Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia uzima na afya njema. Vilevile, kwa mara nyingine tena ninamshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, kwanza kwa kuendelea kuliongoza vyema Taifa letu hili na kuendelea kudumisha amani na utulivu nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kumshukuru sana kwa kuendelea kuwa na imani na mimi katika nafasi hii. Namshukuru tena Mheshimiwa Daniel Sillo, Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini lakini pia Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kwa umahiri wake mkubwa ambao ameuonesha kwa muda mfupi tu toka ameaminiwa kwenye Wizara hii. Kwa kweli amekuwa na msaada mkubwa sana kwangu na hata ninyi ni mashahidi. Maeneo mengi ambayo leo tulitakiwa tuyatolee ufafanuzi, ameweza kuyatolea ufafanuzi kwa umahiri mkubwa. Hivyo, kuifanya kazi yangu hapa leo kuwa siyo kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza na kuwashukuru watendaji wote wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, watumishi wote na askari wote walio chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa ushirikiano wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuishukuru sana Kamati yetu ya Bunge chini ya Mwenyekiti, Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa, kwanza kwa jinsi ambavyo amewasilisha taarifa yao vizuri na hoja zilizotulia kweli kweli. Nichukue nafasi hii pia kuwashukuru na kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wale ambao walipata nafasi ya kuchangia walikuwa ni Wabunge kama 23. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yangu kuwa kama muda ungekuwa wa kutosha Wabunge wengi wangeweza kuchangia lakini hawa waliochangia wachache wamewawakilisha. Basi pamoja na taarifa ama hoja za Kamati baada ya zile ambazo Mheshimiwa Naibu Waziri amezitolea ufafanuzi na nitaomba nichukue nafasi hii kuzitolea ufafanuzi baadhi ya hoja hizo. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba hoja zote ambazo wamezitoa, hata zile ambazo hatutapata nafasi ya kuzitolea ufafanuzi hapa, tumezichukua na tutazifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa ambalo nimeliona katika michango ya Waheshimiwa Wabunge ni kwamba, ni dhahiri kabisa kwa michango ya Waheshimiwa Wabunge ambayo tumeisikia hapa inakwenda sambamba na Dira ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia 4R zake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nayasema hayo kwa sababu ukiangalia michango ya Waheshimiwa Wabunge ambayo imechangiwa hapa, mingi imejikita katika kuhakikisha na kuona Wizara yetu ya Mambo ya Ndani ya Nchi pamoja na Vyombo vyake inaendelea kuimarika na kufanya kazi zake vizuri ili hatimaye iweze kutoa huduma bora kwa wananchi. Maeneo ambayo nadhani Waheshimiwa Wabunge wameyagusia ili kutimiza azma hiyo ni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, wamegusia sana katika eneo la kuangalia haki na stahiki za askari wetu. Vilevile, wamegusia katika maeneo ya kuhakikisha kwamba vyombo vyetu vya usalama vinakuwa na miundombinu bora na ya kisasa katika kutekeleza majukumu yake, ikiwemo nyumba za askari za kuishi, vilevile na vituo vya askari vya kufanyika kazi na Vyombo vyote vya Usalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo nimeona Waheshimiwa Wabunge wameigusia ni eneo la kuhakikisha kwamba askari wetu wanapata vitendea kazi vya kisasa na vilivyo bora ikiwemo: vyombo vya usafiri, mifumo na miradi mbalimbali ya TEHAMA ya kuweza kurahisisha utekelezaji kazi wa majukumu yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hayo ni miongoni mwa mambo ambayo Waheshimiwa Wabunge wameyagusia na ni mambo hayo hayo ambayo Mheshimiwa Rais amekuwa akiyapigania na akituelekeza tuyasimamie. Ushahidi wa hayo ni pale ambapo Mheshimiwa Rais alipoamua kwa makusudi kuunda Tume ya Haki Jinai. Baada ya kuunda Tume ya Haki jinai ambayo imetoa mapendekezo ya kukabiliana na changamoto hizi zote zilizoelezwa hapa Bungeni na nyinginezo ambazo nitapata nafasi ya kuzifafanua, kuna mambo ambayo Mheshimiwa Rais ameshaanza