Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Daniel Baran Sillo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Babati Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili nichangie kwenye hoja yetu hii ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025. Awali ya yote naungana na wenzangu waliotangulia kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa afya njema na hatimaye leo kuwa katika Bajeti ya Wizara yetu ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka huu wa Fedha 2024/2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa anayofanya na pia, kwa maelekezo yake mahususi kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika kuboresha majeshi ambayo tunayasimamia. Pia, nampongeza Mheshimiwa Makamu wa Rais ambaye anamsadia Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ambayo anaifanya katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Mwenyekiti wa Kamati yetu ya NUU, Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa, pamoja na Makamu Mwenyekiti, Mheshimiwa Vicent na Wajumbe wote wa Kamati hii kwa kazi kubwa wanayoifanya. Ushauri na maelekezo ambayo wanatupatia sisi Wizara hii hakika umekuwa ni msingi mzuri wa utendaji kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri wetu, Mheshimiwa Engineer Masauni, kwa kazi kubwa na uongozi wake mahiri ndani ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ndani ya Nchi. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi tunajiita ni kijiji kimoja chini ya Mwenyekiti mmoja, Mheshimiwa Hamad Yussuf Masauni. Hongera sana Mheshimiwa Waziri, nakuhakikishia nitakuwa msaidizi wako mahiri sana katika kutenda kazi. Pia, nawapongeza Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, pamoja na watendakazi wote walioko chini ya Wizara hii. Halikadhalika navipongeza vyombo ambavyo vipo chini ya Wizara yetu ya Mambo ya Ndani ya Nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, waliochangia hoja hii ni Wabunge 24. Pia, Mwenyekiti wetu aliwasilisha Hoja ya Kamati, tunampongeza sana yeye pamoja na Waheshimiwa Wajumbe wote. Nawahahikikishia kwamba, hoja zenu zote tumezichukua, tunazithamini, tunaziheshimu sana na tutazifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kutoa ufafanuzi kwa hoja chache na nianze na hoja ya kwanza kuhusu Jeshi la Zimamoto. Hoja hii imetoka kwa Mheshimiwa Aleksia Asia Kamguna, Mbunge wa Viti Maalum, ambaye alizungumzia habari ya changamoto ambazo zipo katika Jeshi hili la Zimamoto ambazo ni upungufu wa rasilimalli watu hasa waokoaji wa majini, vitendea kazi pamoja na vituo hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali kupitia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji inaendelea kuboresha mazingira ya Ofisi kwa kujenga na kukarabati vituo vya zimamoto na uokoaji. Katika Mwaka wa Fedha unaokuja 2024/2025, Jeshi linaendelea na ujenzi wa vituo saba katika Mkoa wa Geita, Manyara, Katavi, Songwe, Njombe, Kagera na Simiyu, ambapo miradi hii imetengewa kiasi cha shilingi 2,600,000,000 katika Mwaka wa Fedha unaokuja 2024/2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lina jumla ya Maafisa na Askari 104 hawa ni kwa ajili ya ukokoaji majini. Aidha, katika Mwaka wa Fedha 2023/2024, Jeshi limepata kibali cha kuajiri askari wapya 246 ambapo kati ya hao, askari 25 wapo kwenye mafunzo ya uokoaji majini. Vile vile, katika Mwaka wa Fedha huu unaokuja 2024/2025 Jeshi limepanga kuajiri askari wapatao 425.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo kazi kubwa inafanyika katika Wizara hii. Juzi, tarehe 13 mwezi wa tano, Mheshimiwa Waziri kwa niaba ya Mheshimiwa Rais alizindua nyumba sita za Makazi ya Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji zenye thamani ya shilingi bilioni 7.1. Sambamba na nyumba hizo pia, Mheshimiwa Waziri alizindua magari 12 ya zimamoto ambayo yamegawanywa katika mikoa mbalimbali hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ni kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge Martha Mariki. Yeye amesema katika Mkoa wa Katavi hakuna gari la zimamoto na kwamba, Jeshi liwekeze katika sayansi na teknolojia na liwe na vifaa maalum badala ya kutumia karatasi katika kurekodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimwarifu Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kwamba, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limepata mkopo wenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 95. Kupitia mkopo huo Jeshi litapata magari 150 ya zimamoto na uokoaji, magari haya yatakwenda kwenye wilaya na mikoa yote hapa nchini ambayo haina magari ya zimamoto, ukiwepo Mkoa wa Katavi ambao amesema Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Iringa, amezungumza habari ya gari la Mkoa wa Iringa. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Wilaya zipo 139, magari yapo 150. Kwa hiyo, mikoa yote ambayo haina magari itapata magari ya zimamoto na uokoaji katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa sayansi na teknolojia, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linaendelea kuboresha shughuli zake kwa kuwekeza kwenye sayansi na teknolojia. Kwa Mwaka wa Fedha wa 2024/2025, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limetenga jumla ya fedha kiasi cha shilingi 345,259,900.