Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwanza kabisa nianze kwa kukupongeza kwa maamuzi yako magumu ya kuunda hii Kamati na kwa kweli Kamati imetutendea haki kama Wabunge. Nimpongeze sana Mwenyekiti, Mheshimiwa Profesa Manya kwa kuiongoza Kamati ambayo kwa kweli kwa wale tuliokuwemo toka mwaka 2015 hili suala la Malonje siyo geni na lilimwondoa Malocha. Pia hata Mbunge aliyepo kama Bunge na Serikali hawatamsaidia na huyu watamla kichwa. Tunapambana na watu ma-giant, lazima tuwaambie ukweli. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni lazima tuchukue maamuzi magumu, najua ameitwa mchochezi, lakini mimi kama Musukuma namwona ndiye atakuwa Mbunge wa kudumu pale kama Bunge na Serikali litaamua kumsaidia kwenye hili suala. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, taarifa ni nzuri sana, Kamati imefanya kazi nzuri na sisi Wabunge ambao hatukwenda kule tumeona taarifa ni nzuri. Nilikuwa najaribu kuona, wakati Mheshimiwa Profesa Manya anawasilisha, Wabunge majirani zangu kama nane hapa walikuwa wanatiririsha machozi, hiyo ni kuonesha kwamba kweli watu wengi wameguswa na suala hili.
Mheshimiwa Spika, najaribu kujiuliza kwa nini tunawaficha hawa watu kwa kutowataja. Kwa sababu Kamati inajaribu kuingia halafu inatoka. Sijui kama kuna sababu za kisheria zinazotukinga kuwataja. Yaani kuwaweka wazi wale viongozi wa mkoa ambao walifika mahali waka-mislead Kamati kwamba nendeni huku halafu Kamati nayo ikajiongeza kwenda kuona hayo mashambulizi yaliyojitokeza.
Mheshimiwa Spika, ningeomba kama itakupendeza kabla hujalihoji Bunge, tungetamani kuwajua ili tuisaidie Serikali. Saa nyingine tusioneane aibu kwa sababu hawa ni viongozi wamepelekwa kwa ajili ya kumsaidia Rais kusimamia wale wananchi na wala siyo kusimamia wawekezaji. Wawekezaji wanakuja baada ya kuwa wananchi wamekaa vizuri. Kama utaratibu utakuruhusu ni vizuri tukawajua ili kama itawezekana tuweze kushughulika nao.
Mheshimiwa Spika, najaribu kujiuliza, hata kabla ya maazimio na hatua za Kiserikali tumeoneshwa mtu amekata mtu masikio, amepigwa risasi, mwingine ana risasi kichwani na viongozi wapo na waliotoa hizo PF3 wapo. Hivi hawa viongozi wanaotakiwa kupelekwa kushtakiwa wakiwa madarakani ni akina nani kama siyo hao walioko huko mikoani? Inawezekanaje mpaka Kamati ikatuletea hizi taarifa? Ina maana wao hawajawahi kuyaona haya mambo? Maana yake wao wamefunga mipaka ya wananchi kuwaona wao, lakini ni rahisi wao kwenda kuwaona wawekezaji. Kwa hiyo, ni vizuri Serikali isiache kwa kweli hii taarifa ikapita hivi hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, najua Bunge tutatoa maamuzi lakini Serikali tunaihitaji; Mama tunafanya kazi ya kukusaidia, tunaomba atushike mkono kwenye hili. Ingekuwa mimi ni msaidizi wake wa karibu, leo hii tungekuwa tunamaliza hapa na karatasi wanazo mkononi. Haiwezekani tunafumba macho, tunasema tusitaje mtu. Efatha anajulikana ni nani, huyu ni kiongozi na ni taasisi inashughulika na imani za kiroho. Ina kampuni ya ulinzi, inafundisha miezi mitatu, hao wanaofundishwa wanakwenda kupewa bunduki wanatungua risasi tuh tuh! Kwa jina la Yesu! Aah, hapana! Haiwezekani! (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, mimi ni mwenyeji kidogo Nairobi. Haya mambo yalianza kimzaha kimzaha hivi Shakahola, msipite huku, mkipita huku tuh! Kwa jina la Yesu! Anasema eneo la dini, walichokwenda kukikuta ndicho hicho. Kama haya wameyaona machache, wale waliojitokeza kuwaambia, je, wale ambao walikufa wakazikwa bila ninyi kuwaona?
Mheshimiwa Spika, sasa ni vizuri Serikali iwe serious. Hili suala limechukua muda mrefu na watu wamekwishajulikana na hizi Imani, Mungu anisaidie tu niendelee kubaki kwenye Roma kwa kweli. Naona kama tunataka kuingia kwenye majaribu. Wiki jana tu hapa tumefukuza kiboko ya wachawi huku tena tunaibuka na Efatha…
MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, kwa kweli tufike mahali tulimalize hili suala…
SPIKA: Mheshimiwa Musukuma, sijui ni nani alikuwa anasema Taarifa kabla kengele haijagonga. Mheshimiwa Mwijage.
MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa Mzungumzaji kwamba, tusisahau suala la watu kuuawa katika ardhi yao ndani ya Tanzania, nina imani kama kuna mtu alilia nadhani huyo amenifuata mimi. Mheshimiwa umenifuata mimi na ufuate mfano wangu!
Mheshimiwa Spika, kama ni kulia mimi nimelia, kama ni kudhalilishwa, mimi nimedhalilishwa, lakini imani haikuhusika. Nimewahi kusema there is the problem of governance ina-centre kwenye governance.
Mheshimiwa Spika, nikueleze dwell around the governance, issue ipo kwenye governance, hawa ambao hawatimizi wajibu ni governance haina mahusiano yoyote na dini. Sikupenda kuzungumza hili, nimelia mpaka ofisini kwako sikuja na tasbihi au na rozali au na maji ya kukanyaga ni governance, yaani governance, huyu amelia kufikia mimi huyu? Aah! (Kicheko/Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Musukuma unaipokea taarifa hii?
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, naipokea.
Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie kwa kusema hivi, mimi ni mkopaji wa mabenki lazima niwe wazi, kama valuation imetoa milioni 600 baada ya mwaka mmoja hujaendeleza chochote ukapata bilioni tatu, it means valuation yake ilienda bilioni tano na kitu, sasa huyu aliyeipitisha shilingi milioni 600 akaja akapitisha na ya bilioni tano..
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, kuna kitu gani jamani au…
SPIKA: Mheshimiwa Musukuma naona kuna taarifa mbili unataka kupewa na muda wako ulikuwa umeshaisha, nilimsikia Mheshimiwa Kigwangalla kwanza kabla yao. Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla.
TAARIFA
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, jambo analoliongelea la valuation ni katika mambo muhimu sana yaliyopelekea sisi kutoa hayo mapendekezo, sasa nimeona nisiliache likapita hivi hivi niliweke sawa, kwamba paliuzwa bila valuation kufanyika, paliuzwa bila mipaka ya shamba kuhakikiwa.
SPIKA: Mheshimiwa Musukuma unapokea taarifa hiyo?
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, naipokea kwa sababu napiga mambo ya kidaktari, kwa hiyo naipokea taarifa ya daktari mwenzangu.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na, naunga mkono hoja ya Kamati. (Makofi/Kicheko)
SPIKA: Mheshimiwa kuna taarifa nyingine, Mheshimiwa Flatei Massay.
TAARIFA
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Musukuma pamoja na mchango wake mzuri, valuation isingeweza kufanyika kwa sababu upo msamiati unasema “penye uzia penyeza rupia”. Kwa hiyo hicho kisingeweza kufanyika kwa sababu rupia ilipenya. Ahsante. (Kicheko)
SPIKA: Mheshimiwa Musukuma unapokea taarifa hiyo?
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa hiyo.
Mheshimiwa Spika, namalizia kwa kusema Kamati imefanya kazi nzuri Mheshimiwa Spika wetu umefanya kazi nzuri na Bunge lako hatutakuangusha kwenye maamuzi. Baada ya maamuzi yetu tunaiomba Serikali inayoongozwa na Mama Samia Suluhu Hassan, wasomi na wataalam wako wengi mtaani, iondoe wote kule ipeleke wapya.(Makofi)