kuyafanya kwa vitendo hata kabla Tume hii haijaundwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tokea alivyoingia madarakani siku ya kwanza, jambo la kwanza kubwa Mheshimiwa Rais alilolifanya ni kuhakikisha anaongeza Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kutoka shilingi bilioni 937 kufikia shilingi trilioni 1.2 kwa muda wa mwaka mmoja. Waheshimiwa Wabunge leo ni mashahidi, nimesoma bajeti hapa ikiwa na shilingi trilioni 1.7. Tafsiri yake ni kwamba, Mheshimiwa Rais kwa muda wa miaka mitatu ameitoa Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kutoka shilingi bilioni 937 kuja shilingi trilioni 1.7. Hiyo inadhihirisha ni dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais ya kuona mabadiliko makubwa yanatokea katika Wizara hii hususan Vyombo vyake vya Usalama vilivyopo katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine ambalo ni muhimu sana Waheshimiwa Wabunge wakalikumbuka. Ni kweli bado Waheshimiwa Wabunge wamezungumzia juu ya changamoto ya baadhi ya miradi kutokukamilika au baadhi ya fedha kutokufika kwa wakati. Nikiri kwamba, katika eneo la kuwezesha Vyombo vyetu vya Usalama, Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imejitahidi sana. Mbali na fedha hizi ambazo zimetengwa kwenye bajeti ambazo kwa mfano katika bajeti ya mwaka jana iliyokuwa karibu takribani shilingi trilioni 1.29, mpaka Mwezi wa Aprili, fedha ambayo ilikuwa imetoka ni shilingi 1,000,068,000,000/= ambayo ni sawasawa na 83%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kana kwamba hiyo haitoshi, fedha hii 83% imetoka katika kipindi cha mpaka mwezi Aprili lakini kuna fedha ambayo ni nje ya bajeti ya kiasi cha shilingi bilioni 127, zimetoka nje ya bajeti. Kwa hiyo, kwa kweli mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Serikali ya Awamu ya Sita imejitahidi sana kuviwezesha Vyombo vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika fedha hiyo, zaidi ya shilingi bilioni 51 zimeelekezwa mahususi kwa ajili ya kulipa madeni, madeni ya askari na madeni ya wazabuni. Madeni haya ni ya muda mrefu, lakini kwa mfano katika mwaka huu pekee, Mheshimiwa Rais ametoa shilingi bilioni 15 kupunguza deni la shilingi bilioni 77 la Jeshi la Polisi, katika deni ambalo limehakikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Tume ya Haki Jinai ambayo pamoja na mapendekezo mengine imetoa mapendekezo ya namna gani ambavyo stahiki na haki za Jeshi la Polisi zitakavyoimarishwa, kuboreshwa na kupatia ufumbuzi wa kudumu changamoto ya maslahi ya askari wetu. Nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kazi hiyo inaendelea vizuri. Tume ambayo imepewa kazi ya kufanya uhakiki imeshakamilisha kazi yake na sasa hivi andiko hilo limewasilishwa katika mamlaka husika katika ngazi mbalimbali za Serikali kwa ajili ya kutolewa maoni ili baadaye litolewe uamuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yangu kwamba, malengo haya ya Mheshimiwa Rais ya kuhakikisha anaongeza mishahara, posho, na haki na stahiki za askari wetu lakini hata ile hoja ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikiwagusa Waheshimiwa Wabunge na Mheshimiwa Rais alishaitolea maelekezo, hoja ya kuangalia stahiki zao kwenye upande wa pensheni kwa maana ya kikokotoo na yenyewe inakwenda kupatiwa suluhisho kwenye mchakato huu ambao tunakwenda nao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilizungumza kwamba, mbali na mambo ambayo Tume ya Jinai imefanya lakini kuna mambo ambayo Mheshimiwa Rais ameyatekeleza kupitia bajeti yetu. Kwa mfano katika eneo la upandishaji wa vyeo, katika upandishaji wa vyeo, katika mwaka 2020/2023 watumishi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wa Vyombo vyote 9,397 wamepandishwa vyeo. Mwaka huu tunakwenda kupandisha vyeo watumishi 26,876 kwa bajeti hii ambayo nimetoka kuisoma leo ikiwa Waheshimiwa Wabunge wataipitisha na naamini wataipitisha kwa mambo haya yalivyo makubwa na mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mafunzo; takribani askari 11,000 na watumishi 11,167 wamepata mafunzo