Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hii ambayo ni kichocheo kikubwa cha uchumi wa nchi, lakini vilevile ni kichocheo kikubwa cha ajira ambazo tunazihitaji sana kwa vijana wetu wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza sana Rais wangu kwa jinsi ambavyo amekuwa akitenda haki katika bajeti za Wizara mbalimbali. Wizara hii ilikuwa na bajeti ndogo sana lakini Mheshimiwa Rais ameonyesha nia njema ya kuongeza bajeti japokuwa bado haitoshi kulinganisha na umuhimu wa Wizara hii lakini kwa kiasi kikubwa tunaona mabadiliko kulinganisha na hali halisi ilivyokuwa huko nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri, Naibu Waziri na timu yake nzima kwa jinsi ambavyo wamekuwa wakijitahidi kufanya kazi kwa weledi katika Wizara hii na sisi kama Wanakamati, kwa kweli tunaridhishwa na jinsi ambavyo kazi zimekuwa zikifanyika ndani ya Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitachangia kwenye mambo mawili tu. Jambo moja linahusu zao la alizeti ambalo linalimwa kwa wingi katika jimbo langu la Iramba Mashariki, Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama na Mkoa wa Singida kwa ujumla. Zao hili linapolimwa inabidi liende kiwandani kwa ajili ya kutoa mafuta ya kula, kitu ambacho kimekuwa ni changamoto kubwa kwa nchi yetu hasa kwa ajili ya kupoteza fedha nyingi za kigeni kwa sababu ya ku-import mafuta ya kula kwa kigezo kwamba mafuta yanayozalishwa ndani hayatoshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Mheshimiwa Waziri imesema kwamba viwanda vipo, lakini mbegu za alizeti hazitoshi. Mimi nataka tu niende kidogo tofauti na statement hii. Mwaka wa kilimo uliopita Mkoa wa Singida pekee ulizalisha alizeti tani 1,400,040 ambapo mbegu huwa zinatoa mafuta takribani 30%. Kwa hiyo, 30% ya tani hizi ni kama lita 330,000 za mafuta, kwa Mkoa wa Singida tu, tukiacha maeneo mengine ambayo wanalima kidogo kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, utaona kwamba hiki ni kiwango kikubwa sana cha mafuta. Kwa nini viwanda vinasema havina mbegu? Hili jambo siyo la kweli. Kwa kiwango hiki na kwa tani hizi ulitegemea viwanda viendelee kusaga?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichotokea ni kwamba, mafuta ambayo siyo ya alizeti yanayotoka nje yanaingia nchini kiholela, yanaingia mafuta mengi kiasi kwamba mafuta yetu ya ndani ambayo yanatokana na mbegu hizi yanashindwa ku-compete kwenye bei. Kwa hiyo, kilichofanyika, wakulima wengi walikaa na mbegu zao ndani, kwa sababu anaona akipeleka kuuza kiwandani bei anayopewa hairudishi hata robo ya gharama alizotumia. Matokeo yake viwanda vinaona kwamba havina mbegu, ukidhani kwamba wakulima hawajalima, kumbe wakulima wamelima mbegu imeanguka. Matokeo yake ni kwamba mbegu haziendi kiwandani kwa sababu mtu akipeleka anaona ni hasara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kitu ambacho kinatakiwa kifanyike hapa ni kudhibiti uingiaji wa mafuta ya kula. Mafuta haya hayana mwenyewe. Mafuta ya kula yanaingia tu, yaani kama bidhaa. Mtu analeta tu anavyotaka, hakuna regulation yoyote, na Wizara haijapata takwimu sahihi za mafuta kiasi gani yamezalishwa nchini ili gap pekee ndilo liagizwe kutoka nje, kwamba kile kilichopungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa sababu hakuna data, watu wamekaa na mbegu ndani, na kwa sababu mafuta ya kutoka nje yamejaa sokoni, matokeo yake kila mtu anaingiza mafuta anavyotaka. Sasa hii inasababisha watu wasiendelee kulima na matokeo yake tunaona kama viwanda vyetu havina mbegu kumbe watu wameziweka ndani kwa sababu hazina bei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba sana Serikali na Wizara sasa