Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi kuweza kuchangia katika hoja iliyopo mbele yetu ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Kwanza nasema, bila shaka Wizara hii ni miongoni mwa Wizara chache ambazo ni kwa bahati nzuri zimepata nyongeza ya bajeti tofauti na Wizara nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa pamoja na nyongeza hii waliyopata, imekuwa pia ni bahati mbaya nyongeza hii haijaelekezwa kwenye mambo muhimu na ya msingi ambayo sisi Waheshimiwa Wabunge kama wawakilishi wa wananchi, hapa ndani ya Bunge, mara zote tumekuwa tukisema na tukieleza, na katika mijadala mbalimbali hata kama siyo ya hapa, kwenye Kamati, nje ya vikao hivi, lakini adha ambazo wanapata wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wananchi wetu kwenye maeneo yetu, tumekuwa tukijadili habari ya wanyama wakali na waharibifu katika maeneo yetu. Bahati mbaya pamoja na bahati hiyo waliyoipata Wizara hii, fedha hizo ambazo wamepata kama nyongeza, hakuna ambayo imeelekezwa kuweka nguvu kubwa katika suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa takwimu, karibia asilimia 49.5 ya halmashauri zetu kwa maana ya halmashauri 91, ndizo halmashauri ambazo kwa kiwango kikubwa zimeathirika na suala la wanyama wakali na waharibifu kuingia katika maeneo yetu, kumaliza mazao, wananchi kuuawa na wengine kujeruhiwa. Kwa bahati hiyo waliyoipata, sisi kama wanakamati, hawajatushawishi kuonesha ni namna gani wanakabiliana na matatizo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati hiyo waliyopata ya nyongeza ya fedha ya shilingi 19,000,000,000, matokeo yake wanasema katika fedha shilingi 19,000,000,000 walizopata, shilingi 14,000,000,000 inaenda kwenye matumizi ya kawaida, na shilingi 5,000,000,000 peke yake inaenda kwenye fedha za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitarajia tuone mikakati hiyo kutokana na hii nyongeza. Tulitarajia pia, tuone mikakati ya namna gani tunaokoa shoroba kwa sababu mwisho wa siku pia wanyama wanaingia kwenye maeneo yetu shoroba zote zimevamiwa, namna gani wanakuja na mkakati. Pia, namna gani mkakati wa kutangaza utalii kwa sababu utalii kwa nchi hii ni sehemu ambayo inaingizia Pato la Nchi na ni Sekta ambayo pia inasaidia nchi kupata fedha za kigeni, imekuwa ni bahati mbaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii imetusikitisha kama wanakamati na mimi ni mmoja wa Kamati lakini tunaamini, kupitia Bunge hili sasa na Waheshimiwa Wabunge, tutahakikisha hiki ambacho wameongezewa, kinaelekezwa katika maeneo muhimu ya kukabiliana na masuala yote ambayo tumesema na changamoto ambazo wananchi wanakutana nazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, hizi taasisi zetu ambazo zimeachiwa kitu kinaitwa retention, huko nyuma walikuwa wanapewa retention, baadaye ikaja ikaondolewa, na sasa hivi tumerudi kwenye ule mfumo kwa maana ya TANAPA na NCAA kwa maana ya Ngorongoro. Lengo la kuachia hizi fedha wakusanye wenyewe na wazitumie, na baadhi ya percent iende kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali inaeleweka kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatarajia kuona kwamba baada ya fedha hizi kubaki mikononi mwao, tutarajie kuona ufanisi wa taasisi katika utendaji wao wa kazi. Hatutarajii kuona upigaji ukifanyika wa hizi hela, tunatarajia kuona hizi taasisi zinafanya vizuri katika suala zima la kuhifadhi maeneo yetu yote ya hifadhi kama ni Ngorongoro, ni TANAPA, lakini miundombinu iliyoko ndani ya hifadhi hizi zinaboreshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, tuna barabara ya kutoka Ngorongoro kuelekea Serengeti, kipindi cha mvua, na tunaenda kupindi cha high season, ile barabara ni mbovu, ni mbovu, ni mbovu. Tunatarajia sasa, kwa sababu mmepewa retention hii, tuone matokeo ambayo tunatamani kuyasikia na kuyaona kwa macho tukitembelea na kuona vitu hivyo kwa maana ya kwamba kuboresha miundombinu kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, msifanye ule wakati ambao ni high season. Bahati mbaya sana ikifika tena wakati wa high season, Wazungu mfano, watalii wameingia crater, unakutana na ma-grader ndiyo vifusi vinaanza kumwagwa huko, ndiyo ma-grader yanaanza kusambaza, sasa what’s that? Hiyo ni nini? Huo ni utalii au ni vurugu? Maana