Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia. Kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipatia nafasi kusimama hapa kuchangia kwenye bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi anayoifanya hasa ya kutangaza utalii, ukichukulia filamu ya Royal Tour ambayo imevutia watu wengi na kuleta watalii wengi Tanzania, kwa hiyo, tunamshukuru sana kwa kazi hii nzuri aliyoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano ameweza kuitangaza na watalii wameweza kuongezeka kuanzia milioni 1.4 kwa mwaka 2022 mpaka milioni 1.8 kwa mwaka 2023. Kwa hiyo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. Pili, ameweza kuongeza bajeti kwa kuwa anaithamini sana Wizara hii hasa kwa upande wa utalii kwa kuongeza bajeti ambayo mpaka sasa hivi tunasema ni shilingi 348,125,119,000. Kwa hiyo, tunamshukuru sana kwa namna anavyoithamini sekta ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, nampongeza sana na kumshukuru Mheshimiwa Waziri Angellah Kairuki, kwa kweli anafanya kazi kubwa sana, pamoja na Naibu wake, Katibu Mkuu na Wizara nzima kwa kazi wanayoifanya. Ninyi wenyewe ni mashuhuda mmeona kuwa licha ya matatizo yanayojitokeza lakini kwenye hotuba yake amesema kuwa pato linalotokana na utalii limeongezeka, watalii wameongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeweza kufika namba moja kwa nchi zote za Afrika kwenye mambo ya utalii. Kwa kweli mimi nampongeza na nawapongeza watendaji wa Wizara wote kwa kazi nzuri mnayoifanya, kama kuna matatizo mengine yatatuliwe, naamini kuwa Wizara itakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ninaloongea hapa ni kuongeza vivutio vya utalii. Naomba sana ili watalii waweze kuongezeka pamoja na pato la nchi liweze kuongezeka lazima tuongeze vivutio vya utalii. Vivutio vya utalii kila Kanda na kila Mkoa vilikuwepo, kulikuwa na himizo la kusema kila Mkoa uweze kuvumbua na kutangaza vivutio vyake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano nikija kwenye Mkoa wangu wa Morogoro, tuna vivutio vingi sana. Nikianza na Bwawa la Mwalimu Nyerere, tunamshukuru sana Dkt. Samia kwa jambo hili alilolifanya. Nikija kwenye milima ya Uluguru, nikija kwenye barabara, nikija kwenye hoteli, kwa kweli tuna mambo mengi, utamaduni, utalii siyo lazima uwe ni wanyama, hata maua, hata vyakula na uvaaji wa watu wanaoishi kwenye Mikoa hiyo nayo ni utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuangalie kuvutia na kuongeza vivutio ambavyo vitaweza kuongeza utalii kwenye nchi yetu ili kusudi watalii waweze kuwa wengi na tuweze kuongeza vivutio na uchumi uweze kukua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wanyama waharibifu. Mheshimiwa Waziri Angellah, wanyama waharibifu wamekuwa tatizo. Tembo wamekuwa ni tatizo, tembo kwenye Mkoa wangu wa Morogoro kwa wastani, Mikoa yote ya Tanzania kwa wastani ni tembo ndiyo wanaoongelewa. Hata hivyo, ninawashukuru na kuwapongeza kwa jitihada mnayoichukua ya kufanya utafiti wa jinsi ya kuwadhibiti hawa tembo. Kwa mfano, mabomu baridi, kwa kweli mmefanya kazi nzuri tumeiona, ila mimi najiuliza, mkishawatupia wakakimbia, je, hapo baadaye hawarudi? Kwa hiyo, naomba sana tuangalie huo utafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mmesema mnawafunga mikanda na helkopta, safi, tumieni tafiti tuweze kuona tafiti zinafanya kazi kusudi tembo waache kuharibu mazao ya wananchi. Wanaharibu mazao ya wananchi, wanaua watu, kwa hiyo naomba sana Tembo ni mzuri lakini kwa mfano ukipita pale Mikumi, wewe mwenyewe unafurahia kuwaona walivyo, ni mnyama mkubwa sana anapendeza, lakini tuangalie wasiharibu mazao ya watu pamoja na kuleta vifo kwa watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya ardhi na hifadhi. Imekuwepo lakini wananchi wengine hawaelewi kuwa kuna sheria, wanaingia kwenye hifadhi wanadhulumiwa. Kwa hiyo, nilikuwa naomba, natoa ushauri kuwa elimu iendelee kwa hawa wananchi wanaoishi karibu na hifadhi, waweze kujua ni sheria ambayo inawakataza kuingia kwenye hifadhi, waelewe vizuri, kuwe na ushirikiano wa kupima mipaka kati ya ardhi ya wananchi pamoja na ardhi ya hifadhi. Waweze kuelewa na kushirikishwa kuwa hii huwezi kuingia na hii huwezi kufanya nini ili kusudi tupunguze migogoro inayojitokeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu rasilimali misitu. Misitu ni mali, misitu ina faida, inaleta hewa, inaleta mvua, inazaa carbon kwa hiyo ni utajiri kwa nchi yetu. Kwa hiyo, naomba ile miche inayozalishwa iweze kupelekwa kwenye taasisi mbalimbali na ikiwezekana na wananchi wagawiwe kama mnavyofanya TFS. Mnafanya vizuri, tuendelee kustawisha hii miche. Angalizo ni kuwahimiza watu wa halmashauri kwa kushirikiana na TAMISEMI kuwa hii miche inayogawiwa iweze kutunzwa, isiwe ni kupanda tu na kuisahau, iweze kufuatiliwa ili kusudi iweze kustawi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kuongeza utalii tumeona kuna ujenzi wa viwanja vya ndege ambavyo vitajengwa na kukamilika mwezi huu wa Nane. Kwa mfano, kuna kiwanja cha ndege Mikumi kitajengwa, kuna kiwanja cha ndege Nyerere kitajengwa, kuna viwanja viwili Ruaha, vitajengwa. Kwa kujenga hivi viwanja vya ndege vitaongeza watalii kuja nchini kwetu na hapo hapo tutaweza kuongeza uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nashauri, pamoja na hivyo tuendelee kuboresha na kujenga viwanja vya ndege kwenye hifadhi zetu ili kusudi watalii waweze kuja kwa wingi tuongeze kipato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ufugaji wa nyuki. Ufugaji wa nyuki ni kitu kizuri sana hasa kwenye kuhifadhi misitu. Ukiweka nyuki kwenye misitu, watu hawawezi kuingia hovyo hovyo kukata hiyo misitu. Kwa hiyo, nilikuwa nasema hivi, elimu iendelee kutolewa kwa wananchi hasa kwenye vikundi vya vijana pamoja na akinamama, waweze kupewa mizinga kama mnavyofanya ili kusudi waweze kufuga hao nyuki na waweze kupata ajira kwa kujiajiri wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazao ya nyuki ni dawa, nyote mmeona asali, nta, kwa hiyo ni jambo zuri pamoja na mazao mengine yaweze kutolewa elimu ili watu waweze kuendelea kufuga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ufinyu wa bajeti. Licha ya kumshukuru Mheshimiwa Rais lakini naomba waongezewe bajeti ili kusudi iweze kuwatosheleza na iweze kuonekana vizuri na kusimamiwa vizuri kusudi iweze kufanya mambo yaliyopangwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na ubarikiwe na Mwenyezi Mungu kwa kunipatia nafasi.(Makofi)