Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Tarimba Gulam Abbas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii nyeti, Wizara ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niruhusu kwanza kwa haraka sana niweze kuchukua nafasi hii kupongeza juhudi za kitaifa kuipongeza klabu ya Young Africans kwa kuweza kuchukua ubingwa mapema zaidi na hivyo kuashiria kumalizika kwa ligi ingawa kuna watu wanahangaika na ushindi wa pili na ushindi wa tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita katika Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. Nilikuwa nikiangalia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Ukurasa wa 53 hadi 59, Waziri anazungumzia zaidi masula ya uzimaji wa moto. Hata ukiangalia ujenzi wa vituo na kuleta magari, nashukuru kuna juhudi kubwa sana ya Serikali katika kuongeza uwezo wa jeshi hili katika kukabiliana na majanga ya moto. Sijaona sana ni kwa kiasi gani jeshi hili linapewa nyenzo za uokoaji, eneo la uokoaji mimi sijaliona zaidi ya uzimaji wa moto, sasa tuzungumzie hayo hayo ya moto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa nizungumzie changamoto ambazo ziko Dar es Salaam. Tunakumbuka mwaka 2021 Soko la Kariakoo lilipoungua. Vilevile, kule Jimboni kwangu Kinondoni katika Kata ya Magomeni kuna nyumba mbili ziliungua pale na pale hatuko mbali sana na kituo cha magari ya Zimamoto kinachoitwa Fire ni karibu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto za barabara zetu kuwa finyu na msongamano wa magari inapotokea matatizo ya moto siyo rahisi sana kwa magari yale ya Zimamoto hata kama ni mazuri kiasi gani kuweza kuwahi kufika katika eneo ambalo nyumba zinaungua ili kuweza kusaidia kuokoa hata mali zilizobakia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nikifuatilia hata wakati taarifa hii ya kuungua kwa soko la Kariakoo inatolewa kulikuwa na sababu karibu 10 ambazo zinaonesha jinsi matatizo ya majanga haya yanavyotokea, lakini mimi nikachukua moja lile wanasema kutokuwepo kwa chemba za maji, wanaita fire hydrants. Mheshimiwa Waziri ameizungumzia katika paragraph ya 138, amelizungumzia suala hili kwa uchache sana lakini hii kitu ni muhimu sana. Magari ya Zimamoto yanapofika katika nyumba zinazoungua wakimaliza maji ambayo wameyachukua katika magari yao inabidi watafute kizimba cha maji kilichopo karibu, sasa kwa Dar es Salaam vizimba vya maji ni matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka Aprili mwaka 2013 kuna taarifa ilitolewa na wakati ule kulikuwa na bwana mmoja ni Kamishna anaitwa Fikiri Sala alisema kwamba, “Dar es Salaam fire hydrants 1,268 hazifanyi kazi” na taarifa zilizopo ni kwamba nyingine zimefukiwa na nyingine watu wamejenga juu, wengine wajenga ndani ya nyumba na kadhalika. Hili ni kosa la kijinai kabisa kuweza kufanya vitendo ambavyo vinafanya fire hydrants ipotee na isiweze kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika taarifa hiyo walisema kwamba fire hydrants mwaka 2013 zinazofanya kazi ni 74 tu. sasa utaona hali ilivyo ngumu ingawa taarifa zilizopo sasa hivi wamezihuisha, ahsante sana kwa kuzihuisha na kufikia 108 lakini ni ndogo sana. Sasa nikiangalia fedha ambazo Mheshimiwa Waziri anaziomba shilingi milioni 150 kwa Tanzania nzima mimi naona Serikali bado haijaingiza nguvu katika suala zima la kutengeneza fire hydrants. Hii ni hatari kwa sababu tutakuwa tumerudi kulekule kwenda kumalizia kuokoa nyumba isiungue sana lakini mali hazitokuwepo kwa sababu magari yakimaliza maji lazima yatafute fire hydrants na vizimba hivi sasa hivi havipo pale Dar es Salaam havifanyi kazi na kwa hali hiyo naiomba Serikali itilie mkazo suala la kujenga vizimba. Sasa sijui Waziri atapokuja atatueleza nini juu ya kuhakikisha kwamba shilingi milioni 150 inakwenda kujenga vizimba wapi na wapi kwa sababu bila hivyo hataweza kutusaidia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yamezungumzwa mengi sana kuhusiana na biashara ya bodaboda. Biashara ya bodaboda ni biashara muhimu sana. Hadi ilipofika Februari mwaka 2003, naomba tufahamu kwamba tumetumia dola za kimarekani milioni 136.7 sawa na shilingi bilioni 319 kwa ajili ya kuagiza pikipiki. Hiyo ni industry kubwa sana. Kuna ma-graduates wanafanya kazi mule ndani, lakini kutokana na umuhimu wa biashara hii mbona Serikali haionekani kuisaidia hii biashara? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini iisaidie? Tunaiachia ijiendeshe yenyewe na ndiyo maana Wabunge wengi wakisimama wanalalamikia utaratibu wa usimamizi wa sheria za barabarani, hamzisaidii. Nakumbuka nilivyoingia Bungeni mara ya kwanza kabisa niliuliza swali linalohusiana na masuala ya bodaboda. Ukweli ni kwamba Serikali mnatuambia tu, mnatutoa barabarani kwamba mnatoa elimu, hata hiyo elimu tangu imechukua miaka mitatu tangu itolewe, hata chuo kikuu mtu amesha-graduate. Ni lini basi atakaa aelezwe umuhimu wa ufuataji sheria za usalama za barabarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Usalama Barabarani ya Mwaka 2007 iko wazi kabisa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa hitimisha hoja yako.

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nahitimissha kwa kuiomba Serikali iweke utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba biashara ya bodaboda inaendeshwa vizuri ili watu wasiendelee kupata ajali. Nataka ujue pale Muhimbili Moi watu 280 kwa mwezi wanapelekwa kama majeruhi wa pikipiki ni watu wengi sana hao.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hali hiyo naiomba Serikali ikija hapa itueleze ni kitu gani kinawazuia wasiweze kusimamia sheria za usalama barabarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)