Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Haji Amour Haji

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makunduchi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. HAJI AMOUR HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuweza kunipa nafasi hii na mimi niweze kuzungumza mambo mawili matatu yanayohusiana na Wizara ya Mambo ya Ndani. Kabla ya yote, nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa namna ambavyo alikuwa anayalea majeshi yetu haya yaliyokuwa katika Wizara ya Mambo ya Ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nizungumze wazi kwamba hakuna kazi ambayo ni ngumu sana kama kazi ya ulinzi. Kazi ya ulinzi ni kazi moja ngumu sana na ni kazi ambayo inahitaji weledi. Kwa kweli, nasema wale wanaoongoza yale majeshi, wanaoongoza askari wetu, wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri, pamoja na watendaji wao wote ni watu ambao wanatakiwa wawe na hekima kubwa sana kwa sababu ni kazi ngumu na ni kazi inayohitaji hekima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite katika mchango wangu hapa, kwa leo nizungumzie suala la Jeshi la Polisi. Kwa kweli, nizungumzie katika masuala yanayohusiana na hizi kamisheni za kipolisi. Jeshi la Polisi lina kamisheni nane, katika kamisheni hizo nane mimi nitaziangalia kamisheni mbili tu katika kuzitolea mchango wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kamisheni ya kwanza ambayo nitaweza kuizungumzia ni suala la kamisheni ya ushirikishwaji wa jamii pamoja na ile kamisheni iliyokuwepo kwa upande wa Zanzibar. Kwa nini nimesema nitazichagua kamisheni hizi mbili? Kwanza, katika suala la kamisheni ya ushirikishwaji wa jamii, kuna tasnia moja ambayo ni muhimu sana; nimejaribu kuangalia katika hotuba ya kibajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Jeshi la Polisi nikasema kwamba hii tasnia inaachwa na ni tasnia ambayo ni muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tasnia hii ni tasnia ya ulinzi wa kampuni binafsi ambayo nayo tukiangalia kwa upande wa nchi yetu wanatoa msaada mkubwa sana. Sasa, nikawa najaribu kuangalia shughuli muhimu hasa zinazofanywa katika hizi kamisheni zetu. Hasa nikaiangalia hii kamisheni ya ushirikishwaji wa jamii, nikajaribu kuziangalia zile task au zile kazi zilizopo pale ambazo kubwa zaidi zinazungumzia masuala ya ulinzi wa kijamii hasa upande wa polisi jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nikawa najiuliza haya makampuni ya ulinzi, katika uwasilishwaji wa bajeti yetu, hasa wanaingia kwa upande gani? Wakati mwingine nasema kwamba ni kampuni ambazo zimekuwa kama yatima. Kwa nini nasema ni kama yatima? Kwa sababu hata katika ule mchango ambao upo kwa upande wa Jeshi la Polisi unaozungumzia suala la mapato ambayo yanaingia katika Jeshi la Polisi sikuona kama kuna mchango wowote, hasa wa kifedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kwa upande wa Tanzania tuna karibu kampuni binafsi 2,000 mpaka 3,000. Kampuni hizi kwa kawaida huwa zinasajiliwa na Jeshi la Polisi na wanaposajiliwa maana yake kuna vibali. Kibali unaposajili kampuni mara ya kwanza unatoa shilingi 300,000. Tujiulize kwa upande wa Tanzania nzima, tuna kampuni kama 2,000 mpaka 3,000 ni kiasi gani ambazo zitakuwa zimeingia? Mbali na hivyo, sikuweza hata kuona mchango wao ukizungumzwa katika hii bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kulizungumza katika hali ya haraka haraka kabla muda wangu haujaisha, ni suala la vibali. Wakati mwingine, IGP yupo hapa; tunaona kwamba hizi kampuni ni za kibiashara na kama hizi ni kampuni za kibiashara maana yake zinafanya kazi kwa mujibu wa sheria za kibiashara (Kampuni ambazo zinaendeshwa kwa mujibu wa taratibu za kibiashara).

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuna pande mbili, kuna upande wa Zanzibar na kuna upande wa Bara ambazo zote zinasimamiwa na Jeshi la Polisi. Hata hivyo, kitu ambacho kilikuwa kizito na cha urasimu zaidi ni pale unapoomba kibali cha ulinzi. Maana yake kufungua kampuni ya ulinzi, kibali kile ni mpaka taarifa zije Dodoma wakati Zanzibar kuna kamisheni ambayo ina mamlaka ya kufanya shughuli hizo pale lakini inaachwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi pengine ningeliomba Jeshi la Polisi kupitia kamisheni ya Zanzibar, kuhusu shughuli za vibali. Kwa vile taratibu za kibiashara kwa upande wa Zanzibar zinakidhi haja, wapewe mamlaka ya kuweza kutoa vibali kupitia ruhusa ya IGP wa Tanzania. Kuliko ile kwamba taarifa zao zichukuliwe Zanzibar kuja upande wa Dodoma, zinachukua siyo chini ya mwezi mmoja mpaka miezi mitano. Jambo hilo mimi nitaliomba Jeshi la Polisi waweze kufanya hivyo ili kuondoa urasimu uliokuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili katika hivi vibali, kampuni maana yake itakuwa na kibali mama. Shida inayojitokeza ni kwamba kila unapokwenda kufungua taasisi nyingine katika mkoa unatakiwa uwe na kibali kipya ambapo vile vibali vyote maana yake vinafanya kazi moja. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Haji, muda wako umeisha, hitimisha.

MHE. HAJI AMOUR HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante mengine nitaandika kwa maandishi kwa sababu mchango ulikuwa mrefu. Naomba kuunga mkono hoja na ahsante. (Makofi)