Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Mrisho Mashaka Gambo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arusha Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya changamoto ya muda, mimi nitajielekeza kwenye maeneo makubwa mawili; eneo la kwanza ni eneo la changamoto na eneo la pili ni mawazo yangu kwenye namna gani tunaweza tukafikia idadi ya watalii 5,000,000 kama ambavyo Ilani ya CCM imeelekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna changamoto kwenye eneo la service levy, ambayo kwa mujibu wa sheria inatakiwa wafanyabiashara walipie 0.3%. Changamoto iliyopo kwenye sekta ya utalii fedha ambazo wanazipokea siyo zote ni fedha zao. Wanapokea kama hela kwa ajili ya park fee, nyingine kwa ajili ya concession fee, nyingine kwa ajili ya masuala mbalimbali yanayohusiana na suala la utalii, ambayo mwisho wa siku wao wanakwenda kuyalipa pengine Ngorongoro, TANAPA na kwenye hoteli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo hiyo, inakwenda ku-charge-iwa kwa mwenye hoteli kwa maana ya service levy lakini pia ana-charge-wa na tour operator. Tulidhani kwamba ni vizuri Sheria ikaangalia badala ya ku-charge kwenye turnover pengine tuka-charge kwenye gross profit ya wafanyabiashara. Pia, kuna hali ya kutumia nguvu kwenye kukusanya nadhani masuala kama haya yamepitwa na wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni changamoto kuhusiana na mountain climbing TALA ambao wanalipa wale wanaopandisha watu wa utalii. Kubwa zaidi wanaofanya hiyo kazi ni Vijana wa Kitanzania ambao wamejiajiri kwenye fursa hizo na gharama yake ni dola 2,000. Tulikuwa tumetoa mawazo toka huko nyuma badala ya dola 2,000, walipe dola 500 kwa sababu mchakato huu ulifanana na tour operators. Zamani walikuwa wanalipa dola 2,000, utaratibu ukabadilika ikatoka dola 2,000 ikawa gari moja mpaka tatu dola 500. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunadhani kwamba kwa wenzetu mountain climbing TALA wao gharama ya kupandisha watalii; pengine kwa wanaopandisha watu 50 mpaka 100 walipe dola 200; wanaopandisha watu 100 mpaka 300 labda walipe dola 300; watu 300 mpaka 500 walipe dola 500; na 500 na kuendelea iwe dola 1,000, kadiri ambavyo Wizara itaona inafaa ili kutoa fursa ya ajira hasa kwa Vijana wa Kitanzania ambao wanatumia fursa hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, changamoto tatu, Mheshimiwa Waziri, wale watu wote wenye camp kwenye hifadhi zetu labda Serengeti, ukienda Ngorongoro wanapokwenda kule ndani wafanyakazi wa camp wenyewe wanalipishwa fedha na Serikali yetu shilingi 3,500 kila siku. Mtu ameajiri watu wanakwenda kutoa huduma ya kupika, kuhudumia watu na kufua, lakini bado Serikali pia inakwenda kuwa-charge fedha mpaka hao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani hili jambo Serikali ingetengeneza vitambulisho maalumu vya kuwatambua wafanyakazi wote wanaofanya kwenye camp. Wasilipe chochote, kwa sababu wao ni wafanyakazi tu, kuwapa mzigo wa kulipa nadhani siyo sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata magari ambayo yanapeleka vyakula na vitu vingine, kila yakipita kwenye mageti yana-charge-iwa fedha. Tunadhani kwamba magari pia yangetambuliwa yasilipe chochote ili kuendelea kutoa motisha na fursa kwa watu wetu wa utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamo ya nne ni kuhusiana na ile guiding fee; guiding fee hii ni leseni tu, ni utambuzi tu. Leo Serikali inachukua dola 50 kwa kila guide. Wakati leseni ya magari pia wanalipia 70,000 kwa miaka mitatu. Tulidhani kwamba kama hatuwezi kutumia leseni ya magari kuwatambua, kwa sababu hawa ma-guide ni madereva. Basi pengine uweke utaratibu wa miaka mitatu basi leseni yao ya utambuzi izisidi kiasi cha shilingi 70,000 kwa hiyo miaka mitatu ili Serikali iwatambue na iwe rahisi kuweza kufanya shughuli zao vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto pia kubwa ya barabara kwenye hifadhi zetu; nenda Ngorongoro, nenda Serengeti hali ya barabara ni mbaya sana, kwa sababu Serikali imechukua fedha zote. Halafu kwenye kurudisha imekuwa ni mtihani. Tumefurahi kuona mwaka huu umekuja na pendekezo ya kwamba fedha zile waachiwe Ngorongoro na TANAPA na mamlaka nyingine ili waweze kukusanya na kuweza kutumia inaweza kuwa ni rahisi pia kwenda kusimamia hali ya barabara zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, hoja yangu ya pili, ni kuhusiana na mwenendo wa utalii duniani. Leo ukiangalia sisi Tanzania tumepeana target ya watalii 5,000,000 lakini tuangalie dunia ipoje? 