Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chake Chake
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa kwanza jioni hii ili nasi tupate kutoa mawazo yetu na michango kwenye Wizara au hoja iliyopo Mezani leo, hoja ya Wizara ya Viwanda na Biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, kabla sijaenda kwenye mchango wangu, naomba nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya, uzima na nguvu. Pia nawashukuru wananchi wa Chake Chake kwa namna wanavyoendelea kuniombea dua Mbunge wao ili niendelee kuwapambania na kuwawakilisha kwa yale waliyotuma kwenye Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue fursa hii kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Tanzania, Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa anavyoendelea kutupambania. Halali usiku na mchana, anaendelea kupambana kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Tanzania inaendelea kuwa salama kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipokuwa napitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri, nilikuwa very disappointed. Moyo wangu ulivuja damu nilipoona anaomba shilingi bilioni 29 kwa ajili ya maendeleo. Wizara ya Viwanda na Biashara ni Wizara ambayo inabeba uchumi wa nchi hii. Viwanda nchi hii ndiyo ajira. Asilimia 75 ya Watanzania, kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022, kwenye population yetu ni vijana wenye umri wa miaka 35; na ndio hao ambao wao wapo kwenye soko la kutafuta ajira za nchi hii lakini Serikali haiwezi kuwaajiri wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwaajiri wapi zaidi ya kujenga viwanda vingi, maeneo ambayo ndiyo tutakayoweza kuwaajiri? Sasa nilivyoona shilingi bilioni 29, nikajiuliza, are we serious kweli? Shilingi bilioni 29 tunakwenda kufanya nini? Wizara hii ndiyo inayobeba sera, inabeba sera ya viwanda vya nchi hii. Unaipa shilingi bilioni 29 ikakarabati, ikafanye tafiti, ikaanzishe, ikaboreshe! Siyo sawa, siyo sawa hata kidogo. Hizi fedha hazitoshi, ni kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutarudi hapa mwakani, tutaimba the same song, nyimbo ile ile kila siku. Mheshimiwa Waziri anakwenda kufanya nini na shilingi bilioni 29? Shilingi bilioni 29 anakwenda kufanya nazo nini? Atakwenda kufanya yote hayo kwa shilingi bilioni 29? Hazitoshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaiomba Serikali walitazame kwa jicho la huruma na kwa jicho la pili, wamwongezee Mheshimiwa Waziri fedha ili akafanye kazi ya kuviinua viwanda vyetu. Kila mtu aliyeinuka hapa amelia, kwamba viwanda vimekufa, kila mtu aliyeinuka hapa amelia kwamba ana raw materials lakini hana viwanda. Tunakwenda kuvianzishaje? Anakwenda kuhamasishaje watu waje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ombi langu la kwanza na la msingi ni kwamba tukamwongezee fedha Mheshimiwa Waziri; kama tupo serious na tunataka sekta ya viwanda na biashara, kwamba itutoe na itupeleke kwenye zile ndoto ambazo Watanzania tunaziota za kufikia Tanzania ya Viwanda. Hilo lilikuwa ombi langu la msingi na la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi la pili. Wakati Mheshimiwa Prof. Muhongo anatoa mchango wake hapa asubuhi aliomba kwa Mkoa wa Mara akajengewe viwanda; kwa sababu ana pamba, akajengewe textile industry. Akasema yeye ndiye mvuvi mzuri, hivyo akajengwe viwanda vya ku-process mazao ya samaki. Akasema yeye hapa ni mkulima mzuri, kwa hiyo, akajengewe pia viwanda vya ku-process mazao yanayotokana na kilimo na mifugo. Akalia kwa sababu ya viwanda vyake vilivyokufa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wakati natafakari mchango wake nikawa najiuliza, hivi huyu mwenye sera ambaye ndiye Wizara ya Viwanda na Biashara ambaye ndiye amekabidhiwa hii sera, anasimamia nini sasa hivi? Ana nini mkononi anachokisimamia? