Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Momba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naomba niungane na wenzangu kutumia nafasi hii kukupongeza sana kwa jambo zuri na kubwa ambalo umelifanya la kuunda Kamati hii ya kizalendo. Pia nitumie nafasi hii kuendelea kuwapongeza Wabunge wenzangu ambao walikuwa ni Wajumbe wa Kamati hii kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wamefanya. Siyo kwamba wamefanya kwa watu wa Jimbo la Kwela (Malonje), wamefanya kwa ajili ya Watanzania wote. Pia, naamini hata Watanzania ambao wanasikia mjadala huu wanaendelea kuwaombea
Mheshimiwa Spika, changamoto kama hii ipo katika maeneo mengi kwenye nchi yetu na katika nyakati tofauti inawezekana Wabunge wamekuwa wakija hapa wakieleza, wakati mwingine kupuuzwa na kutokusikilizwa. Matokeo yake ndiyo yanaleta madhara makubwa kama haya. Laiti kama Wabunge wangekuwa wakija na kusema changamoto zao hapa na zikachukuliwa harakaharaka na watu wakaacha kulindana, yamkini tungekuwa hatufiki kwenye matokeo kama haya ambayo tunaendelea kufika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimeshawahi kusimama hapa Bungeni, juzi tu hapa kwenye Bunge la Bajeti ambapo Waziri akiwa ni Mheshimiwa Jerry Silaa. Nikarejea maneno ya Baba wa Taifa ambayo aliyasema mwaka 1958 na leo narejea tena. Baba wa Taifa alisema hivi:
“Katika nchi kama yetu ambamo Waafrika ni maskini na wageni ni matajiri kuna uwezekano mkubwa kwamba, mwafrika akiruhusiwa ardhi yake katika miaka 80 au 100 ijayo, ardhi yote ya Tanganyika itamilikiwa na matajiri na wageni na wenyeji watakuwa watwana, lakini hata kama wageni wasingekuwa matajiri litaibuka tabaka la Watanganyika (ambalo ndilo hawa akina Efatha Ministry) matajiri na wajanja. Tukiruhusu ardhi iuzwe kama njugu, katika muda mchache kutakuwa na kundi dogo la Waafrika wakiwa na ardhi na wasiokuwa na ardhi watakuwa ni wengi ambao watakuwa ni watwana.” Maneno ya Baba wa Taifa yaliyoongelewa mwaka 1958.
Mheshimiwa Spika, wako Watanganyika wenzetu wajanja ambao ndio hao akina Efatha Ministry, ambao wameibuka kwa sababu wana misuli na wana pesa wanaendelea kusumbua wenzao.
Mheshimiwa Spika, mfano tu, kama wa sakata hili la Shamba la Malonje; kule Momba kuna mwekezaji mmoja pia ana tabia kama hii hii, anafanya matukio kama haya haya na anaendelea kunyamaziwa. Wanataka kuna siku tuje hapa tuanze kueleza mambo mengi, ameshadhuru watu, watu wameshaumia na wameshateseka. Nafikiri Serikali itumie wakati huu kujifunza kupitia Shamba la Malonje. Kwa maeneo mengi ambayo hayapo hapa Tanzania na yanapitia changamoto kama hizi na Wabunge wameshawahi kueleza.
Mheshimiwa Spika, halafu tabia ya kuwadhihaki Wabunge, Mbunge akija akiongea hapa wanasema ni mambo ya siasa. Huwa najiuliza Rais anafanya jambo gani? Mheshimiwa Rais wa nchi hii kupatikana na watu wote aliowateua kama Mkuu wa Mkoa na viongozi wote, ni kiongozi wa siasa na ndiyo atatengeneza mfumo tulionao. Bunge tunafanya kazi kwa siasa. Tukija kutetea watu hapa, kwa nini wanaibua maneno ya kusema ni mambo ya kisiasa?
Mheshimiwa Spika, kule Momba kuna huyu mwekezaji anaitwa Jihumbi, ameshawahi kuteka watu zaidi ya watu 50 kijijini. Alivyowateka akawanyang’anya simu na mengine ambayo aliyafanya huko anajua yeye mwenyewe. Yupo tu anaendelea na anaendelea kuchukua ardhi ya kijiji.
Mheshimiwa Spika, kwa nini tufike hatua ambayo wanawake wanabakwa kwenye ardhi ya kwao wenyewe? Halafu ni tabia gani watu waliotunza ardhi yao wenyewe miaka na miaka, wamezaliwa na babu zao wamezaliwa hapo, halafu anakuja mtu mmoja tu eti kwa sababu ni Mtanzania ambaye ni bepari (beberu) anakuja anaanza kuwatesa wenzake, anaangaliwa tu eti kwa sababu ni Mtanzania na anaruhusiwa kumiliki ardhi mahali popote pale.
Mheshimiwa Spika, kwa kweli nafikiri hata hii sheria pia inapaswa kubadilishwa, kwa sababu kusema tu Mtanzania anabidi akamiliki ardhi mahali popote inawatesa baadhi ya watu, inawaumiza na ndiyo matendo kama haya yanaendelea kuja. Nafikiri ni wakati sasa Serikali itumie tukio hili la watu wa Jimbo la Kwela kujirekebisha na kwenye maeneo mengine ili Watanzania wasiendelee kunyanyasika.
Mheshimiwa Spika, tunakushukuru sana kwa jambo la kiungwana na Wabunge wenzangu ambao walipata hiyo nafasi Mungu awabariki kwa uzalendo. (Makofi)