Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu ambayo ndiyo imebeba maudhui na maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nianze kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutegua kile kitendawili cha siku nyingi ambacho eneo la uchimbaji wa madini ya chuma kule Liganga na Mchuchuma, lilikuwa limesimama kwa muda mrefu na limekuwa ni kitendawili cha muda mrefu sana. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kutoa fedha hizo ili angalau sasa tuanze kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, chuma ni muhimu na madini yote yanayopatikana pale yatachangia katika uchumi mkubwa wa nchi yetu. Pia, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri, Watendaji wote, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu na Watendaji wote wa taasisi zilizoko chini yake kwa kazi nzuri waliyoifanya. Pia nawapongeza kwa hotuba nzuri. Hotuba haiendani na rasilimali, lakini ni nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema Wizara hii ni muhimu sana kwa sababu ukiangalia katika uhalisia, wenzetu wanasema neno ‘uzalishaji’, limegawanyika kwenye maeneo matatu; eneo la kwanza ni viwanda, eneo la pili ni biashara na eneo la tatu ni huduma za jamii. Sasa ukiangalia viwanda na biashara, vinaangukia kwenye Wizara hii na hili ndiyo eneo ambalo tunatarajia liweze kutatua matatizo ya msingi ya nchi yetu, ambapo matatizo ya msingi ya nchi yetu ni pamoja na umasikini mkubwa ambao uko kwa wananchi wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, umasikini huu utatokana na viwanda tutakavyoweza kuvijenga hapa nchini. La pili, biashara mbalimbali watakazofanya, ndiyo wataweza kuchangia uchumi wa nchi yetu, lakini uchumi wetu unategemea sana katika hili eneo. Kwa hiyo, ili tuondokane na umasikini na ili tutengeneze ajira za vijana wetu zote, ziko kwenye Wizara yako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kwenye viwanda tunasema, vipo viwanda vya kutafuta malighafi (extractive industries), ambapo hapo kuna kilimo, mifugo, ufugaji, madini, misitu na kadhalika. Hivi vyote sisi tunaita ni viwanda (extractive industries). Vipo viwanda vya kuongeza thamani (Manufacturing Industries) na vipo viwanda vya kuunda miundombinu (constructive industries). Sasa utaona kwa hiyo, ina maana kilimo, uvuvi, misitu na madini, vyote Mheshimiwa Waziri wa Viwanda ndio anabeba sera ya viwanda hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukiangalia katika uhalisia, nchi ambayo inategemea kilimo. Kilimo chetu hatuwezi kutegemea kiendelee kuzalisha mazao tunayauza kama malighafi. Lazima tuwe na viwanda vya kuongeza thamani ya hiyo malighafi. Tuwe na viwanda vya kuchakata kahawa na tujenge mpaka hadi kahawa ikamilike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mlowo, Mbozi pana kiwanda cha kukoboa kahawa, tunataka kisiishie kukoboa, tunataka kitengeneze kahawa ili Watanzania wanywe moja kwa moja kutoka hapa badala ya kuagiza nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka tunapouza mahindi ambayo tunalima sana katika maeneo mbalimbali, mahindi yale tuyasage tupate unga. Unga ule ndio twende tukauze DRC Congo na nje ya nchi, bidhaa ambazo zimeshakamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yoyote ambayo inauza mazao kama malighafi, hiyo maana yake imechagua kuwa nchi masikini duniani. Sisi Tanzania hatujachagua kuwa masikini, tunataka tuwe Tajiri; iwe ni nchi ya kimkakati ambayo italeta maendeleo ya nchi hii. Kwa hiyo, tunataka lazima tuwe na mkakati wa kutosha wa kuhakikisha kwamba tunaongeza thamani ya mazao yetu, kuongeza thamani ya madini yetu, kuongeza thamani ya misitu yetu na kadhalika ili nchi hii iweze kutengeneza ajira, tuweze kuondokana na umasikini na tuweze kujenga uchumi mkubwa wa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri na timu yake unayo hiyo dhamana ni yeye mwenyewe hapo. Sasa hivi nimefurahi sana kusoma kwenye Hotuba yake amesema, “Tunavyo viwanda vya kutengeneza, kuunda magari,” lakini hebu tuangalie hivyo viwanda vya kuunda magari alivyovisema, ni viwanda vichache. Ni hatua nzuri, tunampongeza lakini tunahitaji viwanda zaidi vya kuunda magari. Magari ni madogo kwa sababu ni eneo ambalo tunachukua fedha nyingi sana za kigeni kwenda kuzipeleka nje na kununua magari. Tunataka magari haya yaundwe hapa. Ikiwezekana tutengeneze hapa hapa na vipuli, itatusaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka zana za kilimo cha nchi hii ambapo Watanzania zaidi ya asilimia 65 ni wakulima, zana za kulima zitengenezwe hapa. Tunataka viwanda vya mbolea na madawa yatengenezwe hapa. Hapo ndipo tutakapoweza kujenga uchumi mzuri na wenye maendeleo mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kwenda bila viwanda. Viwanda ndiyo mhimili wa maendeleo ya nchi. Hebu tuangalie kidogo katika nchi zilizoendelea... (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Hasunga kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Janejerry.
