Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ili na mimi niweze kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya mwaka huu 2024 /2025. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo ada nichukue nafasi hii kumpongeza sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi nzuri na ubunifu mzuri katika sekta hii ya utalii. Wakati anaanza na ajenda ya Royal Tour, tuliona kama ni kitu cha kawaida lakini sasa tumeona matunda ya ubunifu wake, kwa kweli tunampongeza sana Mama apewe maua yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Angellah Kairuki, Waziri wa Maliasili na Utalii, pia nimpongeze Naibu wake pamoja na Katibu Mkuu Dkt. Abbas kwa kazi nzuri ambayo mnaendelea kuifanya na delegation yenu yote, kwa kweli mnafanya kazi nzuri sana, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nampongeza Naibu wake pamoja na Katibu Mkuu Dkt. Abbas kwa kazi nzuri ambayo mnaendelea kuifanya na delegation yenu yote. Kwa kweli mnafanya kazi nzuri sana, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mafanikio kama hayo, hakukosi changamoto. Nimeona hapa kuna suala linahusiana na utambuzi wa maeneo ya malikale nchini na kuyatangaza kuwa Urithi wa Taifa. Nilipokuwa napitia hii bajeti, kwa kweli nimekutana na kitu ambacho kilinisononesha sana. Yametajwa maeneo kama 11 ambayo yatawekwa kama urithi na kumbukizi ya maeneo hayo yakiwepo Morogoro, Rukwa, Songwe, Mbeya, Katavi, lakini Ruvuma haijatajwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ruvuma sisi tuna Makumbusho ya Majimaji, Wajerumani walikuja pale sisi ndiyo mashujaa wenu Wangoni. Tulisimama tukapigana kuhakikisha kwamba adha ile haiwakuti huku lakini mnashindwa kutambua kwamba kuna Makumbusho ya Majimaji. Kwa kweli hatujatendewa haki, tunataka Wizara iweke suala hili la Makumbusho ya Majimaji na iletewe pesa ili Makumbusho ya Majimaji iendelee kukua na iweze kuletewa watalii wengi kwenye eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo kumbukumbu kubwa sana, kwa sababu ya muda, naamini kabisa katika historia ya vitabu, kila Mtanzania anajua. Pia, naomba kusema, katika kumbukumbu hizi za Makumbusho ya Majimaji, yuko Chifu Mbano, babu yetu sisi. Alikatwa kichwa chake na kichwa chake kikapelekwa Ujerumani, mpaka leo kichwa kile hakijarudishwa. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri, mnapokezana tu hapo, Mheshimiwa Waziri huyu, Mheshimiwa Waziri huyu, Mheshimiwa Waziri huyu lakini hamrudishi kichwa cha babu yetu, tunadai kichwa cha babu yetu Mbano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtuletee kichwa cha babu yetu, kinafanya nini Ujerumani? Yule ni Mngoni na wala siyo Mjerumani. Tafadhali sana tunaomba mturudishie kichwa cha babu yetu ili tuweze, katika yale Makumbusho ya Majimaji, sasa kichwa kile kitatuletea watalii wengi sana. Watakuja kuona kile kichwa kilikuwa na madini ya aina gani na hata aliweza kunyongwa karibu mara tatu alishindwa kufa mpaka wakaamua kumpiga risasi. Mheshimiwa Waziri tutaelewana mimi na wewe, utakuwa best yangu kama kichwa cha babu yangu Mbano kitarudi kule. Wanaruvuma wanahitaji kichwa cha babu yao Mbano, ahsante. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niende kwenye Ziwa Nyasa. Ziwa Nyasa ni ziwa ambalo kimsingi limezungukwa na mambo mengi mazuri yanayohusiana na utalii. Nataka kusema tu kwamba, kuna Kisiwa cha Ndumbi pale, kisiwa kile kipo hakiendelezwi. Jamani kwa nini katika nchi hii mnapoamua kuendeleza masuala ya utalii mnaendeleza upande mmoja tu lakini Ruvuma, upande wa Kusini hamuendelezi utalii? Mbona kila siku tunalia humu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi, Waheshimiwa Wabunge wa Lindi, Mtwara, Ruvuma, Njombe, sisi tunahitaji kukuzwa utalii kule kwetu. Tunahitaji na sisi tuone watalii wanakuja, tuweze kuendelea kukuza uchumi lakini pia watalii wakiendelea kuja, na ajira zitaongezeka, tunaomba tafadhali sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la