Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Mwantum Dau Haji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia hali ya uzima hivi sasa. Pia, niwashukuru Wajumbe wenzangu waliokuwamo humu katika Bunge hili Tukufu, ambao sasa hivi wataweza kunipigia makofi mengi humu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda sana kumshukuru Waziri wangu Mheshimiwa Engineer Masauni pamoja na Naibu wake. Mheshimiwa Engineer Masauni, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kweli unaifanyia kazi hii Wizara. Tutasema yeye ni big up na wala asitokee mwingine, siku zote namwombea dua ukae hapo hapo ili uiendeleze Wizara hii uifanyie kazi vizuri. Mama hakufanya vibaya, kakurejesha hapo kakuona wewe mpiganaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ninalotaka kuzungumza hapa, ulikuwa wewe pamoja na Mheshimiwa Sagini, na yeye namshukuru. Kwa hiyo, sasa hivi Mkoa wa Kusini unang’ara na kesho kutwa utazidi kung’ara, hasa katika sherehe za mwaka kesho kutwa. Watalii wengi watakwenda kule na wataiona Makunduchi ilivyokuwa imegeuka. Mheshimiwa Waziri nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuendelea Makunduchi kuna nyumba moja ya makazi ya polisi bado haijaguswa kabisa. Nyumba moja umeijenga lakini bado haijaisha, Mheshimiwa Waziri nakuomba Serikali ichukue jitihada zile nyumba zimalizike. Ndiyo maana nikasema kwamba kule kutang’ara. Kwa hiyo, mimi naishukuru sana Serikali yangu kwa jitihada zake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vituo vya Mkoa wa Kusini vimekwishakumalizika na kingine amekifungua DC juzi na sasa kinafanya kazi huko Makunduchi. Mheshimiwa Waziri, Kituo cha Dunga nacho tayari kimeshafunguliwa, kinafanya kazi lakini kina changamoto. Pale mbele ikinyesha mvua kuna tope, tena pale inakuwa kero kubwa. Pia, kuna eneo pale limalizwe kununuliwa ili liwekwe maeneo ya kuwekea magari. Pia, hawana gari, gari lao mpaka waende Tunguu, wapige simu hadi lije huku kama kumetokea uhalifu basi tayari uhalifu unakuwa umeshaharibika, kwa sababu gari halipo Dunga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, jitihada za pale Dunga waweke mambo madogo madogo, choo cha nje hakuna hapo Dunga. Watu wanaingia ndani wanaenda kutuchafulia Kituo kama kile kilivyokuwa kinang’ara namna ile, kweli ni vizuri vile? Siyo vizuri. Mheshimiwa Waziri jitahidi na yale madogo madogo uyatengeneze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Jambiani nao hawana gari na makazi pale. Kimekwisha lakini nyumba za makazi hakuna. Kituo cha Paje, kimeshakuwa kuukuu kuu sana, naomba nacho kifanyiwe ukarabati. Ukitegemea ukanda ule ndiyo ukanda wa watalii zaidi: Paje, Jambiani mpaka Michamvi, upande ule watalii wanakwenda wengi sana. Kwa hiyo, namwomba Waziri, Kituo kile kipo nje, kipo wazi, akifanyie kazi Mheshimiwa Waziri ili nacho kipate kung’ara. Kusini ipate kung’ara kuliko inavyong’ara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri pamoja na Mheshimiwa Sillo na yeye pia aje Kusini atembee aone maendeleo ya Kusini yalivyo. Mheshimiwa Sillo, jamani nawapa big up wanafanya kazi vizuri sana. Askari wangu, wanafanya kazi vizuri sana, usalama barabarani waufanyie kazi vizuri sana. Jamani, mnafanya kazi kubwa na mnapiga kazi kwa hiyo mimi nawapa hongera zenu mfanye kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hizo pongezi, sina la kusema. Nakushukuru Waziri wangu pamoja na Rais wangu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, anapiga kazi kubwa sana katika Wizara zake. Ahsante sana kwa mwanamama yule, Mungu amjaalie heri, ampe baraka, hekima na busara ya kutuongoza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)