Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati Maalum iliyoundwa Kuchunguza Mgogoro wa Ardhi kati ya Mwekezaji kwenye Shamba la Malonje na Vijiji Vinavyolizunguka Shamba hilo Kikiwemo Kijiji cha Sikaungu katika Jimbo la Kwela

Hon. Joseph Anania Tadayo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati Maalum iliyoundwa Kuchunguza Mgogoro wa Ardhi kati ya Mwekezaji kwenye Shamba la Malonje na Vijiji Vinavyolizunguka Shamba hilo Kikiwemo Kijiji cha Sikaungu katika Jimbo la Kwela

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Spika, nami naungana na wenzangu kukushukuru kwa kunipa fursa ya kutumika ndani ya Kamati hii ambayo taarifa yake imewasilishwa leo.

Mheshimiwa Spika, naungana kabisa na Mwenyekiti kwa taarifa aliyoisoma na mapendekezo aliyoyatoa pamoja na wachangiaji wenzangu ambao wametangulia.

Mheshimiwa Spika, pendekezo kubwa la kwanza la kubatilisha umiliki wa shamba hili la Malonje kama ambavyo nitaeleza, ni pendelezo or rather ni maamuzi ambayo Serikali ilishayafikia mwaka 2015 lakini ikafika mahali kukatokea mkwamo ambao nitauelezea huo mkwamo ulitokana na kitu gani.

Mheshimiwa Spika, kishindo ambacho tumekiona uwandani ambako tulikuwa na maeneo mengine wakati wa Kamati hii ni vizuri sana kuelezea mambo machache ambayo ni vizuri tukayaona, mambo yenye utata katika mchakato huu mzima wa kubinafsisha shamba hili kwa mwekezaji huyu husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa aliyeomba kununua shamba, kampuni iliyoomba kununua shamba ni Kampuni inayoitwa Efatha Foundation Limited kwa barua ya tarehe 24 mwezi wa Machi, 2007. Mchakato ukaendelea na kwa mujibu wa barua ya RAS kwenda kwa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo ya tarehe 17 mwezi wa Januari, 2008, aliyeshinda ile zabuni na kupewa kununua lile shamba na kwa mujibu wa ile barua ilisema aliyesaini mkataba ni huyo huyo Efatha Foundation Limited, lakini uhalisia wa mambo ni kwamba mkataba wenyewe wa tarehe 28, mwezi wa Agosti, 2007 ulisainiwa na Registered Trustees of Efatha Ministry.

Mheshimiwa Spika, kisheria hawa ni watu tofauti kabisa na tulijaribu kufuatilia kama kuna uhaulishaji wa huo mkataba kutoka kwa yule ambaye alipewa originally Efatha Foundation Limited kwenda Registered Trustees of Efatha Ministry, hapakuwa na kitu kama hicho.

Mheshimiwa Spika, hati ya kumiliki ardhi ikatolewa kwa Registered Trustees of Efatha Ministry, ambao ndio waliosaini mkataba, lakini kwa sasa hawa Registered Trustees wa Efatha Ministry wamebadilisha jina na kuwa Registered Trustees of Efatha Church, lakini mpaka Kamati ikiwa kazini bado hati ilikuwa inasomeka vilevile Registered Trustees of Efatha Ministry. Kwa hiyo, utakuta kwamba aliyepewa shamba, aliyesaini mkataba na anayeendesha shamba kwa sasa tena ni kampuni nyingine inayoitwa Efatha Heritage.

Mheshimiwa Spika, sasa mimi siamini kabisa kwamba huu utata ni wa bure bure tu. Huu utata una sababu yake, nami nasema kwamba tunapoingia katika mambo makubwa kama haya, ni vizuri tukawa na uhakika kwamba tuna-deal na kampuni gani, inaitwaje, Wakurugenzi ni akina nani na kadhalika. Tusiruhusu hii kubadilisha badilisha kunakofanyika kinyume na mkataba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa hivi ni kwamba, ule mkataba uliosainiwa haujatekelezwa kwa sababu kifungu cha (6) na Kifungu cha (7) cha mkataba huo kinaweka masharti ya dhahiri kabisa kwamba eneo lile litumike kwa ajili ya ufugaji na mambo ya chakula cha mifugo, lakini matumizi kwa sasa ni mengine na hatujaona kwamba kuna addendum yoyote ya mkataba au mabadiliko yoyote yale ya mkataba.

Mheshimiwa Spika, sasa haya mambo yenye utata ni vizuri hata tunapotekeleza marekebisho haya tunayokusudia kuyafanya tuzingatie mambo kama haya. Kwa sasa shamba linalindwa na Kampuni inaitwa Funguka Security. Kwa wanaojua lugha nyingi wanafahamu kwamba Funguka maana yake ni Efatha na kwenye official search inaonesha kwamba wanaomiliki kampuni hii ni Efatha Foundation Limited na Registered Trustees of Efatha Church. Kwa hiyo, ni mtu yule yule anazunguka huku na huku.

Mheshimiwa Spika, hapa kuna swali la msingi kabisa kwamba ni kwa kiasi gani hizi taasisi zisizo za kiserikali, taasisi za kidini na vyama vya siasa, vinaruhusiwa kumiliki makampuni ya ulinzi yanayobeba silaha za moto? Hili jambo kuna haja ya kuliangalia vizuri kwa sababu litatuletea matatizo makubwa sana.