katika Mwaka wa Fedha 2023/2024, mwaka huu tunazungumzia zaidi ya 10,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa ajira, ajira 8,542 katika mwaka uliopita, mwaka huu tunazungumzia ajira zaidi ya 4,857. Yote haya yana lengo la kuhakikisha kwamba tunasaidia askari wetu waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine ambalo Waheshimiwa Wabunge wamelizungumzia sana. Wako Wabunge ambao wamelalamika kwamba kuna upungufu wa magari katika majimbo yao. Wako Wabunge ambao wamelalamika katika majimbo yao kuna upungufu wa vituo vya polisi. Wako Wabunge ambao wamelalamika kuna changamoto ya uchakavu wa nyumba na upungufu wa nyumba za askari kwenye majimbo yao.

Mheshimiwa mwenyekiti, naomba niwakumbushe, kupitia bajeti ambayo nimeisoma leo hii kuna kazi kubwa sana imefanyika katika eneo hili. Nikianzia kwa upande wa vyombo vya usafiri peke yake; nilisema hapa leo asubuhi, Jeshi la Polisi limepokea magari, kwanza tumepokea magari 44 aina ya GWM kati ya magari 200. Magari 156 kati ya haya 200 yanatarajiwa kuingia wakati wowote kuanzia sasa hivi. Tunatarajia hata kabla ya mwaka huu haujamalizika tunaweza tukapokea magari hayo 156 ili kutimiza idadi ya magari haya 200.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna shilingi bilioni 72 ambazo Mheshimiwa Rais ameridhia zitoke kwa ajili ya kununua magari mengine. Kati ya fedha hizo, tayari shilingi bilioni 15 tumeshaagiza magari yanayogharimu shilingi bilioni 15 ambayo ni magari 147. Magari haya tunatarajia yaende kwenye ofisi za polisi mikoa na ofisi za wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Makamu wa Rais, juzi wakati tunazindua kituo cha kisasa hapa Dodoma - Mtumba, aliweza kuzindua mchakato wa makabidhiano ya magari kwa ajili ya Ma-OCD. Nawapongeza Waheshimiwa Wabunge ambao wanatoka katika majimbo yale ambayo yana changamoto ya wakulima ambapo tulitumia fursa hiyo kuweza kuwapata magari yale. Yako magari mengine ambayo yameshakwenda katika wilaya na sehemu ya magari machache ambayo yamebakia yatakwenda kumaliza wilaya zote na hivyo Waheshimiwa Wabunge katika wilaya zenu zote Ma-OCD wenu sasa watakuwa na magari ya uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, si hivyo tu, Wabunge wamezungumzia kuhusu changamoto ya mafuta. Maelekezo ya Mheshimiwa Rais aliyoyatoa ni kwamba utaratibu ambao tumeshaanza kuutekeleza wa mafuta kufikia mikoani sasa haupo. Sasa hivi mafuta moja kwa moja yanakwenda kwa Ma-OCD ili magari haya yaweze kutumika vizuri. Kana kwamba hiyo haitoshi, katika Bajeti ya Mwaka 2023/2024, zilitengwa shilingi bilioni 11.6 kwa ajili ya ununuzi wa boti 10 na kazi hiyo ya manunuzi inaendelea vizuri. Boti hizo zitasambazwa katika maeneo mbalimbali yenye changamoto katika bahari pamoja na maziwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zimenunuliwa pikipiki 24, kuna pikipiki ambazo ni kwa ajili ya misafara ya viongozi, kuna pikipiki ambazo zinakwenda kwenye kata. Nitalizungumzia hili baadaye nitakapozungumza mkakati wa Polisi Jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, jumla ya shilingi bilioni 36 ambazo zitanunua magari mengine 181 zimeshatengwa pamoja na shilingi bilioni 118 kwa ajili ya kununua vifaa mbalimbali vya kijeshi. Shilingi bilioni 40.5 kwa ajili ya kununua mifumo mbalimbali ya TEHAMA ikiwemo redio za masafa mafupi na masafa marefu. Kwa kweli mambo ni mengi sana ambayo yamefanyika katika kuhakikisha kwamba tunaimarisha vyombo vyetu vya usalama katika nyanja zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande makazi, Jeshi la Polisi limekamilisha miradi 15 ya ujenzi. Ni kweli ninatambua kuna maeneo Waheshimiwa Wabunge wamezungumzia hapa, kwamba maeneo yao yana changamoto ya makazi. Ninataka niwahakikishie kwamba, kwa yale maeneo ambayo mmezungumzia bado kuna changamoto ya vituo vya polisi ambayo mmezungumza leo katika hili Bunge, bajeti ya matumizi ya Mfuko wa Tuzo na Tozo kwa mwaka ujao hatujaikamilisha. Nawahakikishia kwamba tutachukua na tutaingiza katika bajeti ijayo. Ni kweli ni maeneo ambayo ni ya msingi na tutayaangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kama nilivyosema mwanzo kwamba, tumekuja na mkakati kabambe wa kuimarisha ulinzi katika ngazi za chini. Imani yetu ni kwamba, tukiimarisha ulinzi katika ngazi ya kata itasaidia sana kupunguza changamoto ya uhalifu. Kwa sababu, kwenye kata ndiyo wahalifu wote wanaanzia kuishi lakini kwenye kata ndiyo kwenye taarifa zote za uhalifu. Ndiyo maana tukaja na mpango kabambe wa kupeleka askari kata, tena askari hawa wenye elimu ya chuo kikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hiyo ya kuendelea kusambaza askari hawa inaendelea lakini hata upelekaji wa vyombo vya usafiri, tumepata fedha tayari kwa ajili ya kununua pikipiki kama nilivyoeleza, zitakazokwenda katika kata. Najua safari hii ni ndefu, lakini safari ni hatua, tumeshaanza na naamini kabisa tutafika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, tumeamua kuja na mkakati wa ujenzi wa vituo vya polisi katika kata. Nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa maelekezo yake aliyoyatoa alipokuja kwenye shughuli ya Jeshi la Polisi. Alitutaka mimi na Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI tukae pamoja na kuangalia uwezekano wa kuzishirikisha halmashauri zetu katika kujenga vituo vya polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI pamoja na timu yake yote. Tulikaa tukakubaliana na Mheshimiwa Rais kama nilivyoeleza katika hotuba yangu kwamba tumeanza mkakati mwaka huu. Tutaanza mkakati wa ujenzi wa Polisi Kata kupitia halmashauri zetu. Hivyo, Waheshimiwa Wabunge niliwaahidi hapa mwaka jana na niliwahamasisha kwamba waanze kujenga vituo vya polisi katika maeneo yenu na sisi tutavimaliza. Katika mkakati huu wa TAMISEMI, vituo vyote ambavyo Waheshimiwa Wabunge mmeshiriki pamoja na wananchi katika kupeleka nguvu zenu ndivyo ambavyo tutaanza navyo. Karibu vituo vya polisi 77 tunaanza navyo katika mwaka huu wa fedha, lakini tutajenga vituo vingine vya polisi 12 vya ngazi ya kata kupitia utaratibu huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Mfuko wa Tuzo na Tozo ambapo kupitia maboresho ambayo tunaendelea nayo kupitia Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi, tunatarajia kujenga vituo vya ziada vya kata ili kuweza kuchangia jitihada za kazi nzuri ambayo itafanywa na halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawahakikishia Waheshimiwa Wabunge, wale ambao wataamua kuhamasika tena safari hii kuanza ujenzi wa vituo kata katika majimbo yao niwaahidi kwamba, mara ambapo tutakuwa tunaanza awamu ya pili ama awamu ya tatu ya ujenzi wa vituo hivi, aidha kupitia kwa utaratibu wa halmashauri ama utaratibu wa Mfuko wa Tuzo na Tozo kupitia Shirika la Uzalishaji la Jeshi la Polisi tutawapa kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo Waheshimiwa Wabunge walilizungumza ni hoja ya kuimarisha utendaji kazi ama kulifanya Jeshi la Polisi liwe la kisasa. Nataka nichukue fursa hii kulipongeza sana Jeshi la Polisi, Jeshi la Polisi limeanza kutumia mifumo katika kufanikisha azma hii, katika lengo hilo matumizi ya mifumo yameshaanzishwa, zaidi ya mifumo 22 sasa hivi ya Jeshi la Polisi inaitumia kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake mbalimbali ikiwemo katika maeneo ya haki jinai, katika usalama barabarani, masuala ya utawala, mfumo wa manunuzi ya umma, mfumo wa ukusanyaji wa madeni na hata mifumo mingine mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kulipongeza sana Jeshi la Polisi kwa kuimarisha uwezo wa askari wetu katika kufanya majukumu haya. Mifumo hii imesimamiwa na kutayarishwa na Askari Polisi wenyewe. Mifumo hii inakwenda kusaidia sana, nitoe mfano wa mfumo mmoja ambao umeweza kusaidia sana kutatua changamoto ama malalamiko yaliyokuwa yakilalamikiwa kwa muda mrefu kwenye vituo vyetu vya polisi, mfumo ambao unaitwa case file information system. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi mfumo huu ambao umeandaliwa na wataalam wetu wa ndani ya Jeshi la Polisi unasaidia kuhakikisha kwamba mtu yeyote ambaye anakwenda kuhudumiwa katika Jeshi la Polisi taarifa ambazo anazitoa zinasomeka katika vyombo vyote wa kijinai, ikiwemo Ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka, Mahakamani na kadhalika ili kuepusha malalamiko ya muda mrefu ya wananchi kubambikiwa kesi, wananchi kutozwa rushwa na mengineyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi mfumo huu umefungwa katika maeneo vituo 23, lakini lengo letu ni kuhakikisha kwamba mfumo huu unasambaa maeneo yote ya nchi nzima. Ni imani yetu kwamba katika mwaka huu wa fedha tutafanya kila jitihada kuhakikisha kwamba mfumo huu unaendelea kusogea katika maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mfumo mwingine ambao kuna malalamiko ya Waheshimiwa Wabunge kuhusiana na changamoto ya rushwa kwa Askari wetu wa Barabarani, wakati huo walipokuwa wakipokea tozo na faini za barabarani kwa njia ambazo zilikuwa siyo za kisasa. Kupitia mfumo wa TMS sasa hivi kumekuwa na udhibiti mkubwa sana wa maduhuri ya Serikali, ingawa siyo lengo hilo, lakini imesaidia kupunguza malalamiko ya wananchi katika eneo hili la rushwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka nilizungumze ni hoja ambayo imeibuka ama imeibuliwa na Mheshimiwa Mbunge wa Konde. Niliona hoja hii isingekuwa sawa kuiacha bila kuzungumza. Mheshimiwa Mbunge wa Konde amezungumzia hoja mbili, moja ni hoja ya suala la uhalifu wa mtandaoni na akagusia kuihusisha hoja hiyo na masuala ya ubaguzi. Hoja ya pili alizungumzia suala la passport, nadhani hili ilitoka kama taarifa lakini akaendelea kusisitiza mtazamo wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwahakikishie kwamba Jeshi la Polisi litaendelea kuhakikisha kwamba linasimamia sheria na sheria ni msumeno na hakuna mtu ambaye yupo juu ya sheria. Matendo yote ambayo yanafanyika kupitia mitandao, ni kweli uhalifu wa mitandaoni ni masuala ambayo yamekuja kutokana na kasi ya utanuzi wa teknolojia, hivyo inahitaji tufanye kila jitihada kuhakikisha kwamba tunawezesha Askari wetu ama Jeshi la Polisi kuweza kukabiliana na aina hiyo mpya ya uhalifu na kazi hiyo inafanyika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafanya kuhakikisha kwamba tunajenga uwezo kwa askari wetu ili kuweza kuwa na uweledi katika kukabiliana na matatizo ya uhalifu wa mitandao, pia tunafanya jitihada kuhakikisha kwamba tunawasaidia na kuwawezesha Askari kuwa na vifaa vya kisasa kukabiliana na changamoto hizo. Nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba sheria zote zinazohusu uhalifu wa mtandaoni ikiwemo Cyber Crime Act na nyenginezo ni sheria ambazo zimetungwa na Bunge hili Tukufu na tutaendelea kuzisimamia. Hivyo mtu yeyote ambaye anakiuka sheria hizo Jeshi la Polisi linaendelea kuchukua hatua mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyozungumza hatua zinaendelea kuchukuliwa, kwa hiyo hakuna mtu ambaye atavunja sheria hizi akadhani kwamba tutamfumbia macho. Niendelee kutoa tahadhari kwa wananchi, iwe wa ndani ya nchi ama nje ya nchi kuhakikisha wanaendelea kutii sheria za nchi vinginevyo sheria itachukua mkondo wake, inawezekana isiwe leo lakini ikawa kesho, kwa kadri ambavyo hali ya upelelezi itakavyokamilika sheria itachukua mkondo wake, hivyo nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba asidhani kwamba Jeshi la Polisi linafumbia macho aina yoyote ya uvunjifu wa sheria za mitandao ambazo zipo wazi kabisa kwenye sheria hizo zilizoainishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya passport ambayo ameizungumza, kwanza lazima Mheshimiwa Mbunge na wananchi wafahamu kwamba passport ni identity ya nchi na ni mali ya wananchi, passport inaku-identify wewe kama ni raia wa nchi gani na passport hii nimezungumza ni ya wananchi na wananchi wana haki kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 17(1) inatoa uhuru wa mwananchi kwenda anapotaka. Kwa hiyo, raia yeyote wa Tanzania alipo popote ana haki ya kwenda anapotaka na ndiyo maana passport hatuitumii kwa ajili ya matembezi au mizunguko ya ndani ya nchi kwa sababu ni identity ambayo ni ya Taifa