Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Musoma Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Hii bajeti ya Viwanda na Biashara, Waheshimiwa Wabunge, naomba tuipitishe japokuwa ni ndogo. Kwa kuwa, ndiyo tunaendelea kujenga viwanda tuipitishe, lakini ni ndogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naanza kwa maombi kutoka Mkoa wa Mara. Kuanzia miaka ya 60 mpaka 90 Mkoa wa Mara tulikuwa na viwanda, lakini kwa sasa hatuna kiwanda hata kimoja. Kwa hiyo, ombi namba moja ni kama tuko kwenye mapinduzi ya viwanda mahali pa kuweka viwanda ni Mkoa wa Mara. Kwani ni wakulima bingwa wa pamba, tunaomba ginneries zetu tatu zifanye kazi. Tunaomba kiwanda kipya cha nguo, hakuna masuala ya kufufua MUTEX. Machines za MUTEX ni za zamani sana, hazina hata vipuri duniani hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi ni wavuvi mashuhuri. Kwa sasa hivi hatuna kiwanda hata kimoja cha samaki, kilichopo kinafanya kazi chini ya 15% kwa hiyo, tunaomba angalau viwanda vitatu vya samaki. Sisi ni wafugaji bingwa, tulikuwa na viwanda viwili vya maziwa, lakini sasa havipo. Kwa hiyo, Mkoa wa Mara tunaomba viwanda vipya vya maziwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Tarime tunalima Kahawa. Tunaomba vile viwanda vya Kahawa vipewe fursa ya kupanuka zaidi. Haya ninayaomba najua siyo ya Wizara ya Viwanda, lakini tunaomba Wizara ya Viwanda ishirikiane na Wizara nyingine, angalau Mkoa wa mara turudi kuwa na viwanda visivyopungua 10. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa baada ya hilo la jimboni na Mkoani kwangu, mimi leo naomba niongelee Liganga na Mchuchuma. Nadhani nipo kwenye nafasi nzuri kuliongelea hilo na unajua hiki kitu ni nyeti, kwa hiyo, nikifika mwisho huko uongeze muda tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba ile Liganga na Mchuchuma niwarejeshe nyuma; imekuwepo enzi ya utawala wa Mjerumani na Muingereza. Kazi muhimu zilizofanyika mwaka 1928 mpaka 1948 tukiwa na Geological Survey Department ya Muingereza ndio walienda huko Liganga wakafanya mapping. Ripoti zao zipo kwenye archives za Geological Survey ya Uingereza, Nottingham.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mwaka 1952 Kampuni ya Canada ilifanya airborne survey magnetic. Mwaka 1956 mpaka 1957 kampuni kubwa za Australia, Reo Tinto na BHP, ambazo bado ndiyo kampuni kubwa kweli kweli duniani za kuchimba chuma, zilienda Liganga. Tunavyoongea sasa hivi ni lazima tuisaidie hii Wizara, huu mgodi una historia ndefu sana, msije mkawahukumu hawa labda hawahusiki, ni sisi wote, tuache ya nyuma tusonge mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaanza 2011 wakati NDC ilipoingia ubia na kampuni ya Wachina. Sasa Liganga yenyewe na watakaoenda kufanya majadiliano na uwekezaji wa Liganga. Liganga kitaalam ni kwamba, kuna madini zaidi ya hicho chuma, lakini kwa wepesi utakuwa unaongelea chuma cha Liganga.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kitaalamu tunasema ni polymetallic, yaani una metals zaidi ya moja; kuna chuma, kuna titanium, kuna vanadium, kuna chromium, halafu madogo kama aluminium pia, yapo. Kwa hiyo, unavyoenda Liganga usijadili chuma tu, wakati inagundulika watu walikuwa hawapendi vanadium na titanium, ilikuwa haitumiki duniani. Kwa hiyo, watu walisema sisi tuna chuma Liganga, lakini tatizo kinachafuliwa na titanium na vanadium.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi titanium na vanadium ndiyo madini ambayo ni muhimu zaidi kuliko hicho chuma. Kwa hiyo, deposit yetu sijui mashapo, Kiswahili ni nini? Watu wa Kiswahili, deposit?
