Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Nkasi Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi niweze kuchangia jambo hili muhimu sana. Nachukua nafasi hii kukushukuru wewe kwa kuunda Kamati hii, ni kamati ambayo imelitendea haki Bunge, imetutendea haki Wanarukwa, imewatendea haki sana wananchi wa Mkoa wa Rukwa, hasa wanaotokea Wilaya ya Sumbawanga Vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati taarifa inasomwa hapa akili yangu ikawa inafanya rejea. Mwaka 2016 nikiwa Mbunge wa Viti Maalum nilitoa hiyo taarifa hapa Bungeni, malalamiko juu ya manyanyaso ambayo wanapata wale wananchi. Mwaka 2017 wakati nazungumza nikapewa taarifa na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kwela, 2017. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, zimeshafanyika taratibu mbalimbali kwenye eneo lile, tume mbalimbali zikitumia fedha za Serikali ambazo hazikuweza kuleta matokeo chanya mpaka limefika hapa ndani Bunge. Nashukuru kwa namna ambavyo kamati imeenda kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa. Wamefanya kazi kwa kujituma na wamekuja kuleta matokeo ya kile ulichowaagiza, kwa ulivyowaamini na wao imani hiyo wameilinda, wameleta hicho kitu hapa Bungeni.
Mheshimiwa Spika, pamoja na athari ambazo zimezungumzwa hapa ikiwemo unyanyasaji kwa wanawake na wananchi wa maeneo yale kuanzia mwaka 2014 mpaka 2017 nilikuwa naishi kwenye hayo maeneo. Natambua tuna kiasi cha kusema hapa ndani Bungeni, nakubaliana na mapendekezo yote ya kamati, lakini naendelea kulishauri Bunge lako, hatua stahiki zichukuliwe kwa kwenda kufanya tathmini ya kina na uchunguzi wa kina juu ya athari zilizojitokeza katika yale maeneo miaka yote hii mfululizo.
Mheshimiwa Spika, wapo wanafunzi ambao nilikuwa nasoma nao kuanzia 2014, baada ya machafuko yaliyokuwa yanaendelea waliacha masomo, maisha yao yameharibika mpaka leo. Hatuwezi kujua, pengine tungepata Rais kutoka pale, maisha yao yaliishia pale. Ninajiuliza, hivi tumefikaje hapa? Nini kilikosekana miaka yote mpaka leo? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza, nikagundua tulikosa uzalendo kwa wale waliopewa nafasi ya kuaminiwa kumsaidia Mheshimiwa Rais. Malalamiko haya yametolewa ndani ya Bunge zaidi ya mara 17, lakini yamekuja kuonekana na uzito zaidi na Mbunge wa Jimbo wa sasa. Pamoja na nia njema ambayo uliionesha na dhamira hii kwa hatua ambayo tumefikia sasa hivi, Taifa letu hatuwezi kusema hatuwahitaji wawekezaji, tunawahitaji wawekezaji, lakini tunahitaji uwekezaji wa namna gani? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba, kinachofanyika leo pale, Serikali inachopata na athari walizopata wananchi ni sawasawa? Athari zilizojitokeza mpaka leo kuna haja ya kuendelea kufikiria kuwa na wawekezaji wa namna hii? Najiuliza, shida ilikuwa ni makubaliano yaliyowekwa kwenye mkataba?
Mheshimiwa Spika, shida ilikuwa kuna jambo lingine lililokuwa nyuma ya kile kilichoandikwa kwenye documents zile? Shida ni kuwa mpaka hapa tulipofika ni kwamba viongozi waliokuwepo kipindi chote na hawakujua athari za haya yaliyojitokeza au tuliamua kuweka pamba masikioni?
Mheshimiwa Spika, leo yule ambaye anayeishi na risasi kichwani, tunaweza kuthaminisha na nini kwenye nchi yetu? Yule mama ambaye alibakwa, sijui hata kama walikwenda kupimwa. Inawezekana kuna athari kubwa zaidi ambazo wamezipata; ndiyo maana naendelea kusisitiza kuna haja ya Serikali kwenda kufanya tafiti za kina juu ya athari ambazo zimejitokeza. Hata kama haya ambayo yameelezwa hapa yakithibitika kwamba ni kweli yalifanyika, ni kweli yalitokea, hatua siyo kubatilisha tu. Hatua zichukuliwe kwa wote ambao wamefanya makosa haya kwa mujibu wa sheria zetu za nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kufanya hivyo wananchi wataendelea kuamini kwamba Serikali imesikiliza na imechukua hatua. Kama wamekwenda wameona makovu, siku ambayo Mbunge wa jimbo anatoa hoja yake hapa ndani tukasimama, yule mgonjwa akawa amekimbizwa Hospitali ya Rufaa Mbeya. Hatua zilizochukuliwa mpaka leo ukiziangalia angalia unagundua yanaonesha hapo katikati kuna mambo ya rushwa.
