Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Morogoro Kusini Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia, naipongeza Wizara ya Fedha kwa ujumla. Nampongeza Kaka yangu, huyu ni dokta wa uchumi, kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu. Anafanya vizuri sehemu nyingi, anakosea sehemu moja tu na siku akijua kama hapa anakosea, atahamia kwa mnyama. Kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu unapokuwa Yanga ni makosa makubwa sana, kama hujui, pole sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nampongeza Mheshimiwa Rais, kwa kuitengeneza na kuiunda Wizara ya Mipango, naamini Wizara hii ina watu ambao ni mahiri sana. Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo, huyu alikuwa Mwenyekiti wa Kamati yetu ambayo ilikuwa inasimamia Wizara mbili, lakini pia, Mheshimiwa Rais hakuishia hapo akamleta Naibu wake, babu yangu huyu wa Kisukuma, Mheshimiwa Nyongo, pia, alikuwa Mwenyekiti wa Kamati yetu akisimamia Wizara nne.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mwigulu mmeletewa watu haswa. Huyu Mheshimiwa Nyongo ni mjanja, ni simba kwa hiyo, ujue kabisa mmeletewa watu ambao watakusaidia, mkishikana vizuri tutafika mbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naanza na Wizara ya Usafirishaji. Kwanza naipongeza, sasa hivi sisi wakazi wa Morogoro tayari treni inafika, lakini ukiwa unashuka kwenye treni unakwenda kuitafuta barabara ya lami, yani ukiingia hapo unapiga vumbi mpaka basi. Huu ni mtihani, kama tumesema tunataka kwenda kisasa ile treni abiria anakwenda ana vumbi mpaka kwenye macho kwa sababu, tu tumeshindwa kuwasaidia wenzetu wa TRC kutengeneza lami kutoka pale kituo kilipo mpaka wanapoelekea watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, basi wangetengeneza hata kilometa tano au kumi. Sisi wakazi wa Morogoro tukishuka kwenye treni pale, tunachezea vumbi, sijui bodaboda, sijui nini, Mheshimiwa Waziri tuiangalie hii. Dhamira ya Mheshimiwa Rais ni kutufanya tuwe modern, dhamira ya Mheshimiwa Rais ni kufanya watu wafurahie usafiri wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tunaona leo hii treni inafanya kazi, inafika mpaka Morogoro. Mimi ni mkazi wa Ngerengere, basi tupeni lami hata kilometa tano ilimradi wakati unasogea na bodaboda lile vumbi linakuwa limepungua, triii unaingia. Mheshimiwa Mwigulu, Kaka yangu, haya unayaweza sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, narudi kwenye kilio ambacho juzi nilipata bahati ya kukaa karibu na Mheshimiwa Spika, nikaji-beep, namba yangu amei-save Bigwa – Kisaki, heee! Nimesimama hapa over four years, huu ni mwaka wa nne, nalia na Bigwa – Kisaki mpaka Mheshimiwa Spika akaona abadilishe jina kwenye simu yake ani-save Bigwa – Kisaki. Kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu, hapa nitakusifia na hata ukisema ubaki na Yanga yako, nitaibakisha tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuomba, Mheshimiwa Bashungwa tumempa mzigo wa kutusaidia sisi wana-Morogoro vijijini, ile barabara inakwenda kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere. Mheshimiwa Rais akitaka kwenda kukagua bwawa ni lazima mumshushe na helikopta, basi timizeni ahadi ya Mheshimiwa Rais, marehemu, pia, mtimize ahadi ambayo Mheshimiwa Mama Samia ameongeza kilometa 78. Nimeongea juzi na Mheshimiwa Waziri, anasema kila kitu kashamaliza, mpira upo kwako.
