Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Yahya Ally Mhata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyumbu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye ameniwezesha mchana huu kusimama mbele ya Bunge lako hili Tukufu kutoa mchango wangu kwenye bajeti hii ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha kwamba Wizara hii inafanya kazi ya kuinua uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wote ni mashahidi tumeona jinsi alivyoshiriki katika filamu ile ya Royal Tour na jinsi gani filamu ile ilivyoweza kuongeza mapato ya nchi yetu, lakini pia yeye pamoja na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar walivyoshiriki katika hii filamu ya Amazing of Tanzania ambayo nina uhakika ita-boost uchumi wa nchi yetu na kuwavutia watalii kwa wingi. (Makofi)

Naomba nimshukuru Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana na Wizara hii kwa jinsi alivyoingia katika Wizara hii na alivyowashirikisha Wabunge wote, kukutana nao na kuweza kutoa changamoto zetu mbele yake. Nina imani yale ambayo tulimweleza Mheshimiwa Waziri atayafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Naibu wake kwa kweli amekuwa msikivu sana. Naibu muda wowote ukimpigia simu anapatikana na anatoa ushirikiano mkubwa sana. Kwa hiyo, ninaombwa nimwambie Mheshimiwa Waziri kwamba anaye naibu makini na afanye naye kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie maeneo yafuatayo; kwanza kuhusu wanyama waharibifu. Tumekuwa na changamoto sana katika nchi hii ya wanyama waharibifu. Kwa mfano, ndani ya Jimbo langu la Nanyumbu tunao hawa wadudu wanaoitwa tembo au wanyama tembo. Wanyama hawa wamekuwa waharibifu na huhatarisha maisha ya watu wetu. Tarehe 9 Mei, 2023 kuna mama mmoja Bi. Mwanaali alipoteza maisha kwa kushambuliwa na tembo, lakini juzi tarehe 10 Mei, dada yetu Zena Maganga alipokuwa nyumbani kwake, akienda kuchota maji alishambuliwa na tembo na kupoteza maisha, lakini jambo la kusikitisha Wizara haijatoa rambirambi kwa wafiwa hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti naomba Wizara ijiongeze itoe rambirambi kwa wafiwa pindi wanapopata taarifa hizi za kuhuzunisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tembo wamekuwa kikwazo ndani ya jimbo langu, ndani ya mwaka huu wameshambulia ekari 460 za mazao, lakini mpaka hivi navyozungumza ni ekari 11 watu watatu wamelipwa fidia, ekari 460 unalipa ekari 11, hii tunafanya mchezo na maisha ya watu, wale watu shamba ndiyo maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Sengenya, Nangomba na Lumesule wananchi wameathirika na mazao yao, lakini mpaka sasa hivi wizara imekaa kimya pamoja na kuwapatia taarifa. Kwa hiyo, ni matarajio yangu kwamba hili kesho atakapohitimisha Mheshimiwa Waziri lazima atoe kauli, wananchi wangu watalipwa lini fidia ili na wao waweze kujikwamua na maisha yao, vinginevyo, kesho hatutaelewana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni wanyama waharibifu (mamba), mimi napakana na Mto Ruvuma. Hivi ninavyozungumza zaidi ya watu kumi wameawa na mamba na mpaka leo ni watu watatu tu wamelipwa kifuta jasho. Maisha ya binadamu yanapotea kwa sababu ya wingi wa mamba ndani ya Mto Ruvuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikiliza hotuba ya Waziri, hakuna mahali palipozungumziwa jinsi gani ya kuwapunguza mamba katika Mto Ruvuma au kujenga vizimba ndani ya Mto Ruvuma, hili jambo halikubaliki. Tumepoteza watu zaidi ya kumi, watu zaidi ya 30 ni walemavu, hili jambo linahuzunisha sana. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, nakuomba kesho utakapokuja utupatie utaratibu utakaoutumia kupunguza mamba wale au jinsi gani ya kujenga vizimba ndani ya Mto Ruvuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni hizi pesa ambazo zimeongezwa na Mheshimiwa Mama Dkt. Samia ndani ya Wizara hii. Mimi naomba nitoe ushauri, kwanza nakubaliana na mawazo ya Kamati, naomba sasa fedha hizi zitumike kwenda kulipa fidia kwa wananchi ambao wameathirika na wanyama waharibifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani wananchi wanateseka halafu pesa zitoke zikafanye shughuli ambayo haina tija. Hebu jichukulie Mheshimiwa Waziri kama ungekuwa wewe shamba lako limeliwa, halafu fedha inaletwa inakwenda kutumika vile, ungekubali? Usiruhusu mambo yanafanyika ndani ya Wizara yakow ewe unayatazama, hili jambo halikubaliki Mheshimiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi naomba sana fedha hizi zitumike kwenda kuwalipa fidia wananchi ambao wamepoteza mali zao na wengine wamepoteza maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine naomba kuzungumzia kuhusu WMAs hizi ambazo ni hifadhi za wanavijiji wetu. Wanavijiji wameanzisha hizi hifadhi kwa lengo zuri la kuhifadhi wanyamapori wetu, lakini Wizara au Serikali haiwaungi mkono, hivi ninavyozungumza fedha nyingi za hizi WMAs ziko chini ya Serikali na wananchi sasa wamekwishaanza kuona kwamba hawanufaiki na jitihada wanazozifanya katika kuwatunza hawa wanyama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tuchukue wazo la Kamati, fedha zote ambazo zimechukuliwa na Hazina zirejeshwe kwa wananchi, zirejeshwe ndani ya vijiji ili wanavijiji waweze kuzitumia fedha hizi kwa malengo yaliyokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani fedha hizi ndizo ambazo zilikuwa zinajenga shule, vituo vya afya kule vijijini na kulipa mishahara ya hawa watu wanaolinda maliasili zetu. Leo hii kila kitu kimekuwa abandoned na matokeo yake ujangili umeongezeka kwa sababu wananchi hawaoni faida ya kuwa na hizi maliasili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama tumerudisha fedha kwa TANAPA, kama tumerudisha pesa kwa Ngorongoro na hizi WMAs zirejeshwe ili wananchi zirejeshwe ili wananchi waweze kuzitumia kwa shughuli za kuleta maendeleo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kwangu ninayo WMA ambayo imejenga madarasa mpaka usawa wa lintel. Wameshindwa kuendelea kwa sababu hawana fedha, fedha zimechukuliwa na Serikali na hazirejeshwi. Kwa hiyo, nashauri fedha hizi zirejeshwe ili wananchi waweze kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kuna maombi yasiyopungua 16 ndani ya wizara yako wananchi wanaanza kutaka ku-register hizi WMAs, bado hazijafanyiwa usajili. Kwa hiyo, nakuomba Mheshimiwa Waziri mara baada ya kupitisha bajeti yako hebu nenda kazipitishe zile WMAs ambazo zimebaki ili wananchi waweze kwenda kuzifanyia kazi na hatimaye kulinda maliasili zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, ila hili ambalo nimelizungumza kama kesho sitapata majibu nitashika shilingi. (Makofi)