Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nashukuru kwa kunipatia nafasi hii. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa rehema zake za pekee, kutuwezesha jioni hii njema kuingia katika Bunge hili. Pia, namshukuru sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri ambayo anaifanya katika nchi yake. Mungu aendelee kumbariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nazidi kuvipongeza hivi vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri ambazo wanafanya. Ningewezakutaja majina ya mtu mmoja mmoja, lakini kwa sasa siwezi kulingana na muda. Nampongeza sana Waziri, Mheshimiwa Masauni, kwa kazi nzuri ambazo anafanya pamoja na Naibu Waziri, Mheshimiwa Sillo, ahsanteni sana kwa kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza moja kwa moja kwa upande wa Jeshi la Polisi, linafanya kazi nzuri sana nchini Tanzania. Linafanya ulinzi wa mipaka yetu na raia, usalama wa wananchi na kila kitu, wanafanya kazi nzuri, lakini kwa kweli, kuna kitu kimoja ambacho tunawafanyia, naona wakati mwingine hata raha ya kazi wanaikosa, hawana makazi mazuri. Kwa kweli, wana nyumba za ajabu, nyumba ambazo ni za zamani, zimepitwa na wakati, lakini ndizo wanazokaa. Inabidi Waziri Masauni, kaka yangu, naelewa yeye ni msikivu, tunaomba awajengee nyumba askari wetu ili waweze kuwa na utulivu wa akili kuanzia nyumbani mpaka kazini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naingia katika Mkoa wangu wa Simiyu. Nashukuru sana kwamba, viongozi wetu wanafanya kazi nzuri, lakini kuna wilaya moja kongwe, Wilaya ya Maswa ni ya siku nyingi sana kwa kweli, ina nyumba za ajabu sana, zimechoka na ni fupi kama vibanda, tunaomba waweze kujengewa nyumba ambazo ni nzuri. Kwa kweli, tunawafanya wanakaa katika mazingira ambayo siyo rafiki. Mtu anapofanya kazi, basi utulivu uanzie pale anapoishi, anapolala na anapotoka kwenda kazini anakuwa vizuri. Tunaomba maaskari wetu wawajengee nyumba nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, habari nyingine ni ya kikokotoo. Kikokotoo kwa upande wa Jeshi la Polisi tunaomba wakiondoe, lakini siyo kwa Polisi tu, bali pia, kwa wafanyakazi wengine wote, hii ni kero. Unashangaa mtu kafanya kazi Serikalini muda wa miaka 35 au 40, mwisho wa siku anakuja kupata shilingi milioni 28 kwa kweli, hiyo siyo sawa. Mtu apewe haki yake yote apange utaratibu wa mambo yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusema kwamba, viongozi wetu hawa tunaamini wanafanya kazi vizuri, lakini pia, hawana magari. Magari yao mengi ni chakavu na hawana hata hela za service. Muda mwingi wanahangaika, hawana hata mataili ya gari, service hakuna, mafuta ni shida, tunaomba OC inapoenda hawa watu wapate mahitaji yao muhimu, ili waweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naenda upande wa Jeshi la Zimamoto. Jeshi la Zimamoto wanafanya kazi vizuri sana chini ya kiongozi wetu John Masunga. Juzi tu hapa tumeona kuna magari 11 yametolewa, tunamshukuru sana Rais wetu. Mbali na magari haya, pia, kuna nyumba sita za ghorofa ambazo wanakaa wanajeshi 60. Hizi ni nyumba ambazo ni nzuri na zimejengwa kwa shilingi bilioni 7.1 kwa kweli, ni nyumba nzuri na wanaokaa mle ni askari wa chini wa kawaida kabisa. Kwa hilo, kwa kweli, namshukuru sana Mheshimiwa Masauni kiongozi wetu wamefanya kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naingia katika Mkoa wangu wa Simiyu kwa kweli, hatuna magari ya Askari Polisi. Hawana magari kabisa, tunaomba magari yapelekwe. Rais wetu amesema magari ya zimamoto yanaletwa kwa nchi nzima, tunamshukuru sana mama yetu, nchi nzima kuanzia Wilaya na Mikoa yake wote tutapata magari hayo. Magari hayo yatasaidia utendaji wa kazi wa maaskari wetu maana wanafanya kazi katika mazingira magumu, lakini wakipata yale magari watafanya kazi vizuri, mambo yote yataenda vizuri na tutaendelea kuwashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Wafanyakazi wa Jeshi la Magereza ni kwamba, Magereza ni chombo ambacho kinafanya vizuri sana, kule wanawafundisha wafungwa. Sasa hivi urekebu wanajifunza mambo mbalimbali, lakini hawana vitendea kazi na miundombinu imechoka. Magereza nyingi ni za siku nyingi, hata Gereza letu la Mkoa wa Simiyu, Wilaya ya Meatu, ni gereza ambalo kwa kweli, limechoka, ni kama banda. Mheshimiwa Waziri afike kule ajifunze, aone, siyo nyumba ni banda tu limejengwa hata mfungwa akiamua kufanya vurugu mle anatoka kwa sababu, hata ukuta wenyewe haupo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri aiangalie sana Wilaya ya Meatu tupate magereza ambayo ni nzuri hata wafungwa wanapokaa mle, wakae sehemu ambayo ni safi na salama. Kwa sababu, binadamu yeyote yule hata kama ana makosa anatakiwa kukaa sehemu iliyo salama, lakini gereza hili halina hata bwalo la chakula. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi letu la Magereza tunaona jinsi linavyofanya kazi, wanalima na sehemu nyingine wanajihudumia chakula wao wenyewe, lakini kwa ajili ya kukosa miundombinu mizuri ndiyo maana hata vyakula hawaivishi. Mvua zinanyesha sana, lakini hatuna mabwawa ya kuhifadhi maji, basi naomba magereza wachimbiwe mabwawa, kwa ajili ya kufanyia shughuli zao za kilimo. Waweze kulima muda wote, wakati wa kiangazi na wakati wa masika, ili waendelee kufanya uzalishaji mkubwa. Watakula kile chakula na kingine wanaweza wakauza wakaongeza kipato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuunga mkono hoja. Ahsante sana kwa kunipatia nafasi. (Makofi)