Mheshimiwa Naibu Spika, namalizia basi, kama Pacome ZouZoua, ehee! Ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu nakuomba kabla haujamaliza hii bajeti usimame utuambie sisi wana-Morogoro Kusini Mashariki unaleta lini hii pesa, kwa ajili ya mkandarasi aanze kujenga Barabara yetu ya Bigwa – Kisaki. Vilevile Barabara yetu ya Ubena – Zomozi inayopitia Ngerengere kuelekea Mvuha. Hizi barabara zinakwenda kufungua uchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wana-Morogoro Kusini Mashariki juzi niliongea wakati tunafanya utekelezaji wa Ilani kwenye Jimbo letu la Morogoro Kusini Mashariki, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wetu kaka yangu Mheshimiwa Adam Malima amekwenda ku-modernize kule biashara ya spice. Sisi baada ya miaka 10 tunakwenda kuwa wakulima wa kwanza na wakubwa wa spice Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla, lakini hatuwezi kukua na barabara ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukitaka ujue kama tunatokea kwenye kijiji kina mateso leo hii nenda, hakuna barabara. Tumetoka kwenye mvua juzi, mashimo mtoto mdogo anajificha gari linapita juu, huu ni mtihani sana. Nakuomba sana kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu kabla haujamaliza bajeti hii usimame useme, mkandarasi anataka advance yake tu shilingi 20,000,000,000 ukimpiga nayo usoni, tunamuona mkandarasi site anafanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunakuwa sehemu ya kuimba iyena iyena yenye nguvu kwa Mheshimiwa Rais wetu. Asikuongopee mtu, uchumi ni barabara pia. Leo hii, sisi tunatamba kusema tunanywesha juisi na kulisha matunda Mkoa wa Dar es Salaam, Mkoa wa Dodoma na Mkoa wa Iringa kwa barabara ileile mbovu, lakini kesho na keshokutwa mkituletea pesa, mkithamini kama sisi wana-Morogoro Kusini Mashariki na wana-Morogoro Vijijini kwa ujumla tunahitaji ile barabara, mtakuwa mmetunza kura za Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kumshukuru Mheshimiwa Rais, kwetu sisi Morogoro Vijijini na Morogoro Kusini Mashariki, ametuletea Mradi wa Morong’anya wa zaidi ya shilingi 23,000,000,000 na Vituo vya afya kwenye Kata yetu ya Mkulazi, hapakuwahi kuwa na kituo cha afya, ametuletea kituo cha afya, ametuletea zahanati. Kiukweli kabisa mimi leo hii nasema 2025 Mheshimiwa Samia kwanza, mengine baadaye na mimi nijipakulie tu ukoko hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hiki Kiti nitakukuta nacho, lazima nirudi 2025. Ninarudi kwa sababu ya yale ambayo Mheshimiwa Rais ameyafanya, nitarudi kwa yale ambayo sisi tunaona kabisa ni ndoto, lakini, ili tuamke kabisa tuleteeni barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe hili jambo kidogo kwenye upande wa Wizara ya TAMISEMI, upande wetu wa Kituo chetu cha Afya cha Ngerengere. Wewe ulikuwepo hapa wakati nikikiombea pesa Kituo cha Afya cha Ngerengere miaka miwili iliyopita, hiki kituo tumerithi kwa mkoloni, hatuna kituo cha afya. Leo hii hatuna kituo cha afya na gari tulipewa miaka kumi na tano iliyopita kwa hiyo hatuna kituo cha afya, hatuna hata gari la wagonjwa kwenye Kituo cha Afya cha Ngerengere.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sisi wakazi wa Morogoro Vijijini mtutazame. Umesoma bajeti ambayo tunaona kabisa inakwenda kutafsiri maendeleo, inakwenda kutafsiri ile lugha ambayo Mheshimiwa Rais anasimama kuzungumza, ya mabadiliko ya maendeleo ya nchi. Sasa na sisi tuwe sehemu ya hayo mabadiliko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nashindwa kuzungumza kwa nguvu kwa sababu kuna sehemu nimepewa vitu najisikia raha. Leo hii sina shida ya maji kwa sababu ya huu Mradi wa Morong’anya. Leo hii Kata yetu ya Mkambarani tumeletewa shilingi bilioni nne kwa sababu ya mradi wa maji Alhamdulilah. Hapa nimesimama nalia tu kwa sababu ya barabara, kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu nakuomba nisadie basi yaani hata ukisimama kutaka kumaliza hii bajeti useme neno maana kuondoka na shilingi yako ni kuondoka na shilingi za Wizara zote. Sema neno juu ya hii Barabara ya Bigwa – Kisaki…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Taletale, ahsante.
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)