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ukiangalia ki-theory tumemwambia yeye ndiye akasimamie viwanda. Practically, viwanda vyote vikubwa vya nchi hii ambavyo vipo kwenye mazao ya kilimo vipo Wizara ya Kilimo. Viwanda vya sukari, pamba, chai na vya coffee (kahawa); viwanda ambavyo vipo kwenye mazao ya mifugo (nyama, maziwa, ngozi) anavyo Mheshimiwa Ulega. Ndiye anayevifuatilia anavi-control anahakikisha ubora; yeye ndiye atakuja kusema maduhuli ya makusanyo. Sasa mwisho wa mwaka ukimwuliza Mheshimiwa Dkt. Ashatu au Mheshimiwa Waziri wa Viwanda anasimamia nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi mwekezaji mkubwa wa viwanda akija anaanza kwa Mheshimiwa Waziri wa Uwekezaji. Huku atakwenda ataomba apewe ardhi, ataomba asajiliwe BRELA, wao ndio watakaomsaidia na one stops centre yao. Sasa yeye ndiye tuliyempa sera, lakini tumemweka katikati sasa hivi, sijui hata nisemeje kwa lugha nyepesi. Kama vile tumempa sera aisimamie, lakini wenye infrastructure ni watu wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii ndiyo Wizara mama na ndiyo Wizara iliyopewa isimamie sera ya viwanda ya nchi hii na biashara pia. Hawa wafanyabiashara ambao Kamati iliwasema hapa asubuhi, sasa hivi Wamachinga wapo TAMISEMI. Kwa hiyo, unabaki tu dilemma. Atakuja hapa kila mwaka, atatueleza hatuoni kitu ambacho kipo tangible moja kwa moja kwake ambacho kitakuwa legacy yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ajili ya legacy yake Mheshimiwa Waziri na Serikali wakasimamie viwanda vidogo vidogo kupitia SIDO. Akasimamie CHEMCO, akasimamie TIRDO kufanya research, akapambane na KMTC, akapambane na CAMARTEC. Huko ndiko kwenye legacy yake Mheshimiwa, akapambane huko. Tuje tuone jina lake linatajwa kesho kwamba yeye alikuwa revolutionist aliyepigana kwenye mapinduzi ya viwanda ya nchi hii ambayo kila mtu ataimba jina lake; lakini aombe aongezwe fedha, asione aibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawezi kupambana kama hana hela za kutosha. Shilingi bilioni 29 hazimtoshi, hatafika popote, hatafanya chochote. Kila siku tutakapokuja itakuwa ni the same story. Amwambie Mheshimiwa Waziri wa Fedha ampatie fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2023 niliposimama hapa nilichangia kuhusu maendeleo ya viwanda vidogo vidogo vilivyopo katika nchi yetu na wajasiriamali wa Kitanzania wanaovianzisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kati ya industry niliyoichangia ni industry ya tailoring, industry ambayo kwa sasa inakua rapidly, kwa kasi sana Tanzania; na inaajiri. Mshoni mmoja ana wastani wa watu 50 wamemzunguka. Nikasema mwaka 2023, na maneno hayo ninayarejea, bado hatujawasaidia wajasiriamali wadogo (Watanzania) wanaoanzisha viwanda Tanzania. Hatujawasaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, akija mwekezaji akitaka kuanzisha kiwanda cha misumari au cha kutengeneza tenki anapata incentives za kodi akileta raw materials. Kwa mfano, akileta raw materials za wire roads kwa ajili ya kutengeneza msumari atapata incentives za kodi kwenye raw materials, tutakuja kumkamata baada ya msumari kuwa umekwishakuwa msumari au tenki limeshakuwa tenki na linauzwa. Tunawasaidiaje hawa tailoring? Akinunua kitambaa anakileta Tanzania kama bidhaa, siyo kama raw material, ni kama bidhaa amekwenda kukinunua India, China au Uturuki. Akinunua cherehani haileti kama mashine, analeta kama bidhaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, atengeneze suti, akishatengeneza hiyo suti anakuwa ameshalipa cherehani na kitambaa. Kwa hiyo, anaipandisha bei kiasi kwamba inashindwa ku-compete na bidhaa zinazotoka China. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suti ya China unaweza kuinunua kwa 150,000 hadi 200,000 lakini customer made suit iliyotengenezwa hapa hapa, designer wa Kitanzania hawa wanaopambana watakuuzia kuanzia 350,000 hadi 400,000; na kwa sababu kutokana na kwamba hatuwalei, hakuna incentives za kuwasaidia wapambanaji wa Kitanzania wanaopambana kwenye kukuza viwanda vya nchi hii. Hiyo ni sekta moja ambayo inaweza kututoa tulipo. Sasa hivi kuna mtu anaweza akataka suti pea 200 hadi 300, akaagiza China au Uturuki. Kwa hiyo, ni kwa sababu ya bei na urahisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nilisema niwatambue Watanzania wazalendo wanaopambana kwenye sekta kama hizo. Mmoja ni JM Collection, ni kijana wa Kitanzania mpambanaji tu. Mwingine ni Suti Bega kijana wa Kitanzania ni designer, wanafanya vizuri tu. Mwingine ni Mtani Design, mwingine ni Kikoti, Dada yangu nje ya Bunge hapo (Careen) Carenito na kuna Marafiki Suits. Hao ni vijana wa Kitanzania wanaopambana kukuza viwanda vya Tanzania, lakini hatuchukulii kama tailoring inaweza ikawa sekta moja kati ya sekta ya viwanda kwa ajili ya kusaidia kukuza ajira, kupata fedha za kigeni na sisi kuuza bidhaa zetu. Tutaagiza mpaka lini? Tutavaa kutoka nje mpaka lini? Tupo mwaka wa 60 wa uhuru hatujaweza, tutaweza lini sisi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndiyo uliokuwa mchango wangu kwa leo, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)