Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chaani
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii asubuhi ya leo kuwa mchangiaji wa pili kwenye hotuba hii ya taarifa ambayo ameiwasilisha Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, ambaye ni Mheshimiwa Masauni. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia hata leo hii nikaamka mzima. La pili, nikushukuru wewe Mheshimiwa Mwenyekiti kwa umaridadi wako wa kusimamia kiti vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa nina makosa makubwa sana nisipompongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna alivyofanya kazi kwa kipindi kifupi tokea kuwa madarakani, hususani kwenye Wizara hii ya Mambo ya Ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa mambo makuu matatu, hususani kwenye Wizara hii. Moja tumeshuhudia zaidi ya magari 181 ambapo 71 sasa hivi tayari yameshagawiwa kila wilaya. Kwa hiyo mpaka sasa hivi ninavyozungumza ma-OCD wetu wa wilaya huko wanatembea na magari kwa neema hii ya Mama Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana pia Mheshimiwa Rais, kwenye zima moto nako pia tumeambiwa kuna magari zaidi ya 150, nayo yapo njiani kwa ajili ya kusaidia huduma hii ya zimamoto nchini kwetu, kwamba kila wilaya itapata gari. Kwa hiyo nampongeza sana Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais nampongeza sana vile vile kwa huduma ya TEHAMA. Tunaambiwa sasa hivi takribani kwenye mipaka yote ya nchi hususani kwenye eneo la airport nako tutapata vifaa vipya ambavyo vitakwenda kwa ajili ya kuzuia uhalifu wowote ambao unategemewa huenda ukatokea katika nchi yetu. Kwa hiyo nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natokea Jimbo la Chaani Mkoa wa Kaskazini Unguja. Ni miaka mingi sana hapa tangu tuingie tukiwa tunalalamika, hususani Mkoa wetu wa Kaskazini Unguja, kuhusiana na vituo vya polisi. Tuna vituo zaidi ya vitatu tu kwenye mkoa mzima wa Kaskazini Unguja ambapo ukiangalia kwenye Wilaya ya Kaskazini B tuna kituo kimoja tu cha polisi. Kituo hicho kimejengwa tokea enzi za ukoloni na kina daraja C. Naomba sana kwenye bajeti ya Mheshimiwa Waziri, kaka yangu Mheshimiwa Masauni aangalie Wilaya hii ya Kaskazini B; huduma ya kipolisi kwenye vituo vya polisi bado tupo nyuma sana. Tuna kituo kimoja tu kwenye wilaya nzima, kuna vijiji kadhaa zaidi ya ambavyo mimi sivijui idadi yake vinafuata huduma kutoka kwenye...
MHE. SAADA MANSOUR HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa.
TAARIFA
MHE. SAADA MANSOUR HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa kaka yangu hapa pamoja na mchango wake mzuri anaochangia. Katika Wilaya ya Kaskazini B vijiji vinavyotembea masafa marefu ni Kichungwani, Kichwele, Mchanjarike, Mwembemajogoo na Kitope Ndani. Hawa wote wanatembea masafa marefu kufuata Kituo cha Polisi Mahonda.
MWENYYEKITI: Mheshimiwa Usonge unapokea taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge jirani yako hapo?
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa kwa mikono miwili na bahati nzuri naye pia anatokea Mkoa wetu wa Kaskazini Unguja, kwa hiyo nimpongeze sana. Naomba sana wilaya hii tuiangalie kwa jicho la kipekee, tuongeze idadi kubwa vya vituo vya polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa huu wa Kaskazini Unguja una idadi kubwa sana ya wananchi na pia kwenye uwekezaji wa hoteli nao pia unaongoza, lakini huduma ya kipolisi bado ipo nyuma. Kwa hiyo naiomba sana Wizara katika bajeti hii tuongezewe walau kituo kimoja kwenye Wilaya ya Kaskazini B.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye Wilaya ya Kaskazini A Unguja. Wilaya ya Kaskazini A Unguja nako tuna vituo viwili tu vya polisi. Nako pia tunashukuru sana, kwa sababu katika bajeti iliyopita walitenga fedha tukaenda kukamilisha lile jengo ambalo sasa hivi lina grade B. Kwa hiyo naiomba sana Wizara, mara hii twende tukakiangalie Kituo cha Polisi cha Lungalunga ambacho kipo kwenye Jimbo langu la Chaani. Kituo hiki tokea enzi za ukoloni hadi leo hii, nikimpitisha pale Mheshimiwa Waziri hawezi akaamini au akaniambia hiki ni kituo cha polisi. Kituo hakina hadhi kabisa, kituo kimekaa kama kibanda cha kuku. Naomba sana Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana hapa nilizungumza sana kuhusiana na Kituo hiki cha Polisi kilichokuwepo Chaani Lungalunga kwenye bajeti yake na wakatenga bajeti zaidi ya milioni 80, lakini mpaka leo hii ninavyozungumza hakuna hata thumni iliyokwenda pale kwa ajili ya kukitengeneza kituo cha polisi. Kwa hiyo namwomba sana Mheshimiwa Waziri, kituo kile kimekaa kimkakati ukitoka Mahonda ukija Chaani pale, maana yake ndiyo unaingia kwenye eneo la uwekezaji na eneo ambalo tayari kuna population kubwa ya watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye eneo la pili la Pwani Mchangani. Kuna kituo kimejengwa na wawekezaji, ni kituo kizuri chenye hadhi, lakini hadi leo hii ninavyozungumza kituo kile mwekezaji tayari ameshafikia ukomo, tunamshukuru kwa jitihada zake, lakini kinahitaji baadhi ya vifaa, navyo ni, kumaliziwa kupigwa rangi, milango, madirisha pamoja na vifaa vya kiofisi. Gap kubwa mwekezaji huyu ameshalitoa, kwa hiyo naomba sana Wizara twende tukamalizie kile kituo cha Pwani Mchangani ili kuwasaidia wananchi wa Pwani Mchangani na maeneo yote ya jirani pale kupata huduma ya kipolisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu ni Matemwe, nako ndiyo hivyo hivyo, kwamba kuna population kubwa na uwekezaji nao umeshamiri. Kuna eneo kabisa la Serikali limeshatolewa, wameshapewa polisi kwa ajili ya kujenga kituo cha polisi. Kwa hiyo naiomba Wizara kwenye bajeti hii twende kule tukakiangalie Kituo hicho cha Matemwe kuweza kujengwa kwa haraka ili wananchi, wawekezaji pamoja na wageni mbalimbali kuweza kupata huduma za kipolisi kwenye eneo hilo...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante muda wako umeisha.
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Aisee! Naomba kuunga mkono hoja. Ahsante.