Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Buchosa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nikiri kwamba kuzungumza baada ya wazungumzaji wazuri kama hawa huwa ni changamoto kidogo, lakini najua Roho Mtakatifu atanisimamia na nitasema kile ambacho nataka kusema.
Mheshimiwa Spika, kwanza naanza kukushukuru wewe mwenyewe kwa uamuzi wako wa kuona nafaa kuwemo kwenye hii Kamati. Kwangu mimi hii ni privilege, ni heshima kubwa na nataka nikuhakikishie kwamba kazi yako imefanyika vizuri, imani yako haijapotea bure, nimekuwakilisha nilivyotakiwa, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nianze kwa kuunga mkono yote ambayo yamesemwa na Mwenyekiti wangu pamoja na wajumbe wengine wote. Nilichokikuta kule ni kwamba wananchi wa vijiji vile hawana ardhi ya kulima, huo ni ukweli wa kwanza ambao nimeukuta. Sehemu kubwa ya ardhi yao imechukuliwa na mwekezaji. Sasa kwa sababu hiyo, nakubali kabisa shamba hili libatilishwe na shamba hili liweze kugawanywa tena upya na wananchi wapate sehemu kubwa zaidi ya mwekezaji kama atapata.
Mheshimiwa Spika, naomba nikiri kwamba huwa ni mtetezi sana wa wawekezaji wa ndani, nimeshasimama mara nyingi hapa nikasema nitawatetea sana wawekezaji wa ndani ili waweze kumiliki uchumi wa nchi yao. Wajumbe wa Kamati watakumbuka, nilipokuwa natoa mchango wangu mwanzoni nilikuwa nasema, bwana huyu ni mwekezaji wa ndani lazima tumsaidie na yeye aweze kukua. Tukafunga safari kwenda Sumbawanga, kilomita nyingi.
Mheshimiwa Spika, nilipofika kule, niliyoyakuta, niliyoyaona nilibadilisha mtazamo wangu kuhusu wawekezaji wa ndani. Nimekuta umaskini uliopindukia wa watu wa vijiji vile. Hawana mahali pa kulima. Watu wa Sikaungu mwaka huu hawajalima kabisa, hata chakula kinakuwa tabu kukipata.
Mheshimiwa Spika, nimekutana na watu wamekatwa masikio, nimekutana na akinamama wengine wenye umri mkubwa kabisa wamebakwa. Nimekutana na kijana amepigwa risasi ziko kichwani.
Naomba nikiri nimeokoka na nampenda Yesu, lakini nilipoyaona yale nilijiuliza swali moja, huyu Mwingira, naomba niseme jina, huyu Askofu, na najua ananitazama hivi sasa, hivi huyu ni Askofu kweli? Haya mambo yanaweza yakafanywa na mtumishi wa Mungu kweli? Neno la Mungu kwenye Mithali 14:30 linasema, amuoneaye maskini amdharau Mungu na amhurumiaye maskini amheshimisha Mungu. (Makofi) [Maneno Haya Si Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]
Mheshimiwa Spika, baada ya haya niliyoyashuhudia, nilibadili msimamo wangu kabisa…
SPIKA: Mheshimiwa Shigongo, ngoja tuliweke sawa, jambo hili.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, tuliweke sawa.
SPIKA: Kwa sababu katika wale wawekezaji, zimetajwa kama taasisi. Kwa hiyo, Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Efatha nadhani na Efatha Foundation na kuna mahali nafikiri imetajwa Efatha Heritage. Sasa akitajwa mtu mmoja kwa jina lake atakuwa hajatendewa haki na Bunge kwa sababu zimetajwa taasisi. Yeye anaweza kuwa ni mkuu wa mojawapo ya taasisi hizo, lakini kwa maana ya hapa, mwekezaji ni hizo taasisi. Kwa hiyo, yeye kuwa kiongozi wa dini na hiyo nafasi yake ya uaskofu lazima somewhere atakuwa anaitendea haki hiyo nafasi ya uaskofu, kwa sababu kilichofanya uwekezaji sio Askofu, aliyefanya uwekezaji ni taasisi. Sasa huenda taasisi ziko chini yake, yeye ndiye Mwenyekiti na mambo kama hayo, mimi sijui kwa sababu sijazipitia. Sasa ili twende vizuri kwenye hoja hii, haya maneno hapa tunayaondoa ili yasilete mkanganyiko baadaye ili sisi tushughulike na mwekezaji. Wewe nenda na mwekezaji na hayo makampuni ambayo ndiyo yametajwa kama wawekezaji. Huyu aliyetajwa jina hapa kwa maana ya Askofu hajatajwa yeye kama ndiye mwekezaji. Ahsante sana Mheshimiwa Shigongo.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, naomba nikubali, lakini sasa nirekebishe kauli yangu iwe hivi, hivi huyu Efatha kweli huyu Efatha, Huyu Efatha kweli ni mwakilishi wa Mungu duniani? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, nimeondoa jina la mtu, huyu Efatha. Huyu Efatha amenibadilisha kabisa mtazamo wangu. Nimeokoka nasema nampenda Yesu na Biblia imetamka wazi ya kwamba amuoneaye maskini amdharau Mungu. Kwa matendo haya yaliyofanywa kama kweli ni maelekezo ya huyu Efatha image ya kanisa langu inaingia kwenye utata. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ngoja nielekee kwenye hoja, wananchi hawa ni maskini. Mimi nimezaliwa familia maskini sana na kuingia hapa ndani ya Bunge ni privilege. Mimi peke yangu kufika hapa kuna maskini wengine wengi sana wako nyuma wanaohitaji ardhi iwatoe kwenye umaskini wao.
