Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia kwenye hii bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara. Kusema kweli pale kwangu Musoma Mjini kama tunavyofahamu ni kwamba mji wowote ule au nchi yoyote ile mojawapo ya jukumu kubwa ni kuhakikisha kwamba watu wao wanapata ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa bahati mbaya sana ni kwamba pale Musoma watu wangu hawana ajira kabisa. Hii imetokana na nini? Viwanda vyote vilivyokuwa vinafanya kazi Musoma vimekufa. Tulikuwa na kiwanda cha nguo kimekufa, kiwanda cha ngozi kimekufa, kiwanda cha maziwa kimekufa, viwanda vya samaki vimekufa na hata sasa kimebaki kiwanda kimoja ambacho kinafanya kazi ya kununua, kukusanya samaki na kupeleka Mwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa masikitiko yangu nimekuwa nikilisema hili mara kwa mara lakini response ya Wizara au ya Serikali ni ndogo sana. Wakati mwingine hawafiki hata kukaa tu na wale wenye viwanda na kujua matatizo yao na mambo gani yanasababisha viwanda vife. Kwa hiyo, kidogo kwetu imekuwa changamoto na kutokana na hali hiyo, maana yake ni kwamba watu wetu wengi mpaka leo hivi wanakosa ajira, siyo kwa sababu nyingine, ni kwa sababu viwanda vinaendelea kufa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani kuna haja ya Serikali kuona ni namna gani itaendelea kusimamia na kuvisaidia vile viwanda vilivyopo na kuleta viwanda vingine ili watu wake waweze kupata ajira kwa sababu hilo ni mojawapo ya jukumu kubwa la Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hiyo ni changamoto ya kwanza ambayo nadhani Mheshimiwa Waziri unahitaji uone namna ya kutusaidia pale Musoma na maeneo mengine. Naomba kabisa kwamba basi utenge muda hasa baada ya Bunge hili la Bajeti uje pale tukae tuzungumze na tuone ni namna gani Serikali iko tayari kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, yako haya mashirika ya viwanda vidogo vidogo kama SIDO ambalo linaweza likasaidia sana katika kukuza ajira. Leo ukienda nchi kama pale China viko viwanda vidogo vidogo tu hivi na kazi yake kubwa hasa ni ile packaging. Sasa Shirika letu kama la SIDO lilikuwa linatoa mafunzo mengi mbalimbali ambayo yalikuwa yanasaida vijana wetu kupata ujuzi na vilevile yalikuwa yanawapa mikopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tumeliacha lile Shirika limekufa. Mfano pale Musoma zimebaki zile godown wanapangisha wanapata rent, basi biashara inaishia hapo. Kama tungeona namna ambavyo tungeweza kuwawezesha tafsiri yake ni kwamba nao wangepata nafasi ya kuwawezesha vijana na akina mama mbalimbali kupata mafunzo ya muda mfupi, lakini na kuona namna wanavyoweza kujiendesha ambayo ni pamoja na kuwapa mikopo. Kwa hiyo, na hilo nalo bado ni changamoto kwamba SIDO nayo iko pale lakini inaelekea kufa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi inajitahidi sana kujenga masoko makubwa na masoko mazuri. Bahati nzuri hata mimi mwaka huu nashukuru kwamba nimekumbukwa kwa maana nimeweza kupata fedha kwa ajili ya kujenga ile stendi yetu kubwa iliyokuwa inatusumbua kwa muda mrefu iliyoko pale Bweri. Mbali na hilo, nimepata fedha kwa ajili ya kujenga soko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa changamoto iliyopo unakuta soko zuri linajengwa, lakini wananchi wanafika mahali wanahama kutoka kwenye masoko mle wanahamia kule pembezoni. Wanahama mle kwa sababu wanachokumbana nacho tu ni kodi nyingi na mwisho wa yote wanaona kama ni afadhali akakaa kule pembeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, leo mfano kwa pale Mjini yapo masoko ambayo ni mazuri tu. Kuna Soko Kuu liko pale leo kuna baadhi ya wananchi wanahama kutoka humo. Unakuta kuna soko kama lile la Saa Nane ambalo ni Soko la Wakulima, yako masoko kama kule Nyamatare na baadhi ya masoko mengin, wanahama ni kwa sababu Serikali haijatengeneza mazingira mazuri yanayowawezesha wananchi kukaa mle na wakafanya biashara. Kuna Soko kama la Kamnyonge, limekufa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilichotaka kushauri hapo ambacho Serikali inaweza ikakifanya na leo ikiamua inaweza ikayaboresha yale masoko na yakaenda vizuri kwa sababu tayari baadhi ya masoko yamejengwa na ni mazuri na mengine yanaendelea kujengwa kama hilo Soko la Nyasho kama nilivyosema. Serikali inapaswa kwanza ijitahidi kuhakikisha kwamba kodi ndogo ndogo zenye kero zinapungua mle.