Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Anatropia Lwehikila Theonest

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi nami niweze kuchangia mawili matatu kwenye hoja iliyoko Mezani. Nitakuwa sio mwingi wa fadhila nisipotambua mchango wa Mheshimiwa Waziri Mkuu hususan kwenye zao la kahawa kwa Mkoa wa Kagera. Ukweli ni kwamba, changamoto zilikuwa ni nyingi sana, nimelia pamoja na Wabunge wengine ambao wanazalisha kahawa na mikoa inayotoa kahawa. Tumeongea mara nyingi tukilia kilio chetu kuhakikisha bei ya zao la kahawa inapanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bei hiyo ilikuwa ikipata changamoto ya tozo kadha wa kadha, lakini hizo tozo ziliondolewa na hivyo kusaabisha bei kuongezeka kidogo. Vilevile, kwa Mkoa wa Kagera, moja kati ya kilio changu ilikuwa ni suala la minada kuacha zao la kahawa likawa soko huria kama yalivyo mazao mengine, mwenye kuwa na bei ya kutosha akaweza kushindanishwa na kuuza kahawa. Nashukuru sana kwamba haya yote yameweza kutendeka na leo tunaona bei ya kahawa imepanda kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tuna changamoto nyingi za msingi kwenye zao la kahawa. Hizo kwanza nazi-register kabla sijaanza kueleza hoja nyingine. Kwanza, ni changamoto ya pembejeo. Leo kahawa pamoja na mazao mengine ya migomba yanashambuliwa sana na changamoto inayoitwa mnyauko, lakini nitaongelea kahawa. Kwa hiyo, mikahawa mingi mikubwa inashambuliwa na kuharibika na wananchi kukata tamaa. Pia kuna vidudu vinavyoishambulia hii miche.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tushukuru kwamba kumekuwepo na juhudi za kuwapatia mbegu lakini bado mbegu ni chache ukilinganisha na uwezo wa kuzalisha na nia ya watu wa Mkoa wa Kagera, Wilaya ya Kyerwa na Karagwe kuendelea kuzalisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee upande wa pili, kila neema inakuja na changamoto. Nimkumbushe Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba nili-register wakati tunaongea kwenye kikao nika-register changamoto ya wananchi wa Kyerwa na hasa maeneo ya mpakani kunyanyaswa kwa sababu ya zao la kahawa. Nikaeleza adha wanazozipata wakibambikizwa na kuambiwa kwamba wanavusha kahawa. Nikaeleza vifo vilivyotokea kwa watu kuambiwa wanavusha kahawa bila Ushahidi, lakini bila kufuata due process kwamba mtu kama anavusha kahawa, basi akamatwe, apelekwe Mahakamani ashtakiwe. Mlolongo wa haki jinai tunaoujua ufanyike na mtu apate haki yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitawataja baadhi ya watu. Mtu mmoja ambaye aliathirika anaitwa Jimmy Bagumila Ninondi. Huyu kijana anatokea Kijiji cha Rwabikagati Kitongoji cha Omukagando. Huyu kilichomkuta sasa wakati wanasema huo msako wa kahawa unapita yeye walishamlenga, aligongwa na defender mara mbili, yaani wakamgonga mara ya kwanza, wakahisi kwamba hajafariki vizuri, wakampitia mara ya pili na akafariki hapo hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nijue hao waliofanya hicho kitendo magari yanafahamika, waliofanya hivyo vitendo wapo. Nataka kujua wamechukuliwa hatua gani za kisheria, kwa sababu hiyo siyo namna sahihi. Haki jinai anayoisema Mheshimiwa Rais, siyo ya kugonga mtu na Defender na kumuua. Nataka nijue haki ya huyu mwananchi iko wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wa pili anaitwa Vadi, huyu anatokea Kijiji cha Nyabiaga Kata ya Bugomora. Alikuwa ni dereva akiendesha gari kwenda kata nyingine ya jirani ya Kaisho, akavamiwa akaambiwa kwenye hiyo gari yako unavusha kahawa. Kukatokea taharuki kubwa sana akakimbia. Sasa wale wanajeshi ambao wanajifanya wanalinda kahawa waliwasha kijiji chote kwa risasi. Nadhani mnakumbuka niliwahi kueleza kwenye briefing, risasi za moto zaidi ya 100 zikarushwa zikatafuta hao wanakijiji. Kama haitoshi, huyu kijana akapigwa risasi ya koromeo akapelekwa Bugando. Nilienza incidence yake ikiwa ni pamoja na mwenzake ambaye alikuwa anaitwa Monge Vincent ambaye yeye alipigwa risasi ya kichwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niulize, hata kama wanavusha kahawa na hata kama wanafanya nini? Hiyo ndiyo due process ambayo tunaiongea kila siku? Hiyo ndiyo haki jinai ambayo Mheshimiwa Rais amekuwa akipigania? Nataka nipate majibu ni hatua gani zimechukuliwa kwa hawa wanajeshi pamoja na askari ambao wamekuwa wakinyanyasa wananchi kwa neno moja tu kwamba wanavusha kahawa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sio huyo tu, nakutajia na incidence nyingine. Kuna wanakijiji walikuwa kwenye harusi gari ya defender imekuja ya hawa wanajeshi wakawavamia. Hawa wanajeshi wakala vyakula vyao, wakanywa pombe zao na wakawapiga kwa sababu ya kile kile kinachoitwa kuvusha kahawa. Nataka nieleze wazi, kuna mwingine anaitwa Charles Amos, Mwenyekiti, Afisa Mtendaji Mstaafu wa Kijiji cha Mulongo naye amepigwa kwa sababu anatoa kahawa eneo moja kwenye shamba lake moja kwenda kwenye shamba lingine.