inayoitambulisha nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unapotoa hoja kwamba zamani kulikuwa kuna passport tuirudishe, nadhani ni kukosa uelewa, hakujawahi kuwa na passport. Kilichokuwepo ni matumizi ya hati maalum kwa ajili ya masuala ya usalama na hati hizo mpaka leo zinatumika, tofauti ni mabadiliko ya wakati tu. Kwa mfano, leo ukitaka kusafiri kwenda kutoka Zanzibar kuja Dar es salaam au kutoka Zanzibar kwenda Dar es Salaam au kutoka hata Mkoa mmoja kwenda mwingine unavyoenda kukata tiketi utaambiwa utoe kadi yako NIDA haina maana kwamba ile ni passport, ile ni identity ya kiusalama. Kwa hiyo nataka hii ieleweke kwamba siyo sawa kuhamasisha au kujenga taswira katika jamii miongoni mwa Watanzania ndani ya nchi moja, kwamba kuna matumizi ya passport na mipaka baina ya sehemu moja na sehemu nyingine, Tanzania ni nchi moja na Watanzania ni wamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo limezungumzwa ilikuwa ni hoja ya udhibiti wa taasisi za kidini ambazo zinakiuka sheria. Ni kweli kuna taasisi ambazo aidha zinakiuka sheria ambazo hazijasajiliwa rasmi ambalo ni kosa kisheria, lakini kuna taasisi ambazo zimesajiliwa lakini zinakiuka sheria. Tumeshaanza kuchukua hatua, tumeanza uhakiki wa kuchukua hatua kwa zile taasisi zote ambazo zinatekeleza majukumu yao kinyume na Katiba zilizosajiliwa, mbali na kuchukua hatu kupitia Ofisi ya Msajili tunaendelea kutoa elimu kupitia semina na mafunzo mbalimbali kwa Watendaji wa Serikali katika ngazi za Mikoa, Wilaya, Kata na Mitaa juu ya umuhimu wa kufuatilia kwa karibu mienendo ya jumuiya za kiraia zilizopo kwenye maeneo yao na kubainisha taarifa kwa ofisi za Msajili wa Jumuiya juu ya tabia na mienendo hatarishi ya jumuiya zilizopo nchini ili hatua stahiki ziweze kuchukulia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inaendelea kufanya mapitio ya Sheria ya Jumuiya, Sura Namba 337, kwa lengo la kuboresha muundo wa ofisi ya msajili, kwa lengo la kuongeza tija na ufanisi wa ofisi hii katika kufuatilia na kusimami mienendo na uendeshaji wa jumuiya za kiraia katika ngazi za wilaya ili kudumisha amani na utulivu nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inaendelea na taratibu za kuandaa mwongozo wa usajili na usimamizi wa jumuiya za kiraia nchini unaobainisha nafasi na wajibu wa Wizara, Taasisi na Mashirika ya Umma pamoja na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika utekelezaji wa jukumu la usajili na usimamizi wa jumuiya hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, mwongozo huo pamoja na mambo mengine unabainisha mambo ya msingi yanayopaswa kuzingatiwa na ofisi za Wakuu wa Mikoa pamoja na Wakuu wa Wilaya katika utekelezaji wa jukumu hilo ikiwemo kuwa na ajenda ya kudumu kwenye Kamati za Usalama za Wilaya pamoja na Mikoa kuhusu tabia, mienendo na uendeshaji wa jumuiya za kiraia zilizopo kwenye maeneo yao na zile zinazoomba usajili kwa lengo la kudumisha amani, utulivu na usalama wa Taifa letu. Mwongozo huu unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa robo ya mwaka 2024/2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambazo Waheshimiwa Wabunge walizizungumzia ilikuwa ni hoja inayohusu Idara yetu ya Uhamiaji. Serikali inaendelee kuliwezesha Jeshi la Uhamiaji kupata vyombo vya usafiri ili kuwabaini wahamiaji wasiyo na vibali na kuchukuliwa hatua. Tumezungumzia katika Jeshi la Magereza na Jeshi la Zimamoto, Mheshimiwa Naibu Waziri amezungumzia kwa kina kabisa jinsi ambavyo Serikali ilijipanga katika kuhakikisha inawezesha vyombo vyetu hivyo kwenye eneo la usafiri na mimi nilizungumzia kwenye Jeshi la Polisi. Hata kwa upande wa Uhamiaji, Serikali imetenga shilingi bilioni 3.3 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ili kuwezesha Idara ya Uhamiaji kupata magari 18 ikiwa ni mkakati wa kuimarisha udhibiti wa wahamiaji haramu nchini na kuwachukulia hatua stahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaona kwamba hakuna chombo ambacho kimeachwa, Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto, Jeshi la Uokoaji