Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Joseph Anania Tadayo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata fursa ya kuchangia Wizara hii muhimu ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Naanza kwanza kwa kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Rais, kwa jinsi ambavyo ameweka kipaumbele katika Wizara hii muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati kwa hiyo, ninayo fursa ya kuona mambo makubwa ambayo yanendelea katika Wizara hii nyeti. Pili, ninampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu wake pamoja na timu yake nzima bila kuwasahau Makamishna wetu wanne ambao wanasimamia majeshi yetu haya manne kwa kazi nzuri ambayo wameendelea kuifanya kwa kuiheshimisha na kuiweka salama nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ni nyeti sana. Tunapozungumzia mambo mengi na makubwa yanaanzia katika Wizara hii. Kwa mfano, suala la haki jinai ambalo limepewa kipaumbele sana na Serikali ya Awamu ya Sita linaanzia katika Wizara hii na kuishia Wizara hii. Mhalifu anaanzia Polisi na akitiwa hatiani anakwenda magereza na kote huko ni ndani ya Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, hata suala la uchumi na masuala yote tunayotamba kwenye nchi hii kama utalii, wawekezaji na masuala ya diplomasia yote hayo na hata wageni wakiingia airport mtu wa kwanza wanayekutana nae ni wa Uhamiaji, wa Wizara hii na siku ya kuondoka ni wao ndio wanamuaga na barabarani wanakutana na traffic. Kwa hiyo, ni Wizara ambayo inabeba sura ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa suala la maafa ambalo kwa mwaka huu, nadhani hatujapata somo dogo, tumepata somo kubwa sana. Kabla hatujafikiria kupeleka magodoro na chakula wanaotangulia ni watu wa uokoaji. Kwa hiyo, Wizara hii ni nyeti na ndiyo maana naungana na wote wanaosema fedha za kutosha zipelekwe kwa wakati, fedha za matumizi ya kawaida pamoja na za matumizi ya maendeleo, hasa katika suala zima la mafunzo na kujengewa uwezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara hii, kwa ajili ya huu Mradi wa Kesi Mtandao ambao unaendelea. Ni mradi ambao utaharakisha upatikanaji wa haki wakati kesi inapofunguliwa pale Polisi na Ofisi ya DPP wanaona kinachoendelea. Hii itarahisisha na kuleta ufanisi mkubwa katika masuala ya haki jinai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo Mradi nyeti wa Safer City ambao utatusaidia sana kuleta usalama. Mradi huu utasaidia kuweka utofauti wa kiusalama ukilinganisha na nchi ambazo zina vibaka wengi na watu kupata shida ya kunyang’anywa vitu njiani. hii itatokana na kufungwa kwa kamera ambazo zitasaidia kufanya kila kitu kionekane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi ya mwisho ambayo siyo ndogo, ni kubwa, ni jinsi ambavyo Jeshi la Polisi linaweza kusimamia vizuri maandamano ya vyama vya siasa ambayo yameruhusiwa na Serikali ya Awamu ya Sita. Wanafanya kazi kubwa ya kutuheshimisha na wamekuwa wadau wakubwa wa demokrasia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisisahau kumshukuru Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, kwa ajili ya Gari la Uhamiaji ambalo aliniahidi katika Bunge hili. Nadhani Mwanga sasa tunakwenda vizuri na tutaacha kutembea na vidumu vya mafuta na oil kwenye gari ambalo lilikuwa na hali mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote haya bado changamoto ambazo zimetajwa na wenzangu, kama vile uduni wa makazi ya askari na mazingira yao ya kutendea kazi, ni mambo ambayo lazima yatiliwe mkazo ikiwa ni sambamba na madai yao yalipwe kwa wakati. Hatupendi kuwa na askari ambao wanalalamika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala zito kidogo la kudhibiti kambi za wakimbizi, ili wasipenye huko mitaani, halafu baadaye wakajichanganya na sisi wakawa hatari kwa usalama wetu. Kwa mfano wenzetu wa Malaysia ukiacha hii my card, ile smart card yao inaitwa my card ya Kitambulisho cha Taifa wana nyingine wanaita My PR ambayo wanapewa wageni wanaokaa kwa muda mrefu. Inawezekana kabisa pia tukatengeneza kitambulisho kwa ajili ya hawa wakimbizi ambao wamekaa muda mrefu ili atakapoomba kitambulisho chetu cha NIDA asomeke kule kwenye kile kitambulisho chake kama mkimbizi asiweze kutuchanganya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimevutiwa sana na hoja ya Mheshimiwa Shangazi juu ya suala la RITA na NIDA. RITA kama ambavyo tunafahamu inasimamia mambo ya vizazi, vifo, ndoa, ufilisi na udhamini. Hapa wanahitajika wasomi wa sheria pamoja na ustawi wa jamii, ukija NIDA masuala ya vitambulisho vya Taifa ni masuala ya usalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sioni Wizara ya Katiba na Sheria ikiwa na msuli wa kutosha wa kiusalama wa kusimamia NIDA na wala sioni Wizara ya Mambo ya Ndani ikiwa na ubobezi wa kutosha wa kisheria wa kusimamia RITA. Kwa hiyo suala la kuunganisha hizi Taasisi mbili liangaliwe kwa umakini sana kabla hatujafikia mwisho wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tungefikiria kukua zaidi kama wenzetu wa Malaysia nilisema kwamba wao kitambulisho chao cha NIDA pamoja na kuwa ni kitambulisho cha mtu lakini pia kinatumika kama ATM card, kama driver’s license, kama medical insurance na kadhalika tufikirie kukua zaidi kuliko kuunganishwa. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)