Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Prof. Shukrani Elisha Manya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi ya kuchangia hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii na nikiwa mchangiaji wa mwisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa niwapongeze kwa kazi kubwa za kuendeleza jitihada za kuongeza watalii na kuboresha miundombinu ya vivutio vya utalii hapa nchini, ili sekta hii iendelee kuchangia pato la Taifa kwa kiwango cha juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitangulie kusema kwamba naunga mkono hoja pia naunga mapendekezo yote ya Bunge yaliyotolewa kwa ajili ya kuboresha utendaji kazi wa Wizara katika mwaka ujao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jioni ya leo nijitanue katika jambo ambalo nimewahi kuongea hapa Bungeni, lakini leo nataka niliweke wigo fulani hivi na jambo hili linagusa Wizara ya Maliasili na Utalii pia na Ofisi ya Makamu wa Rais. Ni maeneo haya ambayo yanaitwa geoparks, ambayo malengo yake ya kuyaanzisha ni kukuza utalii pia na mafunzo na kuifanya jumuiya ambayo ipo jirani kuendelea kufaidika na kuanzishwa huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni kwamba jambo hili lina fursa ambazo ni kama sisi kama nchi tunachelea kidogo na sababu ya kusema hivyo ni kwamba, wazo hili la kuhifadhi haya maeneo yenye urithi wa kijiolojia lilianza nchini Ufaransa mwaka 1991. UNESCO ikalibeba mwaka 1997 na kufikia mwaka 2004 UNESCO ikawa imeunda Mtandao wa Geopark wa kidunia unaoitwa UNESCO Global Geopark Network. Sasa hiyo ni 2004 na mabara mengine yakachangamkia fursa hiyo na yamekuwa yakipata fedha kutoka UNESCO kwa sababu ya kuanzisha geoparks katika nchi zao. Hadi sasa nakwenda haraka kwa sababu utanza kugusa gusa microphone yako hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa UNESCO duniani ina geoparks zenye hadhi ya kidunia, maana unaweza ukawa na geopark, lakini hiyo ambayo inatambulika kama UNESCO Global Geopark zipo 243, lakini katika mataifa 48 tu. Afrika tunazo mbili tu, M'Goun Geopark ya Morocco, lakini bahati na habari njema ni kwamba mojawapo ni Ngorongoro Lengai Geopark ya nchini Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii geopark yetu ya hapa Ngorongoo Lengai ambayo ina hadhi inayotambuliwa na UNESCO globally ilipata hadhi hiyo mwaka 2018 na walijumuisha maeneo mazuri ya Crater ya Ngorongoro, Mlima wa Oldonyo Lengai, Nyayo za Binadamu wa Kale za Laetoli pamoja na Tambarare za Serengeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya faida ya kuwa na mfumo huo wa mtindo ambapo geopark yako inatambuliwa na UNESCO kwa ngazi ya kidunia. Fursa zitokanazo na kuwepo kwa hiyo geopark, lile jengo ambalo tunaliona pale Olduvai Gorge lilipata msaada wa fedha kutoka Umoja wa Ulaya bilioni tatu ndipo jengo lile likajengwa, lakini pia utagundua kwamba hata katika utalii wetu ndilo eneo ambalo pia linavuta watalii wengi sana kwa sababu limeanza kueleweka na kutambulika na UNESCO geopark. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hoja yangu ni kwamba kuna fursa hapa ambayo kama nchi tunachelea kuitumia kwa sababu maeneo kama hayo ni mengi mno, yaani kwamba Mlima Kilimanjaro sasa hivi hifadhi yake bado haijatambuliwa kama UNESCO Geopark wakati ni kitu kikubwa sana kidunia na kinaeleweka hivyo kwamba sasa hivi ndipo ambapo Hifadhi ya Kilimanjaro imeomba UNESCO waje kufanya tathmini, ili hatimaye na yenyewe ipendekezwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuna maeneo mengi ya jinsi hiyo Tanzania, Mheshimiwa Mama Lulida anapenda sana kuongea habari ya Tendaguru Site ya dinosaurs ni kitu kikubwa kijiolojia duniani lakini hapa ndani huwa tunakionaona tu tunasema pale alipotoka mjusi na tunamuita mjusi tunapadogosha. Yule dinosaur aliyeko Ujerumani hivi unajua anakaa kwenye hili jengo letu lote hapa, sisi tunaita tu Tendaguru mjusi sio mjusi yule ni dinosauria mkubwa kabisa. Kwa hiyo, haipaswi kitu kama Tendaguru kuendelea kuchukuliwa katika hali ya kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yale Mapango ya Amboni Tanga na yenyewe yametokea, ukienda pale utakutana na mwongozaji ambaye hata hawezi kueleza yametokanaje, tunayaacha tu. Nilishatoa hoja pia ya Mautia Hills na mambo kama hayo, tuna maeneo mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa pendekezo langu ni kwamba fursa hii ipo ila sisi kama nchi hatujaichukulia maanani. Mamlaka ya Ngorongoro mpaka ikapata, ilifanya jitihada binafsi kuunda Kamati ya Kitaifa ya Geopark, ili iweze kukidhi vigezo na kwa jinsi hiyo imekuwa inaifadhili kufanya shughuli zake, lakini kamati hii kama ingetambuliwa kitaifa maana yake ni kwamba tungeweza kupata faida nyingi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa sasa hivi kamati hii yaani inafanya shughuli zake ikifadhiliwa na Mamlaka ya Eneo la Ngorongoro, basi, lakini haitambuliki kisheria na kwa msingi huo nilikuwa napendekeza Serikali ilichukue kama ni Maliasili au Ofisi ya Makamu wa Rais ilibebe, ili liweze kuwa na ngazi ya kitaifa yaani lifanye mambo yake liliwa na mamlaka kamili ya kitaifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikifanya kazi hiyo itaweza kupendekeza maeneo mengi zaidi ili hatimaye Tanzania sasa kama Bara la Afrika tunazo mbili tu. Hebu tufanye fursa sisi tuendelee kuwa wa kwanza katika kupata hizo geoparks ambazo zina level ya UNESCO kutambuliwa kidunia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kamati hii kwa sasa haina bajeti ya kufanya kzai zake kwa sababu ni Ngorongoro iliyoianzisha basi inatoa fedha tu kwa ajili ya kuendelea kukidhi kuwa kama hiyo UNESCO Global Geopark. Kwa hiyo, ipewe bajeti na wazo hiliā€¦

