Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Nami nakushukuru kwa kunipa heshima ya kuwa kwenye Kamati hii maalum.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nianze kuunga mkono hoja ya Kamati iliyowasilishwa na Mwenyekiti makini kabisa, mzalendo na anayejiamini, aliyetuongoza vema Wajumbe wake kuitenda hii kazi mpaka usiku wa manane bila kuchoka na tulikuwa tukianza kwa sala na kumaliza kwa sala. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni Tanzania peke yake ndiyo inaweza kuendelea kuwa na mwekezaji anayekiuka taratibu, anavunja haki za binadamu na bado akaendelea kuwa na eneo akajiita mwekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, aliyemaliza kuchangia, Mwanasheria nguli, Wakili Msomi, Mheshimiwa Tadayo amesema kabisa, mchakato huu uliharibika tangu mwanzo, hivyo Serikali haina kigugumizi chochote cha kwenda kubatilisha hii hati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ilikuwa clear, maelekezo ya Baraza la Mawaziri, Baraza lililopewa mamlaka kwa mujibu wa kifungu 54 (3) cha Katiba yetu, lilitoa maelekezo mahsusi, maana Baraza la Mawaziri linaweza likatoa maelekezo ya ujumla na maelekezo mahsusi. Moja ya maelekezo mahsusi ni kuuzwa kwa hekta 3,000 kwa ajili ya shughuli ya mifugo, na maelezo hayo yalikuwa yanataka mwekezaji akiwekeza kwa ajili ya mifugo kwa zile hekta 3,000 atawasaidia wananchi wa vijiji vinavyozunguka eneo lile kufuga kisasa. Lengo ilikuwa mwekezaji awekeze kwenye mifugo, afuge kisasa ili wananchi wa vijiji vinavyozunguka eneo lile waweze kunufaika na ufugaji wa kisasa na siyo vinginevyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, sasa maelekezo ya Wizara husika ambayo walipewa na Baraza la Mawaziri yalikuwa very clear na msisitizo kuwa mkishindwa kutekeleza agizo hilo mrudi mfanye consultation lakini hawakufanya hivyo. Matokeo yake enzi hizo akiwa Mkuu wa Mkoa, Mzee ninayemheshimu sana Ole Njoolay, aliamua tu kuuza hekta 10,000. Hekta 10,000 ni sawa na ekari 25,000 ndiyo maana nimesema ni Tanzania peke yake ndiyo bado tunaweza tukasema eti hili ni shamba halali la mwekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa hivi kilichoendelezwa, ameendeleza hekari 900 tu. Hapa walikuwa wanasema wameendeleza asilimia nne kwa miaka zaidi ya 17. Tujiulize, mwekezaji alikuwa na dhamira ya kuendeleza au alikuwa na dhamira ya kopoka kwa kuchukua ardhi. Alikuwa ana dhamira ya kuendeleza au alikuwa ana dhamira ya kuchukua ardhi?
Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, wananchi wa vijiji vile hawana sehemu ya kulima, hawana sehemu ya kufuga na ardhi hii haiongezeki lakini wananchi wanaongezeka. Basi sawa amefanya aliyoyafanya; amebadilisha matumizi ya ardhi, sisi tumeenda, hata ukienda kuangalia kwenye ufugaji, ni vibanda tu vya kawaida ambavyo Mtanzania mwingine anaweza kujenga. Ng’ombe pale hawafiki hata 200. Kwa zaidi ya miaka 17 bado anajiita ni mwekezaji! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia, mwekezaji huyu amekuwa akibadilisha matumizi mwaka hadi mwaka. Tumeenda tumekuta kuna mahindi pale yanalimwa, sijui kuna maua kidogo sijui ekari mbili, sijui kuna mkong,e lakini hakuna uwekezaji tangible unaompa mamlaka ya kuendelea kumiliki ekari 25,000 wakati wananchi wa vijiji vinavyozunguka wanapata shida. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumeshangaa tumeenda pale Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa anasema yeye haoni hao wananchi wenye shida ya ardhi. Hao watu wanaomsaidia Mheshimiwa Rais wanafanya kazi gani? Anasema, hakuna watu ambao wamejeruhiwa na risasi wala haki za binadamu zinazovunjwa.
Mheshimiwa Spika, Kamati yako tumeshuhudia, wakati tunawahoji baadhi ya watu wa kule walisema, kulikuwa kuna mazingira ya rushwa, kuna baadhi ya viongozi wanalimiwa mle, na wananchi wanasema hatuna pa kwenda kutoa malalamiko yetu kwa sababu tunaoenda kuwapa malalamiko wana manufaa kwenye lile shamba la mwekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, haya lazima tuyaseme, tuweke misingi ya utawala bora. Hatukatai uwekezaji kwenye nchi yetu, na tunapenda sana tupate wawekezaji wazawa, lakini hawa wawekezaji wazawa wasirudi kwenye kauli ya Baba wa Taifa kwamba Mkoloni mweusi anaweza akawa hatari kuliko mkoloni mweupe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni nadra sana kwenye Taifa letu akajitokeza Mama wa miaka 76 akalia amebakwa na mjukuu wake. Ni nadra sana. Nchi hii tuna mwekezaji ambaye mama ameenda kulima apeleke watoto shule, anakamatwa na walinzi wa mwekezaji kinachomwa kiroba halafu yale maji yake anamiminiwa bibi wa miaka 70 mwilini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumeyaona haya, tumeyaona halafu leo kuna viongozi kabisa wanasema ooh, yule mwekezaji ana haki. Tunahitaji wawekezaji watakaowanufaisha wananchi wanaozunguka maeneo hayo. Tunawahitaji wawekezaji wenye utu, wanaofuata misingi ya utawala bora, wanaofuata misingi ya haki za binadamu, na pia tunamhitaji mwekezaji ambaye atakuwa rafiki na sio adui wa wananchi wanaozunguka eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, watu wanabakwa, watu wanateswa na wanapigwa risasi kwenye nchi yetu ambayo kimataifa inasifika kuwa ni nchi ya amani. Halafu kuna viongozi wanawatetea, na bado wako kwenye hizo nafasi. Kuna wengine walishindwa kutimiza wajibu wao, lakini wapo, wamekuja kuhojiwa wanakwambia, tulifanya haya maamuzi, hatukuyafanya kwa sababu tulikuwa tunataka kukusudia kufanya makosa. Kweli!
Mheshimiwa Spika, umepewa maelekezo ya Baraza la Mawaziri kuuza hekta 3,000 halafu unaenda kuuza hekari 25,000, hekta 10,000 bila kufanya tathmini ya kujua gharama halisi ya eneo lako? Bila kutangaza tender kwa mujibu wa sheria ya nchi yetu, unauza hekari 25,000 kwa shilingi milioni 600 halafu mwekezaji anaenda kukopea kwa zaidi ya shilingi bilioni tatu. Tanzania hii! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa maslahi ya nchi yetu, kwa maslahi ya wananchi wa Mkoa wa Rukwa na kwa maslahi ya kuhakikisha Taifa hili lina wawekezaji wanaoweza kukuza uchumi wa nchi yetu, tubatilishe hati hii, twende tukapange upya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati na Kamati imekuwa na huruma hapa ya kwamba katika mgao tena anakuwepo, lakini ningekuwa mimi siwezi kuipangia Serikali, inaweza ikatafuta mwekezaji mwingine vilevile. Kama mtu amepewa shamba tangu mwaka 2007 hajaweza kuliendeleza, matokeo yake kuna migogoro na anafanya vitendo vya udhalilishaji na ukiukwaji wa haki za binadamu, Serikali ina mamlaka ya kuweka mwekezaji yeyote, sio lazima awe yeye. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa heshima ya kuwa Mjumbe wa Kamati Maalum na ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Naunga mkono hoja. (Makofi)