mafuta ya kula yawe na mwenyewe ili data sahihi zipatikane kwamba ni kiasi gani cha mafuta kimezalishwa ndani ya nchi ili mafuta kiasi gani yaletwe kutoka nje? Pia hayo yanayoletwa kutoka nje yanaingia kwa kiwango kile tu ambacho kinatakiwa ambacho ni tofauti. Hapo utaona kwamba mafuta ya ndani yatakuwa na bei nzuri na wakulima watakuwa na uhakika kwamba wakipeleka mbegu zao kiwandani watapata bei nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwamba sasa mafuta haya yawe na sheria maalum na yawe na mtu kama ilivyo sukari, kwamba una uhakika kabisa. Kwa hiyo, wenye viwanda wanadanganya danganya tu kwamba hatuna mbegu ili wapate wengine na fursa ya kuendelea kuagiza mafuta kutoka nje ili wapate faida kubwa na wakulima wetu wanazidi kukaa na mbegu ndani. Nataka niishauri Serikali, ihakikishe kwamba mafuta ya kula yanakuwa na sheria yake na udhibiti ili tujue kiasi gani cha mafuta kinaingia na kiasi gani kinatakiwa wananchi walime na hapo tutaona viwanda vyetu vitapata mbegu za kutosha katika kukamua mafuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nataka niende kwenye suala la TFDA na TBS. Asubuhi niliona hapa baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wanashauri kwamba TFDA irudi, kwa maana ya kwamba TBS isifanye kazi hizo. Jambo hili siyo la kufuata kabisa, kwa sababu faida tuliyoiona ya TBS kudhibiti badala ya TFDA ni kubwa zaidi ukilinganisha na kama tukitaka kuirudisha TFDA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tufahamu kwamba chakula ni biashara. Usalama wa mimea na mifugo, vyote hivi vinazalisha bidhaa ambazo mwisho wa siku zinakuwa biashara. Sasa biashara inadhibitiwa na TBS. Mtu hawezi kufanya biashara popote, nje na ndani ya nchi kama hana ile nembo ya TBS kuonesha ubora wa ile bidhaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukishasema ubora ndani yake kuna usalama wa chakula. Yaani ukishasema kitu hiki ni bora maana yake ndani yake kuna usalama. Sasa ukikitoa TBS, TBS inabeba hivi vitu vyote kwa pamoja. Kazi ambazo zilikuwa zinafanywa na TFDA ndizo hizo hizo zilikuwa zinafanywa na TBS tangu mwanzo. Matokeo yake ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfanyabiashara alikuwa anapata kazi mara mbili, kwamba TFDA ilikuwa inatoa kibali cha jengo, kwamba lazima iangalie kwamba jengo hili linafaa kutengeneza chakula na kadhalika. Hapo hapo wanachukua sample kwa ajili ya kuangalia ubora wa bidhaa, na hizo sample walikuwa wanazipeleka TBS kwenda kuangalia ubora wa wake ili baadaye wampe huyu mtu kibali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini baada ya hapo huyu mfanyabiashara inabidi aende tena TBS. Kwa hiyo, huku TFDA anatafuta vyeti viwili; cha jengo anachukua na sample kwa ajili ya ubora halafu anakwenda tena TBS na kule TBS hawawezi kumpa ile nembo ya ubora mpaka tena warudie kujua je, huyu mtu anazalishia wapi hii bidhaa? Kwa hiyo, wanarudi tena kwenye jengo hiyo huduma inajirudia mara ya pili. Tena wachukue sample kupima waone kwamba hiki kitu kina ubora gani ili tuweze kumpa hii nembo aweze kufanya biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizo gharama zote ujue zinaenda na tozo, haziendi bure. Maana yake ni kwamba kule kwenye TFDA anatoa tozo kwa kazi ile ile ambayo inaenda kufanywa tena na TBS kwa kutoa tozo. Tulichokuwa tunafanya ni urasimu ambao mwisho wa siku viwanda vingine vilikuwa vinaenda nchi za jirani kwenda kufunguliwa kwa sababu ya vitu ambavyo tunavifanya kwa duplication.