Mheshimiwa Spika, sio mimi tu miongoni mwa wanasheria wako mmojawapo anaitwa Praisegod Lukio anatoka huko Sumbawanga, jirani kabisa na maeneo yale, amesoma shule kimaskini. Elimu imemsaidia kuwa mwanasheria. Tunahitaji kuwasaidia wananchi wa vijiji hivi ili wapate ardhi hii iweze kuwasaidia kusomesha watoto wao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, haitawezekana katika Taifa hili ninalolifahamu mimi kukaa na watu ambao wako juu ya sheria. Hakuna mtu ambaye yuko above the law; wote tunaheshimu Katiba ya nchi yetu, tunaheshimu sheria ya nchi yetu. Haiwezekani mtu mmoja anafanya vitendo vya kinyama kiasi hiki, taasisi moja inafanya vitendo vya kinyama kiasi hiki halafu hakuna hatua inayochukuliwa.
Mheshimiwa Spika, wananchi wanafanyiwa yote haya, mtu hafikishwi hata polisi. Mimi kama Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nitasimama na wananchi wa nchi hii, nitasimama na upande wa haki siku zote za maisha yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niseme, shamba hili ni kubwa sana. Nilitembea shamba lile unaenda umbali mrefu sana uko ndani ya shamba moja. Naomba sana Waheshimiwa Wabunge. Namwomba sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, Taarifa, hapa Mheshimiwa Jacqueline.
SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, kabla sijamsimamisha anayekuwa anazungumza ni kwamba sentensi yake anakuwa hajamaliza. Kwa hiyo na akirejea kwenye kuzungumza hataweza kumaliza ile sentensi yake. Kwa hiyo, ukisema taarifa, nakuwa nimeshasikia, akimaliza akifika mahali nakunyanyua, usiwe na wasiwasi.
Mheshimiwa Shigongo, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani.
TAARIFA
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa mchango mzuri wa Mheshimiwa Shigongo.
Mheshimiwa Spika, nataka niseme tu kwamba kutokana na hoja nzuri ambayo anaizungumza kwamba hakuna sheria yoyote wala hatua zozote zinazochukuliwa dhidi ya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia unaofanyika, maana tumesikia kuna kubakwa, kuna watu kulawitiwa, kuna kukatwa masikio. Sasa naomba kwa niaba ya Serikali Waziri mwenye dhamana ya ukatili wa kijinsia Mheshimiwa Gwajima akaishtaki Efatha kwa niaba ya Serikali. Ahsante.
SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, ili kesi iweze kufika Mahakamani ni lazima uchunguzi ufanyike na nadhani kwenye mapendekezo ambayo Kamati Maalum imeyaleta mbele ya Bunge hiyo ni sehemu kwamba uchunguzi wa kina ukafanyike ili ikijulikana hayo matendo yamefanywa na watu fulani basi watu hao wachukuliwe hatua za kisheria. Kwa hiyo, Mheshimiwa Gwajima yeye hawezi kwenda kushtaki lazima ule utaratibu wa kisheria tuliouweka ufuatwe.
Mheshimiwa Eric Shigongo.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa ya dada yangu Mheshimiwa Jacqueline Msongozi. Sasa nimalizie kwa kusema yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, nafahamu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Rais mwenye huruma, ni Rais ambaye anafikiria sana maisha ya watu wake. Katika hili naomba sana aliunge mkono Bunge lake Tukufu na kama ni kubadilisha hati ibadilishwe hati mara moja na wananchi waweze kupata maeneo ya kulima.
Mheshimiwa Spika, umaskini ni kitu kibaya sana. Naongea habari ya mwanasheria wako Lukio, anatoka maeneo yale yale, amekulia kwenye umaskini ule ule. Wazazi wake wameuza mahindi wamempeleka shule, leo ni mwanasheria. Tunahitaji watu wengine wengi katika nchi hii watoke familia maskini wawe kama sisi. Hawawezi kufika tukiendelea kuwanyang’anya ardhi na kumpa mtu mmoja.
Mheshimiwa Spika, nisiseme mengi sana, naomba niunge mkono hoja na ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)