Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ndanda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Nishati na Madini. Moja kwa moja nielekeze kwanza mchango wangu katika Shirika la Umeme la TANESCO. Mpaka sasa hivi tunafahamu TANESCO wana deni kubwa sana kutoka kwa wazabuni, lakini pia kutoka kwa watu mbalimbali. Namwomba Mheshimiwa Waziri watakapokuwa wanaleta majumuisho yao watueleze wazi wazi, kama kuna mpango wowote wa kukiongezea nguvu Kitengo cha Masoko cha Shirika la Umeme Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wale wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea. Nafikiri kama wanaamua kufanya kazi kibiashara, basi angalau wangekuwa wanazungukia kwenye maeneo ambako kuna ujenzi mpya unaendelea na wao kutafuta wateja badala ya wateja kuanza kuhangaika kwenda kwenye Ofisi za TANESCO kuomba wakaandikishwe. Hata hivyo, watu hao wanaokwenda Ofisi za TANESCO wakishalipa pesa yao kwa ajili ya gharama za kuunganishia umeme, hili zoezi linakuwa refu sana, wamekuwa wenye urasimu mkubwa sana watu hawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii tunaiona zaidi katika maeneo yetu, ukifika maeneo ya Masasi, ukifika maeneo ya Ndanda, hasa zaidi maeneo ya sokoni, kuna watu wengi sana wamejiandikisha pale kupata huduma ya umeme, lakini sasa hivi ni miezi mitatu, miezi minne watu wale wanashindwa kupelekewa umeme ambao tayari wameshaulipia. Sasa TANESCO watueleze kama walikuwa tu wanatumia kiujanja ujanja kutaka kukopa pesa kwa hawa watu wanaotaka kuunganishiwa umeme na hawawekewi umeme kwa muda, wakati masharti ni kuwapelekea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niseme, kwenye biashara ya mafuta, EWURA pamoja na tozo mbalimbali zilizopo kwenye biashara ya mafuta. Mfanyabiashara wa mafuta ni mtu amekuwa wa kuonewa sana kwa kipindi kirefu. Ukiangalia gharama za mafuta sasa hivi japokuwa zimeshuka kufikia sh. 1,600/=, lakini nyingi katika hii pesa inakwenda kwenye upande wa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, tozo za mafuta zinakadiriwa kufikia sh. 500/= mpaka sasa hivi na mfanyabiashara wa mafuta anapata tu pale sh. 200/=. Kwa hiyo, sh. 900/= ni gharama halisi ya mafuta. Kwa nini Serikali isione kuna haja ya kupunguza kodi mbalimbali zilizoko kule ndani ya mafuta hasa zaidi hizi tozo ili mwananchi aweze kununua mafuta kwa gharama nafuu zaidi tofauti na gharama iliyopo sasa hivi? Naamini kwa sababu umekuwa ukipata sifa nyingi na hili jambo unaweza kulichukulia hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kusikitika kabisa niwaambie kwamba, katika eneo letu la Wilaya ya Masasi, suala la kukatikiwa umeme sasa hivi limekuwa kama fashion. Haipiti siku mbili, siku tatu, lazima umeme utakatika. Ukipiga simu TANESCO kutaka kufahamu kwa nini imekuwa hivyo, hata wenyewe wakati mwingine wanashindwa kujua sababu za msingi. Mara utaambiwa mikorosho imedondokea nguzo, mara utaambiwa miundombinu duni katika eneo hili kwa sababu iliwekwa kwenye miaka ya 1990.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sasa tufahamu wazi kabisa Serikali ina mpango gani kuweza kutubadilishia miundombinu katika eneo letu la Wilaya ya Masasi ili tuweze kupata umeme wa uhakika kwa sababu umeme huu unazalishwa katika maeneo yetu ya Mtwara na tumeambiwa kwamba unatumia umeme wa gesi lakini tuseme kweli, sisi hatufaidi umeme ule kwa sababu tunaupata kwa matatizo makubwa sana katika Wilaya zote zinazozunguka maeneo ya Masasi ikiwa ni pamoja na Nanyumbu na maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Ndanda ndiyo kuna vichekesho, kwa sababu katika maeneo haya ndiko unakopita umeme unaokwenda kutumika maeneo ya Masasi, maeneo ya Nachingwea na maeneo mengine. Hata huko Ruangwa maeneo ya kwa Waziri Mkuu umeme wake unakatiza katika maeneo ya Jimbo langu. Wazee na vijana, watu mbalimbali katika maeneo yale walishawishiwa wadondoshe mikorosho yao, wengine wakate miembe ili zipite pale nguzo kwa ajili ya kuwaletea wao huduma za umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimejaribu kumweleza mara nyingi tu hapo Mheshimiwa Waziri katika suala hili, lakini ni ajabu kabisa mpaka sasa hivi tunaingia katika hili Bunge la Bajeti, hakuna hatua zilizochukuliwa za moja kwa moja katika vijiji ambako nguzo za umeme zinapita katika maeneo hayo. Tunaomba tupewe taarifa ya vijiji vile. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda katika Vijiji vya Chipite, Mkwera, Nanganga na maeneo mengine, umeme unapita juu ya vichwa vyao, lakini pale chini watu wale hawana umeme. Kuna wakati ulifika katika Kijiji cha Liputu, Mzee wangu mmoja pale alikuwa haoni umuhimu wa kuwa na zile nguzo shambani kwake, aliamua kuchoma nguzo moja moto. Bahati nzuri wakati huo alifikishwa Polisi, wakati ule Mheshimiwa Mkuu wa Kituo ana busara, kabla hajaamua kujiingiza kwenye siasa, walimaliza lile jambo amicably lakini yule mzee alikuwa haoni umuhimu wa kuwa na nguzo inayopita shambani kwake. Yeye alikuwa anatamani lile eneo alitumie kwa ajili ya kilimo na siyo kupitisha nguzo ambazo zinakwenda kunufaisha watu mwishoni mwa lile eneo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuweza kupunguza gharama, nafikiri wakati mwingine TANESCO ifikirie kuwa na njia mbadala. Kusingekuwa na haja ya kupitisha umeme maporini, badala ya umeme ule kuupitisha kwenye vijiji ambako wanakaa watu, vikakona vikaenda kule. Sisi tumeamua sasa hivi kufuata njia kuu moja kwa moja. Kusingekuwa na haja ya kupitisha umeme katika Kijiji cha Chigulungulu ambapo umeme ule sasa hivi unatakiwa uzunguke Namalembo ili kufika mpaka Msikisi wakati tayari kulikuwa kuna shortcut inayopitia katika Vijiji vya Chiroro na vijiji vingine katika Kata ya Msikisi ili kuweza kupata umeme katika maeneo yale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunashindwa pia kuelewa, pale TANESCO wanapokuja kutaka kuunganishia umeme nyumbani kwako, wao walikuwa na jukumu la awali la kuweka miundombinu iwakaribie watu katika maeneo yao ambako ujenzi unaendelea. Sasa hivi kunaonekana kuna mtindo wa TANESCO kuweka nguzo tu katika maeneo ya barabara. Utakapotaka wewe kuomba umeme ambaye ujenzi wako umemaliza, kiwanja cha tano kwenye mtaa wako, unaambiwa ulipie zile nguzo zote ambazo ziko pale barabarani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunaomba kupata jibu, nguzo hizi mwishoni zinakuwa mali ya nani? Gharama zile nilizolipia mimi kuwekeza kwenye nguzo zile mwanzoni: Je, naweza nikarudishiwa na hili shirika baadaye watu wa hapa katikati ili kufika nyumbani kwangu wakishakuwa wamejenga katika maeneo yao? Tunaomba hili tupate jibu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nilitoa taarifa katika Kijiji cha Chikundi, kuna Zahanati pale inatoa huduma nzuri sana kwa ajili ya akinamama kujifungua ili kuweza kupunguza mzigo wa akinamama wanaokwenda kujifungulia katika Hospitali ya Rufaa ya Ndanda. Sasa hivi wana miaka mitatu, miaka minne inakadiriwa panatakiwa kupatikana nguzo kama kumi, kumi na moja; lakini wale Wamisionari wa Ndanda wamepelekewa quotation ya shilingi milioni 11 ili kuweza kuweka umeme katika ile Zahanati ya Chikundi ambako yule mama pale, Mkunga anajitahidi kuwasaidia akinamama kujifungua akiwamulika kwa tochi. Tunaomba sasa hapa tupate majibu moja kwa moja, mnaweza mkatusaidia vipi katika maeneo yale? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kinachochekesha zaidi, mimi napakana na Mheshimiwa Waziri Mkuu katika Jimbo lake na baadhi ya maeneo fulani. Wanakijiji wengine wanatoka vijijini ambako ni mbali kabisa kufika kule kwa Waziri Mkuu, wanategemea kupata umeme kutokea katika upande wa Jimbo la Ndanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, Vijiji vya Chinongwe, Mandanga, Likwachu pamoja na Vijiji vya Mbecha, wale watu siku za Jumamosi wanafanya maandamano ya kuja upande wa Ndanda kununua ice cream, kwa sababu kule kwao wanakosa hata ice cream. Tumwonee Mheshimiwa huruma, tuhakikishe tunapeleka umeme katika haya maeneo ili watu waweze kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kijiji cha Ngamadani, pale pana gereza kubwa sana, lakini nako penyewe umeme unapita juu ya vichwa vyao. Pana wafungwa pale, pana Askari Magereza pale, siku wakija kupotea msiwalaumu lakini wanaishi kwenye mazingira magumu! Wanashindwa kuvuta maji kwa ajili ya kupeleka kwa matumizi ya wale Maafisa Magereza pamoja na wafungwa wao waliopo katika eneo lile kwa sababu ule mkusanyiko ni mkubwa sana. Tunaomba mtusaidie katika maeneo yetu, hatufahamu sisi tumewakosea nini nyinyi, lakini tunasema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kijiji cha Chingulungulu na kwenyewe umeme unakatiza juu ya vichwa vya watu. Mnashindwa tu kupeleka transformer ndogo ikashusha umeme kwa ajili ya kuhudumia watu pale. Tungepata angalau transformers chache za KV 50 zingeweza kusaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, niliongea na Meneja wa TANESCO siyo muda mrefu, aliniambia makadirio ya nguzo 1,200, pamoja na transformer 30 litaweza kumaliza tatizo la umeme katika eneo letu; lakini mimi nishushe zaidi, hata mkitupa nusu ya hii tutawaelekeza sisi alternative route za kuweza kuwafikia watu kwa kutumia transformer moja katika vijiji viwili au vijiji vitatu ikiwezekana kwa sababu njia za mikato za kuelekea hayo maeneo sisi tunazitambua. Tulikuwa tukifanya kampeni katika hayo maeneo, kwa hiyo, tunajua vizuri. Hii pia itasaidia TANESCO kuweza kupunguza gharama.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kata ya Chigugu, Vijiji vya Mbemba pale kuna zahanati kubwa sana, iko pale toka enzi za ukoloni, lakini mpaka sasa hivi hawana umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. Ahsante. Nasubiri majibu ya Mheshimiwa Waziri.