Ziwa Nyasa, pia kuna samaki wazuri sana wa mapambo; wako aina 400, nayo pia ni sehemu ya utalii. Tunaomba Mheshimiwa Waziri, katika kukuza maeneo ambayo ni vivutio vya utalii, basi na Nyasa nayo itengewe pesa ili iweze kukua kiutalii. Kuna ngoma za asili, na wachezaji tupo wa ngoma hizo. Mheshimiwa Engineer Manyanya, mchezaji mzuri wa ngoma za asili, zimejaa kule kwetu Ruvuma, Nyasa, Songea na maeneo mengine, Namtumbo, Tunduru na maeneo mengine yote mpaka Songea Vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tukifunga kibwewe, tunafunga kwelikweli, kwa hiyo ni sehemu ya utalii. Tunaomba sana, Mheshimiwa Waziri, tunaomba u-promote hivi vitu. Mimi nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson Mwansasu, ambaye ni Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukuza ile Tulia Festival ambayo kila mwaka anaendeleza masuala ya mila na desturi, mambo ya ngoma na nini. Nayo pia ni sehemu ya raha, ni sehemu ya utalii, inaleta raha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi naomba Mheshimiwa Waziri, katika kazi zako unazoendelea kufanya, tunataka tuone mageuzi katika vitu hivyo vidogo vodogo ambavyo vitatuingizia pato kubwa katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, ni suala linalohusiana na tembo. Kwa kweli nataka kusema, nampongeza Mheshimiwa mama Lulida, kachangia vizuri sana, lakini mama yangu Mheshimiwa Jesca Msambatavangu mmh! Yaani tembo wale waanze kuja huku, ameoanisha tembo wa India na tembo wa Tanzania. Tembo wa Tanzania, tembo kwelikweli, huwezi kulinganisha na vitoto vile vya India, vile vya India ni vitoto, Mheshimiwa Jesca tafadhali naona unataka kuwasha mic, utanipotezea muda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kusema, tafadhali sana, hoja yake inawezekana ni nzuri na ina mashiko, lakini itachukua umri mrefu sana mpaka kwenda kuanza kuwafundisha, kuwaelekeza. Kubwa ambalo nataka kuuliza Wizara; je, wamewahi kufanya utafiti kwa nini tembo wanatoka kule porini wanakuja huku? Wamewahi kufanya utafiti? Kama wamefanya utafiti, basi watuletee majibu hapa utafiti walioufanya ni kitu gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi miaka mitano iliyopita, nimepiga kelele sana kuhusu tembo lakini wakati huu, sitaweza kupiga tena zaidi ya kushauri Serikali hii kwamba kule ndani kwenye mapori yale ambayo ya wanyamapori, sasa hivi yamekuwa siyo mapori ya wanyamapori, ni mapori ya wanayamawatu kwa sababu wafugaji wamejaa huko, wanatembeza ng’ombe wao kila mahali. Wanyama kama Wanyama sasa hivi, siyo tembo tu tunawaona tembo kwa sababu wamekuwa na athari kubwa sana katika jamii lakini wanyama wengi: fisi, tumbili, nini, wote tunapishana nao huko mitaani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwa sababu wale wafugaji wanakuwa wana ng’ombe wao, wale ng’ombe wamewafunga kengele, wanapopiga kengele kule katikati ya misitu, tembo wanakimbia na wanyama wengine wanakimbia. Waende wapi? Wanakuja huku kwa binadamu. Kwa hiyo iko haja ya kufanya utafiti na kuhakikisha kwamba tunaondoa wale watu walioko huko ambao wanafanya uharibifu, ambao wanachunga ng’ombe huko tofauti na taratibu na Sheria za nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi nasema kwamba, pamoja na jitihada za Serikali ambayo zinaendelea kuleta mabomu ya kuwaondoa tembo, kuongeza askari, kuongeza risasi baridi, napo itakuwa haitoshelezi kwa sababu tembo watazidi kuwa wanafika tu.

MWENYEKITI: Ahsante sana kwa mchango wako.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika moja tu, sekunde moja. Ulikuwa unakaa hapa, baadaye umehamia hapo, sekunde moja nimalizie. (Makofi)

MWENYEKITI: Hitimisha. (Makofi/Kicheko)

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka kumuuliza Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana, anataka hawa tembo awaone wanaingia Ikulu? Eeh?

MWENYEKITI: Mheshimiwa hitimisha.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)