Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi. Kwanza niende kwa haraka haraka, nimpongeze sana Waziri mwenye dhamana, Mheshimiwa Engineer Hamad Masauni. Pamoja naye nimpongeze Ndugu yangu Mheshimiwa Sillo kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais katika nafasi hiyo na tunamtakia kila la kheri katika kutimiza majukumu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo ameendelea kuiheshimisha nchi na kipekee katika taasisi na hivi vyombo ya ulinzi kwa sababu nchi yetu imeendelea kuwa ni kisiwa cha amani na wananchi wanafanya shughuli zao bila matatizo yoyote. Kipekee pia niipongeze Wizara kwa usimamizi mzuri wa vyombo ambavyo vipo chini na mamlaka yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina eneo moja ambalo ningetaka nianze nalo, ni kuhusu Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA). Tarehe 15 Disemba, 2023, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji ilitoa tangazo la kuunganisha taasisi ambazo zinashabihiana ama zinafanana zikiwa katika eneo moja ama katika maeneo tofauti. Miongoni mwa taasisi hizo ilikusudiwa kuunganishwa kwa taasisi ya NIDA pamoja na RITA. Kwa kuangalia kwa mtazamo wa juu ni kwamba taasisi hizi zote mbili zinahusika kwa namna moja ama nyingine na suala la usajili na utambuzi, lakini ukienda kwa undani zaidi unagundua kwamba majukumu yake kuna mahali yanafanana na kuna mahali yanaachana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka niishauri Serikali kwamba eneo hili ni vyema tukalitazama kwa mapana kwa sababu RITA inasajili ndoa na vizazi; lakini ukija kwenye NIDA inaanza kutambua, kwa maana pia ina component ya uraia na hapa inahusika na suala zima la uhamiaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwangu mimi naona kwamba NIDA ni chombo cha kiusalama wa nchi zaidi; hivyo ni vizuri tukalitazama hili jambo kwa mapana makubwa ili kuhakikisha kwamba chombo hiki tunakiimarisha zaidi. Ingependeza zaidi kwamba badala ya kuvitenganisha ni vizuri tukavitenganisha kwa majukumu. Kwa mfano suala la usajili na utambuzi likawa chini ya NIDA na tukawaongezea pia pamoja na kusajili vizazi, vifo, ndoa, uasili watoto; na haya mambo mengine ya udhamini, ufilisi na mirathi yakabaki kuwa chini ya RITA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tunaweza tukajifunza hata kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, wanacho chombo kinachoitwa ZCSRA ambacho kinatekeleza majukumu ya usajili wa vifo, vizazi, ndoa, talaka pamoja na utambuzi wa watu na kutoa vitambulisho vya Mzanzibar Mkaazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uzoefu, pia katika Mataifa mengine kama vile Rwanda, Botswana na Afrika Kusini majukumu haya yanafanywa na Ofisi za Kabidhi Wasii Mkuu, kwa maana mambo ya udhamini, ufilisi na mirathi. Kwa hiyo tukijifunza hapo tunaweza tukaona kwamba tunaweza bila kuunganisha tutatenganisha tu majukumu. Kwamba yale yanayofanywa na RITA yakaenda moja kwa moja kwenye NIDA ili NIDA ianze kusajili, kama ambavyo Kamati imesema, katika hatua ya kwanza ya mwezi mmoja baada ya mtoto kuzaliwa. Kwa hiyo hilo naliomba sana tulitazame katika muktadha huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili, ziko baadhi ya Nchi ikiwemo Kenya, Zambia, Singapore pamoja na Botswana pia eneo hili lipo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani, kama ilivyo hapa kwetu kwamba NIDA ipo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Hiki ni chombo cha kiusalama na kwa hiyo ni vyema kikabaki kuendelea kuwa chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa ajili ya suala zima la usalama wa nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, nataka nizungumzie jambo moja tu linaohusu mahabusu, hasa wale ambao wanakamatwa na Majeshi Usu ambayo tumeyaanzisha. Mara nyingi majeshi haya siku hizi yanakamata na yanapokamata kwa sababu hayana mahabusu wanakwenda kuwaweka katika mahabusu hizi za polisi, ambapo polisi hawana mamlaka na hawa mahabusu ambao wamekamatwa either na TANAPA, TAWA ama na TFS, kwa mifano hiyo. Kwa hiyo ninachojaribu kuomba ni kwamba, Watanzania wanatambua kwamba Jeshi la Polisi limeanzishwa kwa ajili ya usalama wa raia na mali zao, kwa hiyo hiki ni chombo cha wananchi ambacho kinakamata kwa muktadha wa kiraia. Sasa, haya majeshi yapo ambayo yanapamabana na ujangili, yapo ambayo yanapambana na uhalifu na yapo ambayo yanapamba na uvamizi. Kwa hiyo hata namna ya ukamataji ni tofauti na Jeshi la Polisi linavyofanya. Kwa hiyo nashauri na hili lipo pia katika Taarifa ya Haki Jinai, kwamba suala la kukamata liendelee kubaki chini ya mamlaka ya Jeshi la Polisi na hivi vyombo vingine vikamate kupitia Jeshi la Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)