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, mtu akishakaa mle sokoni basi tuweke utaratibu mzuri wa wao kupata mikopo ya gharama nafuu ili waendelee kufanya zile biashara zao. Sasa unakuta yuko mle, aliyeko nje ya soko yeye halipi ushuru, lakini aliyeko mle bado anadaiwa alipe ushuru. Kwa hiyo, mtu anaona ni afadhali akakaa nje kuliko kukaa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya sana hata mimi nilifanya juhudi binafsi nikawapeleka katika baadhi ya benki zetu ili ziweze kukaa nao zione uwezekano wa kuwapa mikopo. Waliambulia tu kuwaambia, ili waweze kulipia ile kufungua account, baada ya hapo benki zikaishia, na wale wananchi wako pale sasa wanaendelea yaani wanaona kama fedha yao imechukuliwa bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunadhani hilo nalo kuna haja ya Serikali kuangalia na ikiwezekana kwa sababu watu wengi wanajifunza biashara, wale Maafisa Maendeleo wetu wa jamii na wale wote ambao ni wakufunzi wanaofundisha mambo ya biashara wakawepo pale kwa ajili ya kuwasaida watu wetu ili waendelee kufanya biashara zao vizuri. Pia, wapate mikopo na kutokana na hiyo mikopo, basi maisha yao ni imani yangu kwamba yatakuwa mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni suala la tozo. Unajua mpaka leo wapo watu wengi wanalalamika kwa sababu kwanza wanashindwa kutofautisha kodi na tozo. Sasa unakuta zote hizo watu wanaziweka pamoja na zinaonekana kwamba zote ni kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unaambiwa kila mmoja anasema kwamba katika nchi ambazo zina mazingira magumu ya kufanyia biashara ni pamoja na Tanzania. Zina mazingira magumu kwa sababu ukiacha ile kodi unakuta mfano kuna watu wa TBS watafika pale watakusanya hela zao, watu wa fire watafika pale watakusanya hela zao, watu wa NEMC watapita pale watakusanya hela zao, Weight and Measure watapita pale watakusanya hela zao na bado OSHA hujawazungumza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa zote hizo ukizikusanya kwa pamoja ukachanganya na ile kodi, matokeo yake sasa kwa yule Mtanzania wa kawaida anaona maisha ni magumu maana kila kukicha huyu amepita, asipopita asubuhi mwingine anapita mchana na mwingine anapita jioni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hilo nadhani Mheshimiwa Waziri una haja ya kuona namna gani tuta-harmonize na ikiwezekana, basi hizi kodi zote zingekusanywa zikawekwa pamoja ili yule mfanyabiashara akishalipa mara moja, basi ajue kwamba kazi yake amemaliza na sasa anaweza kufanya biashara yake vizuri pasipokuwa na shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana shida moja kwa mfanyabiashara kwanza akiona tu mtu yeyote yule wa Taasisi ya Serikali, yaani anakuwa tayari amejenga hofu. Pia unakuta kwa sababu ya uelewa wetu ni mdogo, wengine hata hawafuatilii. Yaani mtu wa OSHA akija pale anajaribu kuangalia yule mtu wa OSHA hatoi hata elimu kwamba kwa nini anakuja kuomba ile kodi, anasema tu wewe unapaswa kulipa OSHA, basi tupe hii tozo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hajui ni ya nini, anaona ni kama anadhulumiwa; hajakaa sawa mtu wa fire amepita. Sasa mtu anaangalia, hivi hapa kwangu fire atakuja kunisaidia nini? Sasa haya yote ni kati ya mambo ambayo katika nchi yetu hii yanasababisha Watanzania waone kama mazingira ya kufanyia biashara ni magumu na njia pekee sasa ni kuona namna ya ku-harmonize ili hizi kodi zote ziweze kuwa moja na kwa utaratibu huo sasa watu wetu wanaweza wakafanya biashara vizuri pasipokuwa na shida yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani Serikali ina kila aina ya sababu ya kuyaangalia haya ili Mtanzania afanye biashara yake vizuri pasipo mashaka yoyote. Hii ndiyo itakayoendelea kuwapa moyo wa kuendelea kulipa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)