Mheshimiwa Spika, siyo kwamba watu wote hawafahamu, kule Rukwa siyo kwamba hatuna wasomi, siyo kwamba wateule wote wa Mheshimiwa Rais waliopo kule hawajui kwamba kulikuwa na shida, kwa nini wamesubiri?
Mheshimiwa Spika, kuna jambo moja tu la kujiuliza, kama mwananchi huyu amepigwa risasi, tena hatua zilianza kuchukuliwa baada ya ripoti kuja Bungeni, waliopo kule wanaohusika na vyombo vya ulinzi ndio wanaanza kuulizwa wakati wao ndio walipaswa watoe taarifa mapema na hatua zichukuliwe kabla ya kuja hapa ndani Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, changamoto hii iliyojitokeza katika Shamba la Malonje athari yake ni kubwa kuliko hivi inavyoelezwa. Kuna wakati ulifika ukienda kwenye nyumba wanaume wote wamekimbia. Nini kinatokea? Athari yake siyo kwa ajili ya mama tu. Ndiyo maana nasema kuna wanafunzi niliokuwa nasoma nao mimi waliacha shule. Haki yao ya msingi ya elimu wakanyang’anywa kwa sababu ya mazingira.
Mheshimiwa Spika, kuna haja, hatua hii ambayo umeitoa leo, hatua nyingine ziendelee baada ya hapa mapema zaidi. Kama kuna viongozi wameshiriki kwa namna yoyote ile hatua zichukuliwe. Wakati tunakwenda kufikiri kupima upya, tuangalie mazingira ambayo tutaacha wananchi wa eneo lile wakiwa salama. Maisha yetu watu wa Rukwa ni kilimo na ndiyo uchumi wetu. Leo ukiwambia wasilime, unataka wafanye nini? Unataka kuzalisha vibaka mtaani? Maisha ambayo sisi hatukuyazoea. Pamoja na kwamba kuna changamoto kwenye hizo hatua zilizopitiwa hapo, namna ya kuongeza mkataba, mkataba wenyewe.
Mheshimiwa Spika, hivi nchi yetu mbona ina wanasheria wengi nguli kabisa? Kama shida ilikuwa ni kwenye mkataba, hili si lilikuwa suala la kufanya maamuzi tu. Sasa mpaka athari hizi zimejitokeza, tunataka nini kingine kijitokeze baada ya haya mambo yaliyotokea Mlonje?
Mheshimiwa Spika, nashauri pamoja na mapendekezo haya ambayo Kamati imeleta, kuna haja sasa wanapokwenda kuchukua hatua yoyote, ushirikishwaji wa jamii ile uwe wa kina. Hilo ni la kwanza.
Mheshimiwa Spika, la pili wananchi wale wanahitaji kupewa elimu, kama ni uwekezaji wajue wao wananufaika nini na uwekezaji huo na hili jambo limekuwa shida sana kwa Taifa letu. Tunawekeza, wananchi wanaozunguka lile eneo la uwekezaji hawaoni manufaa ya uwekezaji huo. Lazima tujiulize tunawekeza kwa ajili ya nani? Kama ni tunawekeza kwa ajili ya Watanzania, je Watanzania hao wananufaika na huo uwekezaji?
Mheshimiwa Spika, lazima tukae na tuwe tunafikiri tena…
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
MHE. AIDA J. KHENANI: …haya matatizo yanayojitokeza leo yatufundishe…
SPIKA: Mheshimiwa Aida Khenani, kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Felista Njau.
TAARIFA
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ahsante, nilitaka nimpe Taarifa Mheshimiwa Khenani kwamba, pamoja na usaidizi utakaofanyika, tuombe pia wasaidizi wa mambo ya kisaikolojia. Wanawake waliopata shida ya kubakwa na vijana waliopigwa, wapate usaidizi wa kisaikolojia mapema, ahsante.
SPIKA: Mheshimiwa Aida Khenani, unaipokea Taarifa hiyo?
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nimeipokea Taarifa hiyo na niendelee kusema, tunapozungumzia suala la ekari 25,000 ni lazima tujiulize ukubwa wa lile eneo pale na idadi ya watu waliopo. Je, kuna haja ya kuendelea kuwekeza kwa namna hiyo? Tunategemea ile jamii itaishije?
Mheshimiwa Spika, pamoja na nia njema inayoendelea, niendelee kusema kama watajiridhisha, wakagundua kuna ukiukwaji uliofanyika pale wa kina kabisa, sitegemei kwamba tutaipata faida ya yeye kuendelea kuwa mwekezaji kwenye maeneo haya. Kuna haja ya kufikiri upya, kama bado wanafikiri kuhusu mwekezaji, basi ni tutafute mwekezaji mwingine ambaye hawezi kuleta migogoro kama hii na ataleta mahusiano mazuri kati ya yeye mwekezaji na jamii inayomzunguka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja kwa yote yaliyopendekezwa na Kamati. (Makofi)