Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Muhambwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ili niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naungana na wenzangu kwa kuanza kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya katika nchi yetu. Sote ni mashahidi, katika Majimbo yetu pesa nyingi za miradi zimekuja. Kipekee katika Jimbo la Muhambwe shilingi bilioni 52 zilizoletwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndani ya miaka mitatu zimelichechemua Jimbo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri anayoifanya katika nchi hii. Nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu kwa kazi nzuri anayoifanya, tumemwona anavyokimbia kuhakikisha wananchi wetu wanapata umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri Jenista Mhagama na Mheshimiwa Deogratius Ndejembi, Naibu Mawaziri na Watendaji wote wa Wizara hii kwa hotuba nzuri waliyotuletea na kwa kazi nzuri wanayoifanya kuhakikisha kwamba uratibu wa kazi za Serikali unakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakupongeza wewe kwa kiti hicho ulichokalia, kwa kweli kinakutosha. Unatosha na chenji inabaki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio makubwa tuliyokuwanayo katika majimbo yetu, bado ziko athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoendelea katika majimbo yetu. Kipekee katika Jimbo la Muhambwe, madhara ya mvua yamesababisha uharibifu wa barabara nyingi, barabara zimekatika na hazipitiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Kichananga – Kigina - Magarama mto mkubwa umekatika. Wananchi wanapita kwa kulipa pesa, ambapo mtu mmoja shilingi 1,000/= na pikipiki shilingi 3,000/= huku magari hayapiti kabisa. Hii ni Kata ya Rugongwe ambayo katika Jimbo la Muhambwe ndiyo kata inayoongoza kwa uzalishaji wa vyakula. Kwa hiyo, unaweza ukaona ni madhara gani wakulima katika Kata hii ya Rugongwe wanayapata kwa sababu sasa mazao yao yanaharibika katika mashamba yao, lakini hawawezi kupeleka sokoni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Kifura – Nyange hasa pale Mukabuye imekatika na wananchi hawawezi kupita kabisa kwa sababu mto umekatika na barabara imekatika. Barabara ya Kitahana – Nyange kupitia Mto Kahambwe nayo imekatika, wananchi wanapata shida sana. Barabara ya kutoka Kibondo – Nyaviumbu Mto Nyaviumbu umekatika, wananchi hawawezi kupita. Nimejaribu kusema kwa uchache barabara chache zilizokatika kwa sababu ya madhara ya mvua. Mbali na wakulima kupata shida, sasa imekuwa ni changamoto kusafirisha wajawazito, watoto kwenda shule ni changamoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa nasi tulikuwa miongoni mwa wale waliondika maombi ya dharura. Ninavyosikia hapa, wenzangu wamepata fedha za dharura, wanasubiri wakandarasi, mimi nabaki nashangaa kwa sababu, sina hata shilingi moja. Pamoja na wananchi wangu kutaabika kwamba wanavuka mito kwa kutumia fedha, lakini sijapata fedha yoyote ya dharura katika Jimbo hili. Naomba jicho la huruma Serikali hii sikivu, Jimbo la Muhambwe tuko kisiwani kwa sababu ya barabara zilizokatika. Naomba tupatiwe fedha za kutengeneza hizi barabara ili wananchi wangu waweze kusafirisha mazao, kwenda hospitali na watoto waende mashuleni kwa sababu tuko kisiwani kutokana na mvua hizi zinazoendelea katika Jimbo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mabadiliko ya tabianchi yameenda mbali zaidi, imesababisha tumepata madhara makubwa ya makorongo. Nikisema makorongo, unaweza ukafikiri ni jambo dogo, lakini makorongo ambayo yalikuwa ni mfereji mdogo, sasa yamepanuka sana kiasi kwamba yanaleta madhara makubwa. Makorongo haya