Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Eng. Ezra John Chiwelesa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika hotuba hii ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Kipekee niungane na wengine waliotangulia ku-appreciate kazi kubwa inayofanywa na Mheshimiwa Rais kwenye kukuza utalii, amekuwa champion wa utalii katika nchi hii, kwa hiyo na mimi niungane na wengine kwenye kumpongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na msaidizi wake kwa hotuba nzuri, kwa usimamizi wa maandalizi ya hotuba hii na bajeti hii ambayo aliikuta njiani ambayo wameendelea nayo na sasa wanaimalizia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda mimi jambo moja tu la muhimu, nitakuwa na uchangiaji kama sehemu mbili, hasa mambo yanayohusu jimbo langu, halafu baadaye nitakwenda kwenye mambo ya jumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika record za Bunge nadhani nimekuwa nikiongelea sana suala la ardhi kwa wananchi. Mwaka 2022 Mheshimiwa Rais akiwa Bukoba kwenye Uwanja wa Kaitaba tarahe 9 Juni alitoa maelekezo specific kwa Mkoa wa Kagera kwamba tutafute maeneo kwa ajili ya kufanya shughuli za kilimo na ufugaji ili tuweze kunyanyua uchumi wetu na Ilani pia ya CCM imehaidi kwenye habari ya kuongeza maeneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kelele yangu kubwa au jambo ambalo nimekuwa ninaliongea ndani ya Bunge ni kwamba maeneo hayo hayapo kwenye mikono ya watu, ni maeneo ya Serikali, kwa sababu Mheshimiwa Rais anavyoelekeza akasema maeneo yatafutwe, maana yake anaelekeza watu wake watafute maeneo. Sidhani kama anaelekeza wananchi watafute maeneo na wananchi kama walikuwa na maeneo hawana haya ya kuomba maeneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa habari ya Wilaya ya Biharamulo; nataka tu nitoe rekodi nzuri niingia katika rekodi za Bunge. Sensa ya mwaka 2002 Biharamulo ilikuwa na wakazi 159,055, lile eneo letu la makazi na kilimo likiwa hekta 183,400. Mwaka 2012 tumetoka laki moja tukaenda 323,486, eneo bado ni lile lile 183,400. Mwaka 2022 457,114 eneo bado ni lile lile 183,400. Niliposimama hapa Jimbo la Biharamulo ndilo jimbo linaloongoza kwa idadi ya watu kwa Mkoa wa Kagera, lakini miaka zaidi ya 20 eneo la makazi na kilimo bado ni lile lile. Ni jimbo la 20 kwa wingi wa watu Tanzania kati ya majimbo 264.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hatuwezi kila siku idadi ya watu inaongezeka, hatuna shughuli nyingine, sisi hatuna maeneo ya viwanda kama Njombe, shughuli yetu kubwa Biharamulo ni kilimo na ufugaji. Kama idadi ya watu inaongezeka, lakini hatupewi maeneo ya kulima wala kufuga, what is the meaning ya watu kuwepo pale?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikihamasisha watu wazae na kuongezeka, miundombinu inaletwa, lakini watu hawapewi maeneo ya kufanya shughuli za uchumi. Hii inasikitisha na inaumiza. Watu wangu wamekuwa wanaishi kama wakimbizi kwenye nchi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe na Mheshimiwa Waziri anaelewa kwamba nilishapeleka maombi ya kata nne kwakwe. Kata ya Nemba nikaomba hekta 5,000 tu tuanzie, nikaomba Kata ya Nyanze eneo la Rukako hekta 5,000 tu tuanzie, nikaomba pia Kata ya Nyakahura waongezewe eneo, nimeomba Nyakanazi waongezewe eneo pale hekta 5,000, pia nimeomba na Kata ya Katahoka waongezewe eneo. Tukishapewa haya maeneo hawa watu wanaofuga na kulima wataweza kupata maeneo mengine, hatuwezi kuongeza idadi ya watu ambao hawana maeneo ya kufanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi mifugo yao hata na maisha yao ya kawaida wananchi wanateseka. Mimi niliuliza hapa kwenye taarifa za Kamati wakati uliopota, nadhani ilikuwa Bunge la mwezi wa pili, hivi mtu anayekwenda kuokota kuni, kama kweli mnatufanya sisi maeneo yale yapo kwetu, tumezaliwa hapa na sisi ndio wahifadhi wa kwanza, kwa sababu muhifadhi ambaye ametoka darasani si muhifadhi wa kwanza, asingeyakuta, wahifadhi wa kwanza ni wananchi wa lile eneo wale watu lazima washirikishwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi unashangaa ulinzi shirikishi ni wa nini? Mbona polisi hawa wa kawaida tunashirikiana nao vizuri, tunakuwa na ulinzi shirikishi? Wanajeshi mbona hawagombani na wananchi? Shughuli nyingine au vyombo vingine mbona havigombani na wananchi? Kwa nini kila siku TFS tu?