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

TAARIFA

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa kaka yangu Profesa pale, tunashukuru umetaja Mapango ya Amboni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mapango ya Amboni ni miongoni mwa geopark ambayo ninaamini kabisa kwenye ile rock weathering kama somo ambapo katika vyuo vyetu, inaweza ikatumika wanafunzi kwenda kujifunza pale. Mapango ya Amboni unapita chini kwa chini mpaka unatokea baharini. Ni miongoni mwa geopark ambayo haijafanyiwa tafiti ya kutosha namna gani tunaweza tukanufaika. Kule Japan nilishawahi kwenda sehemu kama Mapango ya Amboni na namna gani kama Taifa lao linanufaika, tuyatumie Mapango ya Amboni. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante. Profesa Manya unaipokea Taarifa kutoka kwa Engineer?

MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea taarifa hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mchango wangu naelekeza kwamba, hebu Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais waweze kurasimisha kamati hii iweze kuwa ni Kamati ya Kitaifa ya Geopark. Kwanza tupate hilo jambo, tukishalipata hilo jambo, itengewe bajeti ifanye kazi, ikishafanya kazi, vile vivutio vyote vilivyopo hapa ndani ikiwa ni Mapango ya Amboni na mambo mengi ambayo yanayoeleweka katika nchi hii maana yake yakishapata hadhi ya kidunia UNECSO Global Geopark, kwanza tutapata fedha kutoka UNESCO ambazo tunazikosa kwa sasa, maana yake tutakuwa tunaongeza pato letu la utalii kutoka Fedha za Mfuko wa UNESCO, pili, tutaongeza watalii na hivyo kuongeza fedha za kigeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mchango wangu hasa nataka kusisitiza kwamba hii Kamati ya Kitaifa ya Geopark isiendelee kubaki kama mtoto wa Mamlaka ya Ngorongoro, ili kufanya mambo yao ya kuendelea kuwa geopark ya kidunia yafae, badala yake ije hapa juu ipate hadhi ya kuwa Kamati ya Kitaifa ipewe bajeti, ili iweze kufanya kazi tuweze kupata UNESCO Global Geopark Tanzania za kutosha na tutagundua kwamba tutakuza mafunzo kwa watu wetu, tutakuza utalii, lakini pia tutapata fedha kutoka katika Mfuko wa Taifa wa UNESCO. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)