Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Wizara nzima kwa kazi nzuri wanayoifanya. Mkoa wangu wa Morogoro ulikuwa ni Mkoa wa viwanda kwa miaka mingi ya nyuma lakini baadaye viwanda vimekufa, kuna viwanda baadhi ambavyo vinafanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kujua mpango wa kuvifufua viwanda vya Mkoa wa Morogoro ambavyo mpaka sasa hivi havifanyi kazi, hivi viwanda vilikuwa vinaleta ajira kwa vijana pia na wanawake ambao vijana hawana ajira mpaka sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kwa kusisitiza kuhusu Liganga na Mchuchuma. Liganga na Mchuchuma ni miradi ambayo ni ya muda mrefu. Ni miaka mingi ambayo miradi hii ya Liganga na Mchuchuma imeanza. Mheshimiwa Waziri, umeongea vizuri, hotuba yako ni nzuri sana kuhusu mipango ya Liganga na Mchuchuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana na ninasisitiza kuwa mipango aliyoitoa kwenye hotuba yake iweze kutekelezeka, mazungumzo anayoongea pamoja na mwekezaji yaweze kufikia mwisho ili kusudi watu wanaoishi Ludewa, na Watanzania wote waweze kufaidika na Liganga na Mchuchuma. Mkaa uendelee kuchimbwa hasa kuhusu chuma ambacho tunakihitaji sana hapa nchini kwenye miradi mingi ambayo tunaiendeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa hivi tunapoteza fedha nyingi, tunatumia fedha nyingi za kigeni kuagiza chuma kutoka nje na huku tuna chuma chetu ambacho Liganga ingekuwa imemalizika tungeweza kutumia chuma chetu hapa nchini Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kuhusu kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji. Tukiweka mazingira mazuri kwa wawekezaji, wataweza kujenga viwanda vingi vya kila aina. Kwa mfano, kwa kutumia malighafi yetu tunayotumia, kwa upande wa Kilimo tunazalisha sana pamba, tunazalisha mafuta, viwanda vya mbolea, tungeliweza kutumia malighafi yetu ya hapa nchini kwa kuweza kuwawekea sekta binafsi, mazingira mazuri kusudi waweze kuwekeza hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa kupata viwanda vingi vikiwemo vya mbolea, Watanzania wengi waliopo hapa nchini ni wakulima wataweza kupata mbolea ya kutosha ambapo sasa hivi inasemekana bado tuna viwanda viwili tu, lakini Mheshimiwa Waziri, kwa upande wako kwenye viwanda tunaweza tukaongeza viwanda vingine vya mbolea kusudi tuweze kupata kilimo cha kisasa pamoja na mapinduzi ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania tumebahatika, Tanzania tunafanya vitu vingi. Kamati imetembelea viwanda mbalimbali ikiwemo kiwanda cha CAMARTEC, TEMDO pamoja na Tafiti ya TIRDO pamoja na KMTC.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli nakuomba kama hujafika, ufike na wewe. Wanafanya vitu vizuri sana, wanazalisha vitu vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kama Waheshimiwa Wabunge ambao tunavyosema kuwa Serikali isomane, unaweza ukatumia vitu vyetu tunavyozalisha hapa hapa bila ya kuagiza nje. Kwa mfano, ukienda CAMARTEC wanatengeneza matrekta ambayo ni ya bei nafuu kuliko kuagiza matrekta ya nje. Watanzania nimeshasema kuwa wanategemea sana kilimo kwa asilimia 65.5, wanategemea sana kilimo ambapo wangeweza kuelezwa na kununua hizi trekta zinazotengenezwa CAMARTEC na kuzitumia vizuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, CAMARTEC wanatengeneza mashine za kutengeneza majani ya mifugo, wangeliweza hata wafugaji wakanufaika kwa upande huo, wanatengeneza pia mashine za kukamua asali ambazo asali nayo wafugaji wa nyuki wangeweza kufaidika huko huko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye KMTC, KMTC imesimama kwa kweli kwa muda mrefu, kwa miaka zaidi ya 30 lakini sasa hivi nawapongeza sana Mheshimiwa Rais, na