Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Dr. Christina Christopher Mnzava

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, kunipa afya njema na kuweza kusimama katika Bunge lako Tukufu na kutoa mchango wangu katika Bajeti Kuu iliyoko mbele yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia namshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo anaifanya kwetu Watanzania. Tumeona ni jinsi gani ambavyo anaendelea kuongeza bajeti ili maendeleo ya nchi hii yaweze kusonga mbele. Pia, nimpongeze sana Kaka yangu Dkt. Mwigulu Nchemba kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. Kazi ngumu ya kuhakikisha kwamba mapato ya nchi hii yanaendelea kuimarika na kuendelea kusimamaia matumizi katika sekta mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna ongezeko kubwa la bajeti. Ukiangalia kwa mwaka wa fedha tunaoumaliza, kwa maana ya 2023/2024, tuliidhinisha hapa takriban shilingi trilioni 44.39 lakini kwa mwaka huu wamekuja na ongezeko la karibu trilioni 5. Kwa kweli hili ni jambo ambalo linaonyesha ni jinsi gani Serikali ya Mama Samia inaendelea kuwajali Watanzania kwa kuendelea kuongeza fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika sekta ya afya, kwa mwaka wa fedha 2023/2024, sekta hii ilitengewa shilingi trilioni 1.24 hadi Machi zilitolewa takriban shilingi bilioni 838, kwa hiyo, hii ilikuwa karibu asilimia 68 ya fedha ambazo tulikuwa tumezipitisha katika Bunge hili ziliweza kupelekwa kwenye Wizara husika. Hii siyo katika sekta ya afya peke yake, hata sekta na Wizara zingine fedha zimepelekwa kwa kweli kwa mtiririko mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika fedha ambazo ziliidhinishwa na Wizara ya Afya, tumeona zimefanya kazi nyingi sana. Kuna maboma ambayo yamejengwa, katika sekta ya afya kuna zahanati zimejengwa, kuna vituo vya afya vimejengwa, kuna vitendea kazi, vifaatiba vya uchunguzi na ugunduzi vimenunuliwa, takriban Mikoa yote. Kwa kweli hii inaonyesha ni jinsi gani Serikali ya Mama Samia inavyowajali Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika sekta hii ya afya napenda niseme kitu kimoja, pamoja na mazuri yote ambayo Mama Samia anafanya, kuna changamoto ambayo mimi naona ni ndogo sana, na Wizara hii ya Fedha ambayo ndiyo inabeba mfuko mzima wa Serikali inaweza ikatatua. Wananchi wa Tanzania hususan katika Mkoa wa Shinyanga, kulikuwa kuna Sera ya Afya ya kuhakikisha kwamba kila kijiji na kila mtaa unakuwa na zahanati na kila Kata inakuwa na kituo cha afya, Sera hiyo haijawahi kufutwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kuna wananchi ambao kwa mapenzi na kwa hamasa waliyoipata waliweza kujitolea kujenga maboma, maboma yamefika katika lenta lakini yanaachwa, hii ni kuwavunja nguvu Watanzania, kuwavunja moyo Watanzania ambao walitumia nguvu zao katika kuendeleza maendeleo ya Tanzania yaani wakajitolea kwamba na sisi tuwe sehemu ya maendeleo ya nchi yetu, wamejenga yale maboma, yamefika kwenye lenta mengine yamepauliwa, lakini Serikali inashindwa kutoa fedha kumalizia yale maboma. Nikuombe sana Mheshimiwa Mwigulu, utakapokuja kuhitimisha bajeti yako utuambie, mna mpango gani kwa zile nguvukazi ambazo wananchi wa Tanzania walizitumia kuhakikisha kwamba, wanajenga maboma, wamejenga, mtawasaidia vipi kuhakikisha yale maboma yanakamilika ili na wao wawe sehemu ya mchango ambao Serikali ya Mama Samia inatoa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ningependa kuwapongeza sana Wizara hii ya Fedha kwa jinsi ambavyo mmeweza kuwasaidia watoto wetu na wanawake wa Tanzania, kwa kutoa kodi katika malighafi ya kutengeneza taulo za kike. Kwa kweli, nawashukuru sana. Pamoja na kutoa hiyo kodi ambayo ni asilimia karibu 10 mpaka 25 kwa wazalishaji, naomba sana usimamizi uwepo hasa katika sekta nzima ya viwanda na biashara, kwa sababu ninyi mmetoa kodi lakini wanaokuja kusimamia ule utekelezaji ili wananchi waweze kupata unafuu wa hiyo kodi ambayo Serikali imewaonea huruma inasimamiwa na Wizara ya Viwanda na Biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta kodi imetolewa, kwa sababu siyo mara ya kwanza, Wabunge