TAARIFA
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mchangiaji kwamba, viwanda tunavyo. CAMARTEC inatengeneza matreka hapa Tanzania, lakini kikubwa ni hizi Wizara kuungana na kutumia viwanda vilivyo nchini; Wizara ya Kilimo na Wizara ya Uvuvi. Nenda kwenye maonesho pale vitu vyote viko pale. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Hasunga, unaipokea hiyo taarifa?
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima yake naipokea tu, lakini nataka nimwambie, viwanda vilivyopo ni vichache mno, havitoshelezi mahitaji ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachozungumzia sisi, ni kwa uwanda mpana kuangalia mahitaji ya Taifa letu. Tunahitaji viwanda vingi, kwa mfano, suala la mafuta, nchi ya Tanzania tunaagiza mafuta ya kula nje ya nchi. Dola nyingi tu zinakwenda huko, hiyo kwa kweli haikubaliki. Tunatumia fedha, sasa hivi tunaagiza hadi sukari nje ya nchi, haikubaliki. Haya yote tuna uwezo wa kuzalisha hapa, matrekta na majembe, tunahitaji tuzalishe hapa hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilikuwa nasema, kuna kitu kilitokea ambacho inabidi tuliombee Taifa hili. Nchi ya China mwaka 1949 walipopata uhuru, waliweka mkakati wa industrialization na wakafanikiwa kujenga viwanda mpaka leo China ni nchi ya pili duniani kwa viwanda. Nchi ya India waliweka mkakati wa namna ya kujenga viwanda, mpaka leo India wamefika hatua kubwa, nao walipata uhuru unaoendana hapo hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumepata uhuru mwaka 1961, tulichukua hatua za kuanza kujenga viwanda, tumejenga viwanda vingi karibu kila maeneo tulikuwa navyo, lakini hapo katikati shetani alipita, viwanda vyote vikakufa. Hatuwezi kukubali hili, tuangalie tulipokosea, turudishe viwanda vyote ambavyo vimepotea. Hili ndiyo litatuwezesha sisi tuweze kufika mahali pazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji kuimarisha biashara...
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Kuna taarifa ya Mheshimiwa Condester.
TAARIFA
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumwongezea mchango Mheshimiwa Hasunga, alichokuwa anaongea yuko sahihi. Sisi hata Tanzania hatuna viwanda vya kutengeneza ila tuna viwanda vya kuungaunga. Mfano, CAMARTEC, injini za matrekta hawatengenezi wao, zinatengenezwa nje. Kwa hiyo, Mheshimiwa Hasunga yuko sahihi kwenye mchango wake. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Hasunga, unaipokea hiyo taarifa?