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ujue kwamba kazi za TFDA zinaweza kumezwa TBS kama zilivyofanyika, lakini kwa mujibu wa kisheria kazi za TBS haziwezi kwenda kufanywa na TFDA. Kwa hiyo, ilikuwa ni lazima mmoja amezwe ili kuondoa huu mlolongo wa tozo na usumbufu na upotevu wa mali ambao ulikuwa unafanyika. Kwa sababu kama mfanyabiashara inabidi sample apeleke TFDA zikapimwe, ni gharama; halafu akichukua sample nyingine apeleke TBS kwenda zikapimwe, ni gharama pia. Kwa hiyo, analipa tozo mara mbili na anapeleka vifaa mara mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata Serikali inabidi ununue mitambo ya kupima kwenye maabara za TFDA halafu hiyo hiyo mitambo tena na hizo maabara ukanunue tena TBS ambako na huko tena mtu akafanye. Kwa hiyo, tunafanya kazi mara mbili, na haya ndiyo malalamiko. Hata mchangiaji aliyepita hapa alipokuwa analalamika masuala ya OSHA na mengine yanamuumiza mfanyabiashara, ndiyo haya ambayo yalikuwa yanafanyika kwa kuwepo TFDA na TBS.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, busara ya Serikali iliyofanyika na ikaleta sheria hapa Bungeni kuivunja TFDA na kuipeleka TBS lilikuwa ni suala la busara sana. Kizuri zaidi, wale wataalamu wote waliokuwa TFDA na mitambo yao, hakuna mtu aliyefukuzwa kazi, wala mitambo haikupunguzwa; walibebwa kama walivyo wakapelekwa TBS na wakaenda kuendelea na ile kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kizuri kwa mfanyabiashara na mwananchi wa kawaida, zile tozo ambazo zilikuwa TFDA hazijahama, kwa sababu zile tozo tayari zilikuwepo TBS, zilikuwa ni mara mbili. Kwa hiyo, ina maana kule wale wamehama na mitambo na tozo zao mbovu wakaziacha huko huko. Kwa hiyo, wameenda kuendelea na tozo zilizokuwepo TBS.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tayari ule mzigo wa mfanyabiashara na mwananchi umeshapunguzwa. Maana yake ni kwamba na mazingira bora sasa ya biashara yameshafanyika kwa sababu tumepunguza vitu ambavyo vilikuwa duplication na ambavyo vilikuwa vinaleta hasara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Afya wanayo mambo mengi sana ya kufanya, kama wanatamani sana TFDA yako mengi ya kufanya hayajafanyika na ambayo ni ya muhimu. Kwa hiyo, naomba hili suala libakie huko huko TBS...
WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Isack kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Ummy.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naisubiri.
TAARIFA
WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mchangiaji ajikite katika hoja yake. Wizara ya Afya tuna mambo mengi kweli, wala hatung’ang’anii ku-regulate masuala ya chakula na vipodozi. Ni michango ya Waheshimiwa Wabunge. Kwa hiyo, ajikite katika michango ya Waheshimiwa Wabunge. Serikali ni moja na tunafanya kazi kwa kushirikiana kama Serikali, ahsante sana.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Isack unaipokea taarifa hiyo?
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hiyo naipokea, lakini nilikuwa nawajibu wale ambao walisema kuhusu Wizara ya Afya, hakusimama Mheshimiwa Waziri ili aseme tuna mambo mengi ili wasiendelee kusema. Kwa hiyo, nimesema kwa mujibu wa wale ambao walitaka mambo haya yaende Wizara ya Afya wakati huku Wizara ya Viwanda na Biashara chini ya Kamati yetu pia hili jambo ni zuri na linawapendeza wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali, na nawapongeza TBS kwa kazi nzuri na mpaka wameweza kupata vyeti mpaka huko nje ya nchi kwa jinsi ambavyo wameendelea kufanya kazi hii nzuri na tumepunguza mlolongo wa tozo kwa wananchi wetu. Naomba hili liendelee na TBS najua ina watu makini sana, wengine ni mate wangu tulisoma wote. Kazi hii inakwenda vizuri na tutaendelea kuisimamia vizuri Wizara yetu kuhakikisha hili jambo linawafurahisha wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja.