Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika bajeti hii ya Wizara ya Viwanda na Biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizi zaidi ya shilingi bilioni 15 kwa ajili ya kulipa fidia kwa ule mradi wa Liganga na Mchuchuma. Tunamshukuru sana Rais, Mama amekuwa ni mwema, hapigi kelele, lakini kazi inayofanyika ni kubwa sana katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo za Mheshimiwa Rais, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Dkt. Ashatu Kijaji kwa kazi kubwa ambayo unaifanya katika Wizara hii. Niendelee kuwapongeza wananchi wako wa Kondoa Vijijini na hata pale walipokuita jina la Kamsese hawajakosea. Nani kweli, ni kamsese. Ila bila kusahau nitoe pongezi kwa Naibu wako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye mchango wangu. Nimejaribu kuangalia Taarifa ya Wizara wakati Waziri anaisoma lakini pia nimejaribu kuangalia Taarifa ya Kamati. Nilitamani kuona jambo moja ambalo nakumbuka tarehe 13/4/2023 kwenye mchango wangu wa Wizara hii nilileta jambo mahususi jambo la Matrekta ya Ursus.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kiti chako na naomba unifikishie salamu za wananchi kwa Mheshimiwa Spika wa Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya kutoa mchango ule wa kero ya Matrekta ya Ursus, Mheshimiwa Spika aliamua Kamati ya Bunge iweze kwenda Manyara na baadhi ya maeneo ili kukutana na wakulima na kuona changamoto hiyo. Hakika tunamshukuru sana Spika wetu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwatendea wananchi na wakulima wa Tanzania haki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumpongeza Mheshimiwa Spika, baada ya Kamati, Mheshimiwa Spika alitoa maelekezo hapa kwamba Serikali ije na hitimisho la jambo hili. Kwa namna ya kipekee kabisa na kwa namna ambavyo ninamfahamu Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji, mama na jirani yetu watu wa Manyara na Hanang ninaamini utakapokuwa unahitimisha bajeti yako utasema neno ili roho za Wakulima wa Tanzania ambao walipata hasara kupitia Matrekta ya Ursus na kwa sababu wanamjua Rais wao Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni mama mlezi, ni mama asiyependa uonevu, ni mama ambaye anataka Watanzania waende mbele na hususan wakulima hawa ambao haki yao ilipotea kupitia Matrekta ambayo kwa kweli yamewatia hasara kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nategemea Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atasema neno ili wakulima wale wapone na walale usingizi ambao hawajalala kwa miaka kadhaa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati naendelea kufuatilia hili zipo tetesi kwamba kuna dalili njema ya tamko la Rais na kwa sababu Mheshimiwa Waziri yupo na tetesi hizo wakati nikifuatilia baadhi ya wakulima wameshaanza kupigiwa simu kutakiwa taarifa ya kile ambacho wamekipoteza. Ahsante sana Mheshimiwa Waziri, ahsante sana Serikali ya Awamu ya Sita, ahsante Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwasikiliza Wakulima wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hili, nihitimishie hapo kwa sababu najua Mheshimiwa Waziri utakuja kuitoa kauli ambayo sasa wakulima wataisikiliza na watakuwa na kauli moja na kuachana na ubabaishaji wa simu tofauti tofauti na watapata maelekezo sahihi ya Rais wao mwema Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwenye hilo naomba kuhitimisha hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niingie sehemu ya pili. Nchi yetu ina vijana wengi sana ambao wengi wao hawana ajira na Serikali yetu kimsingi kupitia Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Mama msikivu ameendelea kuhakikisha kila kunapokucha anaendelea kutoa fedha kwenye Wizara tofauti tofauti kwa ajili ya kutanua maendeleo ambayo yanaweza kusaidia vijana wengi kuja kuajirika. Kwenye hili naendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo linaweza kutatua changamoto ya ajira kwa vijana wengi wasomi na ambao hawajasoma sana ni viwanda. Viwanda vikifufuliwa katika nchi yetu na niendelee kuipongeza Serikali kwa kuendelea kufufua viwanda, lakini bado tunatakiwa tuongeze speed kubwa ili tuweze kufufua viwanda vingi ili kuweza kuzalisha na kutoa ajira kwa vijana wengi wa Kitanzania, wale wasomi na wale ambao