Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. James Kinyasi Millya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Simanjiro

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya watu wa Simanjiro, kwanza kwa sababu nasimama mara ya kwanza niwashukuru sana kwa kunichagua na kunipa heshima ya kuwa Mbunge wao na kusaidia kuwaondolea kelele hapa Bungeni. Mimi namshukuru Mungu sana kwa hilo na nawashukuru kwa ajili ya heshima waliyonipa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Profesa Frantz Fanon wakati fulani alinukuliwa akisema haya, nanukuu kwa kiingereza; “every generation out of relative obscurity must find it’s own mission and either fulfill it or betray it.” Kwa tafsiri isiyokuwa rasmi sana kwamba kila jamii kwa wakati fulani lazima ikubali kutafuta njozi yake na labda waamue kuikamilisha au kuikataa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la nchi yetu ni kubwa na tatizo hili kwasababu limetokea CCM wakati fulani si lingine bali ni unafiki na uongo. Unakuta viongozi wanaotegemewa na Taifa hili wanaongea uongo kwa sababu ya kujipendekeza, nilishindwaga mimi, nilishindwa!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasemahaya? Ugonjwa huu ni mkubwa kwa sababu unakuta makada ninaowafahamu kwa majina wanajaribu kujivua u-Membe, wanajaribu kujivua u-Lowassa kwa kujipendekeza na Serikali iliyoko madarakani wanawaacha wananchi wanateseka hawasemi ukweli. Huu ugonjwa ni mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoa mifano michache wengine wanasema nisitaje lakini kwasababu sitaki kuwa mnafiki, alikuja Mwenyekiti wa Tume ya mabadiliko ya Katiba, ugonjwa huu ni mkubwa. Katoka kwa wananchi akatetea Katiba nzuri, iliyotoka kwa wananchi kwa mapendekezwa ya wananchi baadaye alipoguswa mahali na CCM akakana matokeo ya wananchi, ni unafiki mkubwa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hili ni kubwa na kama viongozi hatutapona katika hili nchi hii itaenda pabaya. Ninamkosa Baba wa Taifa kama Nyerere, kama Sokoine ambao wakisimama kwa ukweli, watasimamia hiyo kweli na hiyo kweli itawaweka huru milele. Nimewakosa watu hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi kwenye hoja za madini. Sisi watu wa Simanjiro tuna madini ya Tanzanite, kwa miaka mingi sana ukienda Naisinyai, kuienda Mererani – Simanjiro watu ni maskini kweli kweli. Eneo lenye watu karibu 50,000 Mererani na Naisinyai hawana maji, Tanzanite ipo pale, wanachukua wazungu, wanachukua wazawa, watu wetu wanaachwa maskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali, Mheshimiwa Profesa Muhongo ninakuheshimu sana na unajua, nikuombe hata kutokana na yale ambayo yanasemekana si hasara, corporate social responsibility, tusimamie, watu wetu wanaumia sana, wanaonewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa leo hii niongee kwa masikitiko makubwa. Tulikuwa na mgodi mkubwa unaoitwa Tanzanite One, hata Kamati imegusia na kwenye taarifa mbalimbali ipo. Mgodi ambao Serikali ni mbia, STAMICO na mwekezaji uliuzwa kiholela na mimi najiuliza kama Mbunge na ningeomba nipate majibu wakati unakuja kuhitisha hotuba na hoja yako; hivi mgodi ule na ubia ule ulipatikanaje kwa Kampuni ya Sky Associates ambayo nimeaminishwa na najua kwenye maandiko si Kampuni ya Tanzania, wametokea wapi watu hawa? Je, tender hii ilitangazwa lini ili watu wote wa-compete fairly halafu wapewe. Sky Associates kama alivyokuwa anasema Dkt. Mwakyembe kuwa wakati fulani aki-present hoja yake ya DOWANS hii ni kampuni ya mfukoni, ni ya watu wachache waliotengenezewa ulaji na baadhi ya Mawaziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na hapa, sintachelea kusema Simbachawene anahusika kwenye hili. Kampuni hii leo hii inanyanyasa wananchi wote, wachimbaji wadogo naomba niwataje kwa majina, Simbachawene amesainije mkataba kampuni iingie kwenye ubia na Serikali lakini hakuna mtu alieshindana naye? Eti walitangaza kule London Stock Exchange, Watanzana wangapi wangeweza kuona London Stock Exchange? Leo wachimbaji wadogo wanaonyanyaswa kwenye mkataba huo, Mathias Mnama, Sunda, One, Olomi, Mwarabu na mwingine kapoteza maisha kwa sababu ya mitobozano. (Makofi)
Mheshimiwa Profesa, wewe uliunda Tume wakati fulani, Tume mbalimbali zimeundwa kwa ajili ya mitobozano huko ardhini lakini bahati mbaya kuna Tume yako wewe, kuna Tume ya Dkt. Kipokola, kuna Tume ya Jenerali Mboma, wachimbaji wadogo wanaonewa na mgodi huu kwa muda mrefu.
Ninaomba kwa mara ya kwanza unisaidie kama Mbunge na unisaidie kama mwananchi mwakilishi wa wananchi wengi wanaotaka kunufaika na mgodi wao. Hawa Sky Associate waundiwe tume, ni wezi, hawanufaishi Simanjiro. Ninakuomba, wanaiba madini, wananunua mpaka Maafisa wetu wa Serikali, wengi! Naomba Mheshimiwa Profesa utusaidie kwenye hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine; Mheshimiwa Profesa madini yanaibiwa kila siku na kampuni hii. Na bahati mbaya, mimi nimeahidi mara nyingi nitakuwa mkweli mpaka nitakapokufa. Wanapata wapi kiburi cha kufukuza wafanyakazi 201 halafu wamewafukuza, baada ya kuwafukuza wanawapeleka mahakamani hawajawalipa mafao na sheria za kazi zinajulikana, bahati mbaya mama yetu Mhagama naye anatajwa humu ndani kwamba ni shemeji wa mmoja wa mbia wa hapo. Dada anaitwa Asia Gonga ameolewa na Martin Mhagama au Yusuph Mhagama, sasa sijui….
TAARIFA...
MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anakiri kwamba ukoo wake ni mkubwa na mimi ni kwamba nimepata taarifa. Nimetaja taarifa tu kwamba anatajwa. Angesema tu mimi huyo sihusiki naye, simple. Lakini watu hawa wanapatiwa kiburi na nani? Wanafukuza Watanzania halafu sekta yako inayosimamia wafanyakazi haiwasaidii, kwa nini nisihusishe jina hilo na jina lako? (Makofi)
Baada ya kusema haya mgodi huu tunataka tunufaike nao. Madini haya yamechukuliwa kwa muda mrefu lakini kampuni hii ya kitapeli iondolewe mara moja, Wanasimanjiro na Mheshimiwa Waziri nikuombe ukutane na wananchi hawa ukutane na wachimbaji wadogo usikie kilio chao. Tanzanite kwa mara ya kwanza na EPZA, kwa nini msijenge EPZA, madini yetu yanatoroshwa kila siku. Tumeto aeneo kama Simanjiro, liko eneo la EPZA, mnachelewa kulijenga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya naomba kuwasilisha. Ahsante sana.