Kwa hiyo, tulikuwa tunaomba tusaidiwe kupitia Bunge hili, hawa watu ni Watanzania na hili Bunge ni lao lazima nije niwasemee hawawezi kuja humu. Ninachoomba tuongezewe maeneo ili watu wapate maeneo ya kufanyia kazi kwa sababu shughuli zao za uchumi zinakwama. Hilo jambo ninaomba niliweke specific. Wafugaji wangu wanateseka, kwa laki moja, moja hizi sasa imefikia stage watu wamekuwa watumwa. Tulikwishaomba maeneo tuongezewe mule ndani ya hifadhi naamini Mheshimiwa Waziri wakati anajibu hilo atalifanyia kazi

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ninayo Hifadhi ya Burigi pale kwangu, hii hifadhi Mheshimiwa Rais alipopita Biharamulo tarehe 8 Juni, 2022 nilimuomba eneo na geti la kuingilia kwenye hifadhi kupitia Biharamulo Mjini. Hayo ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais, alisema amepokea na akatoa maelekezo lifanyiwe kazi. Kwa hiyo, ninaomba kwenye kuhitimisha Mheshimiwa Waziri, nadhani yeye hakuwepo, lakini Serikali ni ile ile, ningeomba nipate majibu pia wakati anahitimisha ili nijue tunaishia wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Hifadhi hii ya Biharamulo – Burigi, Mheshimiwa Waziri alipokuwa na kikao na Wabunge wa Kagera nilisema, kwamba watu wangu wanakamatwa kwa sababu ng’ombe wanaingia mule, lakini kuna makundi ya ng’ombe wa wageni wengi sana ambao wameingizwa mle. Hii inaharatisha usalama wa nchi yetu na usalama wa Wilaya yetu ya Biharamulo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama unaweza ukahesabu simba ukajua ni wangapi ukatuambia hapa, ukahesabu nyati, ukahesabu chui na vitu vingine, kipindi mnahesabu hawa wanyama hizo helikopta zinazohesabu hao wanyama hao ng,ombe hamuwaoni kweli? Kwa hiyo nilikuwa naomba ng’ombe wale waondoke kwenye hifadhi kwa sababu hauwezi kuweka ng’ombe wa watu wengine, tena si Watanzania, ni wageni halafu ng’ombe wa watu wetu kwenye hifadhi tu ya TFS wanakamatwa. Nilikuwa naomba hilo nipate jibu, nilisema pale wakanihaidi kufanya operation maalumu, operation sijaiona hadi leo naingia kwenye bajeti, kwa hiyo naomba mnisaidie kwenye hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine cha muhimu, Mheshimiwa Waziri alinihaidi kwamba wanahamisha tembo Kimisi mnawaleta Burigi. Sasa ndugu yangu, kelele za tembo hapa zimekuwa kubwa. Watu wa Nyakahura kwangu pale hawalali usingizi. Sasa tena uchukue tembo zaidi ya 200 uwatoe Kimisi uwalete pale, jamani hivi kweli hapa si kuniongezea matatizo Mheshimiwa Waziri?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naomba, kama wanyama wanakuwa wengi tufanye kazi ya kuwavuna, hamuwezi kuwa na vitu visivyovunika, kwa nini tusiangalie jinsi ya kupunguza hawa wanyama? Huenda wamezaliana sana, hivyo tuwapunguze ili wananchi waweze kuishi kwa ahueni hali kadhalika na wanyama wasilete vurugu kwa wananchi. Nilikuwa naomba hilo mliangalie, ni jambo la muhimu sana sana sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia nina kata moja inaitwa Kata ya Kalenge, Mheshimiwa Naibu Waziri anaelewa, kuna viboko zaidi ya 20 kwenye mto ambao upo kijijini. Alikwishatuma watu kutoka Kigoma wakaja wakaangalia. Tunachoomba wale viboko waondolewe, kile ni kijiji cha wananchi siyo hifadhi, waondoeni muwapeleke sehemu nyingine ili wananchi waweze kufanya kazi kwa amani, kwa sababu wamekwishaharibu mazao mengi sana na wamekwishawaumiza wananchi kule na hiyo mnayotuambia fidia kila siku ninapiga simu kwa ajili ya hiyo fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wameshaumiza na wananchi kule, kuna nyati amepiga mwananchi akamuua. Shilingi milioni mbili anayosema wameongeza haina thamani ya kifo cha mtu, hata kama wangeweka milioni 100. Fedha hii bado ni ndogo kwenye kulipa fidia. Nilikuwa naomba aangalie jinsi ya kufanya ili angalau wananchi wanaoumia na wanaoumizwa na hawa wanyama waharibifu kiwango kiongezeke kidogo ili na wao wapate ahueni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi ya kuchangia, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)