hawajafanikiwa kusoma sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku chache niliuliza swali na bahati nzuri lilijibiwa na Naibu Waziri wa Madini. Natolea mfano kwa eneo ambalo ninatoka. Mimi natokea Manyara Wilaya ya Hanang’. Wilaya ya Hanang’ inayo chumvi ya kutosha ambayo inaweza kulisha ndani ya nchi pamoja na nje ya nchi na tukaingiza fedha za kigeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maeneo kama Gendabi, Dawar, Balangdalalu Wilaya ya Hanang’ Mkoa wa Manyara ipo chumvi ya kutosha. Ukienda Babati Vijijini ipo chumvi ya kutosha. Kwa maeneo kama Gendabi kwa mwaka mmoja inazalishwa zaidi ya tani 85,000 na huo ni uchimbaji wa kawaida wa kienyeji kabisa wa kutumia mikono.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Manyara, Singida na hapa Dodoma bado tunahitaji viwanda vingi ili kuweza kuwasaidia ajira vijana wa maeneo hayo na vijana wa Kitanzania. Mheshimiwa Waziri, naomba sana ile chumvi ya Hanang’ isipotee hivi. Tunahitaji kiwanda, tunaomba tusaidiwe wawekezaji wakubwa, tunaomba mwasaidie wawekezaji wetu wa ndani wadogowadogo namna ya kutoka na kuweza kuzalisha chumvi ile kwa uhakika na ukubwa, kutoa ajira na kujipatia fedha za kigeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kile kilichopo Hanang’ ni mali, kile kilichopo Manyara ni mali inayoweza kutanua ajira kwa watu wengi na hasa ukizingatia Manyara hatuna viwanda vya kutosha. Wananchi ni wengi, vijana ni wengi, akina mama ni wengi, tunaomba sana utuangalie katika suala la uwekezaji wa viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa niendelee kuiomba Serikali kuendelea kuwekeza kwenye kiwanda cha Minjingu ili kuhakikisha kwamba mbegu za wakulima wanazopanda zinakwenda kupata mbolea bora inayotokea hapa nchini na kutakuwa hakuna upungufu ili tuweze kulima kilimo chenye tija kitakachokidhi mahitaji ya ndani pia kitakachokidhi mahitaji ya nje ili tuweze kupata fedha za kigeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha kiwanda cha Minjingu, kipo Kiwanda cha Mbolea cha ITRACOM hapa Dodoma, tuiombe Serikali iendelee kuangalia viwanda hivi kwa sababu vinatoa ajira kubwa kwa wananchi na vinao uwezo wa kutusaidia kupata mazao bora ambayo yatakidhi nchi na hadi nje kwa ajili ya fedha za kigeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo gesi asilia kule Mtwara. Hii ni tunu na bahati kubwa ambayo Mwenyezi Mungu ametubariki sisi Watanzania, lakini hakutubariki ili ikae tu ardhini, ametubariki ili tukiitumia katika matumizi sahihi na mapana yanaweza kuwa ni suluhisho la kugawa ajira kwa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ile gesi asilia tunao uwezo wa kuitumia pia katika kutengeneza mbolea ya urea. Mheshimiwa Waziri nikuombe sana kupitia Mheshimiwa Mwenyekiti, tuendelee kufanya uwekezaji katika mbolea na hasa kwa rasilimali hiyo kubwa ambayo inatoka Mtwara, Mwenyezi Mungu ametugawia kwa ajili ya nishati lakini tuna uwezo wa kuitumia kwa matumizi zaidi na ikaweza kuleta tija katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kumekuwa na mlolongo mkubwa wa kodi, Serikali imejitahidi sana kuendelea kupunguza kodi katika nchi yetu, bado niendelee kuiomba Wizara iendelee kufanya kazi kubwa ili kurahisisha mazingira mazuri ya wawekezaji wakubwa pia wawekezaji wetu wa ndani waweze kuwa ni sehemu ya kuvutiwa na upunguzwaji huo wa kodi ili waendelee kuwekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri hapa juu una matarajio makubwa sana, mipango yako ni mizuri sana, unakutana na wafanyabiashara mara kadhaa tunakuona lakini bado una kazi ya kuwaambia watu wako wa chini waweze kujua changamoto zinazowakuta wafanyabiashara wadogo wadogo kwenye maeneo yao ili kuanza kutatua pia twende sambamba na huku juu katika ngazi ya Taifa ambapo unajua changamoto za wafanyabiashara wako wakubwa tofauti na kule wa ngazi ya chini. Waendelee kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara wa ndani ambao siyo rahisi kukufuata hapa Dodoma kila mara lakini wapo wasimamizi wako kule chini, tunaomba wakae na wafanyabiashara katika mazingira ya kujua faida zao lakini pia kujua changamoto zao.
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kuunga mkono hoja na ninakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)