5,000,000 yenyewe ambayo hata hatujaifikia bado.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukienda nchi kama Afrika Kusini kwa mwaka 2022, wao walipata watalii 8,500,000, lakini idadi yao ya watu ni milioni 60.4 na walipata mapato kiasi cha bilioni 13.2. Ukienda Morocco mwaka 2022 idadi yao ya watalii waliopata ni 14,000,000 kwa mwaka 2022, watu wao wapo 38,000,000 na walipa 9.8 billion, ukienda Ufaransa wao walipata watalii milioni 21.6, wapo milioni 64.8 na walipa bilioni 58.9.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi leo tumejiwekea target kama Watanzania ya kupata shilingi 6,000,000,000 na watalii 5,000,000 na ukizingatia kwamba, kwa mwaka 2022, Tanzania tulikuwa na watalii milioni 1.8, tupo milioni 69.4 na tulipa 3.4 billion.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa nadhani kwa maoni yangu, ili tuweze kuanza hata hawa tuliojiwekea wachache wa 5,000,000. Je, tuna mpango gani kama Taifa? Tumejipangaje? Je, viwanja vyetu vya ndege vina uwezo wa kuwa-accommodate watu hao? Ukiangalia leo ili uweze kupokea watalii 5,000,000 kwa mwaka maana yake unahitaji kuwa na international flights 68 kila siku zitue katika ardhi ya Tanzania. Utahitaji pia kila siku uweze kupokea watalii 13,698 na utahitaji pia uweze kuwa na magari ya uhakika kiasi cha 3,424.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukichukua magari 3,424 yakiondoka na watalii kwa mfano kwa siku sita na kila siku kama wanaingia 13,698. Maana yake siku sita zilizobaki hizo wakati magari yale yapo porini unahitaji pia idadi ya magari kama hayo. Kwa hiyo, utahitaji magari 20,544. Je, tumejipangaje kama Taifa kwenye eneo hilo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye accommodation na kwenyewe, kama tunapokea kwa siku 13,698 ili tufikie hao 5,000,000 kwa mwaka mzima. Tutahitaji vitanda 13,698, lakini vitanda hivyo kama leo wamekuja 13,698 na wakikaa siku sita, je, wakija wengine kesho na kesho kutwa watakaa wapi? Maana yake utahitaji vitanda 82,188 kama watalii watakuja kwa 100%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utahitaji pia kuwa na international brands kama Meliá pamoja na Hyatt na nyingine ambazo zinasaidia pia kuleta idadi ya watalii. Pia, utahitaji pia human resources tumejipangaje kwenye human resources sisi kama Taifa? Waiters kwa ajili ya kudumia watu, wapishi, room attendants’ na mangers, kwa sababu ukiangalia watu wetu wahifadhi hao kwa asilimia kubwa wanapambana kupata wahudumu wazuri. Ndiyo maana wengi wanawatoa mpaka nje ya nchi kwa ajili ya kuja kuhudumia. Je, sheria zetu zimekaaje kwenye hii hii tunayouizungumzia human resources? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna TDL (Tourism Development Levy) one percent inafanya nini toka imeanzishwa imekusanya kiasi gani? Impact yake ni nini kwenye kukuza utalii wetu, kuna skills development levy ambayo ni four percent, toka imeanza kukusanywa imeongeza ujuzi wa kiwango gani kwa Watanzania ambao wanatakiwa kuhudumia sekta hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia je, sheria zetu zimekaaje na zenyewe. Kwa mfano unaangalia kwenye VAT, Tanzania VAT 18% ukienda Zanzibar tu, nchi moja na Tanzania yenyewe ni asilimia 15, ukienda Kenya asilimia 16, Africa Kusini asilimia 15, Namibia asilimia 15. Kwa hiyo, unaona kuna changamoto kubwa sana katika sheria zetu ni lazima tuzi-harmonize.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kumalizia…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Gambo ahsante sana hitimisha.

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, samahani dakika moja tu. Hata kwenye wawekezaji wetu kule hifadhini wanapewa maeneo ya kuwekeza lakini hawapewi hata title kwa ajili ya kuwekeza, wanawezaji ku-access finance kwenye maeneo mbalimbali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, kuna changamoto ya muda lakini kuna mengi ya kuchangia kwenye sekta ya utalii.(Makofi)