Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Muharami Shabani Mkenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bagamoyo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kupata nafasi hii. Kwanza kabisa, kwa haraka haraka maana yake muda hautoshi, ningependa kumpongeza Amir Jeshi wetu Mkuu Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya na kuyaongoza Majeshi yetu. Pili ningependa nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Makamanda wote ambao wanaongoza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama katika Tanzania hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja katika suala zima la Jeshi letu la Zimamoto. Kweli kabisa Jeshi hili kwa sasa Serikali iko haja na umuhimu mkubwa wa kuliangalia kwa kiwango cha juu sana, kwa sababu sasa hivi dunia inakumbwa na mabadiliko ya tabianchi. Hali inakuwa mbaya ya mafuriko na majanga mengineyo, Jeshi hili sasa umefika wakati linatakiwa lipewe nguvu za ziada ili liweze kumudu kazi au kasi ya uokoaji katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Wizara wanajitahidi. Juzi tu Jeshi hili limepokea magari 12 mapya kwa ajili ya uokoaji, magari haya ni ya kisasa kabisa ambayo yanahitajika yaende sehemu mbalimbali katika nchi yetu kwenda kufanya kazi ya uokoaji pamoja na kuzima moto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe angalizo moja kwa wenzetu wa Jeshi la Zimamoto, magari haya ni ya kisasa zaidi na yameletwa ili yaje kufanya kazi kwa ajili ya uokoaji, kwa hiyo basi wahakikishe kwamba wanayatazama na kuyatunza magari haya. Magari haya kwa sasa yako chini ya uangalizi wa supply, basi wakae na wao kujifunza waone ni jinsi gani ambavyo wanaweza kuyatumia magari yao. Kujifunza mitambo yake inavyofanya kazi ili kesho na kesho kutwa tusiyakute magari haya yako ubaoni yamechakaa kwa muda ambao haukukusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiachilia mbali magari haya ya Zimamoto bado kuna changamoto kubwa katika Jeshi letu la Polisi. Jeshi la Polisi lina changamoto ya usafiri, magari mengi ya Jeshi la Polisi yamechakaa hayafanyi kazi, mengi yamekuwa stranded, yamekaa hayana mpango wowote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana Serikali itenge bajeti kwa ajili ya kuyafufua haya magari, tusitegemee wafadhili kutufufulia haya magari au kututengenezea, kwa sababu ni hatari kabisa kabisa Jeshi la Polisi kuwa linasaidiwa kila mara. Kama alivyozungumza mzungumzaji aliyepita jirani yangu hapa, Jeshi la Polisi linatakiwa sasa hivi lielekee katika kujitegemea, Serikali ilipe nguvu Jeshi hili liweze kuhudumia vifaa vyake, kwa sababu leo anapotokea mtu mtaani analisaidia Jeshi la Polisi kwa chochote kile, kesho mtu huyo akifanya kosa Jeshi hili la Polisi litashindwa kumdhibiti kwa sababu limekuwa ni mfadhili wao. Kwa hiyo, niwaombe ndugu zangu, Serikali pamoja na Wizara wachukulie umuhimu sana kutoa huduma katika majeshi yetu haya na hususan Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, magari yatakapochakaa watenge bajeti na fungu kabisa la kufanya service haya magari. Tunajua Serikali inajitahidi na inapambana kuhakikisha magari mapya yanapatikana na kweli tunaona juhudi za Serikali, tunaona juhudi za Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anayoifanya. Jeshi la Polisi sasa hivi linapata magari ya kisasa na mapya, lakini wachukulie umuhimu huu wa kufanya service magari yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia nitoe pongezi zangu za dhati kwa Makamanda wetu wa Polisi wa Mikoa, wanafanya kazi kubwa sana hususan kama kamanda wangu wa Polisi wa Mkoa wa Pwani. Nampongeza kwa kazi kubwa anayoifanya Mkoa wa Pwani sasa hivi umetulia, matukio ya uhalifu yamepungua kwa kiasi kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza OCD wangu wa Bagamoyo pamoja na Chalinze kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya katika Wilaya yetu ya Bagamoyo, kwa kweli hali ya usalama imekuwa nzuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile napenda niwapongeze wenzetu wa Jeshi la Polisi kwa kweli, hawa makamanda au Polisi Kata wanatusaidia kwa kiasi kikubwa sana katika nchi yetu. Leo hii katika kata nyingi sana uwepo wa Polisi Kata unasababisha kuwepo kwa amani kwa kiasi kikubwa sana. Wanajitahidi sana tunatakiwa tuwapongeze, tuwape ushirikiano na ikiwezekana tuwaongezee vile vitu ambavyo wanavihitaji ili kufanya kazi zao kwa weledi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la pale Jimboni kwangu Bagamoyo. Bagamoyo tuna changamoto ya gari, hakuna gari ambalo ni zima, ni gari la siku nyingi na limekuwa bovu. Sambamba na hilo, tunahitaji ikiwezekana Wizara ifikirie kutupatia boti la polisi, ili liweze kuangalia maeneo ya bahari kwa sababu, maeneo ya Bagamoyo ni hatarishi ambayo, wakimbizi au wahamiaji wengi haramu wanapata uchochoro wa kupita na pia, magendo mengi yanapitishwa. Askari hawa wa Bagamoyo wakipatiwa boti, watakuwa na uwezo wa kufanya kazi ya kupita baharini katika maeneo yote, ili kuhakikisha wahamiaji haramu pamoja na magendo hayafanyiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine ambalo katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri limejionesha hapa kwamba, Serikali inakusudia kufanya ukaguzi wa vyombo vya moto. Suala la ukaguzi wa vyombo vya moto ni muhimu sana, ajali nyingi zinatokea katika nchi yetu kutokana na magari kuwa mabovu. Kwa hiyo, hili suala ambalo Wizara inakusudia kulifanya kwa kupitia Jeshi la Polisi ni suala la msingi na ninawapongeza sana katika jambo hili ambalo mnakusudia kulifanya. Kwa kweli, ukipita barabarani huko magari mengi ni mabovu kwa hiyo, Serikali ina kila sababu kuhakikisha wanafanya ukaguzi wa magari ili tuweze kunusuru wananchi wetu katika suala zima la usalama barabarani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya machache nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)