Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia hizi hoja mbili za Waziri wa Fedha na Waziri wa Mipango na Uwekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kuwapongeza kwa kazi nzuri ambayo mmeifanya Wizara zote mbili na Mawaziri wote wawili, Naibu Mawaziri wenu na wafanyakazi wote wa Wizara hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri niongee tu kwamba ninavyoangalia bajeti zetu kila mwaka, tukija hapa ni matatizo ya kuambiwa bajeti iliyopitishwa mwaka jana hili na hili halikufanyika, halafu hapo hapo unakuta hata zile barabara ambazo zimewekewa hela zimetengenezwa kidogo, zingine hazijatengenezwa, kunakuwa na wakandarasi ambao wanadai fedha nyingi na mapungufu mengi katika kutekeleza haya tunayopanga. Kwa hiyo, najiuliza hivi tunapanga bajeti kila mwaka ili nini, kama tunayopanga hayatekelezeki? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia hata ukiangalia ripoti ya CAG, nimekuwa Mwenyekiti wa Kamati hii mwaka wa tisa huu na kila mwaka tungepiga total ya fedha ambayo inaonekana kwamba haitumiki vizuri tusingehitaji kwenda kukopa. Kwa hiyo, ukiangalia tunakosa monitoring na evaluation system ambayo inasema haya tunayopitisha hapa yanatekelezwa vizuri? Kama hayatekelezwi vizuri tufanye nini hatua gani ichukuliwe? Kama mwananchi anaona aliahidiwa maji hayafiki, barabara imetengenezwa kidogo, fedha nyingi inaenda kwa wakandarasi, sasa tunapoteza muda wa nini kukaa hapa kupitisha bajeti kila mwaka? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nikaangalia tunaposifu wenzetu wa China kwamba wanatengeneza mipango yao vizuri walikuwa nchi maskini hata miaka ile Mwalimu Nyerere akiwapigania hata waingie wawe na wawakilishi wa kudumu kwenye UN walikuwa chini sana, mpaka wanatetewa na Tanzania, sasa hivi wapo mbali sana, lakini unaona wenzetu wana centrally planned economy ambayo imepangwa vizuri sana, so much so that inafuatiliwa na inakuwa monitored kwamba, kila kilichopangwa kinatekelezwa kilivyopangwa. Hiyo inaleta unafuu hata kwa Waziri wa Fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi namuonea huruma sana mkwe wangu Dkt. Mwigulu Nchemba, kila anayesimama hapa anamuomba barabara yangu haijaisha, hiki na kile hakijaisha. Leo tena tunachangia kama tupo kwenye sectoral budget, sasa mimi nachanganyikiwa kwamba hivi tunachangia za kisekta au tunamsaidia Waziri kwamba bajeti yako iendeje, maana yake tunaanza kuomba tena. Sasa unaona kwamba jamani sijui ni mimi nachanganyikiwa au ni nani? (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nasema kwamba hebu tuangalie na tujifunze kwa wenzetu, Je, ni discipline tunakosa sisi watanzania kwamba, hata mkwe wangu watu wakikufuata wakikupigia magoti kweli hulali, kwa hiyo unasogeza fedha hii tena unapeleka kule. Mwingine kuna matamshi ya viongozi kwa nini hapa hamjaleta maji? Waziri njoo kesho, haya hawa wapate maji kesho, tunakimbia tena. Kwa hiyo, mimi najiuliza hivi mipango yote hii tunafanya inatusaidia nini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, labda niombe tu Waziri wetu wa Mipango na Uwekezaji hebu ajaribu kuunda Wizara yake such a way that, kwa kweli tutakuwa na plans nzuri za short term, medium term na long term ili hata bajeti ikifanywa wao kazi yao kubwa wana-monitor. Kunakuwa na midterm monitoring kuona kwamba hiki tulichofanya kinakwendaje ili tu-arrest the situation kabla mambo hayajaharibika. Tusingoje mpaka aje CAG kuona hapa tuna mapungufu, hapa fedha imeibiwa. Sasa, huo muda wa kuibiwa fedha ni kwa vile hakufanyiwi monitoring na evaluation kila wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi nasema kwamba tujifunze kwa wenzetu Marekani wana mipango miwili centrally planned pia wana ile ya binafsi. Ukienda wenzetu wa Denmark wana system ambayo ndiyo kama tulijaribu kuitumia kwamba, tunagatua madaraka. Sasa, mimi nashindwa