Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vunjo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa fursa. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu wake na uongozi mzima wa Wizara kwa yote yale ambayo wametekeleza katika mwaka huu. Ninaamini kwamba wataendelea kufanya kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza sana kwa kusema kwamba anakutana na wafanyabiashara binafsi na kujaribu kutatua kero zao. Mimi ningeomba kwamba akutane na wazalishaji binafsi wazawa waliozaliwa hapa Tanzania, weupe au weusi. Azungumze nao ajue kero zao ili aweze kujenga mazingira wezeshi kwa uwekezaji katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimekutana na wachache. Juzi nilipokuwa Arusha nimekutana na wachache na wanasema, kusema kweli Mtanzania mzawa kuanza biashara au uzalishaji wowote hapa inakuwa shida sana. Akiingia kwenye ofisi yoyote ya mamlaka au taasisi ya Serikali, wanamwangalia kama vile huyu mtu amekuja kuomba pesa. Kumbe amekuja kujaribu kupata leseni au kufanya malipo ili aweze kuendeleza biashara yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wanalalamika wanasema kwamba kwa mfano, Mheshimiwa Rais aliweka ukomo wa TRA kwa mfano kukagua au kutathmini hesabu za kampuni ili kuona kama vile walilipa kodi yao sawasawa lakini inakuwa ule ukomo waliouweka wa miaka mitatu, watu wanaingiza mbinu ya tathmini (Investigative Audit) ya tax. Kwa hiyo, unaweza ukakuta hata miaka 20 ule ukomo haufanyi kazi, halafu ule ukomo wenyewe haujawekwa kwenye Waraka ambao unakuwa unatekelezeka kwa watu wa TRA. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tungeomba kwamba Waziri wa Viwanda na Biashara ambaye kazi yake na jukumu lake kubwa ni kuweka mazingira wezeshi, aone basi kwamba kila agizo lililotolewa na mamlaka au kila kilicho kwenye sheria kinatekelezeka kwa maslahi ya wawekezaji ili watu waweze kuwekeza kwa amani na wakijua kwamba hawatafuatiliwa ovyo ovyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, kuna tatizo hilo hilo linaweza likaendeleza mambo ya TRA kukagua akaunti za watu kwenye benki. Wanatuma Agency Notices kwamba huyu mtu hajalipa kodi kwa hiyo kama atapata malipo yoyote kwenye akaunti yake hayo malipo yaende moja kwa moja TRA. Haya mambo ni yale ambayo yalikuwa yameisha na mnaamini katika agizo la Mheshimiwa Rais kwamba wasibugudhi wafanyabiashara na wazalishaji hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mojawapo ni hilo kwamba, siyo kutoa Agency Notices ambazo zinawapa watu shida sana katika kufuatilia na pia kutokuwa na amani katika uzalishaji wao. Ninaamini kwenye hilo Mheshimiwa Waziri atazungumza na Mheshimiwa Waziri wa Fedha ili waweze kutatua. Kuna tatizo ulisema kwamba kuna kero 300 zimetolewa, wanatangaza hapa Bungeni, lakini hata mimi ukiniambia hizo kero zilizoondolewa ni shida sana kuziona zimekuwa published kwenye gazeti ili wale ambao wanafaidika na kero zile waweze kutumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri ahakikishe kwamba kero zilizotolewa na amesema nyingine zimetolewa pia kwa wafanyabiashara wa Kariakoo, basi hizo nazo wajaribu kuziweka bayana ili watu waweze kuzitumia kero hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nichangie zaidi kwenye suala zima la mkakati wa viwanda. Mimi sasa hivi nasema kwamba mkakati huu tunaofuata wa viwanda vikubwa kwenda kuomba viwanda vikubwa wanakuja kuweka assembly plans hapa hatutatusaidia sana. Mkakati utakaotusaidia ni kuhakikisha kwamba tunaenda kwa viwanda vidogo vidogo hata kwenye majumba yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi pale Mikocheni ukienda kwenye nyumba nyingi walizopangisha wageni fulani fulani hapa, wageni wa Taifa fulani fulani, wamekuja kuweka viwanda vidogo vidogo huko ndani wanatengeneza yebo yebo, wanatengeneza kila kitu. Halafu wanapeleka sokoni hawalipi kodi kwa sababu hivyo viwanda havijasajiliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naona kwamba wanaharibu biashara za wengine kwa sababu wameweza kuweka viwanda vidogo vidogo. Vimashine vidogo vidogo wanatengeneza chipsi za ndizi, kila kitu wanatengeneza. Halafu tunasema tunakimbizana na viwanda vikubwa wakati tuna kilimo chetu. Kila kaya au kila kata inaweza ikachakata mazao yake kwa kuwa na viwanda vidogo tu na bei rahisi ambazo tunaweza tukaagiza kutoka nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili suala zima la kusema kwamba SIDO kama TXP wanatengeneza mashine, uongo huo. Ni kiwanda kipi kinatengeneza mashine (injini) hapa Tanzania? Mashine ni injini, siyo kudanganyadanganya hapa. Unapoteza hela nyingi kuvumbua kitu ambacho tayari kipo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda utanunua mashine kwa bei nafuu, zile mashine utazi-deploy kwa kila mtu kwa bei nafuu kabisa. Kwa hiyo, hiyo hela ambayo tutatoa ruzuku kwa mashirika haya tunaweza tukawapa kata, kama ni ndizi wakafanya, kama ni viazi au nini, wakachakata. Ina maana wanaongeza thamani halafu pia wanaweka uwezo wa kuhifadhi yale mazao. Kwa hiyo, tukienda hivi tutakwenda haraka. Hatuwezi kufanya tu, yaani leapfrogging maana yake ni ku-imitate. Una leapfrogging kwa ku-imitate na kuorodhesha ile imitation uliyofanya ili uweze kupata tija zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi naomba SIDO wajiangalie na wajitathmini, liwe ni shirika la kubuni, la kuwezesha kuchukua technology nje kui-customize ili iweze ku-fit scale ya production kwenye maeneo yetu na tuanze mara moja kusambaza na kuuza, tunauza cheap. Unawapa kwa mkopo wataongeza thamani watapata fedha nzuri zaidi watalipa mkopo ule. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii TIB nilikuwa ninasema igeuzwe kuwa ni benki ya starter ili watu waweze kupata mikopo kwa urahisi. Kwa hiyo, mimi naona hiyo itakuwa ni njia mojawapo ya kuongeza kasi ya kujenga uchumi wa viwanda katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kila mwaka tulikuwa tunapewa idadi ya viwanda ambavyo vimeanzishwa ile idadi siku hizi hatupewi tena. Sijui ni kwamba imeisha, siku hizi viwanda havifunguliwi na siku zote tunasema kwamba kila wilaya iwe na specialization. Huo ni mkakati, huu mkakati umefia wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba huo mkakati ufuatiliwe tena ili kwa mantiki hiyo kwamba kila mahali kwenye zao, tuwape watu nyenzo hizo za kuanza viwanda na kuchakata na kuongeza thamani ya hayo mazao yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kwamba huko tunapoenda n` i kuzuri na ukiangalia vipaumbele vya mwaka unaokuja vilivyowekwa na Wizara, vipo vizuri vimekaa bayana lakini naomba basi hiyo kasi ya kutekeleza kwa kushirikiana na kuhakikisha kwamba local content inakuwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiangalia hesabu zote tulizoambiwa hapa za exports za mazao na bidhaa za viwanda hatungeweza kuona uhaba wa dola hapa nchini, lakini ubaya hamwoni kwamba siyo sisi, wanatoa bidhaa kwenye export processing zone wanapeleka nje, pesa inaenda kwenye nchi, kwenye mataifa yale ambayo wale wawekezaji wapo, haiji Tanzania. Kwa hiyo, siyo hela yetu ile, hatutozi kodi, hatufanyi nini licha ya wafanyakazi wetu kufanyishwa kazi na kwenye mazingira magumu sana, lakini ukweli ni kwamba inapokuja ni export tunashangilia, tume-export, lakini hela hiyo ya kigeni iko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukifanya sisi hii kuongeza thamani ya bidhaa zetu za kilimo, tukianzia kile tulichonacho halafu tukapeleka nje, nakwambia thamani ya export zetu itakuwa kubwa na zitakuwa earned na watu wetu hapa na ni lazima kweli kubali kwamba lazima tulinde na tujali masilahi ya wazawa. Wazawa, mimi sisemi wazawa ni weusi na weupe ambao wamekaa wanazaliwa hapa tuwatetee. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha, naunga mkono hoja. (Makofi)