Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lupembe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Wizara hii muhimu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Kwanza niungane na Wabunge wenzangu wote kuvipongeza sana vyombo vyetu vya ulinzi na usalama. Napenda kuliambia Bunge lako Tukufu nikiwa kama Mjumbe wa Kamati hii ya Mambo ya Nje Ulinzi na Usalama vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vikiongozwa na makamanda wetu kwa maana CGI, CGP, CGF na IGP wanafanya kazi nzuri sana kwa ajili ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wengi hapa mmesema miaka ya nyuma malalamiko juu ya vyombo vyetu vya ulinzi na usalama yalikuwa makubwa sana. Sasa hivi wote mmeshuhudia hata vyama vya upinzani vinapongeza kazi nzuri ya vyombo vya ulinzi na usalama. Hii maana yake tunakokwenda ni kuzuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii pia kuwaambia Waheshimiwa Wabunge wenzangu hata mipango ya Wizara hii ya Mambo ya ndani ni mipango mikubwa. Tumeshuhudia kwenye Taarifa ya Mheshimiwa Waziri hapa wanakusudia kufunga kamera kwenye miji yote kulinda usalama wa watu wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Waheshimiwa Wabunge tuwaunge mkono na sisi kama Kamati tuko pamoja na Wizara hii na vyombo vyote vya ulinzi na usalama. Naomba nichangie maeneo mawili au matatu kwa mchana huu wa leo. Sehemu ya kwanza nakubaliana sana na hotuba ya Mheshimiwa Waziri juu ya mipango ya Serikali ya kununua magari ya askari wetu na kununua vifaa mbalimbali kwa ajili ya majeshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichangie eneo maalum kuhusu wizi wa mtandao. Dunia inakwenda mbele sana. Zamani wizi mkubwa ulikuwa ukifanyika kwa kutumia nguvu, SMG, kuteka magari na kadhalika, sasa hivi wizi mkubwa upo kwenye mitandao. Hili nataka niliombe Jeshi la Polisi wakishirikiana na watu wa Wizara ya TEHAMA wafanye kazi mahsusi usiku na mchana, kupanga mipango ya kudhibiti uhalifu wa mitandao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naviamini vyombo vyetu vya ulinzi na usalama. Juzi tumeshuhudia pale Makutupora watu wa Mizinga wamezindua bomu la kufukuza tembo nchini. Sina mashaka ya kwamba vyombo vyetu vinao uwezo wa kukaa na kutafuta njia bora ya kudhibiti wizi wa kutumia mitandao. Hata BOT walitoa taarifa miezi miwili iliyopita kwamba benki nyingi sasa hivi zinaibiwa fedha siyo kwa unyang’anyi bali kwa kutumia mitandao. Nafahamu kazi nzuri imeanza naomba jambo hili lipewe mkazo kwa vyombo vyote vya ulinzi na usalama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, naomba niseme kuhusu bodaboda. Wabunge humu ndani ya Bunge wamesema na inaonekana kama kuna lawama kidogo kwa baadhi ya askari wetu kwamba pengine wanawaonea watu wa bodaboda. Mtazamo wangu ni tofauti kidogo, nadhani vijana wetu wa bodaboda pamoja na elimu ambayo wanapewa lakini wengi hawana leseni za kuendesha bodaboda. Kinachotokea ni nini? Wakiona askari wakati fulani wanakimbia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Bunge tulitunga Sheria kusema kwamba bodaboda walipie leseni shilingi 70,000. Nina ombi kwa Serikali na Mheshimiwa Waziri wa Fedha yuko hapa. Wakati wa bajeti ya fedha hili jambo nitalisema na ikibidi nitashika shilingi. Serikali ilete sheria humu ndani ya Bunge, tupunguze gharama ya watu wa bodaboda kupata leseni. Sasa hivi leseni ya bodaboda ni shilingi 70,000, sawasawa na leseni ya dereva wa Grade C. Ni vema gharama hii ya leseni ya bodaboda ikashuka angalau mpaka 20,000 ili bodaboda wote wapate mafunzo mazuri wafanye kazi yao vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ni muhimu pia hao bodaboda wote wakapewa namba maalum za kwenye vituo vyao. Watambulike kwamba bodaboda fulani anafanya kazi kwenye kituo fulani ili Jeshi la Polisi lisilazimike kuwakimbiza badala yake liwabaini kwa namba zao na sehemu ambako wanafanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu kwa mchana huu, nataka niseme kidogo kuhusu Magereza. Naona muda wangu umekwisha lakini rai ni kwamba watu wa Magereza katika vyombo vyote ndiyo ambao wanapata fedha kidogo sana ya kuendesha taasisi yao. Niiombe Serikali wawaongeze fedha watu wa magereza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)