Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika hoja hii ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu lakini pia, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Eng. Masauni, Naibu Waziri Mheshimiwa Sillo, Makamishna Jenerali wote pamoja na watendaji wa Wizara hii. Karibuni sana kwenye kamati yetu na hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Eng. Masauni kwa Mradi wa Safer City. Ule Mradi wa ukianza, hizi hoja ambazo zinazungumzwa hapa kuhusu bodaboda na mambo mengine zinaweza zikaisha, mradi huu utasaidia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ameandika katika hotuba yake kwamba, watafunga kamera 6,500. Wale ambao tulikuwa Rwanda tuliona, pale bodaboda wapo na unaweza ukakuta hakuna askari kabisa kwa sababu, kuna mambo ya Artificial Intelligence ambayo yamewekwa pale, kwa ajili ya kuangalia na ku-monitor mtandao mzima wa waendeshaji wa magari, bodaboda na waendeshaji wengine katika miji na mahali popote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mradi huu ukitekelezeka haya yote ambayo tunazungumza hapa yatakuwa ni ndoto. Kwa hiyo, nakupongeza na ninaomba Wizara ya Fedha, inasikia, watoe fedha kwa Wizara hii. Fedha za maendeleo katika Wizara hii zinakwenda kidogo sana, hawa ni watendaji wetu wa majeshi. Tuna majeshi hapa, hawa hawazungumzi wanatekeleza tu kwa hiyo, kama fedha haziendi tutashindwa kufika mbele na kutekeleza majukumu ambayo tumewapangia. Kwa hiyo, unaona katika maoni ya Kamati sisi tumesema tunaomba fedha zitolewe ili waweze kufanya kazi zinazokusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie majeshi yetu, wakiwa hawapewi fedha wanapata changamoto zipi? Tukianza na madeni. Kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020, 2020/2021 mpaka 2022, Jeshi letu la Magereza walienda kuhakiki wafanyakazi ambao wana madai. Hata hivyo, wafanyakazi wale walipohakikiwa wakaambiwa watalipwa, lakini walilipwa kidogo na sio pesa zote ambazo walikuwa wametarajia kulipwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndiyo maana nasema Wizara ya Fedha iwalipe Magereza na Uhamiaji. Iwape pesa za maendeleo, ili waweze kulipa malimbikizo ambayo wanajeshi na askari wetu wanadai. Kwa hiyo, unakuta kwamba, wale wamefanya kazi kwa pesa zao, wametumia pesa zao, wanadai kwa miaka mitatu, minne, lakini hawajazipata, wana watoto na familia kwa kweli, inatia uchungu kwa hawa watendaji. Tukiwajali watumishi wetu watafanya kazi nzuri kwa weledi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, malipo ya likizo kwa Jeshi la Polisi na majeshi mengine yote bado ni changamoto sambamba na upandishaji wa vyeo. Angalieni upandishaji wa vyeo, ili waweze kupanda. Wanakwenda kwenye mafunzo, basi muwapandishe kulingana na hitaji linavyotakiwa, mtu anapata motisha anapokuwa amekwenda kwenye mafunzo na anaporudi anapanda cheo. Kupanda cheo ni kupata mshahara mzuri na kuendelea kufanya kazi kwa weledi mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni ajira na ikama. Jeshi la Zimamoto lina askari wapya 225, polisi 7,228, Magereza 734 na Uhamiaji 521, hiyo ni ikama mpya. Hata hivyo, ukiangalia Jeshi la Magereza peke yake wanahitaji askari 29,796, lakini waliopo ni 14,592. Bado tuna hitaji la watumishi 15,000 na zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Waziri wa Utumishi aajiri watu waende kwenye haya majeshi, wanapata shida. Pia, katika ajira mnatakiwa ku-consider askari wanawake kwenye haya majeshi. Kwa mfano, Jeshi la Magereza unakuta kuna wafungwa wa kike, wajawazito, wenye watoto, wanaowahudumia ni wale wanawake walioko pale. Kwa hiyo, tunaomba muongeze idadi ya wanawake katika jeshi letu, ili waweze kuajiriwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo nawapongeza Jeshi la Zimamoto, wanafanya kazi kubwa. Wamejenga nyumba za makazi nzuri kabisa, lakini hawa kwa mwaka huu wa fedha hawakupata kabisa fedha za maendeleo, ni sifuri kabisa. Pamoja na kutopata kabisa fedha za maendeleo bado wamekuwa wakifanya kazi kubwa, tumekwenda kuona nyumba za wafanyakazi wa ngazi ya chini ambazo wamezizindua, wamefanya vizuri kabisa, ninawapongeza jeshi hili. Hata hivyo, muendelee kukusanya maduhuli, ili muweze kupata fedha zaidi za kuweza kuendesha shughuli zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naupongeza uhusiano wa Jeshi letu la Polisi na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa kuweza kuungana, ili kujenga Polisi Kata. Hiki ni kitu kizuri sana kwa sababu, tuko kule tuna wananchi na kwenye kata hakuna nyumba za Polisi.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Tendega, malizia.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mahusiano yao hayo yatatusaidia sana kuendeleza Jeshi la Polisi. Nakushukuru sana. (Makofi)