Mheshimiwa Waziri. KMTC sasa imefufuka, inazalisha, lakini bado haijafikia hatua kwa sababu hawana wataalam. Naomba sana waongezewe wataalamu na vifaa vingine bado vimechakaa. Naomba sana waongezewe vifaa ili kusudi waweze kuzalisha vipuli pamoja na mashine. Ni kiwanda pekee sana ambacho kinazalisha vipuli, kinaweza kutuendeleza hapa nchini Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye TIRDO, vijana wale wanafurahisha sana, wanafanya utafiti ambao wanaweza kufanya wakazalisha hata nishati. Hata ukiwa hapa Dodoma unaweza ukawasha umeme wako nyumbani kwako Dar es Salaam, unaweza ukawasha umeme wako nyumbani kwako Kigoma. Kwa hiyo, ni vijana ambao ningeliomba waendelezwe kwa sababu ni wagunduzi, na ni watafiti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia TIRDO iweze kupewa hela bajeti zaidi kwa sababu inafanya mambo mazuri ya kumwendeleza Mtanzania hasa kwa upande wa vijana lakini hawana wataalam wenye ujuzi. Napenda Mheshimiwa Waziri, awaangalie waweze kuendeleza wataalam ili waweze kuajiri wataalam wenye ujuzi TIRDO iweze kufanya kazi ambayo imejipangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, TEMDO wanafanya mambo makubwa mno mpaka wanatengeneza majokofu ya miili ya maiti, wanatengeneza viwanda vya sukari ambavyo unaweza ukachukua pale ukaenda ukasimika mahali ukaanza kutengeneza sukari wewe mwenyewe. TEMDO wanafanya kazi nzuri na yenyewe naomba waongezewe fedha kusudi waweze kujiendeleza vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, siku ile nilimshauri Mheshimiwa Waziri wa Afya kuwa tembelea TEMDO, ukitembelea TEMDO utakuta huko labda delivery beds, wanavyo vitanda vile vya hospitalini hata vya kujifungulia akina mama. Kwa hiyo, naomba sana, kama tulivyosema, Serikali ikisomana tunaweza tukaishia hapa Tanzania kutumia na kununua vifaa vyetu tunavyotengeneza hapa nchini bila ya kutumia fedha nyingi kwenda kununua vifaa nje ya nchi kwa kutumia fedha za kigeni. Jambo la muhimu ni kuvitangaza hivi viwanda ambavyo vinafanya kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikitoka hapo naomba niongelee kuhusu lumbesa. Wakulima wanaomba sana, vipimo vipo, kwa hiyo, naomba wapate elimu kusudi tuweze kuondokana na lumbesa. Tukiondokana na lumbesa tutaweza kumfaidisha mkulima kwa sababu anahangaika sana kwenye upande wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijamaliza niongelee masoko. Masoko mengine yamechakaa kwenye Halmashauri zetu, na kwenye Miji yetu. Naomba uwepo mwongozo kwa Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na TAMISEMI waweze kutengeneza haya masoko. Nashukuru kwa Mkoa wangu wa Morogoro tunalo soko moja ambalo ni soko kubwa, ni soko la kisasa, ni soko zuri sana hata hapa Dodoma tuna soko la Ndugai ambalo ni zuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia soko lingine la Mawenzi Mkoani Morogoro, Manispaa ya Mjini naomba liangaliwe, kwa sababu unakuta wafanyabiashara wengi wanakwenda kwenye soko la Mawenzi. Kwa hiyo, ningeliomba Mheshimiwa Waziri kwa sababu na wewe unatembelea sana pale Morogoro uweze kuliangalia soko la Mawenzi kusudi liweze kupewa kipaumbele. Kama ni wewe au unasaidiana pamoja na TAMISEMI kwa kushirikiana, soko la Mawenzi liweze kupewa kipaumbele kusudi liweze kujengwa, liweze kuonekana kwa sababu wanalitumia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, mengi nimeyaongea, yanatosha kwa leo. Nawaomba sana wananchi wote waweze kutumia bidhaa zetu tunazozalisha hapa nchini, TBS inafanya kazi nzuri, kwa hiyo, tusipende bidhaa za nje, tupende bidhaa za hapa. Ahsante sana Mheshimiwa Waziri, naomba mwendelee vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)