yake magari yanapita yanatembeza watalii, humohumo unakuta ma-grader tena yanaanza kuchonga barabara, mara sijui imefanya nini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatarajia sasa, baada ya hili, kwa sababu tuliliomba muda mrefu na tulilisemea, tuone mabadiliko makubwa yanafanyika katika maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, asilimia 32.5 ya ardhi ya nchi hii, ni kwa ajili ya uhifadhi kwa maana ya maeneo ya hifadhi pamoja na misitu. Hii maana yake ni kwamba, hizi ni ardhi ambazo tayari ziko katika eneo hilo. Tunatambua ardhi haiongezeki, watu huongezeka, mahitaji ya utumiaji wa ardhi yanaongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutarajie na kuona kwamba hiki ambacho kimetengwa kwa ajili ya hifadhi kibaki hapo hapo. Kwa sababu tukiendelea kuongeza maeneo ni sahihi kabisa, ukija kwenye logic kwamba umuhimu wa utalii na umuhimu wa uhifadhi na vitu vyote vinavyohusiana na utalii kwenye kiuchumi, lakini kwa ajili ya mapato ya nchi ni suala zuri kabisa, lakini tukiendelea kusema kwamba tunapandisha baadhi ya mapori, tunachukua baadhi ya maeneo na kuyafanya hifadhi, nafikiri hapo tulipofika inatosha, hebu tuyatunze haya tuliyonayo kwanza tuyahifadhi, kwa sababu tukiendelea kupanua ndivyo tunavyendelea kuwa na migogoro na wananchi, ndivyo ambavyo tunaona hawa askari wetu wa Jeshi Usu ndilo linakwenda kupambana na wananchi kwa sababu wao kazi yao ni kulinda kile walichoambiwa, mwananchi yeye hakuelewi. Mwananchi yeye ana ng’ombe, anataka kufuga, anataka kulima na anaona ardhi yenyewe haitoshi, kule population inaongezeka, mahitaji ni makubwa, ardhi ni ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutarajie pia kwamba haya ambayo yamepimwa na kutambulika kama maeneo ya hifadhi na misitu ibaki kama ilivyo ili ardhi nyingine iendelee kupimwa, wananchi waendelee kutumia ardhi, lakini kuwepo na matumizi bora ya ardhi kwa maana ya kwamba kuwe na kukishirikiana kati ya Wizara hii na Wizara nyingine ya Adhi ili kuhakikisha kuwa ardhi ya Watanzania inawanufaisha watu wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti jambo lingine, mimi ninatoka Wilaya ya Karatu, pale Karatu tupo jirani na Ngorongoro. Karatu ndicho kitovu cha utalii, kwa maana ya kwamba watalii wote wanaokwenda kutembea Ngorongoro atatoka alikotoka anakuja kulala Karatu na Karatu tuna hoteli nzuri za kitalii (five stars hotel) karibia 68, ni nzuri kabisa. Huko nyuma nimechangia mara nyingi sana; tunaomba Karatu muufanye uwe mji kweli kweli wa kitalii. Tunaomba tuwe na culture tourism. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na programu inatwa Karatu Culture Tourism Center. Kuna timu iliundwa baina ya halmashauri na watu wa Ngorongoro, kuna kusuasua katika jambo hili. Tunaomba jambo hili lilifuke upya ili watalii wanapoenda Ngorongoro kutalii wapitie na Karatu, kuwepo na hiyo center ya culture tourism waangalie. Tuhakikishe kwamba tunaufanya Mji Karatu kuwa ni mji wa kitalii, tunauendeleza, tunauwekea miundombinu kwa kushirikiana na TAMISEMI na Wizara zingine ili kuhakikisha kwamba na sisi Karatu pale tunafaidika na watu wanaokwenda kutalii, kwa sababu ndiyo barabara ya kwenda Ngorongoro, ndipo ambapo watu wote wanapita pale kwenda huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili liende sambamba, kwenye Taarifa ya Kamati tumeonesha kabisa kwamba kuna uhaba wa vyumba vya kulala wageni, pamoja na hoteli tulizonazo lakini bado hoteli hazitoshelezi.

Kwa hiyo, tunaomba kuwepo na mikakati kati ya Wizara hii; pamoja na kwamba Kamati tumependekeza zile hoteli ambazo zilikuwa za Serikali zichukuliwe na kufufuliwa, lakini wako wadau ambao ni private sector, wako wadau ambao wana interest kuwepo na mazingira ya kuwawezesha. Wizara ije na mkakati wa kukaa na wadau, benki na watu mbalimbali kwa pamoja. Watu wenye interest wawezeshwe, lakini tuandae maeneo, kama pale ni Karatu ni Mto wa Mbu, maeneo jirani yote yapangwe, maeneo yatambuliwe kabisa kwamba maeneo haya ni kwa hoteli, maeneo haya ni kwa ajili ya uwekezaji wa wadau mbalimbali ili tuweze kufanikiwa na kuhakikisha ule upungufu wa vyumba tuliokuwa tuweze kuutosheleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya ninakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)