanzania kuwa na elimu bora, kwa kweli inaweza ikawa ni ndoto. Kwa hiyo, naomba sana, Kamati ilipowasilisha hapa taarifa yake Kamati inayoshughulikia Elimu, Utamaduni, Michezo na Sanaa ilipendekeza kwamba ajira za walimu ziongezwe ili kusudi tuweze kuwasaidia Watanzania na watoto wetu waweze kupata elimu bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ukisikiliza michango mingi ya Waheshimiwa Wabunge tangu wakati ule wamependekeza walimu waongezwe na maswali mengi hapa Bungeni huwa yanaonesha kabisa kwamba walimu wanahitajika katika shule zetu. Kwa hiyo, naiomba Serikali izingatie ushauri wa Waheshimiwa Wabunge ili tuweze kutoka hapa tulipo na kwenda katika hatua ya mbele zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa afya nichukue nafasi hii kushukuru sana Wizara ya Afya ikiongozwa na Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu, pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Mollel kwa kazi nzuri ambayo wameifanya kule Mkoa wa Mtwara katika Hospitali yetu ya Rufaa. Tuliomba mahitaji mengi sana ambayo yalikuwa ni upungufu karibia items 25 lakini waliweza kutekeleza na hatimaye hospitali ile imezinduliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa safari moja huanzisha nyingine, ila siyo safari lager, ni safari ya kuimarisha afya ya wananchi. Wameongezeka wagonjwa wengi sana na wengine kutoka nchi za nje kuja katika ile hospitali. Tatizo kubwa ambalo liko hapa sasa ni upungufu wa madaktari. Kuna upungufu mkubwa wa wataalam wa afya katika hospitali hii. Tunahitaji wataalam zaidi ya asilimia 50, ndiyo upungufu uko hapa. Ukiangalia mfano wa department ya radiology wanatakiwa wawe minimum ya watumishi saba, lakini wapo watatu tu na tuna vifaa pale vingi. Kwa hiyo, vingine vinashindwa kutumika kwa muda unaostahili, lakini pia kwa upande wa akina mama kuna kifaa cha fluoroscopy, tunahitaji pale tupate mammography ili kusudi akina mama wasiweze kupata rufaa kwenda Dar es Salaam kwa kitu kidogo kama hicho waweze kutibiwa pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande mwingine, ile ni hospitali ya rufaa, lakini utaona kwamba watoto njiti wanapelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kutoka juu kupelekwa chini, hakuna kitengo cha watoto njiti pale, lakini ajabu ni kwamba jengo la mama na mtoto tayari lina michoro, ila tunasubiri tu ujenzi. Kwa hiyo, nikumbushe Serikali iweze kujenga jengo la mama na mtoto ili tuondokane na hii adha ya kutoa watoto njiti pale Hospitali ya Rufaa Kanda kupeleka katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa Bima ya Afya unategemea sana huduma. Tukiwa na huduma karibu na wananchi, wengi wataitikia na wengi wamependa sana hili suala la Bima ya Afya kwa Wote, lakini kinachotia hofu ni zile huduma. Kwa hiyo, naomba sana, Serikali izingatie kila Mkoa uweze kupata watumishi, kila Hospitali ya Kanda iweze kupata watumishi na vile vifaa vya muhimu ili kuondoa usumbufu wa rufaa za kwenda Dar es Salaam na kuleta msongamano. Hii inaweza ikaleta vifo ambavyo siyo vya lazima. Kwa hiyo, naomba hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo napenda kuomba ni Kituo cha Afya cha Likombe. Kile kituo cha afya kina huduma nzuri sana za uzazi, lakini kuna shida ya miundombinu, haitoshi. Imelazimu nyumba ya daktari ichukuliwe, daktari ahamishwe ili kusudi nyumba yake waongeze vitanda sita kwa ajili ya huduma ya wazazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana, Mungu awabariki. (Makofi)