kuelewa sasa hivi tumesimama wapi, mipango yetu ipo wapi? Maana kila leo unavurugwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mwingine kapata fedha yake nje huko, anakuja anamwambia Waziri wa Fedha nina fedha hii nimeleta nataka kufanya hivi, sasa hata Waziri anachanganyikiwa anaona nifanye nini sasa? Tumepanga mpango huu, kuna haya yanayokuja na hatujui ni mikopo au ni misaada, na hiyo misaada inakuja kwa njia gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu ambacho nimeona tuna tatizo kubwa sana, tunakosa land masterplan, sasa tumesema hapa kwamba uti wa mgongo wa nchi yetu ni wakulima ambao wengi ndiyo wameajiriwa huko vijijini. Pia tumeona kila siku kama siyo ng’ombe wameingizwa kwenye mashamba basi usiku ni tembo, bado ndege wa kweleakwelea, bado wafugaji na wakulima wanavyopigana mishale, sasa tunasema haya yote ni ya nini? Halafu tukija kupitisha bajeti ya Wizara hii ya Ardhi tunapitisha sawa sawa na mtu mwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi nafikiri Waziri wetu wa Mipango na Uwekezaji hebu liangalie hili kwamba, utafanya nini kuwe na land masterplan ambayo inaonesha vividly kwamba sasa hapa bwana, na tulisikia juzi watu wamejenga kwenye vijiji chini kuna madini, haya tunafanya nini? Tunayafukia, tunamng’oa yule mwenye nyumba ili uchukue madini yako? Wengine wanasema ukilima bangi ni ya kwako, lakini kwenye madini ni ya Serikali yakiwa nyumbani kwako. Sasa tusiwe na double standard. Kwa hiyo, tuseme hivi, tuwe na masterplans ambazo zinatusaidia. Land masterplans is very important ili hata mipango hii ya kufanya compensation, leo tunapanga barabara inapita hapa lazima hawa wavunjiwe nyumba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mlinipa mradi kule wa barabara yetu ya kutoka Ndungu hadi Mkomazi, Mkandarasi yupo site lakini fedha ya compensation haijapelekwa. Fedha ya advance ya Mkandarasi haijapelekwa. Sasa hizi compensation kwa nini ziwepo? Zinakuwepo kwa vile hatuna masterplan kwamba, hapa itapita barabara, wananchi waishi hapa, mkulima ni hapa, mfugaji usivuke hapa na wewe eneo lako hilo, lakini sasa ni mixed grill ambayo hatujui tunakwenda wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ni National Water and Sanitation Masterplan. Kila anayelia hapa maji. Tunajua maji ni uhai, hii nchi haiwezi kwenda kama hatuna maji, hata tungepata dhahabu majengo na kila kitu. Kama hakuna maji hamna anayeweza ku-survive. Kwa hiyo, niombe sana ndugu yangu Prof. Kitila Mkumbo najua unaweza sana, hebu tuangalie hivi vitu vyote tuvisimamie, Wizara yako ni ya mipango I am sure muda huu ni mfupi sana na bado una mobilize resources na watu. Hii ni Wizara ambayo inatakiwa iwe Wizara Mama ambayo kila Wizara inachukua mipango yake kama ilivyopitishwa na Wizara yako ya Mipango. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wapo Mawaziri Wakuu na ambao walikuwa Mawaziri wa Fedha ambao bado wanaishi, Mheshimiwa Msuya, walijua mipango huko nyuma ilikuwa inakwendaje, amekuwa Wizara ya Fedha alipokuwa Waziri pale, tukiwa-consult hawa wanaweza kutusaidia halafu tuwapeleke vijana wetu nje wakasome. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi vitu siyo vya kubahatisha tu kwamba leo umewekwa unaweka hapa, msaidiane kabisa na Waziri wetu ili tuwe na mipango ambayo ipo very systematic halafu monitoring and evaluation tusilindane, kama mtu hafanyi kazi basi, siyo leo ameharibu hapa anahamishiwa kesho kule, anaachishwa kazi kesho anakuwa appointed kazi ile pale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona hata ripoti za CAG hapa wengine ambao tuliona waliwekwa pembeni…
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Kaboyoka, kengele ya pili.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Basi naomba hiyo Wizara yetu ya Planning ifanye kazi yake properly ya planning, ahsante sana. (Makofi)