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea. Vyote hivyo ni viwanda, hata vya kuungaunga tunavihitaji. Maana yake ni lazima kwanza tuanzie kwenye viwanda vidogo vidogo ili tupige hatua tuje tufike kwenye viwanda vikubwa. Kwa hiyo, hata vidogo tunavihitaji, hakuna cha kidogo, kwa sababu hata Waingereza walianza kwenye cottage industries; walianzia nyumbani, wakajenga viwanda mpaka wakafika walipofika na sisi lazima tuanzie hapo hapo ndiyo tutakuja kufika huko kwenye viwanda vikubwa ambavyo tunavitaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nazungumizia eneo la biashara. Nchi hii ni lazima tuigawe katika zone muhimu za biashara. Kwa sababu ni nchi ambayo iko strategically located. Tuangalie ni aina gani ya biashara zinaweza kututoa na ni maeneo gani yanaweza kututoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyosema kule kwenye Mchuchuma na Liganga kutatutoa, lazima tuweke fedha. Sasa Mheshimiwa Waziri, ukiangalia bajeti ya maendeleo ya shilingi bilioni 29 uliyopewa, una bajeti ya shilingi bilioni 110. Bajeti ya Maendeleo ya kufanyia kazi shilingi bilioni 29, hii inatuonyesha we are not serious. Hatuwezi kujenga viwanda kwa shilingi bilioni 29. Hiyo tutakuwa tunatania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Bunge tukae vizuri, tuliangalie kama kweli tuna nia ya kwenda. Kwa hiyo, kwenye biashara, maeneo kama Tunduma, Tunduma iko mpakani ni lango la SADC, zijengwe biashara, Watanzania wawezeshwe wawe na biashara kwenye maeneo yale mengi ya mipakani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Mbozi, Vwawa wajenge ma-go down na maduka makubwa, Wazambia, Wazimbabwe na watu wengine waje kununua. Iwe ni hub ya kununua kama ambavyo tunataka kufanya Kariakoo na maeneo mengine. Tukiangalia hivyo, tutaweza kufanya biashara na nchi yetu itaweza kupiga hatua kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kuna changamoto mbalimbali za wafanyabiashara. Hilo naamini Wizara ya Fedha watalishughulikia vizuri ili kuondokana na hiyo changamoto. Tunalo tatizo la masoko, Wizara yako imebeba dhamana ya kushughulikia masoko ya mazao yetu na bidhaa mbalimbali, hiyo mtashirikiana na Wizara nyingine mhakikishe kwamba kwa kweli masoko yanapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema, tunahitaji mfuko wa kuchochea ujenzi wa viwanda, bila mfuko, hapa tutakuwa tunaimba tu na Bunge hili ili tutengeneze historia. Ni lazima tuunde mfuko wa kuchochea viwanda. Mfuko huo tukiwawezesha Watanzania wakajenga ile miundombinu inayojitosheleza, watu wanaotaka kwenda kununua teknolojia huko wawezeshwe, hawawezi kupata fedha kutoka kwenye benki zetu hizi. Ukienda kule kwenye benki, wanakwambia hili wazo zuri, una mtaji gani? Wewe umejiandaaje na una dhamana gani? Mtanzania yupi mwenye dhamana ya kuweza kununua kiwanda kutoka nje akaja akakiweka? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi teknolojia ya viwanda iko kule inatakiwa ikanunuliwe ije isimikwe, Mheshimiwa Waziri, kila mwaka tunatakiwa tutengeneze mkakati, Watanzania 500 wawezeshwe. Tukiwa na programu ya miaka 10, baada ya hapo tutakuwa tumepata walipa kodi wengi, tutaweza kujenga viwanda tukiwa na mfuko wa viwanda. Kwa hiyo, hili mimi naamini kwamba ni muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, tuwe na mfuko wa kuwasaidia wafanyabiashara. Wafanyabiashara wetu wanateseka sana, wengine wana uwezo wa kufanya biashara na wana uwezo wa kufurukuta, lakini hawana mitaji. Mitaji hiyo itaweza kupatikana tu kama Serikali itaweza kuwa na mfuko wa kuwasaidia wawekeze. Nchi zote duniani zimefanya hivyo na ndiyo zimeweza kufikia hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika moja tu, misingi ya maendeleo ya nchi yoyote duniani, tunahitaji mtaji wa asili yaani ardhi, maji, madini, misitu, wanyamapori na kadhalika, huo ni misingi ya kwanza na Tanzania tunao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi wa pili ni ujenzi wa miundombinu, yaani tunahitaji physical capital ili viwanda viweze kwenda mbele, tatu, tunahitaji rasilimali fedha ili tuweze kuijenga nchini na mwisho tunahitaji rasilimali watu na wahusiano (Human capital na social capital), hivi ndiyo vitatusaidia kuendesha nchi yetu na kuisukuma katika viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja na ninawatakia kila la heri, ahsante. (Makofi)