Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Issaay Zacharia Paulo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia baraka zake katika Taifa letu. Nachukua nafasi hii kuungana na Watanzania wenzangu wote kuendelea kuliombea Taifa letu baraka, amani, upendo na mshikamano kwa Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kuungana na wananchi wa jimbo langu la Mbulu Mjini kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi anavyoliongoza Taifa letu pamoja na Serikali nzima ya Awamu ya Sita kwa jinsi wanavyosimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020 hadi 2025, hongera sana Mheshimiwa Rais na waandamizi wako wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza pia Wizara hii ya Mambo ya Ndani na vyombo vyetu vyote vya ulinzi na usalama nchini. Pia naipongeza pia Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba kutoa mchango wangu kupitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri na maoni ya Kamati yetu ya Bunge yaliyowasilishwa mbele ya Bunge letu leo hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru sana Serikali kuondoa kigezo cha uhitimu wa mafunzo ya JKT kwa vijana wetu kujiunga kwenye majeshi yetu yote kwa kuwa siyo vijana wote nchini wenye sifa mbalimbali wamefanikiwa kupata mafunzo ya JKT nchini. Hivyo basi tunaiomba Serikali iangalie kwa mapana suala la urefu wa kimaumbile kwa vijana waombaji kama sifa mojawapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunajua urefu wa binadamu ni maumbile aliyomjalia Mwenyezi Mungu hivyo basi katika sura nyingine kigezo hiki kinaweza kuwa kinyume na haki za binadamu kwa kuwa ni zaidi ya uwezo wake wa sifa na jitihada zake binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga hoja mkono 100% na naomba kuwasilisha.