Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia bajeti ya Mheshimiwa Waziri. Jambo la kwanza ninaunga hoja mkono bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nipende kumpongeza Mwenyekiti wa Kamati hii ambayo mimi pia ni Mjumbe, Mheshimiwa Timotheo Mnzava Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa kazi kubwa ambayo ameifanya ya Kibunge ya kuheshimisha Bunge lakini pia kuangalia mustakabali mpana wa Taifa letu, maono na vipaumbele vya Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba Kamati inaleta ripoti ambayo inaakisi maisha halisi ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa na mambo machache. Jambo la kwanza Mheshimiwa Waziri hatuna nia mbaya na Wizara yako, haya yote tunayafanya kwa ajili ya mustakabali wa Taifa letu. Mheshimiwa Waziri hatuna kabisa nia mbaya na watendaji wako, haya yote tunayazungumza kwa mustakabali wa wananchi wetu walioko nje ambao nao wanategemea sisi kama Wawakilishi wao tuguse maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa Makete tuna hoja moja Mheshimiwa Waziri kuhusu re-grow. Mradi wa re-grow phase two tunawaomba sana mtupangie hifadhi yetu ya Kitulo iweze kuingia katika mradi wa re-grow phase two. Tuna uhitaji wa barabara, tuna uhitaji wa kiwanja cha ndege pale Kitekelwa nashukuru wataalam walikuja lakini kuna uhitaji wa accommodation. Mheshimiwa Waziri re-grow ikija Kitulo itaisaidia hifadhi hii ya kipekee Barani Afrika, hifadhi ya maua lakini pia tulileta pendekezo kwenu la kuongezewa idadi ya wanyama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wanyama mlituletea nadhani utafiti utakuwa umekamilika kwa sababu wanyama wamekaa zaidi ya miaka kumi pale. Inawezekana umeshakamilika utafiti huo, tunahitaji kuongezewa idadi ya wanyama ili tuongeze idadi ya watalii kwa maana ya Jimbo la Makete. Mheshimiwa Waziri ninakuomba sana kwenye re-grow phase two Kitulo isisahaulike.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwenye suala la bilioni 19. Waheshimiwa Wabunge kama Kamati tuliliona hili jambo la bilioni 19. Kwanza nia njema ya Mheshimiwa Rais, kwa sababu sisi kama Kamati tulishapitisha Bajeti ya Wizara ya Maliasili kwenye Kamati yetu lakini Mheshimiwa Rais akaona ni vyema Wizara hii aiongeze bilioni 19. Sisi kama Kamati tukaangalia mgawanyo wa fedha ulioletwa na Wizara hauna tija kwa maslahi mapana ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nyongeza ya bilioni 19 unatoa bilioni 5 pekee ndiyo unapeleka kwenye shughuli za maendeleo, the rest bilioni 14 inaenda kama OC, wakati Wizara tayari ilishapitisha OC yake kwenye miradi mbalimbali. Hii sisi kama Kamati tumeona hatuwatendei haki Watanzania, tumeona ni vema Bunge na kama ambavyo Mwenyekiti ametushauri kwenye ripoti yake mtusaidie jinsi gani tuweze kuokoa fedha hizi ziweze kwenda kuleta tija kwa Watanzania. Sisi Wabunge tuliona ni vema fedha za maendeleo zikawa ni nyingi kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, asubuhi ya leo tulitaka tuahirishe Bunge hapa kwa sababu ya changamoto ya mamba kule Buchosa. Wale watu wanachokihitaji ni kuona mamba wanavuliwa na ni fedha hizi zinatakiwa zitumike.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, achana na hiyo ukienda kwenye hifadhi zetu, moja kati ya hifadhi sisi tunatanganzwa kama kivutio namba mbili kwa utalii duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kati ya changamoto kwenye hifadhi ni changamoto ya miundombinu mibovu ya barabara. Achana na hivyo, nenda kwenye suala la kupamba na tembo. Tuna changamoto ya vituo vya askari havipo. Wizara haina fedha ya kujenga vituo vingi. Tuliona kwamba fedha iwelekezwe huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto nyingi lukuki zinazoibeba Wizara ambazo kama tutatumia fedha hizi kugusa maslahi ya Watanzania, tutakuwa tumeokoa jambo kubwa sana. Kwa hiyo, mimi naliomba Bunge lako na