MWENYEKITI: Nimemwona Mheshimiwa Waziri amesimama. Tafadhali Mheshimiwa Waziri.

TAARIFA

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakupongeza lakini nataka nitoe taarifa. Wanajeshi kazi yao ni kulinda amani na mipaka. Kwa hiyo, siyo kweli kwamba wanajeshi wanapiga wananchi kama ilivyoelezwa, labda Mbunge atoe uthibitisho wa hilo analolisema, ahsante.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Anatropia unaipokea taarifa ya Mheshimiwa Waziri?

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, with due respect, naomba Mheshimiwa Waziri afuatilie kinachotokea Kyerwa. Natambua juhudi Wanajeshi, lakini ninavyoongea, inapofika wakati wa kahawa wanatumiwa kwa kile kinachoitwa kulinda kahawa isivuke. Kwa hiyo, ninachokieleza, it is with facts, nakielewa. Naomba niendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha pili ambacho nataka nieleze ukiachana...

MWENYEKITI: Samahani Mheshimiwa Anatropia. Mheshimiwa Waziri, tafadhali.

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, bado naomba uthibitisho wa hayo anayoyasema, atoe ushahidi.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Anatropia, Mheshimiwa Naibu Spika, alikaa kwenye Kiti hiki asubuhi, akatoa maelekezo juu ya utaratibu wa vithibitisho pale tunapokuwa na allegations kubwa kwa Serikali. Mheshimiwa Anatropia, kadri ya Majibu ya Mheshimiwa Waziri au kadiri ya taarifa ya Mheshimiwa Waziri, wote tunajua kazi ya Jeshi la Wananchi ni kulinda mipaka ya nchi yetu. Kama Jeshi la Wananchi linafanya tofauti na hayo ambayo yanatarajiwa kufanywa na Jeshi letu, basi naomba andaa taarifa yako yenye vithibitisho na uilete kwenye Meza ya Spika, na Serikali chukueni hiyo taarifa kama alert ili muweze kufuatialia na ninyi muweze kujiridhisha kwa upande wenu.

Mheshimiwa Anatropia, endelea.

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, tumechukua muda mrefu, naomba niishauri Serikali, na hiyo ndiyo hoja ninayoileta, kwamba uchunguzi ufanyike ili kufahamu nini kilitokea katika msimu wa kahawa mwaka 2023 na kujua matukio yaliyofanywa na wanajeshi na matukio yaliyofanywa na Polisi kwa wananchi. Hapa tupo kwa ajili ya kutetea maslahi ya wananchi, hivyo kila mwananchi aliyeumizwa aidha kwa watu kukiuka sheria kwa makusudi au bahati mbaya, wanapaswa kupata haki yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naiomba Serikali, na nimewahi kumweleza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye kikao kilichofanyika Kyerwa, nikashauri kuwepo na tume ya kwenda kuchunguza na kuondoa changamoto zilizotokea Kyerwa. Hiyo ndiyo nasisitiza kwamba ni lazima ifanyike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaenda kufungua msimu mpya wa kahawa, kama changamoto zilizojitokeza mwaka 2023 zinaenda kujitokeza tena, sisi kahawa siyo neema, ni kifo. Narudia, changamoto zilizojitokeza mwaka 2023 kama hazitafutiwi ufumbuzi na waliofanya kwa makusudi kutesa wananchi, kuiba kahawa zao na kadhalika, wachukuliwe hatua, na kama itatokea basi changamoto itakuwa kubwa katika miaka inayokuja… (Makofi)

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu.

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba muda wangu ulindwe.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Anatropia, muda wako wa kuzungumza umekwisha.