waliotangulia katika Bunge hili walishasimama hapa hasa wanawake niwapongeze sana, wakaomba hizi pedi, taulo za kike ziweze kupunguziwa kodi, ilitolewa VAT ikawa haina VAT, lakini wafanyabiashara ambao siyo waaminifu hawakuweza kupunguza bei za taulo za kike. Kwa hiyo, mtumiaji ambaye ni mwananchi wa kawaida ambaye hana uwezo wa kununua pedi kwa gharama kubwa aliendelea kununua pedi kwa gharama ile ile ambayo pamoja na kwamba Serikali imepunguza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sana Wizara inayohusika, kama Wizara ya Fedha, kama Serikali ya Mama Samia imeamua kutoa kodi hiyo kwa mali ghafi, kwanza tuangalie tuna viwanda vingapi Tanzania ambavyo vinazalisha? Isiwe kwamba tunapunguza kodi, tunanufaisha watu wengine ambao wanaagiza hizi pedi kutoka nje au wanaangiza raw materials kutoka nje hapa wanakuja kufanya final touches za hizo bidhaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sana Wizara inayohusika ihakikishe kwamba inafuatilia, inasimamia lile punguzo la kodi kwa ajili ya malighafi za kutengeneza taulo za kike basi linawanufaisha wananchi ambao ni wa kawaida. Tukitaka kujua ni akina nani wananufaika, tuangalie wananchi ambao wananufaika na huu mpango wa TASAF, ni rahisi sana kuwapata wananchi ambao wanastahili, kwa sababu siyo wanawake wote Tanzania au familia zote ambazo hazina uwezo wa kununua hizo taulo za kike, wengine wana uwezo lakini wale ambao wanatoka kaya maskini ndiyo hasa ninaona ni walengwa ambao wanatakiwa wanufaike na hizo taulo za kike. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ambalo napenda kulizungumzia, tumeona hapo wakati wanawasilisha taarifa ya nishati, tuliletewa magari hapa ambayo yanatumia gesi, tukaanza kuelimishwa na kuhamasishwa na kuna baadhi ya wananchi wameshaanza kutumia magari ambayo yana mfumo wa gesi. Ningeomba sasa badala ya kupandisha hii bidhaa ya gesi, mmepandisha kama shilingi 300 na kitu, sina kumbukumbu vizuri, sasa kama mnapandisha, wakati tunahamasisha kutunza mazingira, wakati tunahamasisha matumizi ya gesi na gesi asilia tunayo sisi watanzania huku ndani, ni kwanini tusiweke mazingira mazuri tukapunguza bei ya gesi lakini hata tukapunguza kodi kwenye ile mifumo maana kufunga mfumo wa gesi ndiyo tatizo, ndiyo gharama kubwa lakini gesi haina gharama kubwa zaidi. Ningeomba hili ambalo mmepandisha Mheshimiwa Waziri karibia shilingi 300 na kitu kwa ajili ya gesi ya magari ningeomba muiangalie, muipitie, muweze kupunguza ili wananchi wengi wenye magari waweze kuhamasika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, ningeshauri sasa Serikali tuoneshe mfano. Tunajua tuna safari ndefu, tuna safari nyingi, magari ya Mawaziri, Makatibu Wakuu, Watendaji wa Halmashauri, mna safari za hapa na pale kwa ajili ya kuwahudumia wananchi. Wekeni utaratibu muwe wa kwanza kufunga hiyo mifumo ya gesi ili muweze kutuhamasisha hata sisi Wabunge tuweze kufunga mifumo ya gesi, kwa sababu, kiongozi anaonyesha njia, onesheni njia kwa nyinyi Serikali magari yote yafungwe mfumo wa gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya hapo hakikisheni kwamba vinakuwepo vituo vingi. Kama kuna vituo Dar es Salaam, basi na Dodoma viwepo na Mwanza viwepo na Kilimanjaro viwepo ili kila mwananchi aweze kushawishika na kuhamasika kuhakikisha kwamba anatumia mfumo wa gesi katika magari.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe kabisa anayeumia ni mwananchi wa kawaida, mkiongeza kodi yoyote, mkiongeza kitu chochote, anayeumia ni mlaji wa mwisho kwa sababu ndiye anayelipa kodi kule chini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, nimtie moyo endelea kufanya kazi, kazi siyo ndogo na unapofanya kazi nzuri ni lazima utatupiwa mawe. Ukitaka kusifiwa sana jua hufanyi kazi. Ukiona unasifiwa kwa kila kitu jua kwamba haufanyi kazi vizuri, lakini kama kuna mishale jua kwamba anhaa! kumbe majukumu niliyopewa ninayatimiza vizuri. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Ahsante.

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hivyo, ninaunga mkono hoja, ninawatakia kila la kheri na Mungu awabariki sana. (Makofi)