Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba nitumie fursa hii kutambua kazi kubwa na nzuri ambayo inafanywa na Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na wasaidizi wake wote. Kama ambavyo wamezungumza wachangiaji wengine, ninaipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu ikiongozwa na Waziri Mkuu mwenyewe na wasaidizi wake kwa kazi nzuri ambayo wanafanya na hasa kazi nzuri ya kuisimamia Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe ushauri kwenye maeneo machache. Kwanza, nianze na jambo moja ambalo niliwahi kutoa ushauri huko nyuma. Kwenye mtandao wa kuomba ajira (Ajira Portal) ule mfumo umetengenezwa kwamba mwombaji anapoingiza zile credential zake siku ya kwanza, akiingiza kwamba amesoma Fisheries, next time kama huyo mtu alikwenda kusoma kitu kingine ule mfumo hauwezi kupokea. Sasa hali ilivyo sasa kutokana na uhaba wa ajira, vijana wengi wanakuwa ni multi professional, wanasoma vitu vingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mtu aliyeanza akasoma certificate ya Wildlife Management anapofikisha miaka 25 kwa mujibu wa taratibu za watu wa maliasili, haajiriki tena. Huyo mtu ana-opt kwenda kusoma kozi nyingine, lakini kwa sababu kwenye mfumo mle ndani tayari anasomeka aliwahi kuingiza Wildlife, ule mfumo unam-reject. Mnafahamu vizuri kwamba mfumo ukishamkataa na umri umeenda, hawezi kuajiriwa tena na kozi ile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wengi wanaanza kusoma siku hizi, wanakwenda kwenye technical schools. Anaanzia technical school, anasoma diploma, anakwenda anasoma degree, halafu anasoma masters. Ukiingiza cheti cha diploma ukija kuingiza cha degree unaku-reject. Sasa sijui huwa wananielewa nikizungumza. Hebu naomba mlichukue jambo hili mlifanyie kazi, kwani linasababisha vijana wengi kushindwa kupata ajira kwenye mfumo. Nalizungumza hili kwa mara ya pili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la pili, tunaishukuru Serikali kwamba baada ya hali mbaya ya hewa, barabara nyingi sana ziliharibika. Tumepata pesa ya emergency shilingi milioni 400 katika Jimbo la Geita Mjini kwa barabara ambayo inatuunganisha kati ya Geita na Nyang’hwale, lakini pesa hiyo imeenda kujenga daraja moja peke yake. Ile barabara ina madaraja manne yaliyokatika na hakuna tena mawasiliano. Kwa mujibu wa taarifa iliyopo ni kwamba ile shilingi milioni 400 ndiyo imetosha. Kwa hiyo, hamna kilichofanyika pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Geita hivi tunavyozungumza hakuna barabara, zote zimeharibika kwa sababu ya mvua nyingi. Sasa naomba jambo hili lifanyiwe kazi kwa sababu katikati ya mji pamejitengeneza vijito, barabara zimekatika, magari yanatitia. Mtu anaacha gari nyumba ya sita ndiyo anakwenda kwenye nyumba yake. Naomba barabara hizi zitengenezwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, tunaishukuru Serikali, tumejenga shule nyingi na tumejenga zahanati nyingi. Tatizo kubwa sasa limekuwa ni wafanyakazi. Naiomba Serikali ifanye takwimu. Mimi kwa miaka mitatu pekee ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan nimejenga shule mpya sita. Shule nne nimepata pesa kutoka Wizarani, lakini kwa miaka mitatu wameleta walimu 12. Sasa shule sita on average shule moja inahitaji walimu 24, umeleta walimu 12. Maana yake ni kwamba walimu tumewatoa kwenye shule nyingine zisizokuwa na uhaba wa walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuna shule mpya ambayo tayari ina wanafunzi 4,000 ina walimu watano. Sasa hiki kinakuwa kichekesho. Mwaka 2023 Mheshimiwa Waziri Ndejembi kabla ya kuhama Wizara, aliniahidi ataniletea walimu, hakuleta mwalimu hata mmoja kwenye halmashauri ya mji. Sasa tumejenga shule sita, halafu hakuna walimu kwenye hizo shule, sasa zinafanya