Mheshimiwa Spika, sababu mojawapo ya ushahidi wa mdomo ambao tuliupata kwa wahusika wenyewe wa hii kampuni ni kwamba, yule Meneja wa pale anasema, hawaajiri mtu ambaye amepita JKT wala Mgambo, wala mstaafu wa jeshi lolote lile. Kwa maana kwamba, wanaajiri watu wapya na training wanaifanya wao wenyewe. Sasa hii ndiyo inayoleta vitendo kama hivyo vya uvunjifu wa haki za binadamu ambavyo kama ingekuwa ni watu ambao ni trained vizuri, wangeweza wakavi-manage tu kwa utaratibu ule ule kulingana na wananchi walivyo, lakini hawa wanatumia nguvu kubwa kupita kiasi, matokeo yake haya mambo ndiyo yanatokea kwa sababu ya kukosekana kwa weledi kwa hawa watu ambao wanahusika.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa ajili ya haya makando kando yote na mambo ya uvunjifu wa haki za binadamu, Serikali iliazimia kwamba ifute. Haya maamuzi tunayopendekeza leo mwaka 2015 tayari Serikali ilishasema yafanyike, ikatoka ile notice of revocation na ilitoka sahihi kabisa, imetolewa na Afisa Ardhi Mteule kwa niaba ya Kamishna wa Ardhi, sasa changa la macho likaanzia hapo.

Mheshimiwa Spika, Registered Trustees of Efatha Ministry wakaenda Mahakamani wakaishtaki Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, watu ambao sio wahusika, sio wanaomiliki wa ile Hati na siyo waliotoa ile notice. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nawachekesha watu, nikasema ni sawasawa na mimi nikupangishe nyumba yangu halafu ukashindwa kulipa kodi, nikakupa notice ya kuhama, halafu unaenda unamshitaki mwanangu, halafu mnakwenda Mahakamani mnakubaliana. Ndiyo sasa ikafanyika Deed of Settlement kwamba huyu atakaa mpaka afe, asibughudhiwe na mtu yeyote, na yeye ndiyo mmiliki halali, lakini walioko Mahakamani ni Mwekezaji na Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga ambao sio waliompa shamba na siyo waliotoa notice of revocation, lakini kesi ikaendelea hivyo hivyo na hiyo settlement ikapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa yale maamuzi yamekuwa yakitumika kama hirizi. Akiguswa kidogo, aah, mimi nina amri ya Mahakama hii inanitambua. Thubutu! Amri ipi hiyo ambayo wala haipo! Mimi nasema hata sasa hivi Kamishna wa Ardhi akiamua kufuta ile miliki, anaweza kwa sababu hakuwepo kwenye kesi na wala amri haimhusu na amri iko very clear inamhusu yule aliyekuwa Mahakamani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ukiacha hiyo, bado sasa signatories waliosaini ile Deed of Settlement, upande wa mdaiwa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, Mstahiki Meya anasema mimi sikuwahi kusaini na hii signature imeghushiwa, anasema yeye mwenyewe. Upande wa mdai, Efatha Ministry aliyesaini ni mdhamini mmoja tu, yule mwingine alieyesaini ni District Church Pastor, ambaye kwa search ambayo tumefanya kule RITA hayupo katika trustees na pale walitakiwa wasaini wadhamini wawili waweke na lakiri ndiyo ule mkataba uwe halali. Kwa hiyo, amri hii ya Mahakama ambayo imekuwa ikitumika kama hirizi, mimi nasema siyo, yaani ni amri ya Mahakama inayohusu watu ambao wala hawamo kwenye mchakato huu kihalali na wala haizuii chochote kufanyika, labda tu kwa taratibu za utawala bora, basi kuwe na utaratibu tu wa kuiondoa ile amri ndiyo hilo lingine lifanyike.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo ripoti imeeleza, shamba lile liko ndani ya Halmashauri mbili. Liko Halmashauri ya Manispaa na Halmashauri ya Wilaya, lakini mchakato wote kuanzia mapatano yale na kusaini mkataba na malipo, vyote vimeenda kwenye Halmashauri ya Manispaa. Halmashauri ya Wilaya ambako hasa ndiyo tatizo kubwa liliko hawakuhusishwa, wao wameshangaa tu mtu ameingia amekaa hapo, ndiyo baadaye ikatoka amri kwamba na wao wagawiwe fedha kidogo. Laiti wangeshirikishwa leo hii wangejua kwamba kuna Mwekezaji anakuja katika eneo hili, lakini wao wameshangaa tu mtu anaingia pale.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninachosema ni kwamba, pendekezo lile la kwanza ni muafaka kabisa kwamba mchakato huu umevurugika kuanzia mwanzo. Ni null and void ab initio, yaani kuanzia kule mwanzo kabisa ulishavurugika huu mchakato. Kwa hiyo, leo hii mimi nalishawishi Bunge lako kwamba lisione wala lisisite kuunga mkono pendelezo hili kwamba miliki hii ya shamba la Malonje ibatilishwe na kazi ianze upya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)