ninamuomba Mheshimiwa Waziri, hatuna nia mbaya; tunajua ni mchapakazi sana na kwa kweli ametuhusisha sisi Waheshimiwa Wabunge kwenye shughuli nyingi za utatuzi wa matatizo ya wananchi wetu, lakini kwenye hili la shilingi bilioni 19, sisi kama Waheshimiwa Wabunge hatuwezi tukawa tayari. Lazima tulinde fedha ya Serikali yetu na ni lazima tuguse maisha ya wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni muhimu sana mgawanyo wa fedha hii tukaachana na mambo ya OC ambayo mlikuwa mmeyapanga ya hizo shilingi bilioni 14 kwenda kwenye matumizi ya kawaida twende kwenye utaratibu wa kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni issue ya nchi. Tukizungumza wataalamu wanakuja na lugha nyingi za kwamba, unajua ukomo wa bajeti framework, kikaenda yaani panda shuka nyingi. Sisi tunazungumzia maisha halisi ya Mtanzania ambaye ukimwambia suala la ukomo wa bajeti au framework ya bajeti haifanyi kazi hawezi kufahamu. Anachofahamu kuna tembo wanasumbua kwenye eneo lake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sisi kama Kamati tuliona ni vyema Mheshimiwa Waziri utusaidie hizi fedha ziende kuleta tija kwa wananchi wetu. Hatuko tayari kuona kwamba huu mgawanyo wa fedha unaenda huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, naipongeza Serikali. Watu wa NCAA na Watu wa TANAPA fedha imerudi kwenu; mnakusanya na mnapanga matumizi. Hili lilikuwa ni kilio kikubwa cha Wizara kuona hili jambo linafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi letu ni moja. Moja kati ya kashfa kubwa za TANAPA na NCAA ni matumizi mabaya ya fedha. Ninayo Report ya CAG, ukisoma Report ya CAG, TANAPA na Ngorongoro hawana record nzuri kwenye Report ya CAG kwenye matumizi ya fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kurudisha fedha hizi hatutegemei kuona tena bodi zinaenda kukaa Ulaya. Hatutegemei tena kuona matumizi ya fedha yakiwa mabaya. Tunategemea udhibiti mkubwa wa fedha hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajua baada ya kurudisha fedha hizi kukusanywa TANAPA na NCAA, kuna msururu wa watendaji wa Serikali wataanza kuomba kazi kwenye NCAA na TANAPA kwa sababu tayari wameshaona kichaka na asali ya fedha iliyoko kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunakuomba Mheshimiwa Waziri, simama imara, dhibiti matumizi. Mheshimiwa Rais anakutegemea uta-control hili jambo, baadaye Serikali isituone burden kwa sababu moja kati ya hoja ya Serikali kuondoa hizi fedha kukusanywa na Serikali Kuu ilikuwa ni matumizi mabaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumezirudisha, tunaomba Mheshimiwa Waziri simamia fedha hizi zikusanywe vizuri ziweze kuleta tija na hifadhi zetu lazima tuone development. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu haya magari ametoka kuzungumza hapa Mheshimiwa Mbunge wa Moshi, magari ya four wheels hizi zinazotumika sasa hivi kwenye hifadhi zetu zimepitwa na wakati. Sasa hivi watu wanataka kutumia magari ya kisasa lakini barabara zetu haziruhusu. Ni fedha hizi zitaenda kutumika kusaidia huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo yalikuwa ni ya kwangu. Mwisho kabisa, tunaiomba Bodi ya Utalii ndiyo custodian wa utangazaji wa utalii... (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa, muda wako umeisha.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, najua. Jambo moja tu kwenye suala la utalii kwa sababu Mheshimiwa Rais ameonesha njia, siyo kila mtu anafaa kutangaza utalii. Mheshimiwa Waziri unajua hata wewe mtu wa kukuombea kura, siyo kila mtu atakuombea kura ushinde. Kuna mtu akikuombea kura unaanguka. Tunaomba utalii wetu utangazwe na watu smart na muwaachie custodian wa utalii watangaze utalii wa nchi hii... (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Sanga, muda wako umeisha; umeeleweka.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na Mungu akubariki. (Makofi)