yamefikia kiasi yanang’oa miti na hata nyumba. Lile korongo la Migombani pale limeng’oa nyumba ya mwalimu, nyumba ya vyumba vinne imeng’oka kwa sababu ya maji yanayopita kwenye korongo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna korongo la Mto Katunguru ambalo lina urefu wa zaidi ya mita 800 na upana wa zaidi ya mita kumi. Tuna Korongo la Kanyamahela, hili lina urefu wa zaidi ya mita 368 na upana wa mita nane. Tuna korongo la Kumwai ambalo lina urefu wa zaidi ya mita 418 na upana wa mita kumi. Tuna korongo la Twabagondozi ambalo lina urefu wa mita 246 na upana wa mita nne. Tuna korongo la Migombani la mita 625 na upana wa mita sita. Nimeyataja kwa uchache hayo yaliyoko Kibondo Mjini lakini hata Kata za Bitale na Kagezi zina makorongo. Kwa hiyo, madhara ya makorongo katika jimbo hili nayo yanaleta madhara makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, nyumba zinaondoka kwa sababu ya yale maji mengi yanayopita kwenye makorongo, miti inang’oka, na sasa wananchi hawawezi kupita, na kwa upande mwingine inasababisha madhara ya utoro shuleni kuwa mkubwa kwa sababu hawezi kupita hata kama nyumba iko hapa na shule iko hapa, inabidi mtoto azunguke njia ndefu sana ili aende shule, matokeo yake mtoto haendi shule. Pia wagonjwa hawawezi kupita kwa sababu hakuna barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefanya ziara pale kwenye makorongo na engineer wa TARURA, lakini akaniambia haya ni makorongo, hii siyo barabara, mimi siwezi kutengeneza. Naiomba Serikali sikivu, kupitia vifungu vya majanga, haya makorongo nayo katika Jimbo la Muhambwe ni janga. Kupitia wadau tulipambana tukampata mdau wa maendeleo Ernesto akatusaidia kujenga korongo moja ambalo lilikuwa karibu na club ya akina mama kwa teknolojia ya gabion. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii teknolojia wanaweka mawe na nyaya na wanapanda miti mle. Hata hivyo, ametengeneza daraja moja tu kwa hii teknolojia ya gabion. Halmashauri yetu kupitia mapato ya ndani haiwezi gharama za kutengeneza hayo makorongo. Naiomba Serikali sikivu, waje Muhambwe, kwani haya makorongo nikiyasema mtu hawezi kuelewa. Waje Muhambwe ili waone madhara tuliyoyapata kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi katika Jimbo letu la Muhambwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kifanyike? Kwa sababu takwimu zinaonesha kuwa hekta 400,000 za miti zinaendelea kuteketea kila mwaka kwa sababu ya moto kichaa na kukata miti ovyo, pamoja na ukataji miti ambao unatumia vibali maalum, nadhani ni muda muafaka, turejee nyuma tuone zile sheria zilizopitishwa za kuvuna miti, kwamba je, ni kweli tunavuna na kupanda? Je, uvunaji miti unaenda sambamba na upandaji? Kama ingekuwa hivyo, madhara haya yasingekuwa hivi. Naiomba Serikali tuachane na habari ya kupanda miti kwa ajili ya kupiga picha na sasa tupande miti ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa sababu kwa kweli madhara ni makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kuishukuru Serikali kwa kazi nzuri ambayo inafanya Jimboni Muhambwe. Kipekee, tunashukuru kwa barabara ya lami kilometa 47 kutoka Kibondo – Mabamba. Barabara hii imeanza ujenzi na mkandarasi anaijenga kwa kasi. Kwa masikitiko makubwa, wananchi walioathirika na barabara ile bado hawajalipwa fidia. Kutokulipwa fidia kwa wale wananchi kumesababisha mkandarasi ambaye tayari alikuwa site ashindwe kuendelea na kazi. Wananchi wanadai shilingi bilioni 1.2. Kwa heshima na unyenyekevu naiomba Serikali sikivu iwalipe wananchi hawa ambao wameathirika na barabara hii ili kazi iendelee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)