kazi gani? Nataka kuiomba Serikali kwanza tupate hawa walimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye afya tumejenga zahanati za kutosha na tumejenga vituo vya vitatu, lakini havina watumishi. Sasa pengine ni vizuri Serikali ikatafuta takwimu kwanza za zahanati ngapi ambazo ziko tayari na zinataka watumishi wangapi ili halmashauri ziache kuwekeza kwenye zahanati. Tena watuzuie kabisa msijenge nyingine mpaka tukamilishe hizi waweze kutuletea nyingine. Vinginevyo tutakuwa tunatumia pesa halafu zahanati zinakuwa mazalia ya popo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, nilimwona Dodoma akishughulika na migogoro ya ardhi. Nilimpongeza kwa sababu ulikuwa ni ushauri wa Kamati kwamba lazima wale waliotengeneza migogoro ile waweze kushughulikiwa. Sasa mimi ninao mgogoro wa ardhi Geita. Namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, aliushughulikia kabla ya kuondoka na Mkuu wangu wa Mkoa ameushughulikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Madini, kwani tuna tatizo la wananchi wa Nyakabale. Nyakabale ni mtaa ambao una zaidi ya watu 5,000. Watu hawa wako ndani ya vigingi vya GGM. GGM wanakataa kulipa fidia kwa sababu wanasema hakuna sheria. Serikali kwa miaka 24 imeshindwa kuwalazimisha GGM wawalipe fidia watu wa Nyakabale. Matokeo yake vyanzo vya maji vyote vya Nyakabale vinavujiwa na maji machafu; watu wanakosa maji ya kunywa. Hatuwezi kupeleka huduma pale kwa sababu lile eneo huwezi kulipima na liko katikati ya mji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye uchangiaji wangu wa mwanzo niliomba, nikasema, kwa sababu ni upungufu wa kisheria, Serikali ndiyo iliyotengeneza sheria kwamba huyu mwenye mining licence ana miliki eneo lake na kulilinda na kuzuia watu wasiendeleze, lakini hawawajibiki kulipa fidia mpaka watakapotaka kuchimba. Sasa kwa kuwa wananchi wale wameathiriwa na zuio hilo, Serikali yenyewe iwalipe fidia halafu ihangaike na huyo mwekezaji. Kuliko kuwaacha hawa wananchi wakaendelea kuishi kwa umasikini wao na ardhi ni ya kwao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tano, nampongeza Mheshimiwa Jerry Silaa, anafanya kazi yake vizuri. Mkuu wangu wa Idara ya Ardhi alitembelewa na Kamishna wa Ardhi na Kamishna wa Ardhi alikwenda na vyombo vya habari. Akafika akaonesha kwamba kuna mafaili ya watu zaidi ya 100 ambayo hayajashughulikiwa, wanasubiri hati. Mheshimiwa Waziri wa Ardhi akampongeza kwenye Instagram; “Hongera kwa kufanya kazi yako vizuri.” Kesho yake yule Mkuu wa Idara anaandikiwa barua ya kushushwa cheo kwamba amechelewesha majalada 100 kutengeneza hati. Sisi sote hapa ni Wabunge huwezi kuona kwamba ile ilikuwa drama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tangu lini kwanza unakwenda kwenye ofisi kukagua kazi, unakwenda na vyombo vya habari? Pia hakuna mafaili 100, yule anashushwa cheo wakati mafaili yaliyokuwa yanasubiri hati ni 30. Halafu naomba nimalizie katika hayo 30, watu hawana NIDA na hawana mikataba ya mauziano. Sasa huyu Afisa Ardhi afanye kazi gani? Kuonesha kwamba ni drama, siku ile ile Waziri anampongeza, kesho yake huyu Kamishna wa Ardhi anakwenda kuwashusha cheo Maafisa wateule wote kwamba nimewaondoa cheo na kuteua wengine. Tunawaonea watumishi.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika moja.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Constantine Kanyasu, ahsante.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika moja tu namalizia. Sote tunajua haki ya mtumishi kabla hujamchukulia hatua lazima um-charge, umpe nafasi ya kujitetea uone majibu yaliyojificha kama hayana maana ndiyo um-charge. Huwezi kumwadhibu kwanza...
MWENYEKITI: Ahsante Serikali imesikia.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. (Makofi)