Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Urambo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MARGARET S. SITA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja iliyoko mezani, pia namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii na wakati huo huo nawashukuru wananchi wa Urambo kwa ushirikiano wao wanaonipa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza Dkt. Samia, Rais wetu, kwa kazi kubwa anayoifanya ya kutafuta maendeleo ya nchi hii. Pia ninampongeza Mheshimiwa Waziri wa Maliasili, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote walioko katika Wizara hii ambayo inajadiliwa siku ya leo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Urambo uchumi wetu unategemea sana tumbaku na asali. Wananchi wanaofuga nyuki wameunda umoja wao wa wafuga nyuki, waliniomba mimi nikapeleka barua rasmi Wizara ya Maliasili na Utalii ili kupewa mashine ya kusaidia kuchenjua asali ili na sisi tusafirishe ndani ya nchi na nje ya nchi pia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Wizara ilikubali ikamtuma Mkurugenzi akaja, akakagua eneo letu na wakakubali kwamba watatupa mashine. Nawashukuru sana kwa sababu walitupa moyo wa kuongeza mizinga katika mapori yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo huo, Serikali ikaja na wazo zuri la kuwa na hifadhi ya Mto Ugala ambako ndiyo kwetu sisi na maeneo yanayoguswa karibu sana ni Kata za Nsenda, kwenye maeneo ya Lunyeta, Utenge, Mkola na Mtakuja. Pia, Kata ya Ukondamoyo kwenye maeneo ya Tumaini, Nholongo na Utewe na pia Kata ya Kasisi katika maeneo ya Azimio. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa Urambo, naomba nilete ombi siku ya leo. Kwanza kuishukuru Serikali kwa kutupa hifadhi ya Mto Ugala, tunathamini hifadhi hiyo na ninajua kabisa Serikali ilifanya hivyo, kugeuza ule msitu ukawa hifadhi ya Mto Ugala kwa maksudi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu, tunathamini kuwa na hifadhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi tunaloleta kwako Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla ni kwamba, kwa kuwa uchumi wetu unategemea sana asali, tuna haja ya kupeleka mizinga. Kwa bahati mbaya ndani ya hifadhi ya Mto Ugala haturuhusiwi kupeleka mizinga lakini ni zao ambalo tunalithamini na tulikuwa tumeshapata watu wa nje ambao walikuwa tayari kununua asali yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ombi ambalo ninalileta kwa Mheshimiwa Waziri ni kwamba tupewe eneo la kuweka mizinga, kwa sababu ni zao ambalo tunalitegemea kiuchumi. Tatizo moja lililotokea ambalo ninaamini ni kwa bahati mbaya kwa sababu Serikali yetu ni nzuri tu, hawakutoa elimu ya aina yoyote walipokuwa wanageuza huu msitu kuwa hifadhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi hawakuelimishwa kwamba kuwa na hifadhi maana yake ni nini, wao watafaidika vipi na wajibu wao ni nini ili kujenga mahusiano na ujirani mwema. Kwa sababu, tunaamini kabisa mlinzi wa kwanza wa hifadhi hiyo ni mwananchi lakini kwa bahati mbaya elimu haikutolewa kwa hiyo hakukuwa na ushirikishwaji wa aina yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali yetu sikivu ifanye utaratibu wa kuja kuongea na wale wananchi, wajue maana ya hifadhi ni nini na watanufaika nini na wajibu wao. Pia, tunaomba tupewe angalau kilomita 5.5 za eneo ili wananchi waweke mizinga yao kwa zao wanalolitegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ambalo tunalileta ni kwamba, sisi tuna WMA ambayo ni kitu kizuri sana, tunaomba Serikali ilipe stahili zao. Kwa bahati mbaya mwaka 2021/2022 na mwaka 2022/2023 bado Serikali ilikuwa haijalipa lakini tunayo imani na Serikali yetu, tunaomba WMA ipewe fedha zake ambazo Serikali iliahidi kutoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, bado tunarudi kwa Serikali yetu. Mheshimiwa Waziri nakuheshimu, nakuamini pamoja na Naibu na Wizara yote kwa ujumla. Mlikuja mkatoa ahadi kwa wananchi kwamba mtawapa mashine, mtawasaidia kuwa na umeme, mtawapa kisima, wakafurahi na bado wana imani na Serikali yao. Tunaomba mashine ya kuchenjua asali, pia mje mtembelee muone eneo lile, kwa sababu wananchi wamejiunga wana imani na Serikali yao kwamba wataendeleza zao la asali ili waweze kusafirisha na kuinua uchumi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nisingependa kuendelea na maneno zaidi kwa sababu shida zangu ni hizo hizo. Naomba uniruhusu nimalizie kabla kengele haijalia. Kwanza, tunaomba mje muongee na wananchi, kuwapa elimu na wajibu wao. Pili, tunaomba muwape eneo lao la kuweka mzinga, kilomita 5.5 ndiyo pendekezo letu. Tatu, tunaomba WMA ilipwe fedha zao na mwisho tunaomba mashine ya kuchenjua asali kama tulivyoomba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naona kengele haijalia, mwisho kabisa labda nikumbushe kidogo tu, hili suala siyo la leo tu. Mheshimiwa Kigwangalla akiwa Waziri alikuja, bahati mbaya mvua ikanyesha akashindwa. Alikuja Mheshimiwa Ramo Makani kama Naibu Waziri naye akashindwa lakini pia Mheshimiwa Josephat Hasunga naye alifika ili kutatua tatizo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini kabisa Mheshimiwa Waziri aliyepo sasa hivi na Naibu Waziri naamini watakuja waone maeneo haya na nyinyi mtakubaliana na maombi ya wananchi wetu, hayo ambayo nimeyatanguliza siku ya leo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nina imani na Serikali yetu na ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)