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudie. Shilingi 345,259,000 ni kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli hizi mbalimbali za sayansi na teknolojia. Aidha, baadhi ya majukumu ikiwemo ukaguzi wa kinga na tahadhari dhidi ya moto umeanza kufanyika kwa kupitia mifumo ya kitaalam na kupitia mradi huu wa mkopo nafuu, kama nilivyosema hapo awali kutoka Falme za Uarabuni, Jeshi linatarajia kusimika miundombinu ya mawasiliano katika vituo vikuu na kamandi 30 za zimamoto na uokoaji hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ni kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum, Grace Tendega, ambaye amezungumzia mambo kama matano hivi. Jambo la kwanza ni Jeshi lizingatie ulipaji wa malimbikizo ya madeni ya likizo. Pili ni, upandishaji wa vyeo kwa askari wetu. Tatu ni, ajira zinazotolewa na Jeshi letu zizingatie idadi ya wanawake. Nne, ajira zinazotolewa na Jeshi la zimamoto na uokoaji kwanza zizingatie ikama na wanawake. Tano, zimamoto haijapata fedha ya maendeleo na sita ni zimamoto iendelee kukusanya maduhuli, ili iweze kupata pesa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Jeshi kupitia Wizara ya Fedha, linaendelea na uhakiki wa madeni ya watumishi, wazabuni na watoa huduma yenye thamani ya shilingi 2,591,188,845.4. Jeshi likishakamilisha uhakiki huu litawasilisha Wizara ya Fedha, kwa ajili ya malipo ya madeni haya ambayo ameyataja Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kuhusu upandishwaji wa vyeo. Jeshi linaendelea kuhakikisha kwamba, maafisa na askari wanapandishwa vyeo mara baada ya kufuzu mafunzo. Aidha, katika Mwaka huu wa Fedha wa 2024/2025, Jeshi linatarajia kuwapandisha vyeo maafisa na askari 1,224. Hii ni hatua kubwa sana na ya kihistoria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ni kuhusu ajira; katika mwaka wa fedha 2024/2025, Jeshi limepanga kuajiri jumla ya askari 425 ambapo ajira hizo zitazingatia pia, idadi ya wanawake, kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la nne, ni kuhusu fedha za maendeleo. Katika Mwaka wa Fedha 2023/2024, Jeshi lilipokea shilingi 12,865,150,000 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Fedha hizo pia, zimetumika kugharamia malipo ya awali ya asilimia tano ya mkopo wa Dola Milioni 95, kama nilivyosema, kutoka Abu Dhabi Export Trade Agency.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tano, jeshi linaendelea na ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali ambapo hadi Mwezi, Aprili 2024, limekusanya jumla ya shilingi 9,919,243,405 sawa na 90.17% ya lengo la Mwaka wa Fedha uliopita 2023/2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ni juu ya Jeshi la Magereza ambayo ilitoka kwenye Taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati yetu ya NUU. Moja, ilikuwa ni Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi iweke utaratibu mzuri wa kuanza mapema maandalizi ya awali ya kuchochea miradi ya maendeleo. Ushauri huu umepokelewa na Wizara. Ninakuhakikishia pamoja na kamati yako kwamba, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi itaendelea kufanya mawasiliano ya karibu na Hazina, kwa ajili ya kupatiwa fedha za maendeleo kwa wakati ili kuhakikisha kwamba, miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati kama ilivyopangwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ya Kamati ilikuwa ni Serikali iendelee kuboresha hali ya vyombo vya usafiri na usafirishaji kwa majeshi yaliyo chini ya Wizara hii. Serikali inatambua ukubwa wa tatizo la usafiri kwa Majeshi yetu yaliyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Katika jitihada hizo Serikali imekuwa ikitenga fedha, kwa ajili ya kununua vyombo vya usafiri, ambapo katika Mwaka wa Fedha 2023/2024 shilingi 6,691,419,000 zilitengwa na jumla ya magari 25 yameshalipiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025, shilingi 3,540,000,000 zimetengwa ili kununua magari ya Jeshi la Magereza, kwa ajili ya shughuli za utawala na usafirishaji wa mahabusu. Kwa hiyo, namtoa wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba, maelekezo ya kamati sisi tunayasikiliza kwa umakini mkubwa, ili kuboresha utendaji kazi katika Wizara yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ni Serikali iendelee na mkakati wake wa kuboresha hali ya vifaa na vitendea kazi kwa Majeshi yaliyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Katika Mwaka wa Fedha 2023/2024, Serikali ilitenga jumla ya shilingi 3,260,000,000 kwa ajili ya ununuzi wa zana za Kilimo. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali imetenga shilingi 2,378,523,000 ili kununua mitambo na zana za Kilimo. Maboresho haya ya ununuzi wa zana za kilimo, yatasaidia sana kuboresha upatikanaji wa maduhuli kwa sababu, Jeshi la Magereza linategemea sana shughuli za kilimo katika utendaji wake wa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali vilevile imetakiwa iweke mikakati ya kupata hati za umiliki wa ardhi katika maeneo yote yanayotarajiwa kujengwa na yanayomilikiwa na Jeshi la Magereza hapa nchini. Serikali imeandaa mkakati wa kuhakikisha maeneo yote yanayomilikiwa na Jeshi la Magereza yanapimwa na kupatiwa hatimiliki. Nitatoa mfano, katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali ilitenga shilingi 500,000,000 na mwaka wa fedha 2023/2024 imetenga shilingi 200,000,000 na katika bajeti hii inayokuja ya 2024/2025 Serikali imetenga shilingi 492,940,000. Hata hivyo, mpaka sasa Jeshi la Magereza limeshapata hatimiliki 66 na kufanikisha kukamilisha kupima maeneo 144 ambayo yanasubiri hatimiliki. Aidha upimaji wa maeneo 40 yaliyobaki pia unaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo hoja kuwa, Serikali iboreshe matumizi ya teknolojia ya kisasa katika utendaji kazi wa Majeshi yaliyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Serikali imeendelea kuboresha matumizi ya sayansi na teknolojia kwa Jeshi la Magereza katika mifumo ya ulinzi na upekuzi. Kufikia Mwezi Aprili, 2024, Magereza 10 zimefunga mifumo ya CCTV Camera. Aidha, Magereza Kuu tatu zinatarajia kufungwa mifumo hiyo katika Mwaka huu wa Fedha unaoendelea 2023/2024. Vile vile Jeshi la Magereza linatarajia kusimika mifumo ya upekuzi (Work through Scanner) katika Magereza tano katika Mwaka wa Fedha unaokuja 2024/2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ilitoka Fungu 29 - Jeshi la Magereza, lakini hii kutoka kwa Kamati ya NUU ambapo Kamati ilitaka pia fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi ma magereza mapya mawili pamoja na ukarabati wa magereza manne katika Mwaka wa Fedha 2024/2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni na ushauri wa Kamati umepokelewa na ukarabati na ujenzi wa magereza mapya kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024, umepokelewa na utazingatiwa katika mwaka wa fedha unaokuja na kuhakikisha kuwa fedha inapatikana kwa wakati ili miradi iweze kukamilika kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ni Jeshi la Magereza liandae mkakati wa kuboresha miundombinu chakavu kwenye baadhi ya magereza nchini. Jeshi la Magereza tayari limeshafanya tathmini na kuainisha mahitaji halisi ya ukarabati wa magereza pamoja na ujenzi wa magereza mapya ambapo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 yatakarabatiwa magereza manne ambayo yametengewa shilingi 6,491,792,000. Naomba niyataje magereza hayo: ni Gereza la Butimba lililoko Mwanza, Lilungu ambalo liko Mtwara, Ukonga na Keko, Dar es Salaam. Aidha, kulingana na mkakati huu wa fedha kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025, Jeshi la Magereza litakamilisha magereza mawili ambayo ni Gereza la Kilosa na Gereza la Karatu ambayo yametengewa shilingi 4,022,125,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine, Serikali iwezeshe Jeshi la Magereza kupata magari hususan kwa ajili ya kusafirisha mahabusu. Serikali imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba inanunua magari kwa ajili ya kusafirisha mahabusu. Katika Mwaka wa Fedha 2023/2024, Serikali imetoa shilingi 1,930,000,000 kwa ajili ya ununuzi wa magari ya mahabusu. Kwa Mwaka wa Fedha unaokuja wa 2024/2025, Serikali imetenga shilingi bilioni moja kwa ajili ya ununuzi wa magari kwa ajili ya kusafirisha mahabusu kwenda Mahakamani na kurudi katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ni kama sehemu ya kuimarisha Mfumo wa Haki Jinai nchini. Jeshi la Magereza litekeleze kwa ukamilifu na ufanisi mpango wa kuimarisha Huduma za Mahakama Mtandao. Naomba niliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Jeshi la Magereza limezingatia ushauri huu wa Kamati na litahakikisha kuwa vyumba 20 vya Mahakama Mtandao vinajengwa kama ilivyopangwa kwenye Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2024/2025. Katika eneo hili imetengwa fedha shilingi 1,397,680,000 katika mwaka wa fedha kama nilivyosema 2024/2025. Kwa hiyo, nawahakikishia Waheshimiwa Wabunge wote kwamba hoja zenu kama mlivyosema, hoja zote tumezipokea na tutazifanyia kazi kila hoja na kuhakikisha kwamba tunazifanyia kazi na kuzitolea ufafanuzi kwa kadiri inavyowezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa kusema maneneo yafuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia kwa uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu:-

(i) Raia na mali zao wataendelea kuwa salama kupitia Jeshi la Polisi;

(ii) Uongozi na ujenzi utaendelea kuimarishwa kupitia Jeshi la Magereza;

(iii) Uokoaji wa maisha na mali utaendelea kupitia Jeshi la Zimamoto na uokoaji; (Makofi)

(iv) Usalama wa wahamiaji na masuala ya Hati ya Kusafiria na kuboresha mipango yote ya wahamiaji iko salama ndani ya uongozi wa Mama Samia Suluhu Hassan; na

(v) Vitambulisho vya Taifa vitatolewa kupitia NIDA katika uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana kwa nafasi hii na naunga mkono hoja, ahsanteni sana. (Makofi)