kuna uwekezaji mkubwa ambao unaendelea kufanyika katika maeneo yote ikiwemo maeneo ya vyombo vya usafiri katika kusaidia utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi kupitia vyombo hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine ambalo limezungumzwa kuhusu Idara ya Uhamiaji, kwamba Serikali iendelee na mkakati wa kuliwezesha Jeshi la Uhamiaji kufunga mfumo wa uhamiaji mtandao katika ofisi zote za uhamiaji zisizo na mfumo huo sambamba na mfumo wa udhibiti wa mipaka kwenye ofisi za baadhi ya vituo vya kuingia nchini. Mkakati wa kuboresha mfumo wa Uhamiaji mtandao katika ofisi ambazo hazina mfumo umezingatiwa katika bajeti ya mwaka 2024/2025, ambapo Serikali imetenga shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya uhamiaji mtandao ili kuendelea kujenga mtandao huo katika vituo ambavyo havijafungwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo inahusu Idara ya Uhamiaji ni hoja ambayo inahusu mkakati wa kudhibiti mianya ama njia zisizo rasmi zaidi ya 1,000 katika Mikoa mbalimbali ya mipakani, ikiwemo kutumia mifumo ya udhibiti wa mipakani (E-border) kufanya hivi kwani itakuwa ni sehemu ya udhibiti wa uingiaji na utokaji wa wahamiaji haramu pamoja na bidhaa za magendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha kuwa Idara ya Uhamiaji inaendelea kudhibiti njia zisizo rasmi zinazotumiwa na wahamiaji haramu, tumefanya ufuatiliaji na kubaini njia zisizo rasmi 1,029, kazi inayoendelea hivi sasa ni kufanya uchambuzi ili kuamua maeneo gani yanaweza kuanzishwa vituo rasmi vya kuingia na kutoka nchini na kufungwa mifumo ya udhibiti wa mipaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni jitihada za kudhibiti njia zisizo rasmi za Idara ya Uhamiaji imepata kibali cha kuajiri askari wapya 400. Nilizungumzia pale idadi ya ujumla wake ya askari wote walioajiriwa katika vyombo vyote lakini kwa upande wa Uhamiaji kwa mwaka huu tunatarajia kuajiri askari 400, askari hawa watakapomaliza mafunzo yao wataweza kutawanywa katika sehemu mbalimbali ikiwemo katika maeneo ya mipaka pamoja na kwenye Kikosi cha Uhamiaji Wanamaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kwenye Uhamiaji ilikuwa ni hoja ya uboreshaji wa Jeshi la Uhamiaji katika matumizi ya vifaa na vitendeakazi, kwamba uendane na kutoa mafunzo ya askari ili waweze kutumia vifaa na vitendea kazi hivyo kwa ufanisi na kupata tija iliyokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Uhamiaji limeendelea kutoa mafunzo kwa Maafisa na Askari ili waendane na matumizi ya vifaa na vitendeakazi wanavyovitumia katika utoaji wa huduma ambapo kwa mwaka 2023/2024, jumla ya Maafisa na Askari 432 walipatiwa mafunzo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijamalizia hoja yangu naomba nichukue nafasi hii kusisitiza katika eneo moja ambalo Waheshimiwa Wabunge wamelizungumzia sana. Nichukue nafasi hii kwanza kuendelea kuwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge kwa kuendelea kutupa moyo Wizara yetu kwa yale ambayo tunayasimamia na mambo ambayo Waheshimiwa Wabunge wameyazungumza ama yale ambayo tumewasilisha katika taarifa yetu wameendelea kuyaunga mkono, tunawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mambo makubwa ambayo yanakwenda kuleta mabadiliko makubwa sana ya utendaji kazi katika vyombo vyetu vya usalama, hususan Jeshi la Polisi ambapo Waheshimiwa Wabunge wameyazungumzia kwa umahiri mkubwa ni eneo la matumizi, naomba hili nimalizie kwa kulisisitiza niligusia, lakini naomba nimalizie kwa kusisitiza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la matumizi ya TEHAMA na wapo ambao walifikia kulilaumu Jeshi la Polisi juu ya namna ambavyo wanashindwa kudhibiti changamoto ya bodaboda na wakajaribu kutoa mfano na baadhi ya nchi ambazo pengine kuna nidhamu ya bodaboda. Nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, mifano ya nchi ambazo mmetoa na hata zile ambazo hamjatoa zenye utiifu wa sheria kwa watumizi wa vyombo vya usalama barabarani wakiwemo bodaboda zimeshaanza matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika kudhibiti hali hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimeeleza kwenye bajeti kwenye miradi ya kimkakati kuna miradi mikubwa kadhaa ambayo tunaona inakwenda kuleta mabadiliko makubwa katika Jeshi la Polisi. Moja katika miradi ambayo nimeizungumza ni mradi wa Miji Salama, mradi huu utahusisha ufungaji wa camera 6,500 kwa kuanza na Majiji manne. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba miradi hii ikiwemo mradi wa highway road patrol ambao unakwenda kuweka mifumo ya kisasa kwenye barabara kuu, inakwenda kutatua chanagmoto ya uvunjifu wa sheria za usalama barabarani, lakini inakwenda kusaidia kupunguza ajali na kubwa zaidi inakwenda kusaidia kuimarisha usalama na kuwasaidia askari wetu kuweza kufanya kazi kwa weledi zaidi. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa kutuelewa na kutuunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa bado dakika zangu zimebakia nitaomba pia nisisitize mambo mengine ya muhimu machache sana. Moja katika jambo ambalo nimeomba nisisitize sana japokuwa Mheshimiwa Naibu Waziri ameligusia kidogo ni mapinduzi makubwa ambayo tunakwenda kufanya kwenye Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mmeshuhudia hivi juzi tulimwakilisha Mheshimiwa Rais, katika kukabidhi magari 12 mapya ya kisasa ya zimamoto. Waheshimiwa Wabunge, wamekuwa wakilalamika sana kuhusu changamoto hii. Nilimsikia Mheshimiwa Martha, Mbunge wa Viti Maalum Katavi, akizungumzia juu ya changamoto ya gari la Zimamoto katika Mkoa wa Katavi, anasema kuna gari moja lipo Airport inakuwaje, leo moto ukitokea na huku ndege inatua, kwa kweli ni changamoto kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuchukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Amiri Jeshi Mkuu kwa kufanya mapinduzi makubwa sana kwenye Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, ambayo hayajawahi kufanyika katika historia ya nchi hii. Tunazungumzia ununuzi wa magari 150, boti 23, helikopta moja na vifaa vingine mbalimbali vya kuzima moto. Haya mambo ni mambo makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yangu vifaa hivi vitakapokuwa vinawasili na nimshukuru sana ndugu yangu Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kuweza kusaidia kufanikisha upatikanaji wa mkopo huu. Mwaka wa Fedha 2024/2025, tutaanza kupokea magari haya ya ziada, mwaka 2025/2026 tunamalizia awamu ya mwisho ya upokeaji wa vifaa na magari haya ya kisasa. Mara yatakapowasili mikoa yote na wilaya takribani nyingi zitaweza kupata vifaa vya kisasa. Jitihada zinaendelea kuhakikisha kwanza tunaongeza idadi ya askari wa kuzima moto lakini pia, tunawajengea uwezo ili waweze kutumia vifaa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, tumeanzisha mkakati kabambe wa kuhamasisha watu binafsi kujitolea kushiriki katika shughuli mbalimbali za uokozi na uzimaji moto kama nilivyoeleza katika Hotuba yangu. Niipongeze mikoa ambayo tayari imeshaanza kutekeleza wito huo na ni imani yangu kwamba, mikoa mingine itaendelea kutuunga mkono.

MWENYEKITI: Mheshimiwa, hitimisha kwa kuomba hela.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nishukuru sana kwa mara nyingine tena Waheshimiwa Wabunge, kwa michango yao na kama ambavyo nimewaahidi kwamba, yale ambayo hatujapata nafasi ya kuyafafanua, basi tutaweza kuyafanyia kazi na kuyawasilisha kwa maandishi. Ahsanteni sana kwa kunisikiliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa hatujakusikia. Hiyo hoja haijasikika, hebu rudia.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.

MWENYEKITI: Hoja imeungwa mkono. Mheshimiwa Waziri, nasikia hujaomba hela. Nilikuwa nimesema omba hela. Kwa hiyo, tukamilishe kwa kuomba hela. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa Bunge lako Tukufu liridhie shilingi 1,711,710,987,000 ambazo kati ya fedha hizo, shilingi 551,583,381,000 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo na shilingi 870,429,138,000 kwa mishahara na shilingi 289,698,464,000 ni fedha za miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.