Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon Abubakar Damian Asenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilombero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa dakika sita hizi ili kuchangia Wizara ya Mambo ya Ndani. Naanza kwa kushukuru kama wenzangu walivyoshukuru, nasema tunashukuru mara zote ili tuombe tena. Namshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maboresho yake makubwa katika Wizara ya Mambo ya Ndani na hasa katika Jeshi la Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliona na nilisoma sehemu kwamba Jeshi la Polisi, lile shirika la uzalishaji mali lilikuwa linafutwa, lakini Mheshimiwa Rais kwa busara zake, ameacha kulifuta ili liboreshwe, liweze kuendeleza askari wetu. Kwa hiyo nashukuru sana kwa maboresho haya ya modernization ambayo Mheshimiwa Rais anayafanya mpaka huko kwenye mambo ya TEHAMA na kama nitapata muda, nitaisema huko baadaye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumshukuru Mheshimiwa Waziri kwa dhati kwa kweli. Nilimwomba hapa aje Jimboni kwangu Kilombero, amefika, tukatembea na tukafanya ziara hadi usiku. Mheshimiwa Waziri Masauni akafika Gereza la Idete usiku, akasema lazima nifike niangalie mazingira ili niweze kuyaona na kuyaelewa. Mheshimiwa Waziri pia akafika Kituo cha Polisi Kidatu, akafika Mwaya na akafika Ifakara Mjini. Nataka kukiri hapa leo kwamba mambo yangu yote niliyomwomba, nimeyaona leo yakifanyiwa kazi na chini ya OCD wetu Nkuba, kwa kweli yanasimamiwa vizuri sana. Mheshimiwa Waziri ametusaidia na Serikali imetusaidia tumepata shilingi 802,000,000 za ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Kilombero. Ni wilaya kongwe sana, lakini ilikuwa haina kituo, tumepata. Nimemwambia Katibu Mkuu wa Wizara hapa atusaidie ili michakato ikamilike na hati ile irudi kule ili OCD aweze kujenga kituo kile kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu kumkumbusha Mheshimiwa Waziri kuhusiana na maombi yangu. Tulitembelea Kituo cha Polisi cha Tarafa ya Mang’ula ambacho kiko Kata ya Mwaya, kwa kweli ni Kituo cha Polisi cha Mbao. Mheshimiwa Waziri aliingia pale ndani akasaini vitabu. Kwa hiyo naendelea kumsisitiza kwamba Kituo cha Polisi cha Kidatu na cha Mwaya ni muhimu sana tukavijenga upya. Mimi kwa kushirikiana na Waheshimiwa Madiwani, tumeshapata tayari maeneo ya ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na muda, nataka kwenda kama na-mention hivi. Sisi tunamwomba Mheshimiwa Waziri gari la zimamoto kwa sababu Ifakara ipo katikati ya Jimbo la Mlimba, Jimbo la Ulanga na Jimbo la Malinyi. Akitupatia gari la zimamoto pale Ifakara, atakuwa amelisaidia Jimbo la Mlimba, ameisaidia Ulanga na ameisaidia Malinyi na alifika kwenye ziara sehemu zote hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunaomba atu-note katika list ya magari yake ya zimamoto. Tunaomba atusaidie kuboresha Ofisi yetu ya NIDA pale Wilaya ya Kilombero ambayo ipo Ifakara, tunaomba pikipiki kwa watu wetu na askari wetu wazuri wanaofanya kazi kwa bidii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikwambie changamoto ya Wizara hii ni kubwa tunajua, mimi nikiangalia nyumba za askari wangu naona changamoto ni kubwa. Hapa Dodoma tu Makao Makuu ya Nchi ukienda hapo Polisi ukitazama mabanda ambayo askari anakaa huwezi kuamini. Hii yote ni mizigo ambayo sisi tunambebesha Waziri, kila mfuko wake utakapotuna ajaribu kukumbuka askari wetu ili wafanye vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ifakara tulikuwa tunasemwa kwenye mambo ya mitandao tangu afande IGP atuletee afande Nkuba na RPC – Morogoro kasi ile ya vijana waliokuwa wanasemwa semwa wizi wa mitandao imekwisha. Vijana sasa hivi wanajishugulisha na bodaboda, wanajishughulisha na bajaji na uendeshaji wa kirikuu. Mheshimiwa Waziri, ikimpendeza hata mwakani tunaweza tukakubaliana vijana hawa wasamehewe mambo ya faini faini. Maana yake nilikaa nao Ifakara pale kwa Churu, wengi wanalalamika faini zimekuwa nyingi na askari akamati bila makosa, makosa yapo lakini vijana wetu hawa ni muhimu kuwaangalia namna gani tunaweza tukawasaidia ili waweze kufanya kazi yao ya kuachana na mambo mengine na tabia mbaya kujiwezesha katika kutafuta kipato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kwenda moja kwa moja katika Modernization ya Jeshi la Polisi ambalo Mheshimiwa Rais analisimamia na wewe unasimamia, mfumo huu wa kuboresha kuunganisha Mahakama, Jeshi la Polisi na DPP ni mfumo muhimu sana. Katika dunia ya wenzetu sasa hivi ukipata tatizo unaenda Polisi, unazungumza Polisi unarekodiwa video bila mtu kuandika. DPP kule anaona, Mahakama inaona inarahisisha hata katika mambo ya kutoa hukumu, huu mfumo ni mzuri na uendelee kuboreshwa. Mshirikiane na mkongo wa Taifa ambao upo chini ya Wizara ya Habari na Mawasiliano ambao mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Miundombinu, tuliomba huu mkongo urudishwe kwa Serikali ili iweze kutoa huduma hiyo ya kiteknolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani sasa hivi unaenda Polisi unatumia saa zima askari anaandika kwa mkono kwa kalamu kwenye karatasi hii ni dunia ya wapi? Hii dunia imeshapitwa na wakati, tuachane nayo. Nimeona katika ukurasa wa 27 kuhusu kuboresha shirika hili alilosema Waziri la uzalishaji mali wa Jeshi la Polisi, nasisitiza hata huu Mradi wa Tehama wapewe hili shirika ili waweze kuuboresha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wameanza katika mikoa michache Mradi wa Miji Salama ya Kiteknolojia na Kufunga Kamera, lakini katika miji waliyoanza Morogoro wameiacha, sasa Morogoro ndiyo katikati ya kiungo hapa huwezi kwenda mikoa 17 kwa barabara kama hujapita Morogoro. Kwa hiyo, nasisitiza na Morogoro waiweke, nasisitiza Mradi wa High Way Speed, Road Patrol Camera uboreshwem dunia tunayoenda sasa hivi siyo dunia ya kujaza Polisi barabarani. Wizara ifunge kamera za kisasa, wapunguze askari wetu wakaendelee kusaidia wananchi huko walipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasisitiza sana kwamba Mheshimiwa Waziri nikiunga mkono hoja yake, mzigo huu ni mkubwa, mimi nataka nyumba za Polisi, kila Mbunge anataka nyumba za Polisi. Dodoma hapa yenyewe nimesema kuna nyumba, ni aibu kabisa, napita pale nauliza haya mabanda ya nani wanasema ya Polisi, kweli ni shida sana. Tunambebesha Mheshimiwa Waziri, mzigo mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na nashukuru sana, ikimpendeza Mheshimiwa Waziri afanye tena ziara aje katika Jimbo la Kilombero. Ahsante sana. (Makofi)