Mheshimiwa Naibu Spika, deposit yetu ya Liganga mpaka sasa hivi inajulikana tuna tani milioni 129. Sasa, Mchuchuma kwenye makaa ya mawe deposit yetu ni tani milioni 422. Makaa ya Mchuchuma (coal) yanavuka viwango vyote vya kuzalisha umeme kwa sababu, ya kwetu ni ya katikati yanaitwa bituminous coal. Ni ya hapo katikati, haiko chini haipo juu sana, lakini vigezo vitatu vya ash content, carbon content na calorific value, vyote Mchumchuma anafaulu hapo, kwa hiyo, tunaweza kuzalisha umeme Mchuchuma. Sasa tukitaka kuongelea Liganga na Mchuchuma ni lazima tuangalie hali ya chuma duniani ipoje? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, reserve kubwa ya chuma duniani ipo Australia wana tani bilioni 51, Brazil ni ya pili ina tani bilioni 34 na huyu Mchina ambaye ndio partner wetu sasa hivi yeye ana reserve ya tani bilioni 20. Sisi ya Mchuchuma mpaka sasa hivi tuna tani milioni 129, huenda tukiendelea, labda tunayo nyingi. Sasa duniani demand ya chuma ni kiasi gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2023 biashara ya chuma ilikuwa kwenye around 1.6 billion tones na market yake ilikuwa ni dola bilioni 350. Wazalishaji wakubwa wa chuma, hawa ni lazima tuwaangalie, ndiyo tunashindana na Liganga. Kuna wakubwa watano ambao wanazalisha 80% ya chuma chote duniani, hawa ni Australia, Brazil, China, India na Russia. Mtumiaji mkubwa ni huyu huyu partner wetu, China, ndiyo anatumia chuma kingi kuliko wote duniani. Mwaka 2023 ametumia chuma chenye thamani ya dola milioni 134.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimewaambia kuna madini zaidi ya chuma, kuna titanium. Watanzania tukienda kujadili na wenzetu wa China tusiongee tu chuma (iron ore), tuongee na titanium. Titanium ndio inatumika kwenye engine zote za ndege mnazoziona, ni kitu muhimu kweli kweli. Hata wale wanaocheza gofu vile vichuma vyote ni titanium, ina matumizi makubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa duniani titanium inazalishwa, wakubwa ni wawili tu, Australia na South Africa, biashara hiyo ipo kwenye tani milioni sita. China, ambaye ni partner wetu, yeye ndio ana 30% ya reserve kubwa ya titanium duniani. Pia, msisahau kuwa tutaweza kupata titanium, Kenya wanasafirisha titanium. Kama unaenda Mombasa, pale beach ni sawa sawa na sisi tulivyotoa leseni kule Tanga, nadhani na wao watatoa titanium.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa vanadium yenyewe tunayo ambayo demand yake duniani. Kufikia mwaka 2030 itahitajika ya bilioni nne. Sasa nimalizie kwa NDC na China ambapo tunaanza kujadili NDC wana 20%. Kampuni ya China, partner wetu ina 80%, lakini kwenye migodi yote ya chuma duniani China kwenye provinces zake tano ana migodi 114.
Mheshimiwa Naibu Spika, huyu China na huyu mwenye kampuni ambaye wanashirikiana sasa hivi na NDC na kuna mwingine anayekuja anatoka province ya Sichuan. Sichuan ni moja katika province tano za China zenye migodi mikubwa. Mgodi mmoja wa Sichuan wa huyo ambapo tuna mbia wetu, anazalisha tani milioni 6.3. Kwa hiyo, joint venture yetu na hii ya Sichuan inasema itazalisha chuma tani milioni 2.9 ambayo wakii-process watatoa tani milioni moja kwa ajili ya steel na wanataka kuchimba makaa ya mawe tani milioni tatu kwa mwaka na kwa kuwa tuna tani milioni 428, hiyo chuma inatosha kwa zaidi ya miaka mia moja na kitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pendekezo langu naishauri Serikali iongeze kasi na hii kampuni ambayo sasa hivi tunayo ubia lakini imetafuta mbia mwingine Sichuan. Huyu mbia mwingine ni wa Serikali ya Province ya Sichuan.
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, Wachina ni wakubwa sana kiuchumi. Hili jimbo peke yake tunaloshirikiana nalo, GDP yake ni ya bilioni 800, sasa ukichukua GDP ya South Africa ambayo ndiyo kubwa ya bilioni 380 inaingia zaidi ya mara tatu mara nne. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ili Tanzania tufanikiwe na naomba hili siyo la Waziri lakini la nchi, ni lazima tuwe na wataalamu. Sasa hivi wataalamu wa makaa ya mawe (coal experts) ni wachache mno hawavuki watatu wanne; halafu metallurgist (wanaoshughulika sasa na hizo metals tunazozisema) ninadhani nchini hawavuki wawili. Kama wapo, mimi siwafahamu lakini wengi walikuwa wanafunzi wangu ningewafahamu... (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Profesa kengele ya pili hiyo.
MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, haya namalizia. Ni kwamba ninaomba Serikali ya Tanzania ishawishi Serikali ya China iweze kushawishi hizo kampuni ambazo zina ubia na NDC waongeze kasi ya uwekezaji, ahsante sana. (Makofi)