Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Priscus Jacob Tarimo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa nafasi hii ya kuweza kuchangia Wizara hii nyeti sana ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa ninampongeza sana Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii pamoja na Makamu wake na Wanakamati wote, kwa kweli wamefanya kazi nzuri ambayo inaonesha kule ambako wananchi wameelekea. Pamoja na pongezi hizo nimpongeze Mheshimiwa Waziri Dada yangu Mheshimiwa Angellah Kairuki, Naibu Waziri Kaka yangu Mheshimiwa Dunstan Kitandula, Katibu Mkuu Dkt. Abbas pamoja na Naibu Katibu Mkuu CP. Benedict Wakulyamba kwa sababu kwa kweli pamoja na changamoto nyingi zilizopo kwenye Wizara yao, nao wamefanya kazi kubwa, bado tunaendelea kuona namna ambavyo wanapambana, ujangili umepungua, uhifadhi umekuwa bora haya mapungufu kwa pamoja tunaona namna ya kuyarekebisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuwapongeza kwa hatua zao za kusudi kabisa za kuinua utalii. Niliona kwenye habari wiki mbili zilizopita kwamba waliamua kupunguza gharama za leseni zile za utalii kutoka dola 2,000 kwenda dola 1,000 nawapongeza sana na hii ndiyo itakachowasaidia kupata idadi ya watalii. Kwa mfano, Mlima Kilimanjaro target mmeonesha ni kutoka watalii 56,000 kwenda watalii 200,000 hongereni sana na naomba tuwaombee kwamba haya yakazae matunda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze zaidi pale mlipoona umuhimu wa kupunguza fee au leseni ile ya u-guide kutoka dola 50 kwa kila mwaka mkaweka shilingi 100,000 kwa miaka mitatu. Hii itaongeza kipato cha wale watumishi kabisa ambao ni ma-guide ambao tunawahitaji sana katika kuwaongoza watalii lakini niwaombe mkaangalie sasa maslahi ya hao wengine huko chini, wale wapishi, ma-porter na kadhalika. Hawa wanaweza kupata faida zaidi kama mtaweza kuwaangalia hawa wafanyabiashara wa utalii kuwapunguzia zile kodi ambazo zinaonekana nyingi ni za kujirudia rudia ili basi na wao waweze kuwaangalia wale makuli - porters na wapishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wazungumzaji waliotangulia walishaongea, moja ya eneo la kuangalia ni barabara. Pamoja na kwamba mmesema fedha zile zitarudishwa kukusanywa kule, hili suala la barabara mimi nadhani, mbona ni kazi ndogo tu, mkiwa na vifaa ninyi mnaweza mkawa mnatumia wale wataalam wa TARURA. Kwa nini katika kila Wizara ama kama Wizara yenyewe msiwe na vifaa kuendana na zone kwa ajili ya kurekebisha zile barabara hasa zile za kwenye mbuga kama Serengeti, Ngorongoro ili kupunguza gharama lakini ili kuweza kuzifanya ziwe nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku hizi watalii, teknolojia inakwenda mbali watalii hawataki tena kurushwa rushwa, vumbi iliyozidi, barabara ni vizuri ziwe nzuri zaidi kwa sababu hata magari yanayokuja model mpya hayastahimili hizi barabara mbovu sana. Kwa hiyo naomba ma-tour operators wanapata hasara sana kwenye gharama ya kurekebisha yale magari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliona kwenye habari, wanahabari walienda kutembelea hoteli ya Burigi kule Chato, nimeona inaendelea kutengenezwa taratibu, wasiwasi wangu ni kwamba, kasi ya kuweka hela pale naona ni ndogo, ile hoteli nimeisikia muda mrefu. Ni vizuri tupeleke fedha ya kutosha miradi kama hiyo ikamilike lakini iweze kuleta tija haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa mwisho, Serikali haitaweza kuziendesha, nimesikia mchangiaji mmoja amesema na zile hoteli za Serikali zirudishwe, Hapana! hata kama zitarudishwa tutafute wabia. Kuna watu wame-specialize kwenye management, makampuni makubwa tufanye nayo na hii tunaweza kuangalia hata ile Hoteli ya Ngurdoto ambayo nasikia ilikuwa inakufa lakini juzi juzi naona tumefanikiwa kurudisha tena mikutano ya Afrika Mashariki. Namna ya Serikali kulipa lile deni na kununua share na kutafuta management companies hasa hizi za nje ili kuendesha hoteli kama hizo ziweze kuleta tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwepo kwa Wizara ya Mipango kunatakiwa kulete tija ya haraka sana kwenye Wizara mbalimbali. Kwa mfano tu, Wizara ya Utalii kuna component ya conference tourism naona ipo Mambo ya Nje, AICC ipo pale lakini na ile Julius Nyerere Convection Centre sasa ule ni utalii mkubwa kwa sababu kwanza unaleta biashara kwenye hoteli na baadae wanaenda kutembelea vivutio. Nilikuwa naomba hii Wizara ya Mipango ione namna ya ku-link, vitu kama AICC wanapoenda kwenye utalii hawa TTB wanapoenda kutangaza wana- incorporate vipi? Wanaangalia vipi namna ambavyo inaweza ikaunganishwa pamoja na utalii wetu huu wa wanyama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile sehemu kama ATCL linawezaje kusaidia utalii nchini maana kwa mfano tu, kumekuwa na shida kubwa sana ya cancellation kwenye ATCL lakini tulitegemea ATCL ndiyo i-compliment utaliii. Ni namna gani Wizara ile ya Mipango itafanya kazi na Wizara hii ifanye na Uchukuzi ili kuleta tija.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye mahoteli, uwekezaji pamoja na kuweza kupata man power. Kwa hiyo kuna mahali pa kuweza kufanya hizi Wizara ziongee. Wameelezea namna ambavyo wanaangalia man power lakini nataka nikuambie, kwenye man power Tanzania tuna shida kubwa ya customer care, tuna shida kubwa ya kiingereza na lugha nyingine, masoko mapya, Kirusi, Kichina, Kituruki. Ni vyuo gani vinafundisha hayo masomo vizuri ili hao watalii tunaotaka milioni tano watakaotoka kwenye masoko mapya wapate watu ambao wataongea nao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimuhimu sana hayo mambo yaweze kuunganishwa. Nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)